Bunge lilivyopoteza muda kujadili 'hewa'

Ufipa-Kinondoni

JF-Expert Member
Jan 3, 2012
4,582
2,783
Sisi tumebaki kulalamika tu, ila hatujui kutatua.

Angalia hii taarifa:

Katika bajeti hiyo ambayo imebakiza siku 44 ifike ukingoni na utekelezaji wa ile ya 2016/17 uanze, karibu wizara zote mpaka sasa zimepata chini ya asilimia 40 ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge mwaka jana kwa ajili ya maendeleo, huku zingine zikiwa hazijaambulia hata senti moja.

Bajeti hiyo kwa miezi minne (Julai Mosi hadi Novemba 4, mwaka jana), ilitekelezwa chini ya uongozi wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, kabla ya John Magufuli kukabidhiwa nchi Novemba 5, mwaka jana, na kuendelea nayo hadi itakapofika kikomo Juni 30.

Katika bajeti hiyo, Bunge liliidhinisha Sh. trilioni 22.45. Kati yake, Sh. trilioni 16.7 zikiwa za matumizi ya kawaida ambayo ni sawa na asilimia 74.3 huku Sh. trilioni 5.76 (asilimia 25.7) zikiwa kwa ajili ya maendeleo.

Kufika kikomo kwa bajeti hiyo ambayo utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua, ni mwanzo wa utekelezaji wa bajeti ya kwanza inayopitishwa na Bunge chini ya uongozi wa Rais Magufuli.

Mwelekeo wa bajeti ya kwanza ya Rais Magufuli, uliowasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, unaonyesha serikali imepanga kutumia Sh. trilioni 29.53 katika mwaka wa fedha 2016/17.

Kati ya fedha hizo, Sh. trilioni 17.72 zitakuwa za matumizi ya kawaida wakati Sh. trilioni 11.82 (asilimia 40) zitatumika kwa shughuli za maendeleo.

Lakini bado swali linabaki, je, utekelezaji wa bajeti hiyo utakuwa tofauti na zilizotangulia ambazo karibu zote zimekuwa za kusuasua?

KAULI YA SERIKALI

Akizungumza na Nipashe mjini hapa mwishoni mwa wiki iliyopita, Naibu Kamishna wa Bajeti - Mikoa na Halmashauri, Dk. Charles Mwamwaja, pamoja na mambo mengine, alisema utekelezaji wa bajeti inayofikia kikomo ulisuasua kutokana na ukwepaji kodi.

"Watu hawalipi kodi, wanakwepa, wanaingiza makontena nchini bila kuyalipia kodi, maana yake sisi (Wizara ya Fedha na Mipango) hatupati mapato. Na sisi hatuwezi kutoa fedha kwa asilimia 100," Dk. Mwamwaja alisema.

Naibu Kamishna huyo alisema kuna nchi ambazo zina urahisi wa kutekeleza mipango yake ya bajeti kwa sababu zinakuwa na akiba ya fedha tayari.

"Wanapopitisha bajeti, tayari hela wanazo. Kinachokuwapo ni kuchukua fedha na kwenda kutekeleza," alisema Dk. Mwamaja.

"(Lakini) hapa kwetu Waziri wa Fedha anaomba kwanza idhini ya kukusanya fedha. Yaani anakusanya kwanza halafu ndiyo anakwenda kutumia.

"Waziri anapewa idhini na Bunge akatafute, si kwamba fedha ziko Benki Kuu (BoT). Pale Hazina hatuna 'reserve' (akiba) kama mataifa makubwa kama Norway ambao wana 'reserve' ya miaka mitano ijayo."

Hata hivyo, Dk. Mwamwaja alisema anaamini bajeti ya mwaka ujao itatekelezwa kwa kiwango kikubwa kutokana na jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kuongeza mapato ya nchi.

"Mwelekeo sasa ni mzuri maana Rais Magufuli amepandisha mapato kwa kiasi kikubwa. Sasa tunaingiza zaidi ya Sh. trilioni moja kwa mwezi, wakati tulikuwa tunaishia kwenye bilioni tu. Ni lazima tuzifanyie kazi changamoto zilizopo ili watu walipe kodi," alisema.

HALI ILIVYO KWENYE WIZARA

Kambi Rasmi ya Upinzani ililieleza Bunge kuwa katika mwaka wa fedha unaoisha, Sh. bilioni 19.4 zilitengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwenye Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, lakini hakuna hata shilingi moja iliyotolewa hadi Machi 31, mwaka huu.

Kwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, kati ya Sh. bilioni 32 zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo ni Sh. bilioni 5.1 pekee ndizo zilizotolewa.

Katika Serikali ya Awamu ya Nne, wizara hizo zinazogusa zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania, zilikuwa zimetenganishwa, kabla ya Rais Magufuli kuziunganisha alipotangaza baraza lake la mawaziri Desemba mwaka jana.

