Buriani Mo Dahman, Profesa Zawawi

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,239
Na Ahmed Rajab

WIKI mbili zilizopita ulimwengu wa Waswahili uligubikwa na huzuni kubwa kwa kuondokewa na magwiji wawili kila mmoja akiwa amebobea katika tasnia yake. Wa kwanza aliyetangulia alikuwa mtangazaji wa redio Mohamed Dahman, aliyefariki dunia Agosti 2, 2019, hospitalini jijini Köln, Ujerumani, akiwa na umri wa miaka 59. Alifariki baada ya kuugua kwa miaka miwili

Wa pili alikuwa Profesa mstaafu Sharifa Mohamed Zawawi aliyefariki dunia ghafla nyumbani kwake Matemwe, kaskazini mwa kisiwa cha Unguja, akiwa likizoni kutoka Marekani alikokuwa akiishi na kusomesha. Alikuwa na umri wa miaka 85.

Niliwahi kukutana na Dahman Mei 2015, huko Köln alikokuwa akiishi. Hiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza na ya mwisho kuonana naye. Nilimuona mtu mrefu mwembamba, mwenye uso mkunjufu uliokuwa kama umebandikwa tabasamu mdomoni. Hakuwa mtu niliyekuwa nikijuana naye hivyo licha ya kupata kuzungumza naye kwa simu mara kadha wa kadha alipokuwa akinipigia kunihoji kuhusu mada au matukio mbalimbali duniani.

Kwa saa chache nilizokuwa naye alinidhihirikia kuwa alikuwa mtu mpole, mcheshi, mzungumzaji aliyekuwa na staha kubwa. Dahman alikuwa miongoni mwa watangazaji kutoka Zanzibar waliojipatia sifa kubwa katika taasisi za utangazaji za kimataifa.

Alianza utangazaji kwa kufanya kazi Redio Tanzania, Dar es Salaam, na baadaye alijiunga na Idhaa ya Kiswahili ya shirika la utangazaji la Japani, Nippon Hōsō Kyōkai (NHK), jijini Tokyo.

Aliondoka Japani 2000 na kuhamia Ujerumani baada ya kuajiriwa na idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani (DW) ambako alizidi kujipatia umaarufu na washabiki wengi zaidi waliokuwa wakivutiwa na utangazaji wake. Mara baada ya kupashwa habari za kifo chake nilimpigia simu Mohammed Abdul Rahman, aliyekuwa naibu mkuu wa idhaa hiyo na ambaye sasa amestaafu. na akimuelezea marehemu alisema alikuwa mtu wa watu. Alinambia kwamba akiingia tu kazini alikuwa na desturi ya kupiga hodi kila ofisi kuwasabahi wenzake. Kiutendaji pamoja na usomaji wake wa habari kwa ufasaha alikimudu kwa umahiri kipindi cha “Mbiu ya Mnyonge”, kipindi ambacho huwapa sauti wasio na sauti na kuujulisha ulimwengu masaibu yanayowafika.


Aliponambia Dahman alikuwa na “sauti ya dhahabu” nilimuuuliza kwa masikhara “kama yako?” Mohammed Abdulrahman alinijibu: “Hapana ya Dahman ilikuwa ya kipekee”. Papo hapo akanitajia watangazaji wenzake wengine wawili wa zamani waliokuwa pia wakimkosha walipokuwa pamoja kwenye matangazo: Abdulrahman Hassan Sheikh (maarufu Wajihi Sheikh) na Denis Moyo.

Wajihi tuliyefahamiana sana, pia alitokea Zanzibar, alianza kusikika hewani alipokuwa Urusi akifanya kazi katika Idhaa ya Kiswahili ya Redio Moscow miaka ya 1960 na alijiunga na Sauti ya Ujerumani 1970.

Ali Attas, mwandishi maarufu wa vitabu vya kusomeshea Kiswahili na mtangazaji wa muda mrefu kutoka Kenya anayeishi Japani, amenambia kwamba anaikumbuka vyema siku aliyokutana na Dahman kwa mara ya mwanzo. Ilikuwa Julai 4, 1994 na ilikuwa Dahman aliyempokea kwenye idhaa ya Redio Japani.

