Benard Membe, hata mimi nimechukizwa

Benard Membe, hata mimi nimechukizwa

Mphamvu

JF-Expert Member
Joined
Jan 28, 2011
Posts
10,702
Reaction score
3,356


Tanzania-Glassgow-460x350.jpg


​
Michuano ya Jumuia ya Madola ilikamilika wiki iliyopita huko Glasgow, bila timu ya Tanzania kutwaa medali yoyote.
Siku nne kabla Mashindano hayajafika tamati, Waziri mwenye dhamana ya mambo ya Kimataifa alikuja na kauli ya kukerwa na yaliyotokea Glasgow, akionesha kutofurahishwa na kiwango kilichooneshwa na wachezaji waliowakilisha nchi huko.


Kwa upande mmoja wa jicho jepesi, hii ni kauli ambayo inapaswa kuungwa mkono na kila mpenda maendeleo ya michezo hapa nchini. Ndio, wadau wote tunatakiwa tuoneshe hasira zetu za waziwazi kutokana na kufanya vibaya huku kwa wanariadha wetu waliopewa heshima ya kuwakilisha Watanzania milioni 40 na ushee.


Kauli ya Membe inatoka wakati ambapo karibu kila mwanamichezo Mtanzania amevunjwa moyo na ushiriki wetu wa michezo kimataifa na mwenendo wa michezo karibu yote. Wakati ambao matokeo ya mechi ya wali ya mchujo kuelekea AFCON 2015 si mazuri sana dhidi ya Msumbiji.


Wakati ambao bado TFF na Kamati ya Ligi hawajawa na uhakika Ligi Kuu ya Soka itaendeshwa kwa mfumo gani msimu ujao mwa kuwa hawajui kama watatumia tiketi za elektroniki au la na endapo ligi itasimamiwa na kampuni au kamati ya muda. Wakati ambao kuanza kwa ligi kumesogezwa mbele huku hata ratiba yenyewe ikiwa haijatolewa.


Wakati huu huu ambao vyama vya Riadha na Tenisi vina migogoro mikubwa ndani yao. Mingi kati yao ikihusisha madaraka na mambo ya fedha. Ndio, RT wana kashfa kubwa ya uongozi, maandalizi na ufisadi wakati katika tenisi Mama Inger Njau aliachia ngazi mwaka jana kwa vijimambo ambavyo sio tofauti sana na vyama vingine.


Ni turufu ya siasa kujaribu kushikamana na Watanzania kwa kukemea ambayo na wao wanayakemea, na ndicho alichokifanya Waziri huyu.


Lazima tukubaliane kuwa wanasiasa hufanya mambo kwa kusukumwa na upepo wa siasa. Waliosikia hotuba za wanasiasa waandamizi wa Chama cha Mapinduzi wakikemea Serikali yao wenyewe watakubaliana na hili.


Labda pengine Membe ni maamuma wa masuala ya michezo lakini si mgeni na kilio cha Watanzania weledi kuwa ili tufanikiwe katika mashindano ya kimataifa ni lazima tuwekeze katika maandalizi ya ngazi ya chini.


Nawatetea Watanzania wengine wanaosema kuwa wamechukizwa na matokeo mabaya, hata mimi nimechukizwa sana tu. Lakini inakuwaje mtu ambaye yupo katika chombo chenye mamlaka (Serikali) anapogeuka na kuwa mlalamikaji.
Membe anajua fika kuwa yeye anatakiwa kuwa mwajibikaji, ingawa Wizara yake haihusiki moja kwa moja na michezo lakini yeye ni mjumbe wa Baraza la Mawaziri na anahusika kuandaa bajeti na mipango ya Serikali ambayo inagusa michezo pia.


Mimi si mdau wa siasa kwa sana, lakini najua kuwa alichokifanya Bwana Membe ni mchezo wa siasa. Kwanini hakuchukizwa tulipofanya vibaya michuano ya kufuzu AFCON na Kombe la Dunia kwa makumi ya miaka mfululizo? Kwanini hakutoa matamko kama haya wakati viongozi wa RT wanafanya madudu ya kuingia madarakani kinyume na katiba, wakati Suleiman Nyambui anajiteua kuwa kocha wa timu hii iliyofeli Glasgow wakati tayari ni Katibu Mkuu wa RT.


Hakukereka mwaka jana wakati @Anthony Mtaka alipotangulia Moscow kwenye mashindano ya Dunia ya Riadha huku akiacha wanariadha nyuma tena katika hali tete. Au mwaka huu lipotoa kauli tata kuwa Watanzania wasitarajie makubwa Glasgow wakati Serikali imetumia mamilioni ya pesa kuandaa timu nje ya nchi.


Jibu ni sarakasi za urais ndani ya Chama cha Mapinduzi. Na membe amejitokeza kuoneshwa kukereka ili kuvuta usikivu na sapotikutoka kwa wapenda michezo, hakuna kingine.


Alikuwepo wakati Rais anaikabidhi bendera timu ya Riadha ya Taifa wakati iliyokwenda China kujiandaa na michuano hii ambayo matokeo yake yamemkera. Maandalizi yaliyofanyika ni zimamoto na yeye aliliona hilo.
Laiti kama timu hii ingefanya vema angekuja na kauli za kujibaraguza kuwa ni juhudi za Serikali zimefanikisha hili. Lakini katika matokeo mabovu amekuja na kucukizwa tu, ndio kachukia halafu basi.


Inafurahisha wanasiasa wanavyojua kucheza na matukio, lakini kwa hili hapana. Siku zote nimesisitiza kuwaondolea lawama wachezaji na makocha kwani wao hawaandai sera wala mipango ya michezo. Mchezaji anaweza kujituma kwa bidii zote lakini kama mamlaka husika hazijasimamia miundombinu ya michezo ni kazi bure hata kama atafanya mazoezi usiku na mchana.


Kauli ya Membe si ya kitaalamu, ni ya kisisasa na ni vema jamii ya wanamichezo ikakwepa mtego huu wa watu kutumia matukio ya michezo (mazuri na mabaya) kwa manufaa yao huku michezo husika ikidumaa.


Nasubiri tamko la kitaalamu la kwanini tumefanya vibaya Glasgow kutoka kwa kamati na kurugenzi za ufundi za vyama vya michezo husika na sio maneno ya kufura ya wanasiasa wetu. Pamoja na kuwa mimi ia nimechukizwa sana, siungi mkono kuchukizwa kwa Benard Membe, Mbunge wa Mtama na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Chanzo: FikraPevu
 
Back
Top Bottom