Bodaboda chachu ya michepuko

Bodaboda chachu ya michepuko

Donatila

JF-Expert Member
Joined
Oct 23, 2014
Posts
8,247
Reaction score
25,190
NI usafiri wa kasi, unatumiwa sana na wanaotaka kufika haraka na mara kadhaa, na waendao kwenye miadi, hasa ya wapenzi.

Lakini ndani ya urahisi huo wa kufika na hata kuwahi katika kile ambacho sasa kinafahamika zaidi kama “michepuko”, usafiri wa Bodaboda umeghubikwa na mazingira ya vifo na ajali mbaya.

"Kazi yetu inahitaji umakini na usiri mkubwa kutokana na kwamba abiria wetu ni watu wa aina mbalimbali. Miongoni mwa wadau wakubwa ni pamoja na viongozi mbalimbali wakiwamo wake na waume,” anasema kijana mmoja mwendesha Bodaboda ambaye kwa sababu za wazi hatutamtaja.

Mwingine anaongeza: “Shughuli zetu sisi hazina tofauti na za madaktari. Hawawezi kutoa siri ya maradhi ya mteja. Na sisi pia hatuwezi kutoa siri ya abiria wetu. Kitendo cha kutoa siri za wateja ni sawa na kuharibu soko na kujiondolea uaminifu kwa wateja.

“ Kwa mfano anakuja mteja, na ukiangalia unamfahamu hadi mume wake au mke wake, anakuambia nipeleke nyumba fulani ya wageni au hotelini. Ukija kusema taarifa zake Kijiweni tayari wewe umeshajiharibia soko na kupoteza mteja.

“ Tuna siri nyingi za wateja. Lakini pia tunawindwa sana na watu wabaya. Kama unavyojua wengi wetu wamekufa na wameporwa na wengine wamekufa katika ajali.

“ Unaweza kumbeba abiria usimtambue kama ni mtu mbaya. Kikubwa tunachofanya ni kujihami kulingana na maelekezo ya eneo analohitaji kupelekwa.

“ Kwa hiyo kinachofanyika ni kumueleza kwamba huko siwezi kwenda na wakati huohuo unatengeneza uharibifu wa makusudi kwenye pikipiki au Bajaji yako kwa nia ya kugomea safari husika."

Ushuhuda huo wa vijana waendesha Bodaboda na Bajaji unakuja ikiwa ni takriban miaka tisa tangu usafirishaji wa abiria kwa njia ya pikipiki, maarufu kama Bodaboda, uruhusiwe nchini, ukiwa umesababisha vifo vya watu 7,521, majeruhi 36,333 kutokana na jumla ya ajali 38,729 na wengine wakikutwa na umauti kutokana na vitendo vya uporaji.

Takwimu zinasema Tanzania sasa ina jumla ya Bodaboda 1,358, 000, zinazofanya kazi nchini kote.

Hali hiyo inajitokeza wakati takwimu za vyombo vya moto barabarani, kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani, zikibainisha kwamba licha ya idadi hiyo ya pikipiki 1,3458,000 nchi nzima, idadi ya vyombo vingine barabarani ni pamoja na mabasi ya abiria 59,140, magari madogo 56,146 na magari makubwa (malori) 6,170.

Kwa mfano, katika kipindi cha miezi mitano tu ya kwanza ya mwaka huu wa 2017, Bodaboda zimesababisha vifo 302, majeruhi 455 kutoka katika ajali 607 za kipindi hicho cha kuanzia Januari hadi Mei 2017, ingawa pia idadi ya ajali, vifo na majeruhi wanaotokana na ajali hizo imekuwa ikipungua mwaka hadi mwaka katika kipindi hicho cha miaka tisa tangu kuanzishwa kwa usafiri wa Bodaboda nchini.

Uchunguzi wa gazeti hili uliohusisha pia mazungumzo na viongozi mbalimbali wa taasisi zinazosimamia shughuli za usafirishaji, pamoja na usalama barabarani, umebaini kwamba kuna udhaifu mkubwa wa usimamizi wa sheria za barabarani, udhaifu ambao ni sababu ya msingi ya chanzo cha ajali hizo ambazo si tu huua ama kujeruhi watumiaji wa usafiri wa Bodaboda bali pia wapita njia wengine.

