Balozi Lukindo : Nilimwandiakia barua Raisi Nyerere anipeleke kijijini.

JokaKuu

Platinum Member
Jul 31, 2006
30,441
55,018
bul2.gif
Ni kutoka Italia alikokuwa balozi
bul2.gif
Nyerere alishangaa na kuhoji ni balozi wa aina gani huyo?
bul2.gif
Akatolewa Italia na kupelekwa Sumbawanga, Rukwa


Mwandishi wetu, Godfrey Dilunga, wiki iliyopita, alifanya mahojiano na Balozi Raphael Lukindo aliyewahi kuwa balozi wa Tanzania nchi mbalimbali zikiwamo Japan, Italia na Urusi na kustaafu miaka michache baada ya kung’atuka kwa Mwalimu Julius Nyerere.

Balozi Lukindo amewahi pia kuwa mkuu wa itifaki nchini. Siku moja alilazimika kufanya 'mizengwe' ili arudishwe nyumbani kutoka Ughaibuni na kupelekwa vijijini; kama alivyosimulia mwenyewe wakati wa mahojiano hayo.


Rais Mwema: Umefanya kazi maeneo mbalimbali ya kiutawala. Umewahi kuwa balozi wa Tanzania katika nchi nyingi. Picha gani jumla kiutawala umeondoka nayo mara baada ya kustaafu?
Balozi Lukindo: Kabla ya kuanza kazi ni lazima mtu useme unataka ufanye kazi fulani namna gain. Kwa hiyo ni kuweka malengo na dhamira zako sawa. Staili ya kazi ni muhimu sana katika kufikia mafanikio.
Mimi nilipoanza kazi mwaka 1960 hapa Dar es Salaam, kuna bwana mmoja mkoloni aliniambia kuwa wewe Lukindo ni mpole kwa hiyo unatakiwa uwe mkali. Sasa mimi kwa kweli siwezi kuwa mkali bila sababu yoyote ile, nikaendelea kufanya kazi yangu. Lakini jambo kubwa ni mtu utumie haki na uwe dhati… kwa Kiingereza fair but firm.
Huwezi kukosea kama utafanya hivyo. Halafu, utawala ni kazi inayoweza kuwa rahisi sana. Kazi ya utawala imerahisishwa kwa sheria za kazi. Kazi yako unapewa, malengo yake ni haya uifanye hivi na hivi na kama umepewa madaraka ya kuongoza wengine, sheria zipo.


Rais Mwema: Unapozungumzia uongozi ni pamoja na masuala ya siasa. Utawala kwa maana ya utendaji unaathiriwa na siasa. Unazungumziaje hili na hasa kuhusika kwako kwenye siasa?
Balozi Lukindo: Mimi sio mwanasiasa, ingawa kazi nilizowahi kufanya zinaingiliana na siasa. Lakini kuingia kwenye siasa kama ubunge au waziri haya mimi sipendi, kwa sababu utalazimika kujihusisha na kundi fulani na lazima uunge mkono masuala fulani ya chama chako au kundi lako bila kujali ni sahihi au ni ya makosa. Mimi haya ya kuunga mkono uamuzi wa pamoja hata kama kuna makosa ndiyo unaonitia wasiwasi sana.


Rais Mwema: Lakini lengo la utawala unaotokana na nyadhifa za kisiasa maana yake ni kutumikia watu…ndiyo msingi mkuu na kiongozi asiye mwoga anaweza kusimamia ukweli. Je, wewe ni mwoga wa kutetea unachoamini kwa sababu tu wengi watapinga?
Balozi Lukindo: Hapana, mimi si mwoga hata kidogo. Nisichopenda ni kutokuwa mwongo. Mimi ni mtu ambaye nitakuwa upande ambao ni sahihi. Sasa katika msimamo wa pamoja kama kundi kunaweza kuwa na uongo na mkalazimika kuutetea. Hicho ndicho nisichotaka kwenye siasa.
Katika mambo ya siasa haya unaweza kuona kitu kipo wrong wewe mwenyewe, lakini kwa sababu tu ya kwenda na kundi la watu unajikuta ukiunga mkono kitu hicho. Sasa nasema hiyo ni ngumu sana kwangu.


