kbm
JF-Expert Member
- Oct 5, 2012
- 5,224
- 1,676
Licha ya kutowahi kufika Rwanda tangu alipoingia Ikulu Novemba 5, mwaka jana, Rais John Magufuli ameendelea kujijengea heshima kubwa nchini humo na mambo matatu yamedaiwa kuwa ndiyo yanayompandisha chati na kumfanya awe gumzo kila kona kiasi cha Rais Paul Kagame kuahidi ‘kuibia’ machache katika uongozi wake.
Mambo hayo matatu yanayombeba Magufuli yametajwa kuwa ni utendaji wake unaojali muda na vitendo; mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi na dhamira ya kweli ya serikali yake katika kuhakikisha kuwa inainua mapato na kudhiditi matumizi ya fedha za umma kwa nia ya kuboresha maisha ya wananchi wake.
Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Ali Siwa, amebainisha hayo wakati akizungumza na Nipashe katika mahojiano maalumu yaliyofanyika kwenye ofisi za ubalozi wa Tanzania zilizopo Nyarutarama Avenue, jijini Kigali mwishoni mwa wiki iliyopita.
Balozi Siwa alisema watu wa Rwanda wamekuwa wakivutiwa na utendaji wa serikali ya Rais Magufuli chini ya kauli mbiu yake maarufu ya “Hapa Kazi Tu”.
Balozi Siwa alisema kadiri anavyoamini, Rwanda ni mfano tu wa moja ya nchi zinazovutiwa na Serikali ya Rais Magufuli na kwamba, baadhi ya Wanyarwanda hulinganisha umakini wake katika utendaji na ule wa Rais wao, Paul Kagame.
Akizungumza wiki iliyopita, Kagame alisema atafuta safari za nje zisizo na manufaa kwa taifa, kama ambavyo Rais Magufuli ameamuru tangu aingie madarakani.
Aidha, Balozi Siwa alisema kasi ya Serikali ya Rais Magufuli katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi ni sababu nyingine inayomfanya Rais Magufuli awe gumzo nje ya mipaka ya Tanzania kwa sababu hivi sasa, watu wa Rwanda wamenufaika kwa kiasi kikubwa na namna vita yake hiyo inayofahamika kama ‘utumbuaji majipu’ ilivyorahihisha uondoaji mizigo yao kwenye Bandari ya Dar es Salaam na kuwaondolea kero mbalimbali zilizokuwapo kwa muda mrefu.
“Uongozi wa Rais (John) Magufuli katika awamu hii ya tano umeleta msisimko mkubwa kwa Wanyarwanda, hasa kutokana na sifa ya utendaji wake ambao kwa hapa Rwanda wanaufananisha na ule wa Rais wao Paul Kagame,” alisema Balozi Siwa.
“Kwakweli wanamkubali sana rais wetu (Magufuli… yeye (Magufuli) na Rais Kagame wanatabiriwa kuwa watafanya vizuri baada ya kuonekana kuwa wako tayari kuendeleza ushirikiano wa karibu kwa faida ya mataifa yote mawili.”
Akieleza zaidi, Balozi Siwa alisema mabadiliko makubwa kiutendaji yaliyotokea kwenye Bandari ya Dar es Salaam kwa kipindi kifupi baada ya Rais Magufuli kuapishwa ni jambo kubwa ambalo watu wa Rwanda wanalichukulia kuwa ni dalili nzuri ya kuwapo kwa dhamira ya kweli ya kukomesha rushwa na ufisadi unaokwaza shughuli nyingi za maendeleo.
“Bandari ya Dar es Salaam imempa sifa kubwa Rais Magufuli. Kuibua kwake machafu yaliyokuwa yakifanyika na kuendelea kuisafisha bandari hiyo kumewafurahisha Wanyarwanda wengi.
“Ufanisi wa bandari unaonekana sasa ni mzuri.