Kwa mujibu wa takwimu za Jeshi la Polisi – Usalama Barabarani, ajali za pikipiki kwa mwaka 2008 zilikuwa 2,036 kwa nchi nzima, vifo vilivyosababishwa na ajali za pikipiki ni 309, majeruhi wakiwa 1,931.

Mwaka 2009 ambapo ndipo sheria ilipitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa vyombo hivyo kupakia abiria, takwimu za ajali mwaka huo kwa nchi nzima zilikuwa ni 3,406, vifo vikiwa 502, na majeruhi wakiwa ni 3,478.

Mwaka 2010 ajali ziliongezeka kufikia 4,463, vifo vikiwa 683, na majeruhi wakiwa 4,471; ajali ziliongezeka pia kwa mwaka 2011, zikifikia 5,384, vifo vikiwa 945 na majeruhi wakiwa ni 5,506.

Kama hiyo haitoshi, kwa mwaka 2012 ajali zilikuwa 5,763, vifo 930, na majeruhi wakiwa 5,532. Mwaka 2013, idadi ya ajali ilikuwa 6,831, vifo vikiwa 1,098 huku majeruhi wakiwa 6,578.

Mwaka 2014 idadi ya ajali ilipungua ikifikia 4,169, vifo 928, na majeruhi 3,884.

Takwimu hizo za Jeshi la Polisi – Usalama Barabarani zinabainisha kwamba mwaka 2015 ajali zilikuwa 2,626, vifo 934 na majeruhi wakiwa 2,370 na kwa mwaka jana, mwaka 2016 ajali zilikuwa 2,544, vifo 890, majeruhi 2,128.

Mwaka huu, katika kipindi cha Januari hadi Mei, 2017, ajali ni 607, vifo 302, majeruhi 455 ikilinganishwa na Januari hadi Mei 2016, ambapo ajali zilikuwa 1,110, vifo 347 na majeruhi 950.

Akizungumzia hali hiyo ofisini kwake jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Musilimu, alisema sasa matukio hayo ya ajali yamekuwa yakipungua siku hadi siku baada ya Jeshi hilo kuamua kutumia nguvu kubwa katika kukabiliana na wanaokiuka sheria za barabarani.

Mbali na kuamua kutumia nguvu, alifafanua kuwa, elimu ya usalama barabarani inayotolewa na wadau mbalimbali wa usalama barabarani kwa watumiaji wa vyombo hivyo imesaidia waendesha Bodaboda kupunguza vitendo vya ukiukaji wa sheria.

“Uamuzi wa kutumia nguvu kwa kuwaweka wahalifu mahabusu na kisha kuwapeleka mahakamani umefikiwa baada ya kubaini kwamba adhabu ya kulipa faini haikuwafanya wavunja sheria kuacha vitendo hivyo. Tukaamua sasa tuwalaze mahabusu. Sasa ule usumbufu wanaoupata mahabusu, mara mahakamani umesaidia wao kutii sheria kwa hiari yao.

“Suala jingine lililochangia ajali kupungua ni mafunzo ya mara kwa mara yanayotolewa kwa waendeshaji wa vyombo hivi. Japokuwa si maeneo yote yamefikiwa Tanzania, lakini mwamko wao (waendesha Bodaboda) kupata elimu umekuwa mkubwa sana,” anaeleza kamanda huyo.

Hali halisi kitaifa

Raia Mwema limebaini kwamba wakati usafirishaji kwa njia ya Bodaboda unaruhusiwa nchini mwaka 2008 hapakuwa na sheria, kanuni wala masharti juu ya namna ya kusimamia sekta hiyo ndogo ya usafirishaji.

Kimsingi, biashara hiyo iliruhusiwa kufanyika holela nchini. Hapakuwa na mafunzo yoyote ya namna bora ya Bodaboda watakavyokuwa wanatoa huduma kwa abiria.

