Bazil Mramba aikana TRA Mahakamani

armanisankara

JF-Expert Member
Jul 15, 2011
283
49
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imeambiwa na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba (71), kuwa hakupokea barua ya kutoa ushauri kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wa kumzuia asitoe msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Alex Stewart (ASSAYERS) ya Uingereza iliyoingia mkataba wa ukaguzi wa madini kupitia kampuni tanzu ya Alex Stewart (ASSAYERS) Government Business Corporation.

Aidha, Mramba ameiambia Mahakama kuwa barua inayodaiwa kuwasilishwa Wizara ya Fedha (wakati akiwa waziri), ilifika Juni 24, mwaka 2003 wakati mkataba wa kuipa kazi kampuni hiyo ulisainiwa Juni 14, mwaka 2003 hivyo haikuwa na maana yoyote.

Mramba alitoa madai hayo jana wakati akiendelea kutoa ushahidi wa utetezi katika siku ya pili mbele ya jopo la mahakimu watatu wakiongozwa na Jaji John Utamwa na Sam Rumanyika wa Mahakama Kuu.

Majaji hao ambao walianza kusikiliza kesi hiyo mwaka juzi wakati wakiwa mahakimu wakazi, wamepewa kibali na Jaji Mkuu kuendelea kusikiliza kesi hiyo wakisaidiana na Hakimu Saul Kinemela wa Mahakama ya Kisutu.

Upande wa utetezi uliongozwa na Profesa Lenard Shaidi, Herbert Nyange, Peter Swai, Elisa Msuya, Cathebet Tenga na Tausi Abdalah.

Akiongozwa na Wakili Nyange, Mramba alidai kuwa kabla ya kupitisha msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo, hakuwahi kupokea barua ya ushauri kutoka TRA, bali mamlaka hiyo iliwasilisha barua Juni 24, mwaka 2003 kwa Katibu Mkuu wa Hazina wakati tayari mkataba ulishasainiwa na msamaha wa kodi kupitishwa.

Alidai kuwa wizara yake haikuomba ushauri kutoka TRA kuhusu masuala ya kutoa msamaha wa kodi kwa sababu sheria ya Benki Kuu ya Tanzania Tanzania (BoT) inampa madaraka Gavana kuingia na kusaini mikataba mbalimbali ambayo ni lazima itolewe msamaha wa kodi.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya Nyange na Mramba:

Wakili Nyange: Shahidi, unaelewa nini makubaliano ya BoT na watu wengine?

Mramba: Naelewa sheria ya BoT inampa madaraka Gavana kuingia na kusaini mikataba na watu wengine.

Wakili Nyange: Endelea kuileza Mahakama unafahamu nini zaidi?

Mramba: Mikataba aliyoingia Gavana na watu wengine lazima itolewe msamaha wa kodi.

Wakili Nyange: Kwa madai ya upande wa Jamhuri ushahidi wao unaeleza kuwa ulihusika kutoa msamaha wa kodi. Je, ni kweli?

Mramba:
Waheshimiwa mahakimu, kifungu cha 4.3.1 cha mkataba huo, kinasema malipo yote yatakayolipwa katika mkataba kati ya kampuni ya Alex Stewart (ASSAYERS) na Benki Kuu hakuna kodi itakayotozwa.

Pia, mimi sikuruhusu msamaha wa kodi, bali nilitekeleza matakwa ya mkataba huo kama sheria ilivyosema.

Wakili Nyange: Kuna malalamiko kwamba wewe mshtakiwa ulitoa idhini kwa Gavana kumlipa Alex Stewart (ASSAYERS) unasemaje kuhusu hilo?

Mramba: Malipo yalitokana na kifungu cha 4.3.3 cha mkataba huo kinachosema BoT itatoa fedha hizo kwa mkaguzi wa madini kwa sababu ingeilipa benki hiyo hilo deni.

Wakili Nyange: Je, ulimruhusu Gavana afanye nini kwenye mkataba huo?

Mramba
: Nilimruhusu kuwalipa Alex Stewart (ASSAYERS) Dola milioni moja za Kimarekani ili aweze kufanya shughuli za maandalizi na serikali ingezirejesha fedha hizo kwa awamu awamu kuilipa BoT.

Kesi hiyo imepangwa kuendelea kusikizwa ushahidi wa Mramba Oktoba 12, mwaka huu.
Mbali na Mramba washtakiwa wengine ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja.

Katika kesi ya msingi, washitakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Agosti mwaka 2002 na Juni 14 mwaka 2004 jijini Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma kama mawaziri na katibu mkuu, walitumia vibaya madaraka.

Ilidaiwa kuwa kwa kupitia kampuni ya Alex Stewart (ASSAYERS) ya Uingereza iliyoingia mkataba wa ukaguzi wa madini ambapo kupitia kampuni tanzu ya Alex Stewart (ASSAYERS) Government Business Corporation, waliingia mkataba kukagua kiwango cha uzalishaji wa madini ya dhahabu kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.





CHANZO: NIPASHE

 
Back
Top Bottom