Kinachowafurahisha Wanyarwanda wengi ni jinsi makontena na mizigo yao mingine inavyoshughulikiwa haraka na kwa ufanisi. Wengi wanakiri kwamba hivi sasa wanapata huduma bora bandarini Dar na pia usalama wa mizigo yao ni wa hali ya juu,” alisema Siwa.
Akieleza zaidi, Balozi Siwa alisema hivi sasa wafanyabiashara wengi wa Rwanda wamejawa na imani kubwa na Tanzania kutokana na kazi iliyoanza kufanywa na serikali ya Rais Magufuli.
“Wanyarwanda hivi sasa wana imani kubwa na Bandari ya Dar es Salaam na jambo hilo lina faida kubwa kwa Tanzania na kuwaletea unafuu wananchi wa Rwanda.”
Akifafanua kuhusu vita dhidi ya rushwa, Balozi Siwa alisema kinachowavutia Wanyarwanda wengi ni kasi ya Magufuli katika kupambana na tatizo hilo linalotajwa kuwa ni moja ya vikwazo vya maendeleo katika nchi nyingi barani.
“Rais Magufuli anapambana kwa kasi kubwa. Tawala za nyuma pia zilipambana na rushwa, lakini kinachofanywa sasa na Rais Magufuli ni kuhakikisha kwamba vitendo hivyo (vya rushwa na ufisadi) vinadhibitiwa kwelikweli.”
Akizungumzia vitendo hivyo nchini Rwanda, Balozi Siwa alisema siyo tatizo kubwa kwa sababu mikataba mingi yenye maslahi kwa taifa huwekwa wazi na kila mmoja kujionea.
“Kwakweli rushwa nchini Rwanda siyo kubwa. Labda tuseme ni rushwa ndogo ndogo. Mikataba imekuwa wazi na tena ni mambo ambayo yamekuwa yakishughulikiwa kwa muda mfupi na hivyo kumekuwa na mianya midogo ya rushwa,” alisema.
Tangu Rais Magufuli alipoingia madarakani baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka jana uliompa ushindi wa asilimia 58.46 ya kura halali zilizopigwa, hajawahi kutoka nje ya nchi huku pia akipiga marufuku safari holela alizodai hugharimu taifa mabilioni ya fedha zinazoweza kutumiwa kwa shughuli nyingine za maendeleo.
Licha ya kutowahi kusafiri nje, vyombo mbalimbali vya habari vimekuwa vikiripoti kila mara kuhusiana na namna serikali yake inavyodhibiti matumizi holela ya fedha za umma, kuzuia safari holela za Ulaya na pia kuwaondoa madarakani wakuu wa taasisi mbalimbali za umma wanaodaiwa kukosa kasi anayoitaka katika kuwaletea wananchi maendeleo.
RWANDA WATARAJI MAKUBWA ZAIDI
Katika hatua nyingine, Balozi Siwa alisema licha ya kuvutiwa na kasi ya Rais Magufuli, Wanyarwanda wana mambo kadhaa wanayoamini kuwa yakifanyika yatazidi kuongeza fursa za kiuchumi miongoni mwa nchi yao na Tanzania.
“Kwanza, Wanyarwanda wangependa kuona barabara ya Dar es Salaam hadi Rwanda inakamilika na kuunganisha mataifa hayo.
“Wanataka kuona vikwazo barabarani vinaendelea kupunguzwa. Mwaka juzi walikuwa wakilalamikia vizuizi 15 vilivyokuwapo kwenye barabara kuanzia Dar mpaka Rwanda.
Lakini Serikali ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, iliwasikia na kupunguza vikwazo mpaka kubaki vitatu na sasa wangependa kuona kinabaki kimoja,” alisema.
Balozi Siwa alisema jambo la pili ambalo wananchi wa Rwanda wangependa kuona siku moja linafanikiwa ni kukamilishwa kwa mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Rwanda.
“Wangependa kuona reli ya Dar es Salaam hadi Rwanda inakamilika. Hicho ndicho wanachokisubiri kwa hamu kwa kuwa wanaamini usafirishaji utakuwa salama zaidi, wa gharama nafuu na hivyo bei za bidhaa zitapungua na kupunguza pia ukali wa maisha.”