Rais Mwema: Hutaki siasa, lakini unayo kadi ya chama gani cha siasa?
Balozi Lukindo: Hapana, sina kadi ya chama na si mwanachama wa chama chochote. Nasema wazi kabisa ; sina kadi ya chama chochote.


Rais Mwema: Viongozi wengi wanaogopa kuamua kinyume cha ushabiki wa wengi…unpopular decision. Kwenye maisha yako ya uongozi umekwishawahi kuamua kinyume cha matarajio ya ushabiki wa wengi?
Balozi Lukindo: Kwa sababu sikuwa katika ngazi ya Baraza la Mawaziri kwenye utendaji wangu, mara nyingi nakuwa na viongozi wenzangu kwenye ngazi niliyopo. Yamejitokeza mambo kwenye ngazi yetu ya uongozi na nikajikuta nikiwa na uamuzi usio kubalika na wengi lakini wenye ukweli na manufaa.
Kwa mfano, siku moja tulikuwa tunajadili masuala ya kuagiza farasi. Wakati nikiwa RDD (Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mkoa) Mwanza na Rukwa, Mwalimu Nyerere alikuwa na mkutano na wakurugenzi wa mikoa pale Ikulu.
Sasa tulikuwa pale RDD na wakuu wa mikoa, Mwalimu akasema (kwa kuchomekea) kwa sababu ya taabu ya usafiri huko mikoani, labda tufanye kwamba mkuu wa mkoa au mkuu wa wilaya ajue kupanda farasi.
Mwalimu alizungumza kama tahadhari tu ya kawaida hivi. Si kama amri. Lakini Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Sokoine, baadaye akachukua hiyo kama agizo na kutaka kutekeleza. Akaagiza farasi waletwe Tanzania!


Rais Mwema: Aliagiza hao farasi kutoka wapi?
Balozi Lukindo: Kutoka Australia. Sasa mimi nikawashauri msifanye haya mambo ya farasi kwa haraka. Farasi ni mnyama anayehitaji matunzo na uangalizi mwingine wa ziada tofauti na wanyama kama kuku au ng’ombe. Kwa hiyo lazima tujiandae kwanza vinginevyo wataletwa hapa na kufa tu.
Basi, tukawa Iringa pale ma-RDD, Waziri Mkuu Sokoine na Katibu Mkuu nadhani alikuwa Kolimba (Horace) kwenye mkutano na akahimiza hiyo kitu ifanyike haraka.
Mimi nikawaambia msifanye haraka haya mambo ya farasi hadi tujiandae. Wakasema hapana, mkubwa (Nyerere) ametuambia tufanye. Nikawaambia mkubwa amesema lakini ninyi ndiyo wataalamu lazima mumwambie kitaalamu na kwa kawaida Mwalimu siyo mkaidi kushauriwa.
Nikawa peke yangu pale kupinga, lakini kweli farasi wakaja lakini walikufa wengi sana. Kwa hiyo mimi siogopi kutofautiana na watu kuhusu jambo ninaloamini ni la maana. Iko siku moja Mwalimu Nyerere alikuwa anaongoza kama mwenyekiti mkutano pale IFM mwaka 1972. Kulikuwa na mawaziri na wakuu wa mashirika.
Sasa viongozi na mabalozi wakiwa wanasafiri kwa ndege kwenda nje hupanda first class (daraja la kwanza). Balozi wa Tanzania, Uingereza, Marekani wanapanda first class na wakati wanarudi baada ya kumaliza kazi yake huko wanaruhusiwa kupanda first class.
Kwa sababu kwanza balozi akienda huko anapokewa na watu wa foreign affairs na anaporudi baada ya kumaliza wakati wake anasindikizwa na watu wa serikali ya nchi ile alikokuwa anafanya kazi. Nchi nyingine ambazo ni tajiri sana mtu anajilipia mwenyewe ngazi ya juu (kwenye ndege), lakini economy class wanapewa Wazungu kwenye nchi nyingine kama Marekani. Sasa mimi nikanyoosha mkono pale…Mwalimu alikuwa anazungumzia masuala ya maendeleo na jinsi ya kudhibiti matumizi ya serikali.
Nikasema sisi jamani nchi masikini, lakini mbona kila kunapokuwa na mikutano mabalozi wanapanda first class? Kila tukija kwenye mkutano wa chama au mikutano mingine, mabalozi wa Tanzania wanapanda first class kila safari, lakini wale wenzetu ambao ni matajiri (nchi tajiri) mabalozi wao wanapanda economy class, na kama atajitokeza mmoja au baadhi yao wanataka first class, basi, wanaongeza fedha zao binafsi.


