Barua ya wazi kwa mwl nyerere !

Barua ya wazi kwa mwl nyerere !

Bnoke Matiku

Member
Joined
Dec 28, 2013
Posts
14
Reaction score
1
BARUA YA WAZI KWA MWL NYERERE!!

Ndugu Kambarage,
Nakusalimu katika jina la Tanzania. Nchi ya maono na busara yako, nchi uliyoifanya kuwa kimbilio kwa wageni na wenye shida huko kwao. Nchi uliyotamani siku moja iwe ni Taifa kubwa linalo thamini kila kiumbe hai akaaye katika uso wa dunia!!

Mimi ni kijana mdogo ninayetokea katika wilaya ya Nzega, mkoani Tabora. Najua uko uliko utakuwa unasisimkwa kwa kusoma jina la eneo hili ambalo ulipata fursa ya kusoma na baadaye kufanya kazi hapo!!

Ndg Kambarage!!
Imepita miaka 15 toka ulipofunga macho na kututoka katika dunia hii. Lengo la barua hii ya wazi kwako ni kukufikishia yale yanayojiri huku duniani hususani TANZANIA baada ya wewe kuondoka!!

Ndg Kambarage!!
Nianze kwa kusema kuwa si kweli kuwa toka umeondoka hakuna mambo mazuri ambayo yametokea, yapo mengi tu ambayo nisipoyataja ipo siku utakuja kuyajua na kunishangaa kwa nini nilishindwa kukuambia.

Ndg Kambarage,
Toka kipindi ulichoondoka kama Taifa tumefanikiwa kuimarisha miundombinu hasa barabara, zimetengenezwa kilomita nyingi kwa kiwango cha lami, hili si haba na ni jambo la kupongezwa!! Lkn ndg Kambarage uendelezaji huu wa barabara umeendana na uuaji wa reli hapa kwetu. Ile reli uliyokuwa ukiitumia kusafiri na garimoshi kutoka pale Mwanza baada ya kutoka nyumbani Butiama kwenda shuleni Tabora inafanya kazi kwa kusuasua japo kina Mwakyembe wanajitahidi kuifufua lkn bado hakuna matumaini ya kuimarika hivi karibuni!!

Ndg Kambarage toka umeondoka shule nyingi za kata zimejengwa, idadi ya wanafunzi wanaokwenda chuo kikuu imeongezeka baada ya ongezeko la kasi la vyuo vikuu hapa nchini, nikunong'oneze tu kuwa sasa tuna vyuo vikuu zaidi ya 40 hapa kwetu. Pia katika suala zima la umeme tumefikisha umeme kwa angalau 37% ya watanzania ukilinganisha na zile chini ya 10% kipindi unatutoka!!

Ndg yangu, mjamaa mwenzangu kilichonisukuma haswa kukuandikia barua hii sio hayo mafanikio tuliyapata, la hasha sio hayo!! Yapo mengi tu ya kuudhi na kukera ambayo sijui ingekuaje kama ungekuwepo leo. Nafkri labda wangekuonea haya ingawa historia inaniambia kabla hujaondoka walikuwa wameshaanza kukupuuza.Kama umesahau nitakukumbusha, baada ya mgombea uliyezunguka nchi nzima kumnadi mwaka 1995 kuwa watanzania wamchague kuwa Rais wao kwani ndiye pekee uliyeamini ni Mr Clean kuingia Ikulu aliamua kuleta sera ya ubinafsishaji na soko huria, kinyume kabisa na misimamo yako ya ujamaa na kujitegemea. Unakumbuka ulivyopiga kelele kuzuia asiwauzie makaburu wa Afrika kusini benki ya umma ya NBC lakini akakupuuza na kuamua kuiuza benki yetu hii kwa bei ya kutupa!!??

Ndg Kambarage!!
Umoja, upendo, uzalendo, uwajibikaji, utu, imani katika umoja wa Afrika na usawa ulivyotuachia havipo tena!!

