beth
JF-Expert Member
- Aug 19, 2012
- 3,879
- 6,356
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akielezea uzoefu wa Tanzania kwenye ujenzi wa miradi ya mabomba ya gesi na mafuta katika mkutano huo. Kushoto ni Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini Nchini Uganda, Mhandisi Irene Muloni na kulia ni Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa.
Bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi katika bandari ya Tanga nchini Tanzania linatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka 2020.
Hayo yalielezwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufanyika kwa mkutano kati yake na Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini Nchini Uganda, Mhandisi Irene Muloni aliyeambatana na ujumbe wake katika mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam
Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kujadili mpango wa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi katika bandari ya Tanga nchini Tanzania ambapo ulikutanisha wataalam kutoka nchi zote mbili, ambao ni wa ardhi, miundombinu, maji, ujenzi, uchumi,, maji barabara pamoja na makampuni ya mafuta.
Profesa Muhongo alisema kuwa mara baada ya marais wa Tanzania na Uganda kukubaliana kuanza kwa ujenzi wa bomba la mafuta, kinachofuatia ni utekelezaji wa kasi ya ajabu ambapo tayari wameanza kukutana na kuunda kamati ndogo ndogo zitakazokuwa na wataalam mbalimbali kwa ajili ya kuanza mara moja kwa utekelezaji wa mradi huo.
Profesa Muhongo alisema kuwa serikali za nchi zote mbili zimejipanga katika kuhakikisha kuwa ujenzi huo unakwenda kwa kasi kubwa, ikiwezekana ujenzi ukamilike mwishoni mwa mwaka 2019.
Aliongeza kuwa serikali ya Uganda inatarajia kujenga kiwanda kwa ajili ya kusafisha mafuta ghafi Hoima ambapo wametoa hisa 40 zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 4.7 kwa nchi zilizomo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo kila nchi itaweza kununua asilimia nane ya hisa hizo na kusisitiza kuwa Tanzania ipo tayari kununua hisa nane kwa thamani ya Dola za Marekani milioni 150.4
Aliendelea kusema kuwa hisa zitanunuliwa na serikali pamoja na wawekezaji binafsi watakaoonesha nia ya kununua hisa ili waweze kunufaika na mradi huo.
Hata hivyo aliongeza kuwa nchi ya Uganda pamoja na nchi nyingine zilizomo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wameomba kununua gesi kutoka nchini Tanzania na kusema kuwa kwa kuanzia serikali inatarajia kujenga bomba la gesi hadi nchini Uganda ili waweze kunufaika na gesi hiyo.
Alisema kuwa bomba la gesi litasambazwa katika mikoa ya kaskazini na mingineyo ili uchumi wa nchi uweze kukua kwa kasi na Tanzania kuwa nchi yenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 kama Dira ya Maendeleo ya Taifa inavyofafanua.
“ Kila sehemu yenye gesi ya kutosha, lazima tuhakikishe tunaweka bomba la gesi ambalo ni mkombozi wa uchumi wa nchi,” alisisitiza Profesa Muhongo.
Wakati huo huo Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini Nchini Uganda, Mhandisi Irene Muloni, aliishukuru serikali ya Tanzania kwa kuwa tayari kushirikiana na Uganda kwa ajili ya mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la mafuta.
Alisema kupitia uzoefu wa Tanzania katika ujenzi wa mabomba ya gesi na mafuta pamoja na wataalam waliobobea anaamini kuwa mradi huu utakwenda kwa kasi kubwa na kukamilika kwa wakati.
Aliiomba nchi ya Tanzania pamoja na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na makampuni ya mafuta, jamii itakayopitiwa na miundombinu ya bomba la mafuta kutoa ushirikiano ili mradi uweze kukamilika kwa wakati kama ilivyopangwa.
Alisema kuwa mkutano wa pili unatarajiwa kufanyika Hoima nchini Uganda tarehe 27 Mei, mwaka huu na kuendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali yatakayopitiwa na bomba la mafuta.