Bilionea Asigwa
JF-Expert Member
- Sep 21, 2011
- 16,515
- 28,487
Polisi mkoani Arusha, wanazishikilia bunduki 103 zikiwamo za kijeshi wilayani Ngorongoro sambamba na magunia 270 ya bangi wilayani Arumeru.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda alitoa taarifa hiyo juzi katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na kusema; “Arusha sasa ni shwari.”
Alisema ndani ya wiki mbili tu, silaha hizo 103 zimesalimishwa wilayani Ngorongoro na zipo mikononi mwa polisi kutokana na agizo la Serikali kuwataka wananchi wazisalimishe.
Alisema katika kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka jana, jumla ya magunia 270 ya bangi yalikamatwa wilayani Arumeru na ekari 25 za mashamba yake ziliteketezwa.
Ntibenda alisema magunia hayo ya bangi na mashamba yake yamebainika katika operesheni dhidi ya kilimo cha bangi iliyofanyika katika vijiji vya Kisimiri Juu, Ibimbwa, Ngarenanyuki na Oldonyosambu.
“Katika kipindi hicho pia, katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Arusha, jumla ya kilo tatu za dawa za kulevya; cocaine na heroini na kilo 1,800 za mirungi zimekamatwa,” alisema.
Ntibenda alisema watu 180 walikamatwa kwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na 160 kati yao wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma zao.
“Kwa ujumla mkoa wa Arusha sasa ni salama. Napenda kuvipongeza vyombo vya usalama kwa kazi nzuri wanayofanya,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema baadhi ya wananchi waliosalimisha silaha hizo walikutwa na bunduki za kivita aina ya K47 na SMG zisizoruhusiwa kumilikiwa na raia.
Alisema wapo baadhi ambao silaha zao zilikuwa zikimilikiwa kihalali lakini walishindwa kutoa maelezo yanayoridhisha ya mahali walikopata risasi za ziada baada ya 30 za awali kwisha ambazo hutolewa kisheria.
Alisema wanaendelea kuzishikilia silaha hizo na baada ya uchunguzi wanaweza kuwarudishia wanaozimiliki kihalali.
Source: Mwananchi