Kuna mambo mawili duniani hutokea kwa namna mbili:
1. Kwa kutumia nguvukani yenye msukumo wa ziada kufanikisha jambo husika
2. Jambo lenyewe kufanyika kwa ufanisi mkubwa bila nguvukani kubwa na bila msukumo wa ziada.
Tukiishi kwenye dunia yenye mkanganyiko mkubwa. Kimetokea kizazi cha manabii na mitume wanaotumia nguvu kubwa na ushawishi wa ziada kujitangaza na kutangaza huduma zao. Wanatumia kila aina ya nyenzo kuiaminisha jamii kuwa wao ndio wao na wao ni bora na wa kuaminiwa kuliko wengine.
Akaondokea mtumishi wa Mungu aliyeishi kwa neno, akawa mwaminifu akashika neno, akatenda neno maisha yake yote ya utumishi na huduma kiimani na kiroho. Hakuipa shekeli kipaumbele, wala tamaa za kidunia wala karamu za walafi na vitu vya kujionesha na kujikweza.
Ni baada ya kumaliza utumishi wake ulioacha alama za kutukuka. Mungu akaamua kumkirimu baraka. Huyu mtu bila kutumia nguvukani yoyote tena akiwa porini mbali kabisa na dunia ya kileo yenye miundombinu ya kisasa na kila kitu. Alitangazwa akatangazika hadi nje ya mipaka ya nchi.
Pamoja na uduni wa huduma, ubovu wa miundombinu na kila aina ya shida. Watu maelfu kwa maelfu walipanga foleni kumfuata. Hapa ndipo utambue ya kwamba matendo ya Mungu si ya mwanadamu. Baradhuli hatambuliki mpaka uone matendo yake, na hata maneno yake.
Usisahau na maono yake pia. Anaweza kuwa msafi na mtanashati akiwa kavaa nguo za gharama na kupanda gari ya kifahari. Lakini atakaponena ama kutenda ndio utamtambua yeye ni nani.
Baradhuli ana ndimi mbili. Ya kwanza ya kunena. Ana maneno matamu kama yote na ushawishi wa ajabu mno. Atajipigapiga kifua na kuonesha uchungu wake lakini atakapokuja na ya pili. Midomo na mikono yake vinatisha na ni vichungu kama pakanga.
Hakuna binadamu asiyependa kusifiwa. Hakuna binadamu asiyependa kutambuliwa utu wake. Hakuna binadamu asiyependa kuonekana mwema mbele ya wote. Ni mahitaji ya kiasili mno ya kiumbe mwanadamu.
Lakini roho yako ikiwa imekunjamana utayapata haya kwa kulazimisha na kwa kutumia nguvu kubwa. Ila kama roho yako ni safi nyeupe isiyo na chembe ya ubaya. Utayapa haya yote bure na kwa ukubwa usiomilithilika.
Mioyoni mwa watu, mitandaoni, kwenye vijiwe vya kahawa, kwenye magari kila mahali kila wakati gumzo litakuwa juu yako
Wabaya wako watajitahidi kukuandika vibaya, kukubeza na hata kukukejeli lakini matendo ya mwili hayawezi kuzidi ya rohoni. Jua halikingwi kwa viganja na ukimpiga chura teke unamwongezea hatua.
Ukiwa baradhuli pamoja na utanashati wako wote lakini macho ya rohoni yanakuona unavyoumia na kuteseka sana. Sumu inakudondoka moyoni ukitamani wewe ndio ungekuwa yeye. Usikauke midomoni mwa kila mtu. Mijadala yote iwe juu yako. Kitaifa na kimataifa. Uwe wewe. Wewe. Wewe.
Wahenga walisema HIARI YASHINDA UTUMWA. USILAZIMISHE KUPENDWA.
Jr[emoji769]