Hata hivyo, baadaye, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), iliingia makubaliano ya kisheria na halmashauri za manispaa zote nchini kwa ajili ya kuweka utaratibu wa kusimamia shughuli za uendeshaji wa Bodaboda ingawa pia, Raia Mwema limeelezwa kwamba, katika makubaliano hayo Jeshi la Polisi nchini, hususan, Kikosi cha Usalama Barabarani hakikushirikishwa, na hivyo kukosekana uzoefu wa Polisi katika kudhibiti uendeshaji wa sekta hiyo.

Kwa mujibu wa sheria, hasa Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973, majukumu ya usimamizi wa usalama barabarani yako chini ya Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani.

Katika makubaliano hayo ya kisheria kati ya Sumatra na halmashauri za manispaa nchini, miongoni mwa kanuni zilizowekwa tangu mwaka 2010 kuhusu uendeshaji wa Bodaboda na Bajaji ni pamoja na dereva awe na leseni; vyombo hivyo viwe na vituo; Bajaji na Bodaboda zote zisajiliwe; madereva wavae kofia ngumu pamoja na abiria wao; waendesha Bodaboda wasibebe abiria zaidi ya mmoja; wawe na sare zao au alama (za utambuzi) kutofautisha dereva wa Bodaboda wa eneo moja (mfano Temeke na Kinondoni – Dar es Salaam); pikipiki zote kuwa na bima pamoja na kutokubeba mtoto wa umri chini ya miaka minane.

“ Umekuwa ni usimamizi dhaifu wa kanuni kati ya Sumatra, majiji na halmashauri zake, sasa imekuwa ni kugawana asilimia 50 ya mapato yanayokusanywa kutoka kwa waendesha Bodaboda bila kuangalia taratibu za uendeshaji wa shughuli hizi,” alieleza mmoja wa maofisa waandamizi wa serikali katika sekta ya usafirishaji aliyeomba asitajwe gazetini.

Lakini akizungumza na Raia Mwema hivi karibuni kuhusu hali halisi ya sekta hiyo ndogo ya usafirishaji nchini, Afisa Mawasiliano wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, Tabu Shaibu, alisema; “Wajibu wetu ni kutoa leseni kulingana na kanuni zilizowekwa na Sumatra.”

Mkurugenzi wa Udhibiti, Usafiri wa Barabara katika Sumatra, Johansen Kahatano, akizungumzia hilo hivi karibuni jijini Dar es Salaam katika mazungumzo yake na gazeti hili alisema kwamba mbali ya changamoto zilizopo za waendesha Bodaboda, yapo baadhi ya mambo manispaa zilipaswa kusimamia kwa ufanisi, ikiwamo uwekaji wa vituo maalumu vya waendeshaji wa vyombo hivyo.

“Kusema kwamba Polisi haionekani kwenye makubaliano si kweli. Kinachofanyika ni utaratibu ni ule ule wa kushughulikia makosa ya usalama barabarani ikiwamo kuvaa kofia ngumu na mambo mengine,” alisema Kahatano.

Hali ilivyo MOI

Kwa mujibu wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI) jumla ya wapita njia (waenda kwa miguu) 356 wamejeruhiwa.

Akizungumza na Raia Mwema hivi karibuni, Meneja Ustawi wa Jamii na Uhusiano kwa Umma katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Almasi Jumaa alisema kwamba katika semina nyingi zilizohudhuriwa na baadhi ya maafisa ustawi wa jamii kitengo cha Mifupa Muhimbili, changamoto zinazowakabili waendesha Bodaboda pamoja ni ukosefu wa elimu ya usalama barabarani.

“Kati ya waendesha Bodaboda 400, unakuta ni 40 tu ndio wenye elimu ya usalama barabarani. Umri wa waendesha Bodaboda ni kuanzia miaka 14 hadi 29, ukimkuta mwenye umri wa miaka 30 na kuendelea wengi wao ni wamiliki wa hizo Bodaboda.

Lakini pia tumegundua vijana wengi wanatumia vilevi wakiwa kwenye shughuli zao hizo, pia vijana wengi hawalali (wanakesha) hivyo wanaendesha vyombo hivyo wakiwa na uchovu unaotokana na kukosa muda mrefu wa kupumzika hasa usiku,” alieleza.