Rais Mwema: Ni vigumu sana kwa kawaida viongozi wanaponufaika na jambo fulani baadaye kuungana kulikataa. Hali ilikuwaje kwenye mapendekezo yako hayo?
Balozi Lukindo: Baada ya mimi kuzungumza hivyo, akasimama waziri mmoja kupinga akasema Mwalimu siyo kweli. Ilikuwa kweli, lakini mimi nilinyamaza na Mwalimu pia hakutaka kuzungumzia hilo. Basi ikaendelea tu hivyo sijui siku hizi hali ikoje.
Lakini tungepunguza sana matumizi kama tungeweza kuzingatia na kupunguza maeneo ambayo matumizi mengine si ya lazima.
Jingine ni kuhusu nilipokuwa pale Rome (Balozi –Roma, Italia). Mwaka 1974 nilirudi nyumbani na kwenda vijijini kufanya kazi kule Mwanza na baadaye Rukwa kuwa RDD. Watu walidhani kwamba Mwalimu aliniondoa huko Rome kama adhabu na kuja kunipangia kazi kijijini kwenye shida.
Lakini kinyume chake mimi ndiye niliyeomba hivyo. Nilifikiri hivi: Maisha ya balozi yeyote nje ya nchi ni mazuri ukilinganisha na ya hapa nchini vijijini. Na hayo maisha mazuri huko Ughaibuni wanaogharimia ni wananchi wa kawaida hapa nchini ambao wanafanya kazi kwa shida, kulima kwa jembe la mkono na shughuli nyingine ngumu.
Ilikuwa mwaka 1970 marehemu Mloka alipita nilipokuwa balozi Moscow. Alipopita pale nikamwomba nirudishwe nchini Tanzania baada ya muda wangu Moscow kumalizika. Akasema sawa, tutakurudisha nyumbani lakini haikuwa hivyo; kwani baada ya hapo walinipeleka kuwa balozi Roma, Italia.
Nikawa balozi kule mwaka 1971. Nilikuwa balozi wa kwanza pale kufungua ofisi ya ubalozi. Sasa nilipokuwa pale nikajiuliza kwa nini hawakunirudisha nyumbani? Baadaye walinieleza kuwa hawakunirudisha nyumbani kwa kuwa mimi ni mzoefu katika masuala ya balozi, hivyo ni vyema nibaki huko.



Rais Mwema: Huko ubalozini Ughaibuni kulikuwa na chochote kigumu kilichokutia shinikizo la kutaka urejee nyumbani, na hasa ikizingatiwa maisha ya kibalozi ni mazuri mno?
Balozi Lukindo: Nilikuwa naona uchungu kwamba kuna ulazima wa kuja kuwatumikia wananchi vijijini, kushirikiana nao kwenye shida na juhudi zao. Hili ndilo lililokuwa linanisukuma.
Kazi ya balozi niliizoea na nilitaka kuwa katika mazingira mengine na nimezoa kuishi mazingira yoyote ya maisha bila kuogopa. Kwa kweli nikwambie tu kilichonituma na kunichoma moyo wangu hadi nihangaike kurejea nyumbani ni Azimio la Arusha.
Liko kwenye akili yangu kabisa Azimio la Arusha. Mwalimu alipoelekeza watu vijijini, sasa waweze kupata hamasa na wafikie maendeleo. Nikajiuliza mimi nitawezaje kusaidia kitu hicho.?
Sasa baada ya kuona Foreign (Wizara ya Mambo ya Nje) hawanisaidii kunirejesha nyumbani, wakati nikiwa Balozi Roma, Italia, ilipofika Juni 1974 nikaandika barua personally kwenda kwa Mwalimu Nyerere…directly kwake nakala Foreign Affairs (wizara). Wakati huo Waziri wa Mambo ya Nje ni John Malecela. Nao walijitahidi kukwamisha kwa kutoa maoni yao ili nisirudi, Mwalimu alishangaa sana kusikia nataka kurudi nyumbani.
Si kwamba sikutaka kazi ya ubalozi, lakini niliona kwamba nimekaa muda mrefu nje na pia nina hamu ya kushirikiana na wananchi vijijini katika maendeleo yao. Nikamwambia Mwalimu naomba unipe nafasi hiyo.
Nasikia Mwalimu alishangaa sana na akawa anajiuliza; balozi anataka kurudi nyumbani? Balozi gani huyu? Lakini mwishowe nilirudi nyumbani, aliniruhusu Mwalimu. Nikapigiwa simu kurudi.