Kutokana na hali hiyo, Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, imelishauri Bunge kuitaka serikali kukamilisha kwanza miradi iliyopita kabla ya kuanza mipya.

WIZARA YA MAMBO YA NDANI

Katika mwaka wa fedha 2015/16, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iliidhinishiwa Sh. bilioni 79.689 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Adadi Rajabu, akizungumzia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/17, aliliambia Bunge kuwa hadi Machi 31, 2016, wizara hiyo ilikuwa imepokea Sh. bilioni 5.984 tu kutoka Hazina, sawa na asilimia 7.5 ya fungu lote la maendeleo ililotengewa.

Wakati bajeti ya mwaka huu haijatekelezwa, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, aliliomba Bunge jana kuidhinisha Sh. bilioni 47.923 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wizara kwa mwaka wa fedha 2016/16.

WIZARA YA ULINZI

Mwaka huu, serikali imeweka rekodi mbaya ya kutoa fedha chini ya kiwango kilichoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, na baadhi ya mafungu ya fedha hayakutolewa kabisa.

Kwa mujibu wa Balozi Adadi, Ulinzi iliidhinishiwa Sh. bilioni 232.137 kwa ajili ya maendeleo mwaka huu, lakini hadi Februari, ilipokea Sh. bilioni 40 tu, sawa na asilimia 17.2 ya fedha za maendeleo.

WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA

Bunge liliidhinisha Sh. bilioni 35.387 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji mwaka 2015/16. Kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 26.588 ni fedha za ndani, wakati Sh. bilioni 8.799 ni fedha za nje.

Kwa mujibu wa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, hadi Machi 31, mwaka huu, wizara ilikuwa imepokea Sh. bilioni 1.602, sawa na asilimia 4.5 ya fungu la maendeleo lililoidhinishwa.

Wizara hiyo, katika mwaka ujao wa fedha, imeidhinishiwa Sh. bilioni 248, ikiwa ni ongezeko la Sh. bilioni 15.852 (asilimia 6.8) ya fedha za mwaka 2015/16).

OFISI YA WAZIRI MKUU

Kwa mujibu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Waziri Mkuu katika Fungu 37 (Tume ya Taifa ya Uchaguzi), Fungu 61 na Fungu 65 linalohusika na kazi, vijana, ajira na wenye ulemavu, kwa pamoja yalitengewa Sh. bilioni 63.87 kwa ajili ya miradi ya maendeleo mwaka huu wa fedha.
Hadi kufikia Machi 2016, Sh. bilioni 54.911, sawa na asilimia 86 ya fedha iliyoidhinishwa na Bunge, zilikuwa zimetolewa na serikali.

Sehemu kubwa ya fedha hiyo, kwa mujibu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, ilitokana na fedha za nje ambazo ni mikopo mbalimbali, hasa fedha za mradi wa uendelezaji wa miundombinu ya masoko, uongezaji thamani ya mazao na huduma vijijini.

"Katika kiasi cha fedha ambacho hakikupokewa kutoka Hazina, zipo Sh. bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya Waziri Mkuu, unaoendelea eneo la Mlimwa, Dodoma," inasomeka sehemu ya taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, iliyowasilishwa bungeni mjini hapa wiki tatu zilizopita.

Katika mwaka ujao wa fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake, imeidhinishiwa Sh. bilioni 165.196 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ikiwa ongezeko la Sh. bilioni 101.32 kulinganisha na mwaka huu.

OFISI YA RAIS UTUMISHI

Mwaka 2015/16 Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora ilitengewa Sh. bilioni 6.259 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lakini mwaka huu imeidhinishiwa na Sh. bilioni 7.5, ikiwa ni ongezeko la Sh. bilioni 1.24.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Jasson Rweikiza, aliliambia Bunge mapema mwezi huu kuwa hadi Machi, mwaka huu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora ilikuwa imepewa asilimia 74.21 ya fedha za mafungu yake yote, yaliyoidhinishwa kwa ajili ya maendeleo mwaka 2015/16.

WIZARA YA HABARI

Bunge limeidhinisha Sh. bilioni tatu kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo katika mwaka ujao wa fedha, ikiwa ni sawa na fungu ililolipitisha kwa ajili ya miradi hiyo mwaka huu.

Hata hivyo, hadi mwezi uliopita, serikali ilikuwa imetoa Sh. bilioni moja tu kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya wizara hiyo (asilimia 33.3), kwa mujibu wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.

WIZARA YA AFYA


Alhamisi ya wiki iliyopita, Bunge liliidhinisha Sh. bilioni 518.512 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka wa fedha 2016/17.

Kiasi hicho cha fedha ni sawa na ongezeko la Sh. bilioni 77.87 ikilinganishwa na bajeti ya maendeleo ya wizara hiyo mwaka huu ambayo ni Sh. bilioni 440.642.