Takwimu za MOI zinasema tangu Januari hadi Mei 17 mwaka huu, idadi ya majeruhi waliofikishwa hospitalini hapo kutokana na ajali zilizosababishwa na Bodaboda ni 948.

“Kwa mwezi Januari, madereva walikuwa 64, abiria 67, waendao kwa miguu walikuwa 76, hivyo jumla yao ikawa ni 207. Februari, idadi ya majeruhi ilikuwa madereva 62, abiria 60, waendao kwa miguu 67, hivyo jumla yake ikawa ni 189; Machi, idadi ya majeruhi madereva ilikuwa ni 65, abiria 60, waendao kwa miguu 70, jumla ni 195. Aprili, majeruhi madereva ni 54, abiria 48, waendao kwa miguu 73, hivyo jumla ni 175. Mei majeruhi ambao ni madereva walikuwa 60, abiria 52, waendao kwa miguu 70, hivyo kufanya jumla yao kuwa 182,” alieleza.

Kinachoendelea Mwanza

Kutoka jijini Mwanza, takwimu zinabainisha kwamba vifo vya madereva na abiria wa bodaboda vimepungua kutoka 15 hadi kimoja kwa mwezi.

Mafanikio hayo yanadaiwa kutokana na usimamizi madhubiti wa usafirishaji wa Bodaboda unaofanywa na uongozi wa Chama cha Waendesha Pikipiki (CWP) Mkoa wa Mwanza dhidi ya madereva wakorofi wa Bodaboda.

Akizungumzia hali halisi miongoni mwao, Mwenyekiti wa CWP Mwanza, Makoye Kayanda Bunoro anasema: “Kwa sasa ajali zinazotokea jijini hapa, tena mara chache ni za kukwaruzana tu.”

Anaendelea kueleza: “Nimezungumza na uongozi wa Polisi mkoani muda mfupi kabla ya kuzungumza na wewe (Raia Mwema), umeniambia rekodi zao kwa mwezi uliopita (Juni) zinaonesha ni mmoja aliyekufa kutokana na ajali ya Bodaboda. Siku za nyuma, hususan, miaka ya 2014 na 2013 kurudi nyuma tulikuwa tunapata wastani wa vifo vya watu 15 vinavyotokana na ajali za Bodaboda kwa mwezi.”
Maelezo ya Mwenyekiti huyo wa CWP Mwanza katika mahojiano na Raia Mwema jijini hapa juzi, yanafundisha kuwa dhana ya kujisimamia kazini ni bora kuliko kusimamiwa.

“Adhabu kali zinazotolewa na uongozi wa CWP kwa waendesha Bodaboda zimesaidia sana kupunguza ajali za vyombo hivyo. Sasa hivi wanaogopa kukamatwa na viongozi wao kuliko kukamatwa na Polisi,” amesema Bumoro.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa CWP, adhabu zinazotolewa na Polisi kwa mwendesha Bodaboda ‘mkorofi’ ni nafuu kuliko zinazotolewa na uongozi wa chama hicho.

“Mwendesha Bodaboda anayekamatwa na Polisi kutokana na kukiuka sheria za usalama babarabani hutozwa faini kisha kuachiwa na pikipiki yake siku hiyo hiyo.

“Lakini sisi (viongozi wa CWP) tukimkamata tunamnyang’anya pikipiki na kuishikilia kwa muda wa wiki moja au zaidi hadi tutakaporidhika kuwa amejirekebisha,” anasema.

Uongozi wa CWP mkoani Mwanza umejiimarisha kuanzia kwenye vituo vya madereva wa Bodaboda kwa ajili ya kusimamia nidhamu na huduma nzuri kwa pande zote mbili (madereba na abiria).

Aidha, viongozi wa chama hicho wamejiwekea utaratibu wa kukutana na waendesha Bodaboda mara kwa mara kuelimishana na kusisitizana juu ya umuhimu wa kuzingatia sheria za usalama barabarani bila shuruti.

Wizi wa Bodaboda

Hata hivyo, kumekuwapo na wimbi la wizi wa Bodaboda na kujeruhi madereva husika kwa ‘style’ mbalimbali mkoani hapa.