Rais Mwema: Kazi ya kwanza ulipangiwa wapi baada ya kurudi nchini na ilikuwa kazi gani?
Balozi Lukindo: Nilipangiwa kazi Mwanza kuwa RDD (Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mkoa). Ulikuwa mkoa mkubwa sana. Baada ya pale nikapelekwa Rukwa ambako nilikaa miaka mitatu na nusu. Mwanza nilikaa mwaka mmoja na nusu.
Nakumbuka wakati naondoka Mwanza, Mwenyekiti wa mkoa, Mzee Budodi (marehemu) alitoa taarifa yenye mambo ya kushangaza sana.


Rais Mwema: Ni mambo gani hayo ya kushangaza aliyoyatoa?
Balozi Lukindo: Alisema amekaa na watumishi wa chama na serikali miaka yote hii, na hajawahi kufanya kazi na kuaga mtu ambaye amefikia kiwango cha uadilifu na kufuata miiko ya uongozi kama mimi Raphael Lukindo.



Rais Mwema: Ulijisikiaje kwa wakati huo kutokana na sifa hizo za kizalendo?
Balozi Lukindo: Nilijisikia mnyonge sana kwa sababu hapakuwa na kitu kikubwa nilichokifanya binafsi. Yote niliyofanya tulishirikiana na watumishi wote. Lakini nilisikia kwa wakati huo maoni ya watu wengine wakisifu usimamizi wangu unaotanguliza matakwa ya sheria na taratibu za kazi.
Hiyo haiji hivi hivi tu. Ni principles ulizojiwekea kwenye utendaji kazi na maisha yako kwa ujumla, jinsi unavyoishi na wenzako.


Rais Mwema: Baada ya kutoka Mwanza na baadaye Rukwa nini kilichofuata?
Balozi Lukindo: Niliteuliwa kuwa Mkuu wa Itifaki. Ililetwa telex pale (Rukwa). Mloka (marehemu) akaniambia Mwalimu anataka uje uwe Mkuu wa Itifaki. Akaniuliza unapenda? Nikasema hee, Mwalimu anataka hivyo, mimi siwezi kukataa.
Akaniambia nitafanya kazi hiyo kwa miaka miwili halafu nitakwenda nje (balozi za Tanzania nje ya nchi). Nikaja Dar es Salaam. Ilikuwa kazi ngumu (Mkuu wa Itifaki), sikuwa na mazoea nayo. Pale kulikuwa na wengine wakubwa kwangu kiumri, wengine wadogo na wafanyakazi wengine sikuzoeana nao.
Nilipata ushirikiano mzuri sana, na baada ya miaka miwili nikaambiwa na Salim Ahmed Salim (alikuwa waziri kwa wakati ule) kwamba tunaomba uongeze mwaka mmoja. Mwalimu ameipenda kazi yako, halafu utakwenda nje…nikasema sawa.
Lakini baada ya mwaka mmoja, nikaambiwa ongeza mingine.


Rais Mwema: Katika kazi yako ya Mkuu wa Itifaki, changamoto gani ulikuwa ukikumbana nazo?
Balozi Lukindo: Changamoto kubwa ni kwamba lawama ni nyingi sana. Kukitokea kosa sehemu nyingine, linaangukia kwenye watu wa itifaki. Ile kazi inahusisha kutengeneza programu za ziara za wakubwa wa nchi, wafalme, mawaziri wakuu na wengine.
Yaani anapofika uwanja wa ndege hadi anaondoka unampangia utaratibu wa nani watampokea, vyakula atakavyokula, ratiba ya ziara mikoani na maeneo mengine yote…kila kitu.
Sasa mimi sikuwa mzoefu, lakini wenzangu walinipa ushirikiano mzuri hadi wakasema ni kati ya wakuu wa itifaki wa kiwango cha juu lakini hii si sifa kwangu tu kwa wote tulioshirikiana.