“Mkuu wa idhaa, Bwana Ohgami alinichukua kutoka hoteli iliyokiwa masafa machache kutoka jengo la NHK. Kufika idhaani, Mohamed Dahman alikuwa wa kwanza kunikaribisha na kunivutia kiti. Sura yake ilikunjuka kwa furaha kubwa adhimu akiniamkia kwa bashasha na ucheshi mkuu kana kwamba tulijuana kwa miaka.”

“Mwezi mmoja baadaye Mohamed Dahman nami tulishiriki katika kipindi kimoja kirefu. Kipindi hicho kilikuwa kumbukumbu za vita vikuu vya pili vya dunia wakati mji wa Hiroshima ulipodondoshewa bomu la Atomiki Agosti 6 mwaka 1945.

Kipindi kilihitaji sauti zetu zibebe uzito wa vilio vya walioathiriwa na bomu hilo. Sauti ya Mohamed Dahman iliyabeba mazito hayo kwa ustadi na umahiri wa ajabu. Sauti yake ilinigusa na kunisisimua nikijiuliza baadaye, ‘Hivi binadamu anaweza kujaaliwa sauti tunu kama hii?’ Bila shaka sauti yake iliwanasa wasikilizaji wa Redio Japani kama simaku.

“Kifo chake kilinipiga kama dharuba ya radi iliyonipasukia moyoni. Moyo ulijikunja kwa majonzi makuu nikimkumbuka alivyokuwa mwema, muadilifu na mkarimu. Alikuwa na ucheshi wa upeo wa juu akinisimulia masaibu ya ujana wake kisiwani Unguja.

Ilikuwa bahati kuwasili nchi yenye ugeni wa mengi kwangu kumpata Mswahili aliyenifunulia hulka za Wajapani kazini na maishani.”

Attas, kama Mohamed Abdul Rahman na wengi wengine, naye pia ameielezea sauti ya Dahman kuwa ya “dhahabu”. Amenambia kwamba ingawa Dahman ametuaga “lakini sauti yake ya dhahabu bado haijaniaga. Kila uchao naisikia kwa mbali.”

Dahman, kama alivyousia mwenyewe, alizikwa kwenye udongo wa kwao Unguja.

Udongo huo ndio pia uliomwita Dk. Sharifa Mohamed Zawawi, aliyekuwa profesa wa mwanzo wa kike wa Kizanzibari nchini Marekani ambako akifundisha Kiswahili, Kiarabu pamoja na tamaduni za Mashariki ya Kati kwenye Chuo Kikuu cha New York.

Bi Sharifa, aliyewahi kutunga vitabu kadhaa vya kufundishia Kiswahili na Kiarabu, alikuwa likizoni Unguja kutoka Marekani alipokutwa na mauti. Ingawa alikuwa amenunua sehemu ya kiunga cha kuzikiwa watu ili azikiwe huko Marekani majaaliwa yake yalikuwa azikwe katika nchi aliyoipenda.

Bi Sharifa ni mtu niliyemfahamu toka niko mdogo ingawa udogoni mwangu nikimuona kwa mbali na nikimuhusudu na kigari chake kidogo alichokuwa akikiendesha. Nilianza kumjua badaye katika miaka ya 1970 alipokuwa tayari amekwishajipatia jina katika taaluma ya Kiswahili.

Kifo chake kilitugusa wengi tuliouona uungwana wake na kuuonja ukarimu wake. Daima nitaikumbuka karamu aliyoniandalia nyumbani kwake, siku hizo akiishi katika nyumba ya Chuo Kikuu cha Columbia, huko Harlem, New York.

Kwa hakika Idi hii Kuu iliyopita iliwatumbukia nyongo Waswahili wa New York kwa sababu hakuwepo Bi Sharifa aliyekuwa na mazoea ya kuwakusanya pamoja kwa karamu ya Sikukuu nyumbani kwake Bronx, New York.

Sharifa Zawawi alikuwa mpole na mfupi. Lakini maumbile yake yalificha ukakamavu wake na nguvu alizokuwa nazo wakati wa kusomesha. Alikuwa ni mtu wa aina yake. Dunia ya siku hizi haina wengi wenye tabia zenye kufanana na zake.

Sijapatapo kumsikia mtu akimsema kwa vibaya na wala sijawahi kumsikia yeye akimsengenya mtu. Na mtu akisemwa mbele yake humkatisha msemaji huku akikumbusha kwamba hakuna binadamu aliyekamilika.