Mwenyekiti huyo wa CWP Mwanza amelieleza Raia Mwema kwamba Bodaboda tisa zimethibitika kuibwa kwa Juni mwaka huu.

“Mbinu zinazotumika ni kuteka madereva na kuwanyang’anya pikipiki, kuziiba kwenye maegesho nyakati za usiku na wateja (abiria) kuwalewesha madereva kwa juisi na pipi zenye vileo,” amesema Bunoro na kuongeza: “Mbinu nyingine ni wezi kuwatumia mabinti kukodi pikipiki na kujirahisisha kimapenzi kwa madereva husika kisha kuwapeleka vichochoroni na porini ambako huvamiwa na kuporwa vyambo hivyo vya usafiri.”

Hali halisi Arusha

Katika Jiji la Arusha, Raia Mwema, limebaini kwamba licha ya matukio ya ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani, bado mauaji na uporaji wa pikipiki ni changamoto kubwa kwa madereva hao wa Bodaboda au maarufu kama Toyo, wanaotoa huduma katika Wilaya ya Arusha Mjini.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Raia Mwema imekusanya na kuthibitishwa na viongozi wa Umoja wa Waendesha Pikipiki mjini Arusha, katika kipindi cha Januari hadi Juni, mwaka huu, pikipiki zimeibwa na madereva wake 10 kuuawa.

Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, Mwenyekiti wa Waendesha Bodaboda kata Levolosi, Muhidin Salim, alieleza kuwa hali ya usalama kwa madereva na pikipiki zao si shwari tena kutokana na kushamiri kwa vitendo vya mauaji na uporaji.

“Dereva wa mwisho kuuawa tulimzika Jumatano iliyopita na aliuawa na watu wasiojulikana katika eneo la Mianzini na pikipiki yake iliporwa,” alisema Mwenyekiti huyo.

Alieleza kuwa wanaotekeleza mauaji hayo hukodisha pikipiki kama wateja wa kawaida na wanapowafikisha sehemu waliyoelekezwa, huwashambulia kwa mapanga au mashoka na kisha kupora pikipiki na kuondoka nayo. Aliyataja maeneo hatarishi kwa waendesha pikipiki kuwa pamoja na Mianzini, Sombetini, Kwa Mrombo na Mlima wa CCM.

“Kwa kweli hali ni mbaya sana. Tumepoteza maisha ya watu na pikipiki zao pia zimeporwa, na mbaya zaidi, hadi sasa Polisi wameshindwa kujua mtandao unaofanya mauaji hayo,” alidai kiongozi huyo.

Katika mkutano wake na viongozi wa Umoja wa Waendesha Pikipiki Wilaya ya Arusha Mjini, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema suala mauaji ya madereva wa pikipiki ni changamoto. Mkutano huo ulifanyika Ijumaa iliyopita katika ukumbi wa Bwalo la Polisi.

“Kumekuwa na uhalifu wa kutisha kuhusu uporaji wa pikipiki na mauaji ya madareva. Katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu kumekuwa na matukio 10 na tukio jingine ni la wiki mbili zilizopita,” alisema Kamanda Mkumbo katika mkutano huo.

Kamanda huyo alisema hata hivyo si kweli kwamba Polisi wameshindwa kuwapata wahusika wa mauaji hayo kwani tayari kuna watu wanashikiliwa na wamefunguliwa kesi za mauaji.

Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Bodaboda Wilaya ya Arusha, Maulid Makongoro, alisema hata hivyo kutokana na wimbi hilo la mauaji wamekuwa wakitoa ushauri na maelekezo kwa wanachama wao ili wajihadhari.

Mwenyekiti huyo alisema kwa sasa wanachofanya ni kuwahamasisha madereva wote wanaotoa huduma kusitisha kufanya hivyo nyakati za usiku na pia kutowahudumia watu wasiowafahamu nyakati hizo.

“Tumewaambia kuwa mwisho wa kutoa huduma isiwe zaidi ya saa tatu usiku kwa sababu uzoefu unaonyesha kuwa mauaji hutokea kuanzia saa tano usiku na kuendelea hivyo basi ni vyema wakafunga kazi mapema au kuhudumia wateja wao wanaowafahamu,” aliongeza.

