Barua kutoka Mbeya: Hapa ndipo tulipofikia kwenye vita dhidi ya rushwa

wanzagitalewa

Senior Member
Jan 25, 2018
128
84
nyerere-5.jpg

Mwalimu Nyerere katika moja ya mizunguko yake kupata maoni ya wananchi mitaani. Mwalimu alifanikiwa sana katika kupambana na rushwa na ufisadi.

Hakuna maendeleo ya kweli yatakayoweza kupatikana bila kutokomeza rushwa, jambo ambalo ni msingi wa haki. Kama Mwalimu Nyerere alivyowahi kusema, “Wakati wa amani; rushwa na hongo ndio adui mkubwa sana wa ustawi wa watu kuliko vita. Ili ufanikiwe, sharti rushwa ishughulikiwe kama uhaini”.

Mara kadhaa nimeandika kuhusu masuala ya rushwa (unaweza kusoma makala zangu za awali hapa na pia hapa). Kila mara nimekuwa nikifurahia kusoma mirejesho maoni kuhusu makala zangu kutoka kwa watu mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii, na wengine barua pepe. Mirejesho hiyo imenifunza jambo moja muhimu sana. Kabla ya kuwaonyesha mataifa mengine kwamba Tanzania inaongoza katika vita dhidi ya rushwa, tunatakiwa kuwaonyesha ndugu zetu, Watanzania wenzetu ambao ndio muhimu zaidi katika hili.

Maoni mengi niliyosoma kuhusu makala zangu zilizopita yalikuwa yamejikita kuhusu namna ambavyo Watanzania wanaichukulia rushwa. Sio wote wanaoamini kwamba CCM inaweza kutoa dawa itakayoponyesha maradhi iliyosababishwa na CCM yenyewe. Na sio wote wanaamini kwamba, serikali inasema ukweli kuhusu kiwango halisi cha rushwa. Kwa mfano wapo waliosema vita dhidi ya rushwa inalenga tu aina fulani ya rushwa na kuacha nyingine. Pia kuna wengine waliniandikia: vita ya rushwa, ni silaha ya serikali kwa wapinzani lakini si kwa wateule wake yenyewe. Wiki hii Transparency International wametoa repoti kuhusu viwango vya rushwa (Corruption Perception Index). Katika ripoti hiyo, Tanzania imefanya vizuri kupambana na rushwa. Jitihada za serikali zimezaa matunda mbele ya macho ya washirika wetu wa kimataifa. Ripoti hii huandaliwa kwa kutumia maoni ya wafanyabiashara kuhusu hali ya rushwa katika nchi husika.

Tukubaliane kuwa, kama washirika wetu wa kimataifa wanaamini matendo ya serikali, hali hiyo inatakiwa kuwa na manufaa kwenye uchumi wetu na jamii kwa ujumla. Lakini, kama nilivyoandika katika makala zilizopita, nilifikiri namna gani wananchi wetu watapokea matokeo ya ripoti hiyo, kinyume na maoni ya wafanyabiashara wakubwa. Muhimu nilipania kuona urari wa maoni katika makundi hayo mawili. Ripoti ya Afrobarometer kuhusu maoni ya wananchi juu yarushwa imethibitisha hili. Ripoti ya Afrobarometer iliwataka Watanzania kutoa maoniyao kuhusu rushwa. Sehemu kubwa ya maoni yao yalikubaliana na yale ya washirika wetu wa kimataifa. Vitendo vya rushwa vimepungua na serikali imefanya kazi kubwa inayoonekana kuhakikisha kwamba inatokomeza rushwa. Katika ripoti hiyo, asilimia 72 ya Watanzania wanaamini kuwa, rushwa imepungua tangu mwaka 2016. Tukichunguza kwa undani zaidi, kuna matatizo ndani ya jamii yetu ambayo maafisa wa serikali pamoja na mawaziri wanatakiwa kuyafanyia kazi kwa haraka sana kama tunataka kuona hali ikibadilika zaidi. Ni matumaini yakuwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Mkuu, na muhimu zaidi, Rais watasoma makala hii.

Asilimia zaidi ya 30 ya Watanzania wanaamini kuna rushwa kubwa katika jeshi la Polisi. Majuzi Rais alisema hili akiwa bandarini, wakati alipokuta magari yale yasiyo na mwenyewe. Asilimia 20 wanaamini kuna rushwa katika majaji na mahakimu. Asilimia 30 hawaziamini mahakama, tuliona mamia wanakwenda kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar kuomba msaada kutatua kesi zao. Cha kushangaza zaidi ni kubadilika kwa imani kuhusu mahakama. Watu wachache ndio wanaiamini mahakama mwaka 2017 ikilinganishwa na idadi iliyokuwa mwaka 2014. Nilisoma makala moja hivi karibuni iliyokuwa ikielezea mbinu watuhumiwa wa rushwa wanazotumia kuchelewesha hukumu katika kesi zinazowakabili. Kila mara inapokaribia kutolewa hukumu katika kesi zao, hutumia mbinu za kurubuni mfumo wetu wa kisheria ili kuficha sura zao.

Ripoti inaonyesha kuwa, zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wanaamini kuwa, matajiri wapo katika nafasi kubwa zaidi kuliko wananchi wa kawaida kutumia rushwa ili kufanikisha jambo fulani. Matajiri wanaweza kumudu kutoa rushwa. Hili linajumuisha kukwepakodi, kutohudhuria mahakamani, kusajili ardhi ambayo hawaimiliki. Ripoti imeonyesha, watu 2 kati 10 wanaamini kuwa, mwananchi wa kawaida anaweza kufanya hivyo. Hatari ya uwepo wa maafisa wa mahakama wanaojihusisha na rushwa inaweza kuthibitishwa na ripoti za hivi karibuni za watu maarufu walioshtakiwa mahakamani. Hatuwezi kuacha matatizo haya yalete madhara kwa wawekezaji ambao wamekuwa wakilipa kodi kubwa serikalini. Tukumbuke kuwa, hatuwezi kushinda vita dhidi ya rushwa kama hatutowalinda mashahidi. Watanzania wengi wanaunga mkono kauli hiyo ambapo asilimia 70 wameiambia serikali kuwa, wanahofu ya kutoa taarifa kuhusu rushwa kutokana na madhara yanayoweza kuwakumba. Njia mbadala ni kwa Watanzania walio wengi kwenda kwa viongozi wa serikali za mitaa kutafuta adhabu za moja kwa moja, jambo ambalo linathibitishwa na utafiti wa Afrobarometer. Watu wanataka kuona mabadiliko chanya kutoka serikali na mahakama, wajihisi wako salama ili kuleta utofauti mkubwa katika vita dhidi ya rushwa. Faraja ni kuwa bado tuna majaji wengi wazuri nchini. Inawabidi kuwa na busara na kuona mbinu zinazotumiwa na hawa wachache wanaotafuta kuwa juu ya sheria. Rais inampasa kuendelea na kasi yake ya kuunga mkono majaji na maafisa wengine katika utendaji wao wakazi. Lakini pia, inapasa kuwalinda wale wote wanaoshiri nao katika kupambana na rushwa.

Vita dhidi ya rushwa imo ndani ya uwezo wetu. Na inatupasa kushirikiana na serikali kutafuta dawa ya tatizo hili sugu katika jamii yetu. Hata kama hatukubaliani nao katika masuala mengine, lakini hili inatupasa kufanya kwa manufaaya Tanzania.

Ndugu yenu

Wanzagi Talewa Nyaronyo

Butiama, Mara (Safarini Mbeya)
 
Back
Top Bottom