Bunge na CC ya CCM nani zaidi?

Raia Fulani

JF-Expert Member
Mar 12, 2009
10,877
2,758

Josephat Isango​
amka2.gif
SIAMINI, tena sitaki kusikia eti Rais Jakaya Kikwete amesikiliza kilio cha wabunge, vyama vya siasa, wananchi wa kawaida na wanaharakati kutaka mawaziri waliohusishwa na kashfa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wajiuzulu baada ya kukubali kulisuka upya baraza lake.
Huu ni uamuzi wake au uamuzi wa CCM? Rais ambaye anaongozwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano, aliyoapa kuilinda kweli anaweza kufikia uamuzi huo baada ya kushauriwa na viongozi wa CCM? Nani zaidi sasa, CCM au Katiba ya Jamhuri ya Muungano?
Taarifa ya Rais Kikwete kutaka kubadili upya Baraza la Mawaziri inatangazwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye. Huyu ni nani katika serikali yetu? Katibu Mkuu Kiongozi hayupo au amekwenda likizo?
Kazi za Katibu Mkuu Kiongozi ni zipi? Waziri Mkuu kazi yake ni nini? Taarifa za mambo ya serikalini siku hizi zinatolewa na Nape? Tunaelekea wapi? Taaarifa ya kubadili Baraza la Mawaziri inatolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM.
Bado najiuliza Rais Kikwete alifikiri nini mpaka akaamua kupeleka suala la mabadiliko ya baraza la mawaziri kwenye kikao cha Kamati Kuu ya CCM? Hili naona halihitaji mwekezaji kuelewa kuwa mambo yametendwa ndivyo sivyo.
“Hivyo CC tumaridhia na kutaka uamuzi huo uchukuliwe mara moja, tuna imani kuwa rais atafanya mabadiliko haraka iwezekanavyo maana alikuwa amebanwa na majukumu kidogo ya safari nje ya nchi, mazishi ya Rais Bingu wa Mutharika na sherehe za Muungano. Ila sasa wakati wowote atafanya,” hii ni nukuu ya Nape.
Ndugu zangu tangu lini Nape amekuwa msemaji wa Ikulu? Tangu lini Nape amekuwa msemaji wa safari za rais na ratiba zake za utendaji wa kila siku? Salva Rweyemamu analipwa kwa ajili ya kazi ipi? Au hawajui mipaka ya kazi zao?
Hii kauli ilipaswa kusemwa sirini na watu wenye akili, si kuita mkutano wa waandishi wa habari kwenda kuzungumzia kitu ambacho kwanza si wajibu wake, na wasemaji wa mambo hayo wapo? Kikwete aliruhusu vipi shughuli za Ikulu kuzungumziwa na Nape wakati Salva Rweyemamu na Balozi Sifuni Sefue wapo?
Kwa mantiki hii, Kamati Kuu ya CCM ina nguvu ya kimaamuzi ya nchi kuliko Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bunge linapoamua mambo fulani hayatekelezwi isipokuwa mpaka yapitie kwanza kwa viongozi wa CC ndipo yafanyiwe utekelezaji katika nchi. Aibu gani hii?
Tunaipeleka wapi nchi yetu? Tunahangaika sasa kwa kesi za uchaguzi kuwasumbua Watanzania na majaji kulipwa kwa pesa kubwa huu ulikuwa ni uamuzi wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusufu Makamba, kuwashauri wagombea wote wa chama hicho walioshindwa wakate rufaa na CCM ingelipia gharama za kuendesha kesi.
Tunahangaika kila kukicha kwa sababu ya maamuzi mabaya ya CCM, bado na Kikwete tuliyempa madaraka, anasumbuliwa kutokuwa thabiti kwa masuala muhimu yanayogusa masilahi ya taifa.
Kiongozi wetu wa nchi anahitaji kwenda katika CC ya CCM ili kuomba ushauri wa kubadili baraza la mawaziri au la? Hii pengine inatokana na kuwaogopa mawaziri wachafu, ama kwa uswahiba, au kwa matakwa mengine ambayo anashindwa kubeba lawama, badala yake anatafuta sehemu ya kujiegemeza ili lawama zisimkute yeye.
Nakumbuka Rais Kikwete alishawahi kusema kuwa urais wake hauna ubia, lakini kwa hali ya mambo inavyokwenda jambo hilo linaonekana kuwa tofauti, je, amesahau kauli hii?
Mawaziri waliobainika kuwa ni wabadhirifu wa mali za umma wametajwa na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Akataja bila woga kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja; Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu; Waziri wa Fedha; Mustafa Mkulo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi, George Mkuchika.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda na Waziri wa Viwanda na Biashara; Dk Cyril Chami. Je, orodha ya wazi namna hii ilihitaji kweli kuitisha Kamati Kuu ya CCM kuomba ushauri kufikia maamuzi?
Kwanza Waziri Mkuu angekuwa makini kwa hili, angekuwa haogopi uswahiba wa mawaziri hawa na Kikwete, angetoa tamko akiwa anaahirisha Bunge mjini Dodoma, Nape anatamba bila aibu kuwa Kamati Kuu iliyokutana juzi ilipokea taarifa mbili ikiwemo uamuzi huo wa rais kulisuka upya baraza la mawaziri kutokana na ripoti ya CAG.
“Kamati Kuu imepokea taarifa kubwa mbili, taarifa ya Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa CCM na Kamati ya Wabunge wa CCM kwa upande mmoja na taarifa ya Kamati ya Uongozi ya Wawakilishi wa CCM kwa Bara na Zanzibar,” alisema.
Haya ya kwenye kamati za CCM yameingiliaje maamuzi ya Katiba ya nchi na mamlaka ya Rais Kikatiba? Na Kikwete kwanini aliamua kuuchezea urais wake kwa kuwapa CCM waufanyie majaribio?
Najisikia aibu nchi yetu inavyoongozwa, lakini kwa kuwa tunaongozwa na familia ya kambale; baba ana ndevu, mama ana ndevu, bibi ana ndevu, vijana wake kwa waume wana ndevu, basi kila mmoja ni msemaji katika taifa letu kwa jambo lolote.
Aibu kubwa sana kwa uongozi wa nchi kuchukuliwa kiurahisi kiasi hicho. Bunge letu na Ikulu yetu vimedhalilishwa sana kwa misingi ya U-CCM. Siijui hatima ya nchi yetu. Nawaachia changamoto.