Kamanda wa Polisi wa Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha, Nuru Suleiman, alisema hata hivyo bado kuna wimbi kubwa la ajali za barabarani zinazotokana na madereva wa pikipiki na kuwataka kufanya mabadiliko makubwa katika uendeshaji na kutii sheria za usalama barabarani.

“Kwa mfano takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2016 ajali 528 zilitokea na ajali 203 zilihusisha Bodaboda na kati ya hizo madereva 40 walipoteza maisha, ” alisema.

Kamanda huyo alisema kati ya mwezi Januari hadi Juni mwaka huu idara yake ilirekodi ajali 305 na kati hizo 124 zilikuwa za pikipiki na kwa kuangalia uwiano bado idadi ya ajali hizo ni nyingi katika kipindi cha nusu ya mwaka tofauti na mwaka uliopita.


Alisema idadi ya pikipiki mkoani Arusha ni zaidi ya 5000 na kuna vituo 426 vilivyosajiliwa na idadi hiyo ni kiashiria kuwa kama madereva hawatabadili tabia zao ili kutii sheria za usalama barabarani basi idadi ya vifo vya ajali vinaweza kuongezeka.

Hali ilivyo Makao Makuu Dodoma

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani hapa, Marisone Mwakyoma anasema ajali za pikipiki zimepungua kwa asilimia 28.6.

Amesema katika kipindi cha Januari hadi Mei, 2017 kulikuwa na ajali 30 za pikipiki zilizosababisha vifo vya watu 11 na majeruhi 23 ukilinganisha na takwimu za Januari hadi Mei, mwaka 2016 ambapo kulikuwa na ajali za pikipiki 42 zilizosababisha vifo vya watu 16 na majeruhi 21.

Hata hivyo alisema kupungua kwa ajali hizo kunatokana na mikakati mbalimbali iliyowekwa na Jeshi la Polisi ikiwamo ya askari kuunda kikosi maalumu cha kufuatilia na kukamata wote wanaovunja sheria za usalama barabarani ambao ulitekelezwa kwa kuwajengea uwezo askari wa kuijua sheria ya mwaka 2010 inayohusu pikipiki.

Sheria ya pikipiki ya mwaka 2010 na tangazo la serikali namba 144 kifungu cha 13 vinaeleza makosa yote ya pikipiki yakiwemo ya abiria kutovaa kofia ngumu kuwa naye anawajibika kukamatwa na kulipa faini.

Naye Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Ernest Ibenze, katika mazungumzo yake na Raia Mwema hivi karibuni alisema uamuzi wa serikali wa kupiga marufuku matumizi ya pombe za viroba umepunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya majeruhi wa Bodaboda wanaofikishwa katika hospitali hiyo ya rufaa ya mkoani Dodoma.

Idadi hiyo imepungua kutoka majeruhi 40 kwa siku hadi kufikia 20 ambao baadhi yao huwa wamevunjika miguu, mikono na kujeruhiwa vibaya kichwani, kifuani, mgongoni na tumboni.

“Tangu Bodaboda zianze kutumika nchini kulikuwapo ongezeko la ajali zilizosababisha majeruhi wengi ambazo chanzo chake ni uvunjifu wa sharia. Lakini kasi hiyo imepungua baada ya viroba kupigwa marufuku. Awali tulikuwa tunapokea wagonjwa wasiopungua 40 kwa siku.

“Naomba niwatoe hofu wanaopata ajali za pikipiki kuwa wanapofikishwa hospitalini hapa hawawezi kukatwa miguu kama wanavyoambiwa huko mitaani na badala yake watoe ushirikiano ili hospitali iweze kupata takwimu sahihi badala ya kuficha ukweli hadi wanaporuhusiwa,”alisema.

