Luigi Alfred
Member
- Mar 17, 2016
- 65
- 44
Wadau wa njia zote zipitazo maeneo yenye msongamano wa watu imekuwa kero isiyositahimilika hasa msimu huu wa sikukuu. Nasema ni kero kwa sababu vijijini hatuna traffiki wa kudhibiti mwenendo wa vyombo vya moto na madereva wake hasa hawa maarufu kama Bodaboda. Wanaendelesha pikipiki kwa mwendo mkubwa huku wakiwarushia vumbi watembea kwa miguu waliovalia kitanashati kwa ajili ya kusherekea sikukuu. Ajali za kugongana ni jambo la kawaida lakini watu wanaishia kunung'unika tu kwani huku ni kama kisiwa kisichokuwa na ustaarabu. Nadra Bodaboda kumugonga mtu na akaomba msamaha kwa aliyemjeruhi. Nadra kumkuta Bodaboda akiwa na leseni ya kuendesha chombo cha moto. Nadra kukutana na Bodaboda asiyefungia pikipiki yake na mfagio wa kupukutishia vumbi wenye maneno ya vijembe na kejeli mfano jali maisha yako na usinijue. Kwa ufupi ni uharibifu wa barabara kwa kusababisha mmomonyoko wa udongo licha ya uchafuzi wa mazingira. Hima jeshi la polisi huku vijijini hakuna udhibiti wa vyombo vya moto hata kichaa anendesha chombo. Watu wamechoshwa na tabia hizi za mabodaboda ila hawana namna ya kuelezea kero hizi. Kwa uzi huu viongozi wenye dhamana naomba wajue kuwa huku vijijini watu wamejifanya kuwa juu ya sheria. Kama kuna mchangiaji katika uzi huu naomba atoe na mapendekezo namna ya kudhibiti vitendo hivi vya utovu wa nidhamu na uchafuzi wa mazingira. Watanzania wengi kwa sasa mko vijijini kwa sababu ya kutafuta maeneo yenye utulivu tofauti na kelele za mjini lakini si shwari tena!