Kamati Kuu imeamua yafuatayo;

1. Kamati Kuu inatambua na kuheshimu haki na wajibu wa wabunge kujadili utendaji wa serikali yao.Inapongeza juhudi za serikali kuhakikisha kuwa ripoti ya mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali inajadiliwa kwa uwazi na hivyo kuibua mapungufu yaliyojadiliwa.
2. Kamati Kuu imeridhika na imebariki uamuzi wa Rais KULISUKA UPYA BARAZA LA MAWAZIRIna taasisi zingine zilizoanishwa katika ripoti hizo. Imesisitiza utekelezaji wa uamuzi huo ufanywe mapema iwezekanavyo.
Aidha kamati Kuu imeipongeza Kamati Teule ya baraza la wawakilishi Zanzibar iliyoundwa kuchunguza utendaji katika sekta mbalimbali kwenye serikali ya mapinduzi Zanzibar kwa taarifa yao.
Kamati Kuu inawapongeza wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa jinsi walivyojadili taarifa hiyo na pia Kamati Kuu inaipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuipokea taarifa na kuanza kuifanyia kazi.
Nape Moses Nnauye
Chama Cha Mapinduzi
The Ideology and Publicity Secretary
Maoni yangu
Nami Nimelitazama hili suala vya kutosha. Najiuliza, nape ni nani katika serikali yetu? Haya maamuzi yaliyokasimiwa kwa kamati kuu ya ccm yalipaswa kufanywa na Rais mwenyewe. Hii inatupa picha kuwa urais wa JK upo mikononi mwa CC na si waajiri wake ambao ni watanzania


 
Back
Top Bottom