FURSA ZA KIUCHUMI
Balozi Siwa alisema Rwanda ina fursa nyingi za kiuchumi kwa wafanyabiashara wa Tanzania.
“Fursa zilizopo zinahitaji uwekezaji mkubwa... zipo katika maeneo ya kilimo, ujenzi, elimu na hata ufugaji,” alisema.
Aliongeza kuwa hivi sasa, Wakenya wamewekeza zaidi Rwanda katika eneo la elimu kwa sababu tayari wana vyuo vikuu vitatu wakati Tanzania ina chuo kimoja tu, ambacho ni Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT)
FUNZO RWANDA
Balozi Siwa alisema licha ya Rwanda kuonekana kuwa nchi ndogo, lakini yapo mengi ya kujifunza kutoka kwao, hasa kuhusiana na namna ya kutunza amani na utulivu wa nchi na pia njia bora za kupiga vita umaskini.
“Rwanda ni nchi ndogo. Lakini baada ya mauaji ya kimbari mwaka 1994, Watanzania na raia wa nchi nyingine wanaweza kujifunza mambo makubwa mawili, kwanza kufanya maamuzi kwa faida ya taifa lao huku wakiwashirikisha zaidi wanawake kwa kuwapa nafasi kubwa za uongozi.
“Pili, ni kujifunza namna ya kubuni miradi mbalimbali ya maendeleo inayowagusa watu moja kwa moja. Hili linasaidia katika kuongeza kasi ya vita dhidi ya umaskini,”alisema Balozi Siwa.
NIDHAMU, UTII WA SHERIA
Balozi Siwa alisema miongoni mwa mambo ambayo Watanzania wanapaswa kuiga kutoka Rwanda kama watu binafsi ni nidhamu na utii.
“Tunachoweza kujifunza ni kuwa na nidhamu katika kila jambo na utii wa kufuata sheria. Mambo mengine tunayoweza kuiga ni bidii ya kazi na uzalendo wa hali ya juu kwa taifa lao,” alisema Balozi Siwa na kuongeza:
“Wanajisifia kwa hatua wanayopiga kulijenga taifa lao. Kinachowapa jeuri ni kupenda taifa lao. Pia utii wa sheria ni mkubwa… mfano, ukipanda usafiri wa bodaboda, lazima dereva na abiria wake wavae kofia ngumu.”
HALI YA MAISHA RWANDA
Alisema kwa ujumla, hali ya maisha ya jiji la Kigali na sehemu nyingine za Rwanda ni ya juu kuliko ilivyo katika maeneo mengi ya Tanzania kwa sababu nchi yao ipo mbali na bahari na hivyo, vitu vingi huuzwa kwa bei ya juu baada ya kusafirishwa kwa gharama kubwa.
“Vitu vingi vinauzwa kwa gharama kubwa kulinganisha na nchini kwetu. Chakula pekee ndiyo bei nafuu kwasababu wanakizalisha wenyewe kwa wingi kupitia shughuli za kilimo,” alisema.
WASTANI WA BEI YA BAADHI YA BIDHAA JIJINI KIGALI KWA SHILINGI YA TANZANIA
Bidhaa Bei
Mchele kg 1 2,700
Sukari kg 1 2,100
Panadol 600
Soda chupa 900
Mkate mdogo 2,100
Mkate Mkubwa 2,700
Unga kg1 1,200
Nyama ya ng’ombe kg1 8,500
Maji ya kunywa lita 1 1,800
Bia ujazo wa ml. 300 1,200
Bia ujazo wa ml. 500 2,400
Bia za nje ml. 300 4,000
Petroli lita 1 2,700
CHANZO: Uchunguzi wa Nipashe Machi 13, 2016
ELIMU BURE NDOTO RWANDA
Balozi Siwa alisema kati ya mambo ambayo Magufuli anawashangaza Wanyarwanda ni pamoja na serikali yake kuamua kwa dhati kutoa elimu bure kwa kila mtoto wa Tanzania kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne.