Rais Mwema: Kwenye hiyo kazi ya chief protocol tukio gani kubwa unalokumbuka ambalo lilikusumbua au kukufarahisha kiutendaji?
Balozi Lukindo: Mojawapo ambalo watu wanakosea ni kwamba mimi natengeneza skeleton program halafu nakwenda Msasani kwa Mwalimu kumpa. Siyo Ikulu, alipenda kuwa Msasani. Nadhani alijisikia huru zaidi pale. Nikifika atasema; ooh Chief karibu, basi nampa nakala yake.
Sasa kuna jambo moja ambalo watu wanasema Mwalimu alikuwa mkali, haambiliki…mimi nasema hapana. Mwalimu akiona uko makini, unataka jambo fulani, ukweli ni kwamba atakusikiliza na atakuelewa.
Mimi kwa mfano, wakati mwingine alikuwa mkali na kuhoji; kwa nini hapa iko hivi.. Mimi nilikuwa namwelekeza na kumfahamisha na si kuchukua moja kwa moja kwanza kwamba mawazo yake ndiyo mwisho. Namwelekeza kitaalamu kwamba iko hivyo kwa sababu hizi, na mwisho anaelewa na kukubali.
Anaelewa na kukubali, lakini pia wakati mwingine nikiona yuko sahihi, basi, nafuta mawazo yangu na kuchukua yake. Nilifanya hivyo kwa sababu yeye si mtaalamu wa itifaki.
Lazima ujiweke kwenye eneo lako kama mtaalamu. Mkubwa huko juu kwenye suala hilo anakutegemea wewe umshauri. Wakati mwingine wapo watu wanataka kutoa ushauri utakaompendeza mkubwa moja kwa moja…hiyo ni hatari sana.


Rais Mwema: Tueleze kidogo kuhusu hatari hiyo kwa sababu siku hizi ni dhahiri wakubwa wanapewa ushauri wa kinafiki, na hasa unaowapendeza wao na rafiki zao.
Balozi Lukindo: Ni hatari kubwa. Anaweza kuwa na wrong ideas kwa sababu hawezi kuwa na taarifa za kutosha kwenye masuala yote ya utaalamu.
Unapomwachia na kuchukua mawazo yake (mkubwa) bila kuhusisha utaalamu wako, yeye anaweza kuwa na mtazamo au maoni potofu. Sasa wengi kutokana na msimamo wangu kushauri kwa kuzingatia utaalamu kuna walioniona mimi mtu mkali.
Na wapo mawaziri waliokuwa wakiona kama tunaelewana sana na Mwalimu Nyerere na wakati mwingine wakiniambia nikamwambie mambo fulani yanayohusu kazi zao.


Rais Mwema: Haijawahi kutokea ukiwa kama mtaalamu ukatoa ushauri wako kwa Mwalimu Nyerere na akaupinga?
Balozi Lukindo: Haijawahi kutokea. Mambo madogo haya ya itifaki hayakuwa ya kusuguana. Kusahihisha kidogo kidogo ilikuwapo lakini sijawahi kukwaruzana na Mwalimu katika kazi yangu kwa sababu alikuwa anaheshimu sana ushauri wa mtu ambaye anaamini kwamba anampa ushauri sahihi.
Na hilo ndilo suala la msingi kwenye nchi kuwa na utawala mzuri, kutoa ushauri bila kuogopana.


Rais Mwema: Kwa hiyo uliongezewa muda tena baada ya hapo kwenye hiyo kazi ya Chief Protocol?
Balozi Lukindo: Waliongeza mwaka mmoja na baadaye nilikataa. Kwa hiyo wakataka niwe Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje, lakini nilikataa.
Akaja Butiku (Joseph) akaniomba niwe Katibu Mkuu nikamwambia hapana nimeamua nitoke nje ya nchi. Akaja Abel Mwanga alikuwa Waziri wa Utumishi alikuja na nia hiyo.
Nilikataa na hatimaye wakanipeleka Japan (balozi) mwaka 1983 mpaka 1988 nikastaafu nikiwa huko.