Hata hivyo, hadi Machi 31, ikiwa ni robo tatu ya mwaka wa fedha 2015/16, hakuna fungu hata moja ambalo wizara hiyo ilikuwa imepewa fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa angalau asilimia 50 kutoka Hazina, kwa mujibu wa Peter Serukamba, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Wakati serikali ikishindwa kutoa fedha zote zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya maendeleo ya wizara hiyo, takwimu za Benki ya Dunia 2016 zinaonyesha kila siku wanawake 42 nchini hufariki dunia wakati wakijifungua, sawa na wanawake wawili kwa saa.

Aidha, kwa mujibu wa utafiti wa Taasisi ya Afya Ifakara, watoto zaidi ya milioni 2.5 wamedumaa nchini na vifo vitonavyo na utapiamlo nchini ni 430,000 kwa mwaka, sawa na kifo cha mtoto mmoja kila baada ya dakika 12.

OFISI YA MAKAMU WA RAIS - MUUNGANO

Katika mwaka wa fedha 2015/16, Ofisi ya Makamu wa Rais - Muungano ilitengewa Sh. bilioni 3.869 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 2.85 zilikuwa za ndani na Sh. 1.019 ni fedha za nje.

Kwa mujibu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, miradi ya maendeleo ambayo ilipangwa kutekelezwa na ofisi hiyo mwaka huu katika Fungu 26 na 31 ni ujenzi na ukarabati wa Ofisi ya Makamu wa Rais na ujenzi wa makazi binafsi ya Makamu wa Rais.

Mohamed Mchengerwa, mwenyekiti wa kamati hiyo, aliliambia Bunge kuwa hadi Machi 31, Sh. milioni 338.079 zilikuwa zimetolewa, sawa na asilimia 8.7 ya bajeti ya maendeleo.

Fedha ambazo hazikutolewa ni pamoja na Sh. milioni 300 zilizotengwa kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa makazi ya Makamu wa Rais, eneo la Tunguu, Zanzibar.

WIZARA YA KATIBA NA SHERIA


Wizara hii miongoni mwa wizara chache zilizopokea kiasi kikubwa cha fedha za maendeleo zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya bajeti ya mwaka huu.

Katika mwaka wa fedha 2015/16, Sh. bilioni 15.381. ziliidhinishwa na Bunge kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya Wizara ya Katiba na Sheria. Kati ya fedha hizo Sh. bilioni 13.319 ni fedha za ndani, wakati za nje ni Sh. bilioni 2.062.

Hadi kufikia Aprili 30, wizara ilipokea Sh. bilioni 13.209, sawa na asilimia 85.9 ya fedha zote za bajeti ya maendeleo, kwa mujibu wa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe.

Dk. Mwakyembe aliliambia Bunge kuwa kati ya fedha zilizotolewa, Sh.12.645 ni za ndani, wakati za nje ni Sh. milioni 564.727.
0000

WIZARA YA UJENZI

Wakati wizara zingine zikikosa fedha za maendeleo, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ilipewa fedha nyingi kuliko zile zilizoidhinishwa na bunge 2015/16.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alisema Sh. bilioni 883.832 ziliidhinishwa na Bunge kutekeleza miradi ya maendeleo kwa mwaka 2015/16.

Kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 191.619 ni fedha za ndani kutoka Mfuko Mkuu wa serikali, fedha za nje zilikuwa Sh. bilioni 85.753, wakati Mfuko wa Barabara zilitengwa Sh. bilioni 606.64.

Alisema hadi Aprili 30, wizara hiyo ilikuwa imepewa Sh. trilioni 1.08, kati yake, Sh. bilioni 607.35 ni fedha za ndani kutoka Mfuko Mkuu wa serikali, Sh. bilioni 149.503 ni fedha za nje na Sh. bilioni 323.952 ni za Mfuko wa Barabara.

"Sehemu kubwa ya fedha zilizotolewa, imetumika kulipa madeni ya makandarasi na wahandisi washauri wa miradi ya barabara," Prof. Mbarawa aliliambia Bunge.

Katika mwaka ujao wa fedha, Wizara hiyo ambayo sasa imeunganishwa na kuwa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, imeidhinishiwa Sh. trilioni 4.895 ili kutekeleza majukumu yake.

Kiasi hicho cha fedha ni sawa na asilimia 41.4 ya bajeti yote ya serikali maendeleo mwaka 2016/17 ambayo ni Sh. trilioni 11.82.

Kati ya Sh. trilioni 4.895 zilizoidhinishwa, Prof. Mbarawa, alisema Sh. trilioni 2.212 ni kwa ajili ya sekta ya ujenzi, wakati Sh. trilioni 2.587 zitakuwa za sekta ya uchukuzi na Sh. bilioni 95.804 zitaelekezwa kwenye sekta ya mawasiliano.
 
Back
Top Bottom