DK. Ibenze ambaye ni bingwa wa mifupa na ajali aliliambia Raia Mwema kuwa wapo wachache wanaoweza kusema ukweli kwamba walipata ajali ya pikipiki ingawa wamekuwa wakitoa maelezo hayo baada ya kupatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa Dk. Ibenze, katika hospitali hiyo ya rufaa ya mkoa, wodi nne zimetengwa kwa ajili ya majeruhi wa ajali mbalimbali huku akisisitiza kutoruhusu mgonjwa kuwa na kilema kwa kukatwa mguu.

Hata hivyo kwa upande wake, uongozi wa Chama cha Huduma za Usafiri wa Pikipiki na Bajaji Tanzania (TAMOSA) umeunga mkono serikali kuwachukulia hatua waendesha Bodaboda wanaovunja sheria.

“Licha ya Bodaboda kutoa huduma kwenye jamii, wanapokiuka sheria kwa makusudi au bahati mbaya, sheria hiyo hiyo haina kinga dhidi yao,” alisema Mkurugenzi wa Habari, Mafunzo na Utafiti wa chama hicho, Daniel Msangya.

Uongozi huo wa TAMOSA wenye wanachama 6,000 kwenye mikoa ya Singida, Dodoma, Arusha, Dar es Salaam na Morogoro umekuwa ukiwasisitiza waendesha Bodaboda kujiunga pamoja na kupatiwa mafunzo ya sheria za usalama barabarani ili waweze kukubalika kwenye jamii.

Hali halisi Mbeya

Miongoni mwa matukio ya hivi karibuni kabisa mkoani Mbeya yanayohusu ajali za Bodaboda ni pamoja na ile iliyotokea Iwambi jijini Mbeya, baada ya pikipiki kugongana na gari aina ya Toyota Noah.

Pikipiki hiyo ilikuwa ikitokea Iwambi kuelekea mjini, ikiwa na abiria wawili, pamoja na dereva wake wakawa watatu. Wote watatu walifariki dunia papo hapo.

Taarifa za ajali hiyo zinaonyesha kuwa mwendesha pikipiki hiyo alikuwa kwenye mwendo wa kasi, akahama upande wake wa barabara na kwenda upande mwingine ambako gari husika lilikuwa likitokea mjini kuelekea Tunduma, kisha kugongana ana kwa ana.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarai mkoani Mbeya, SSP Butusyo anaielezea ajali hiyo kuwa miongoni mwa matukio ya kizembe yanayosababishwa na vijana waendeshao Bodaboda.

Kwa mujibu wa SSP Butusyo, kijana aliyekuwa akiendesha pikipiki hiyo hakuwa dereva, hivyo ni wazi hakufahamu lolote kuhusu sheria za barabarani.

Taarifa ya kikosi cha usalama barabarani mkoani Mbeya zinabainisha kuwa asilimia 33 ya ajali zinazotokea mkoani humo husababishwa na vyombo hivyo vya usafiri; Bodaboda na Bajaji.

Katika kipindi cha Januari hadi Mei, mwaka huu pekee, kulikuwa na ajali 37 za pikipiki, zilizosababisha vifo 28 na majeruhi. Ikilinganishwa na mwaka jana, kwa kipindi kama hicho, ajali hizo zinaonyesha kupungua. Ajali za mwaka jana, katika kipindi kama hicho, zilikuwa 69 zilizosababisha vifo 34 na majeruhi 72.

SSP Butusyo anabainisha kuwa ajali nyingi za vyombo hivyo hutokea nyakati za usiku, kuanzia saa tatu hadi saa 11 alfajiri.

Sababu kuu inayotajwa kuchangia katika ajali za vyombo hivyo ni pamoja na waendeshaji wake wengi kutopitia mafunzo malumu wa udereva, hujifunzia humo humo barabarani baada ya kukabidhiwa pikipiki na wamiliki kwa ajili ya kufanya biashara hiyo ya usafirishaji.

Ajali nyingine hutokana na mizaha ya waendeshaji wake, ikiwamo kamari kwa kushindana katika mwendo kasi ambapo hutumia barabara zile zile zinazotumika na watu wengine, zikiwamo barabara kuu.