Alisema elimu katika nchi ya Rwanda hugharimiwa, lakini kwa kiasi kidogo cha fedha kisichowakwaza wananchi wao.
Kadhalika, Balozi Siwa alisema baada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, elimu ya msingi na sekondari nchini Rwanda ina mfumo tofauti usiolingana na nchi nyingi jirani ikiwamo Tanzania
“Elimu ya msingi nchini Rwanda hutolewa kutoka darasa la kwanza hadi la sita na sekondari hutolewa kutoka kidato cha kwanza hadi cha tatu. Sekondari ya juu huanzia kidato cha nne na kumalizika kidato cha sita,” alisema Balozi Siwa na kuongeza:
“Licha ya kuwa na miaka michache shuleni, masomo yao kama ya darasa la pili na la tatu yana maudhui mazito, mitaala wanayofuata ni ya nchi za Ulaya na vitabu vingi wanavyotumia ni vilevile vinavyotumiwa barani Ulaya huku lugha ikiwa ni ya Kiingereza.”
Balozi Ali alisema hivi sasa, mbali na Kinyarwanda chao, baadhi ya vijana nchini Rwanda hutumia lugha tatu kubwa za Kiingereza, Kifaransa na Kiswahili.
Kabla ya mwaka 1994, Rwanda ilikuwa ikitumia lugha ya waliowahi kuwa wakoloni nchini humo, Ufaransa. Hivi sasa wanatumia Kiingereza na pia Kiswahili kinapewa uzito zaidi baada ya kujiunga kwao katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), alisema.
UHUSIANO RWANDA, TANZANIA
Kuhusu uhusiano kati ya Tanzania na Rwanda, Balozi Siwa alisema ni mzuri sana na tena ni wa kihistoria. “Miaka miwili iliyopita, uhusiano uliingia dosari kutokana na hitilafu ndogondogo… lakini ndani ya muda mfupi viongozi wa Tanzania na Rwanda waligundua madhara yake na kurekebisha tofauti zilizokuwapo. Hivi sasa uhusiano ni mzuri sana,” alisema Balozi Siwa.
UWEKEZAJI KAMPUNI ZA TANZANIA
Katika jiji la Kigali, zipo kampuni kadhaa za Tanzania zinazofanya shughuli zake na baadhi hujihusisha na uuzaji wa bidhaa ambazo husafirishwa kutoka Tanzania.
Akizungumzia jambo hilo, Balozi Siwa alisema: “Kwenye uwekezaji, Kenya ndiyo waliowekeza zaidi. Baadhi ya kampuni za Tanzania ni pamoja na ya uzalishaji wa magodoro, unga na pia kuna uuzaji mkubwa wa saruji kutoka Tanzania.”
FURSA ZA AJIRA KWA WATANZANIA
Balozi Siwa alisema kuwa kuna fursa nyingi za kazi kwa Watanzania wenye taaluma mbalimbali na kwamba hivi sasa, kuna Watanzania 150 wanaofanya kazi rasmi kwenye taifa hilo na baadhi yao wapo kwenye mashirika ya kimataifa.
“Wapo pia Watanzania wengi waliojiajiri wenyewe kwa kujihusisha na shughuli kama za ufundi magari, ufundi wa umeme na useremala,” alisema.
ULINZI, USALAMA
Akizungumzia hali ya usalama katika jiji la Kigali na kwingineko nchini Rwanda, Balozi Siwa alisema kumekuwa na usalama wa hali ya juu, tena usiku na mchana.
“Usalama katika miji ya Rwanda ni wa hali ya juu sana. Baada ya mauaji ya kimbari mwaka 1994, serikali ya Rais Kagame imejitahidi kuwekeza vya kutosha katika kutunza amani. Polisi na wanajeshi wamekuwa wakitoa ulinzi kila mahali na unapopita mitaani unaweza kushuhudia jinsi kila kona muhimu ilivyokuwa na ulinzi wa kutosha,” alisema.