Natambua jinsi ulivyokuwa adui mkubwa wa ukabila na udini, lkn huku kwetu siku hizi kuwa watu wanapalilia chuki za kikabila na udini!! Wapo mpaka wanaokuzushia kuwa nawe ulikuwa mdini, binafsi siwaungi mkono kabisa!!

Ndg Kambarage!!
Hapo juzi juzi tuliona kama Taifa tuanzishe mchakato wa kuandika katiba mpya, tuachane na ile ya mwaka 1977 ambayo ulituachia!! Si kwamba tunaidharau katiba uliyotuachia bali ni kwa sababu za msingi kama vile kutengeneza katiba yenye political legitimacy kwani zile zingine zote ulizowahi kutengeneza hakuna hata moja iliyokuwa na uhalali wa kisiasa kwa maana ya ushirikishwaji wa wanachi katika mchakato mzima wa uundwaji wa katiba!!

Ndg Kambarage!!
Vijana wako wa CCM wakiongozwa na Mh J. Kikwete yule kijana wako uliyemwambia asubiri kwanza akomae kabla ya kupewa madaraka ya nchi wamehodhi mchakato na kuufanya uwe wao peke yao. Sidhani kama ungekuwepo ungekubaliano nao, sidhani!!

Hivi juzi kimetokea kituko kingine kikubwa zaidi, baada ya CCM kuhodhi mchakato wa katiba katika ngazi ya Bunge Maalum la Katiba (BMK) kukatokea kikundi kinachoitwa UKAWA kikijinasibu kutetea maoni ya wanachi yaliyokusanywa na kijana wako Warioba na timu yake ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Ulitokea mkwamo mkubwa na hawa UKAWA wakaamua kutoka nje ya bunge!!

Baada ya UKAWA kugoma kurudi bungeni, BMK liliendelea kama kawaida chini ya uongozi wa yule kijana wako aliyesoma Tabora Boys kama wewe na mimi!! Nadhani unamkumbuka vizuri Samweli Sitta maana ulishawahi kumtia bakora kidogo kipindi ukiwa magogoni!!

Ndg Kambarage!!

Mwana Tabora School mwenzetu huyu ametuangusha sana, katika upigaji wa kura kupitisha katiba inayopendekezwa ilikuwa ni ngumu kupata 2/3 hasa kwa upande wa Zanzibar kwa sababu wajumbe wengi wa UKAWA wanatoka Zanzibar!!

Baada ya kuona haiwezekani kupata hiyo 2/3 ilibidi Mboyzia Sitta alazimishe upatikanaji wake kwa kuchakachua ( Samahani kwa msamiati mpya kwako). Kasababisha mzee wa watu kumwaga machozi hadharani kwa kumuorodhesha kuwa amepiga kura ya ndiyo wakati sivyo. Kioja kikubwa zaidi mama yake na Zitto Kabwe( Mwanasiasa anayejaribu kufuata nyayo zako ktk baadhi ya mambo) Marehemu Bi Shida Salum kuhesabiwa amepiga kura tena ya wazi wakati tumempumzisha mama yetu katika nyumba yake ya milele tangu julai mwaka huu!!

Ndg yangu Kambarage yako mengi sana ya kukuandikia na kukujulisha yanayoendelea huku, nakuahidi kuwa nitakuandikia tena!!

Katika barua yangu ijayo nitakuandikia jinsi wanasiasa wanavyokutumia kama mtaji wao wa kujijenga au kuwabomoa wenzo kisiasa, wanavyojaribu kuitumia familia yako hasa mwandani wa moyo wako Mama yetu Maria Nyerere isivyofaa!! Pia nitakuambia vita ya urais ndani ya chama chako inavyotishia kukiua chama. Lakini sitoishia hapo pia nitakuambia juu ya upinzani hapa kwetu kushindwa kuwa mbadala wa CCM na badala yake kufanya ujinga wa aina hiyo hiyo wanaoufanya CCM!!

Wasalimie makomeredi kama Mandela, Che Guevera, Hugo Chavez, Kawawa, Machel na usimsahau babu yangu mzee Mashoba!!

Wasalaam!!
John Patrick,
LL.B
UDSM!!
 
Back
Top Bottom