Baadhi yetu tukimwita “Da Sharifa” licha ya kwamba hajatuhusu kwa damu hata chembe lakini heshima zake zilitufanya tumuone kuwa ni dada wa kutegemewa.

Profesa Zawawi alizaliwa Omani katika ukoo wa Zawawi. Ukoo huo wa Mazawawi ni maarufu sana nchini Omani kwa kuwa moja ya koo kuu za nchi hiyo. Mmoja wa wana maarufu wa ukoo huo alikuwa Qais al Zawawi, aliyekuwa waziri wa mambo ya nje na kaimu waziri mkuu wa Oman kwa muda wa miaka mingi mpaka alipokutwa na ajali ya gari na kufariki huko Salala, Oman, mwaka 1995.

Bwana huyo alikuwa jamaa wa karibu sana na Profesa Sharifa Zawawi. Niliwahi kumdhukuru Qais al Zawawi kwenye sahafu hii nilipokuwa nikizungumzia mkutano wangu na Dk Hassan al Turabi aliyekuwa gwiji wa siasa za Sudan.

Asili ya Mazawawi, ambao ni watu wa biashara, ni Saudi Arabia na ndio maana wakawa wanafuata madhehebu ya Sunni huko Oman, nchi yenye wafuasi wengi wa madhehebu ya Ibadhi. Kutoka Saudi Arabia Mazawawi hawakwenda Omani tu bali pia wametapakaa katika sehemu za Afrika ya Kaskazini na hata Malaysia.

Alipotimu umri wa miaka miwili Bi Sharifa Zawawi alipelekwa Unguja ambako alikulia mtaa wa Kokoni kwenye nyumba ya Seyyid Hamoud bin Faisal al Said. Baadaye alihamia Kikwajuni na Mkunazini, ambako ndiko nilikoanza kumuona.

Alisoma skuli ya msingi pamoja na masomo ya sekondari huko Unguja na baada ya kusomesha kwa muda, akiwa na umri mdogo, alipelekwa Uingereza kwa masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Bristol ambako alipata shahaha ya mwanzo ya B.A. Aliporudi Unguja alikuwa akisomesha chuo cha kuwafunza waalimu wa kike na pia wanafunzi wa kike katika skuli ya sekondari ya Seyyida Maatuka ambayo sasa inaitwa skuli ya Ben Bella.

Mwaka 1962 alielekea Marekani kwenye Chuo Kikuu cha Columbia, moja ya vyuo vikuu vya hadhi ya juu nchini humo. Huko alisomea fani ya isimu au sayansi ya lugha na akajipatia shahada za juu za M.A. na PhD. Mmoja wa waalimu wake alikuwa Profesa Noam Chomsky mwenye umaarufu duniani sio tu kwa kuwa bingwa wa isimu na falsafa ya lugha lakini pia kwa uanaharakati wake wa kutetea haki kote duniani. Inasemekana kwamba Bi Sharifa alimfundisha Chomsky Kiswahili kidogo.

Uanaharakati ni sifa ambayo Profesa Zawawi pia alikuwa nayo ingawa uanaharakati wake ulikuwa wa chini kwa chini, wa kimya kimya. Daima alikuwa upande wa watetezi wa haki.

Akiwasiliana na vijana wengi Wamarekani weusi waliofungwa jela. Mara zote akiwahimiza wajiendeleze kwa masomo. Wako baadhi yao waliofunguliwa wakaendelea na masomo na kufanikiwa kimaisha.

Miaka ya mwisho ya uhai wake Bi Sharifa akifanya utafiti mwingi kuhusu lugha za Kiswahili na Kiarabu na akitunga mitihani ya lugha hizo mbili.

Huo mchango wake ni moja ya sadaka zake kubwa. Pia alikuwa na mkono mwepesi uliokuwa ukitoa kwa siri michango kusaidia jumuiya kadhaa za kuwasaidia masikini na akitoa michango mingi kuisaidia Bustani ya Mimea ya New York.

Ingawa alikuwa mtu wa dini Profesa Zawawi hakuwa mtu wa kujiinamia. Alikuwa mtamaduni wa kilimwengu aliyekuwa shabiki wa kuhudhuria michezo ya opera, tamthilia na ule uitwao muziki dhati (classical music).


Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter:mad:ahmedrajab
 
Back
Top Bottom