Mbali na kile ambacho Wanyarwanda walijifunza baada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, Balozi Siwa alisema sababu nyingine ya kuimarishwa kwa usalama ulinzi dhidi ya kundi la waasi walipo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na pia kudhibiti vitendo vyovyote vya uhalifu vikiwamo vya unyang’anyi.
MIUNDOMBINU, UTUNZAJI MAZINGIRA
Balozi Siwa alizungumzia hali ya usafi jijini Kigali na kueleza kuwa kwa kiasi kikubwa, wamefanikiwa kuwa na muonekano wa mazingira unaovutia kwa kuwa hakuna taka zinazorundikwa ovyo barabarani kama ilivyo kwenye miji mingi ya Afrika ukiwamo wa Dar es Salaam.
“Usafi wa jiji la Kigali na Rwanda yote kwa ujumla ni wa hali ya juu. Nchi hii (Rwanda) wana utaratibu mzuri wakufanya usafi kila mwezi. Jumamosi ya mwisho ya kila mwezi huwa ni maalum kwa ajili ya kufanya usafi.
Siku hiyo huduma nyingi husimama na wananchi karibu wote wanapoamka asubuhi hujihusisha na usafi tu,” alisema Balozi Siwa.
“Siku hiyo asubuhi (Jumamosi ya mwisho wa mwezi) huwezi kupata huduma za usafiri, hoteli au nyinginezo mpaka muda ambao usafi utakuwa umemalizika.
“Njia hii imesaidia kuiweka miji yao yote katika hali ya usafi. Pia uwekaji mzuri wa mitaro ya maji umepunguza uharibifu wa miundombinu ya barabara.”
UTALII
Kuhusiana na utalii, Balozi Siwa alisema Rwanda ni nchi yenye eneo dogo na hivyo hakuna vivutio vingi vya utalii kulinganisha na Tanzania. Hata hivyo, vichache walivyo navyo vya kiutamaduni, mbuga ya wanyama na kivutio cha kihistoria hutumiwa vizuri kwa kuvutia watalii mbalimbali ambao husaidia kuwaingizia fedha za kigeni.
“Kivutio kimojawapo maarufu Rwanda ni cha hifadhi ya sokwe. Wakati mwingine wanyama hao huwa wanahamia Uganda, lakini huwa wanatambulika kuwa ni wa Rwanda.
Na kila mwaka, Rais Kagame huandaa sherehe ya kimataifa ya kuwapa majina sokwe wapya wanaokuwa wamezaliwa na hafla hiyo huhusisha mialiko ya wageni kutoka mataifa mbalimbali,” alisema Balozi Siwa na kuongeza:
“Kivutio cha pili kikubwa ni kile cha mbuga ya wanyama ya Kagera. Wakati wa vita miaka ya 1990, wanyama wengi walikufa lakini hivi sasa wameanza kurudi kwa kasi.
Mafanikio hayo yanatokana na ukweli kuwa ujangili haupo katika eneo hilo.
“Kivutio chao kingine ni sehemu ya historia ya mauaji ya kimbari. Watu wengi hutembelea kufahamu kuhusu mauaji ya kimbari yalivyotokea. Makumbusho ya mauaji hayo yapo karibu katika kila sehemu nchini Rwanda,” alisema.
JUMUIYA IMARA AFRIKA MASHARIKI
Balozi Siwa aligusia namna ambavyo Jumuiya Afrika Mashariki inaweza kuimarika zaidi na mwishowe kuwa kiunganishi muhimu cha kiuchumi kati ya nchi za Afrika ya Kaskazini na za Afrika ya Kusini.
Alisema ujio wa wanachama zaidi wapya kama Ethiopia, Sudan na Somalia kama amani itarejea; kuimarishwa kwa miundombinu ya barabara na reli itakayounganisha nchi wanachama; kupatikana kwa nishati ya uhakika ya umeme wa uhakika na pia nchi zote kuunganishwa katika mkongo wa mawasiliano ni miongoni mwa mambo muhimu ambayo yakipatikana yataivusha Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka ilipo sasa hadi hatua nyingine.
Chanzo: Nipashe