Boniphace Jacob (Boni Yai)
ni mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kanda ya Pwani lakini pia amewahi kuwa Meya wa Kinondoni.
Aidha Chama cha demokrasia na maendeleo
CHADEMA kuelekea uchaguzi mkuu 2025 kimekuwa kikiendesha ajenda inayojulikana kama
'No reforms, No election' yenye lengo la kuhamasisha na kuchochea kufanyika kwa
mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi ili kuwezesha uchaguzi huru na wenye haki ili kuepusha malalamiko yaliyotokana na mapungufu yaliyojitokeza katika chaguzi zilizopita. Kupitia ajenda hiyo mara kwa mara, chama hicho kimekuwa kikisisitiza kuwa bila mabadiliko hakutakuwa na uchaguzi.
Kumekuwepo na
taarifa inayosambazwa mtandaoni ikitumia utambulisho wa grafiki za Millard Ayo na kunukuu Ujumbe unaodaiwa kuandikwa na Boniface Jacob kupitia ukurasa wake kwenye mtandao wa X akisema
'nimeandika barua kwa Katibu Mkuu wa chama chetu, kaka yangu @jjmnyika, nikishauri tuachane na mpango wa kampeni ya 29 No Election'
Je, ni upi uhalisia wa taarifa hiyo?
Ufuatiliaji wa kimtandao uliofanywa na JamiiCheck kwa kutumia utafutaji wa maneno muhimu (Key Word Search) umebaini kuwa taarifa hiyo si ya kweli kwani andiko hilo halijaandikwa na
Boniface Jacob, bali ni la kutengenezwa na wapotoshaji.
Aidha grafiki iliyotumika kusambaza taarifa hiyo ni ya kughushi kwani haijachapishwa na
Millard Ayo kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii.
Hata hivyo kupitia ukurasa wake kwenye mtando wa X
akijibu chapisho la Jambo TV, Boniface alisisitiza kuikanusha taarifa hiyo isiyo ya kweli na kusema
"Waambieni kauli ya kila Mwanachama wa CHADEMA ni moja tu NO REFORMS NO ELECTION."