Rais Mwema: Kule Japan ukiwa balozi uliwezaje kuisaidia Tanzania kunufaika kiteknolojia kutoka nchi hiyo?
Balozi Lukindo: Kufaidika…wakati ule mtazamo na malengo yalikuwa ya kisiasa zaidi, uhusiano wa kirafiki. Kutetea maslahi yetu. Mimi nilipokuwa kule nilikuwa naongea ya kwetu kuonyesha kwamba sisi hatupo- hopeless.
Tulionyesha kwamba tuna raslimali zetu kama taifa ambazo pia wao wanazihitaji na hata kama tukiomba msaada kwao si kwa unyonge mno.



Rais Mwema: Tanzania ni nchi masikini, mliwezaje kukwepa huo unyonge wakati wa kubembeleza misaada kwa mfano?
Balozi Lukindo: Siku moja nilitumwa nikaongee na mji fulani. Sasa nikawaambia maofisa huko kabla ya kwenda kwamba nikifika hapo nikakuta picha za watoto wanaoangamia kwa njaa Ethiopia au nchi nyingine Afrika, nitaondoka hakutakuwa na mazungumzo. Nikawaambia tuna shida lakini si kwa kiasi hicho kama inavyoonyeshwa kwenye picha.


Rais Mwema: Lakini huoni kwamba ulikuwa unaficha hali halisi ilivyo kwa sababu tu upo ugenini?
Balozi Lukindo: Kwanza mimi ni Mtanzania, picha zile ni za Ethiopia. Sasa kwa nini image ya ka-nchi kamoja kenye madhara mkitangaze kama ndiyo nchi zote za Afrika?
Hilo ni tatizo la nchi moja si kweli kwamba hata kwetu tuko kwenye hali hiyo. Kwa hiyo ushenzi wa taifa moja hauwezi kuwa ushenzi wa nchi nyingine.
Hata kama wewe unakuja nyumbani kwangu na mimi naomba msaada, sitafunua vitu vibaya vyote kwangu ili kuonyesha udhaifu kwa namna hiyo…hapana.
Kama unaweza kunipa msaada nipe kama huwezi, basi, lakini siwezi kukubembeleza kiasi cha kunidhalilisha utu wangu.


Rais Mwema: Ukiwa balozi tueleze ulivutiwa na jambo gani kule Roma, Italia kwa mfano.
Balozi Lukindo: Ni nchi ambayo watu wakarimu sana. Nilikuwa na rafiki wengi. Siku moja nilikuwa nakula chakula cha mchana na Waitaliano. Sasa Mkuu wa Itifaki huko, Balozi Qont nilikaa kushoto kwake akaniambia unajua sisi Waroma na ninyi Waafrika tunaelewana kuliko sisi na Wazungu.
Kwa hiyo kule utamaduni wao na Afrika kidogo unawiana katika baadhi ya mambo. Sasa Qont akaniambia baba yako anafanya kazi gani? Nikamwabia ni mkulima na sasa amefariki.
Akasema hapana wewe si mkweli hawezi kuwa mkulima. Akaniambia mimi nafikiri baba yako alikuwa chief mkubwa sana. Nikamuuliza kwa nini unadhani hivyo?
Unajua kazi ya ubalozi ilivyo unatakiwa ujiheshimu, sasa akasema tunavyokuona hata sisi tunakuogopa na kuvutiwa nawe kwa jinsi ulivyokuwa makini kwenye kazi zako.


