Bunge limesababisha haya | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Bunge limesababisha haya

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by kibakwe, Apr 25, 2012.

 1. kibakwe

  kibakwe Senior Member

  #1
  Apr 25, 2012
  Joined: May 10, 2011
  Messages: 171
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  KWAMBA ufisadi wa mabilioni ya fedha za walipa kodi nchini umesambaa kila sehemu katika Serikali, idara zake na mashirika ya umma sasa ni siri iliyo wazi. Baada ya miongo mingi ya viongozi wa Serikali kumwaga machozi ya tembo na kuwaghilibu wananchi kwamba umaskini wao siyo tu unatokana na ubeberu, bali pia na ubeberu mamboleo, sasa siri imefichuka kwamba kikwazo kikubwa na adui wa kwanza wa maendeleo ya nchi yetu na watu wake siyo ubeberu wala ubeberu mamboleo, bali Watanzania wenzetu waliopewa dhima ya kuongoza Serikali na mashirika yake.

  Katika nyakati tofauti viongozi wetu wakuu serikalini waliwahi kukaririwa na vyombo vya habari mbalimbali vya nje wakisema hawajui kwa nini Watanzania ni maskini wa kutupwa licha ya Tanzania kuwa na rasilimali nyingi. Pengine ndiyo maana zimekuwapo juhudi za makusudi kuelezea uduni wa uchumi wetu na umaskini wa wananchi kwamba unatokana na ukame, kuvurugika kwa uchumi wa dunia, kupanda kwa bei ya mafuta na bei ndogo za mazao yetu katika soko la dunia na mbinu za mabeberu kutudhoofisha kupitia sera za Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF).

  Lakini matukio mbalimbali katika siku za karibuni hapa nchini yamedhihirisha pasipo shaka na kuthibitisha usemi kwamba kikulacho kiko nguoni mwako. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) imeonyesha kuendelea kuwapo kwa ufisadi wa kutisha serikalini, huku deni la taifa likiongezeka kutoka Sh10.5 trilioni mwaka juzi hadi Sh14.4 trilioni mwaka jana. Ripoti hiyo imedhihirisha kwamba Serikali imetumia Sh544 bilioni bila idhini ya Bunge kama ilivyo kwa balozi za Tanzania nje ya nchi zilizotumia Sh3 bilioni, huku Sh1 bilioni zikilipwa kwa watumishi hewa.

  Sasa ni bayana kwa nini wananchi wanaendelea kudidimia katika lindi la umaskini wa kutisha. Kumbe Serikali imeendelea kutoa misaada ya kodi na ripoti hiyo ya CAG inasema Sh 1.02 trilioni zimetolewa, ikiwa ni asilimia 18 ya makusanyo yote ya Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa kipindi hicho. Nchi yetu sasa iko njia panda na pengine Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge wa Hesabu za Serikali za Mitaa, Augustine Mrema alikuwa sahihi aliposema wiki iliyopita kwamba lazima kiundwe kikosi cha kupambana na mtandao wa wizi katika Serikali na halmashauri.

  Ndiyo maana vilio dhidi ya ufisadi serikalini sasa vinasikika nchi nzima. Katika kuonyesha kwamba suala la uchumi wa nchi halipaswi kupewa sura ya kiitikadi, wabunge wengi bila kujali vyama wanavyotoka juzi waliilaumu Serikali kwa matumizi mabaya ya fedha za umma na ufisadi uliojitokeza katika taasisi zake mwaka wa fedha uliopita. Hasira za wabunge zilitokana na ripoti tatu za Kamati za Bunge za Mashirika ya Umma, Serikali za Mitaa na Hesabu za Serikali Kuu kuonyesha upotevu wa mabilioni ya shilingi katika nyanja mbalimbali.

  Kwa mfano, Sh8 bilioni hazikufika katika halmashauri husika na Wizara ya Afya na Usatwi wa Jamii ilitumia Sh1.10 bilioni kwa maonyesho ya Nanenane ambazo hazikuwa katika bajeti iliyopitishwa na Bunge. Lakini pia jambo la kushangaza ni kwamba, hata Sh21.63 bilioni zilizojulikana kama ‘Mabilioni ya JK’ hazikuwamo katika bajeti iliyopitishwa na Bunge, huku Wizara ya Maliasili na Utalii ikiripotiwa kupoteza Sh875 milioni kwa kufanya uamuzi wa upendeleo wa kutoa mrabaha kwa mazao ya misitu.

  Sisi tunadhani sehemu ya lawama lazima zielekezwe kwa Bunge ambalo kikatiba ndilo linaloisimamia Serikali na linao uwezo hata wa kupiga kura ya kutokuwa na imani na Rais au Waziri Mkuu. Kwa maana hiyo, kelele zinazosikika bungeni za kukemea ufisadi serikalini ni usanii tu kama haziambatani na hatua za kuiwajibisha Serikali. Kwa maoni yetu, Bunge ndilo linalofuga ufisadi huu na itakuwa sahihi kwa wananchi pia kuwawajibisha wabunge husika kwa udhaifu huo
   
 2. m

  mvunjamiwa JF-Expert Member

  #2
  Apr 25, 2012
  Joined: Apr 1, 2012
  Messages: 455
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 35
  Nimependa analysis yako. Exellent. Natazama kama mchakato wa katiba ukienda fair, tunaweza kupata nafasi ya kufanya mabadiliko makubwa ya kuokoa nchi yetu. Kwa sasa madaraka aliyo nayo Rais kwa mujibu wa katiba ni makubwa sana kiasi kwamba ameelemewa mno, hajiwezi hata kama anataka, kila jambo ni lazima ashiriki au aamue!!
   
Loading...