Moja ya ajali hizo ilitokea jijini Mbeya hivi karibuni ambapo vijana wenye kuegesha pikipiki zao eneo la Sokomatola, mkabala na lango la Shule ya Sekondari ya Wasichana Loleza, walikuwa wakishindana kwenye barabara ya Sokomatola- Mafiat. Mwenzao mmoja alifariki baada ya kupata ajali wakati wakirudi, ambapo baada ya wenzake kufika kituoni, walisubiri bila mafanikio, wakaamua kumfuata ndipo walipomkuta akiwa kapata ajali na kufariki dunia.

Mtazamo wa serikali

Kwa upande wake, serikali imekiri kuwapo kwa uvunjifu mkubwa wa sheria za usalama barabarani unaofanywa na waendesha Bodaboda na kuanza kuchukua hatua ya kulipunguza na hatimaye kutokomeza kabisa tatizo hilo.

Mtazamo huo umetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusuf Masauni wakati wa mahojiano na Raia Mwema juu ya hatua zinazochukuliwa na serikali katika kudhibiti uvunjifu wa sheria za usalama barabarani unaofanywa na waendesha bodaboda, sambamba na changamoto nyingine zinazofanywa na madereva hao.

Alisema katika mkakati wa kwanza wa serikali wa kupunguza ajali za barabarani kwa asilimia 10 kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Agosti 2016 hadi Januari, 2017 kipaumbele kilielekezwa kwa Bodaboda.

Masauni anasema mkakati huo ambao ulifanikiwa kupunguza ajali hizo kwa asilimia 11, pamoja na mambo mengine, utekelezaji wake ulihusu usimamizi wa sheria ipasavyo na kuhakikisha kwamba wote wanaovunja sheria za usalama barabarani wanawekwa mahabusu kwa saa 24 kisha kufikishwa mahakamani.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, katika mkakati wa kwanza uliomalizika mwezi Januari, madereva 1,596 wakiwamo wa Bodaboda walikamatwa na kuwekwa mahabusu na kisha kufikishwa mahakamani badala ya kulipa faini kama ilivyozoeleka.

Serikali pia ilitekeleza agizo la Rais kwa kuchomoa matairi ya waendesha Bodaboda wa Dar es Salaam waliokuwa wakitumia Barabara za Mwendo Kasi na kusababisha ajali.

Kauli hiyo inaakisi kauli ya mwezi Juni 2016, iliyotolewa na Rais John Magufuli, kutokana na kile kinachoweza kutafsiriwa kuwa ni kuchoshwa na uvunjifu wa sheria ya usalama barabarani, aliamuru askari wa usalama wa barabarani kukamata vyombo vya moto na hata kuving’oa magurudumu vinapohifadhiwa kwenye vituo vya polisi ili kuwakomoa wamiliki wa vyombo hivyo, ikiaminika kwamba dhana hiyo itasaidia watu kuheshimu sheria husika.

Naibu Waziri Masauni akaongeza; “Leo nafarijika kuona mafanikio yamefikiwa japokuwa ni kwa kiwango kidogo lakini tumeweza kupunguza vifo vinavyosababishwa na ajali za Bodaboda.”

Kuhusu kero za Bodaboda na namna askari wa usalama barabarani wanavyoshindwa kuwadhibiti madereva hao, Masauni alisema, kwa kuwa si rahisi kwa Polisi wa Usalama Barabarani anayeongoza magari kwenye makutano ya barabara kumzuia mwendesha Bodaboda anapovuka bila kufuata sheria, serikali imeweka askari waliovaa kiraia na kupiga picha ili baadaye waweze kukamatwa.

Hata hivyo, Naibu Waziri huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani alisema awamu ya pili ya mkakati huo utazinduliwa Julai, 2017, serikali inaangalia namna ya kuweka kamera za kisasa kwenye barabara ili ziweze kuwanasa wale wote wanaovunja sheria za barabarani na hatua kali dhidi yao ziweze kuchukuliwa.


Chanzo: Raia Mwema

 
Mbona kichwa cha habari hakiendani na maelezo? Umeelezea zaidi bodaboda na waendesha bodaboda… changamoto zao na mafanikio yao na sio habari ya michepuko…
 
Samahani sana joverest nafasi yako hii
 
Back
Top Bottom