Rais Mwema: Kutokana na kufanya kazi maeneo mbalimbali, unakumbuka jaribio lolote la kukupa rushwa ulilokumbana nalo?
Balozi Lukindo: Ndiyo, nakumbuka nilipotoka nje na kupangiwa kazi kuwa RDD Rukwa, nilikuwa naishi na jirani yangu mmoja hivi mfanyabiashara, Mwarabu.
Huyu siku moja akanifuata na kunialika kwenye chakula cha mchana ili tufahamiane vizuri. Nilikubali, lakini nikamtahadharisha kuwa siku hiyo naweza kuchelewa kwenye chakula hicho kutokana na wingi wa shughuli.
Kweli nilichelewa sana hadi saa 10 lakini nilimwomba radhi kwa kuchelewa na kushindwa kufika. Lakini siku iliyofuata asubuhi sana kabla hata sijaondoka kwenda ofisini alikuja kwangu.Tukasalimiana, na akanipa bahasha imetuna hivi (imejaa pesa). Sikujua kuna nini, nilipokea na kuchungulia haikuwa imefungwa…nikaona pesa nyingi..Wamasai wengi.
Wakati ananipa akanieleza hii ndiyo lunch yako ambayo jana ulishindwa kuhudhuria. Nikamrudishia na kumwambia hii lunch gani na mbona hizi fedha ni nyingi mno kwa chakula cha mchana. Hata kama unanunua hicho chakula, tembo hakimalizi.
Kwa hiyo nikamrudishia na kumtaka aondoke haraka sana. Akababaika na jasho ikamtoka na akaondoka pale. Kwa hiyo utaona alikuwa na sababu nyingine na kwa kweli ile ni rushwa tu na kama ningekubali siku nyingine angenitumia pengine kuvuruga taratibu za kazi ili kufanikisha mambo ya biashara zake.
hs3.gif
 
Nimeipenda sana makala hii. Kuna kitu kimoja nimekiona ambayo ndiyo imeni furahisha kupita chochote. Balozi Lukindo alikua akitambua kuwa yeye katika nafasi yake alikua mshauri wa raisi. Alijua kuna kazi nyingi ambazo Mwalimu asingeweza kuwa na ujuzi nao binafsi kwa hiyo ilikua kazi yake yeye kumshauri na kumshauri vyema. Sasa inaelekea civil servants wengi siku hizi haswa hawa ambao wana deal moja kwa moja na wakuu wa nchi wao kazi yao ni kuwa "Yes men" na kukubaliana na chochote kiongozi atakacho sema. It is a waste of talent, skills & experience for a civil servant to just simply acknowledged everything the president says. Hiyo ni fani yako kwa hiyo ni lazima uonyeshe ujuzi wako. Asante sana Balozi Lukindo kwa kusisitiza hili.
 
I knew Sokoine was a Clown. Ku-import farasi kutumika na wakuu wa mikoa shows what Sokoine was lacking.
 
Hivi huyu Balozi Lukindo ana uhusiano na kina Athanas Lukindo?

Article inaonyesa kuna wazee walikuwa Wa-Nyerere kuliko Nyerere mwenyewe, mpaka Nyerere anashangaa.Sio mabalozi wetu wengine wanalowea mabalozini mpaka wanasahaulika nyumbani.

Huu moyo wa kulitumikia taifa siku hizi hamna.Halafu huyu mzee ana confirm nilichokuwa nasema kila siku hapa kwamba Sokoine alikuwa anafanya mambo kwa mapepe bila kupima kwa kina. Nyerere akikohoa tu "yes men" wake tayari washaona ni tamko lisilopingika. Sokoine ndiye alikuwa Sumaye wa Nyerere.

The more interviews like these are aired the better a picture we get of the Nyerere administration.
 
Nimeipenda sana makala hii. Kuna kitu kimoja nimekiona ambayo ndiyo imeni furahisha kupita chochote. Balozi Lukindo alikua akitambua kuwa yeye katika nafasi yake alikua mshauri wa raisi. Alijua kuna kazi nyingi ambazo Mwalimu asingeweza kuwa na ujuzi nao binafsi kwa hiyo ilikua kazi yake yeye kumshauri na kumshauri vyema. Sasa inaelekea civil servants wengi siku hizi haswa hawa ambao wana deal moja kwa moja na wakuu wa nchi wao kazi yao ni kuwa "Yes men" na kukubaliana na chochote kiongozi atakacho sema. It is a waste of talent, skills & experience for a civil servant to just simply acknowledged everything the president says. Hiyo ni fani yako kwa hiyo ni lazima uonyeshe ujuzi wako. Asante sana Balozi Lukindo kwa kusisitiza hili.
Huwatendei haki ukisema watu wanao deal moja kwa moja na wakuu wa nchi kazi yao ni kuwa "Yes men". Tatizo linaweza pia kuwa kwa wakuu wa nchi wenyewe. Wengine hawataki ushauri wowote wanajifanya wanajua kila kitu. Sitegemei kwamba Mkapa ama Kikwete wako tayari kukubali ushauri kila wanaposhauriwa. Labda Mwinyi aliweza kushaurika!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom