Baada ya mama kufariki mtoto alia na kusema

Baada ya mama kufariki mtoto alia na kusema

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Joined
Feb 3, 2009
Posts
43,037
Reaction score
34,742
Maisha na Mikasa

Baba na Mama ndio chanzo cha mateso yangu
lWalipogombana mama akasema mimi si mtoto wa baba
lBibi, wajomba wananidhulumu akaunti na vitu vya marehemu mama
lNisaidieni nipate haki yangu

Na Dalphina Rubyema


"Baba na mama ndio walikuwa wanagombanagombana; ndio wamenifanya niteseke namna hii; kama wangekuwa wanaelewana tangu mwanzoni, kweli nisingekuwa hapa, eti ninaitwa mtoto wa mitaani wakati ... ninapowaona wenzangu wakiwa na wazazi wao, ninawatamani kweli.

... ninapowaona wenzangu wakiwa na wazazi wao, ninawatamani kweli. Wanakaa na familia zao lakini mimi ninatunzwa na watu nisio na ukoo nao.


"...Yaani ukimuona baba na mimi, hutauliza. Tunafanana kweli! Nilivyo, sura yangu haina tofauti na ile ya Baba yeye anayekaa Moshi mjini. Lakini cha ajabu, ninaitwa mtoto wa mitaani. Eti kwa kuwa siku moja mama aligombana na baba na katika ugomvi huo; halafu

mama akamwambia baba kuwa mimi sio mtoto wake; eti baba yangu yupo sehemu nyingine. Siku hiyo hiyo mimi na mama tukaondoka kwa baba wa Moshi Mjini lakini hatukufikia pale, tukapanga chumba eneo la Himo"


"Lakini, mpaka mama anakufa, hakuna siku hata siku moja ambayo alinionesha eti huyu ndiye baba yangu mzazi. Mara kwa mara nikimuuliza anioneshe baba yuko wapi, mara ananiambia yuko mbali, mara nyingine eti anasema amesafiri.


Mama alipokufa, nikawa ninahangaika mno maana kila kitu sasa nilikuwa ninapata kwa tabu huku ninasimangwa. Watoto wenzangu hata wajomba kila mara wananitukana eti mie ni mzigo kwao eti hawakumtuma mama afanye uhuni wake halafu niende kuwasumbua.


Nikateseka teseka mpaka nikaona, heri niende kwa baba yangu yule wa Moshi mjini Nilipoenda yule baba ambaye nilikuwa ninamtegemea, nae akakataa eti nisikae pale eti mimi sio mtoto wake kwa kuwa hata mama alishasema hadharani.


Mhhhh! Tunafanana nae, lakini akakataa kabisa, akasema kama ni kuharibikiwa, mama ndiye aliniharibia maisha tangu zamani.


"Nikaenda tena kwa wajomba zangu ambako mama alikuwa ameacha vitu vyake kabla hajafa. Alikuwa ameacha vitu vingi vingi lakini ninavyokumbuka mimi ni kitabu cha benki na fanicha alizokuwa nazo.


Bibi na wajomba wakakatalia kabisa kila kitu; wakasema eti kile kitabu cha benki kilipotea zamani; wakasema walicho nacho, ni picha ya marehemu mama, na namba ya akaunti."


Maneno hayo ya kusikitisha yalitoka kinywani mwa mtoto George Godfrey (14) ambaye analelewa katika kituo cha kulelea watoto wa mitaani cha Dogodogo kilichopo jijini Dar es Salaam.


Katika mazungunzo na gazeti hili hivi karibuni, mtoto George ambaye ni mwenyeji wa Kotela-Kisambo katika mkoa wa Kilimanjaro, anasema kuwa mwaka ambao haukumbuki alikuwa akiishi Moshi Mjini yeye na wazazi wake Bw. Paschael na Bi. Jacqline Kilenga. Anasema wakati huo aliufurahia uwepo wake pamoja na wazazi wake kwani maisha aliyaona kuwa yenye furaha.


Anasema siku moja wazazi wake walikorofisha na hivyo kukazuka ugomvi baina yao. Katika ugomvi huo, mama yake mzazi alitamka mbele ya mmewe kuwa yeye (George)siyo mtoto wake. Anaongeza kuwa hajui ni kwanini mama yake aliamua kumwambia hivyo mme wake.


Mtoto George anasema kauli hiyo ilimshitua sana baba yake na hata yeye mwenyewe kushangaa kusikia kuwa yule si baba yake hali ndiye anayemfahamu na hata ndiye aliyemzoea.


Lakini kwa vile alikuwa bado mdogo, hakutaka kuwaingilia. Usiku huo huo George aliongozana na mama yake na kuhamia eneo la Himo nje kidogo ya mji wa Moshi ambapo walipanga chumba.


Anasema wakiwa Himo, marehemu mama yake aliweza kupata mimba na kuzaa mtoto wa kike anayeitwa Neema. Baada ya kuona hali ya biashara imekuwa si nzuri (biashara ya kuuza viatu kutoka Nairobi -Moshi), Bi. Jacqline na watoto wake wawili waliamua kuhamia Dar-Es-Salaam walipokaa kwa kipindi kisichopungua miaka miwili.


Mtoto George anaongeza kuwa mama yake alipigiwa simu toka Moshi kuwa mmewe amefariki.


Anasema, "Tulipopata taarifa hiyo, mama akaniambia kuwa huyo aliyefariki ndiyo baba yetu kabisa mimi na Neema. Huyo mtu alikuwa anaitwa Lodi Godfrey. Nilishituka kweli . Wewe utajifikiriaje kama muda wote huo nilikuwa ninamfahamu Paschael huyo anaye kaa Moshi Mjini. ndiye baba, halafu leo ananiambia...


Mimi nilijua kuwa hata siku ilea mama aliposema kuwa mimi sio mtoto wa Pashael, nilidhani alikuwa na hasira tu, ndiyo maana akasema hivyo; sikuamini eti anasema ukweli.

Sasa nikabaki kwenye mataa sasa sijui baba ni yupi kweli," anasema na kuongeza,

"Nilimuuliza mama kama kweli huyo aliyefariki ni Baba yangu kweli ama ni baba yake Neema. Mama akasema eti ni baba yetu wote mimi na Neema."


George ambaye anasoma darasa la tatu katika shule ya Msingi Mburahati anasema, "Basi, mama akaenda Moshi kwenye msiba lakini aliporudi tu, naye akaanza kuumwa.


George anaongeza kusema kuwa kwa vile hawakuwa na mtu wa kuwahudumia, ilibidi warudi Moshi kwenye chumba chao cha Himo lakini muda si mrefu, mama yao alifariki dunia.


Anasema baada ya mama yao kufariki yeye na mdogo wake Neema walianza kukaa kwa bibi yao mzaa mama Bi. Beatrice Bita (naye sasa ni marehemu) eneo la Himo pale pale lakini maisha ya pale hayakuwa mazuri kwani masimango kutoka kwa wajomba na Bibi

yao mwenyewe yalianza kuota mizizi na kushamiri siku hata siku.


Anasema hali hiyo ilimfanya yeye atoroke na kwenda Moshi mjini kwa Bw. Paschael na kufika pale alikuta ameshaoa mke mwingine ambapo baada ya kukaa kwa kipindi cha mwaka mmoja mama yake wa kambo alimgeuka na kuanzakuwa anamsingizia mambo

mbalimbali kwa kusema maneno ya uongo kwa baba-ke (Paschael) hadi Paschel mwenyewe akamtaka aondoke nyumbani hapo kwa madai kuwa mamake amemharibia maisha kwa kutamka kuwa yeye siyo baba yake.


"Baba yule aliniambia niondoke kwake, eti mama ndiye aliyeniharibia maisha, kwa kweli kweli maskini nikaona aibu kwelikweli hata pia nikajisikia vibaya . Sasa nikasema nitaenda wapi kama huyo ananifukuza na huku ndiye ninaona tunafanana naye. Huyo Godfrey mimi nilikuwa simfahamu hata sura," alisema George huku akionekana mwenye majonzi.


Katulia kidogo kisha George akaongeza kuwa baada ya hapo alienda tena Himo kwa bibi yake ambapo baada ya kuona kuwa hakuna mpango wa kusomeshwa alipanga mipango ya kutorokea jijini Dar es salaam ambapo alipokelewa kwenye Kituo cha Kulelea Watoto wa Mitaani cha Dogodogo. (Dogodogo Center)


Mahojiano baina ya Mwandishi na mtoto huyo yalikuwa kama ifuatavyo
:


Mwandishi:
Goerge; hivi nyie mlizaliwa watoto wawili tu, ama kuna ndugu wengine?


George:
Hapana, yupo kaka yetu mwingine; mama mmoja, baba tofauti. Yeye ndiye wa kwanza kwenye tumbo la mama yetu. Anaitwa Songoo.


Mwandishi:
Sasa huyo Songoo si anaweza kukusaidia zaidi kuliko kukaa hapa Dogodogo Center na kuitwa mtoto wa mitaani unaishi katika hali kama hii?


George:
Kwa kweli dadangu, huyo Songoo mwenyewe hata alipo sikujui, isitoshe hata kama ningekuwa nakujua alipo sidhani kama angeweza kunisaidia vya kutosha kama wanavyonifanyia hawa watu wa Dogodogo, wamenipokea na wanaendelea kunitunza vizuri. Shule wananipeleka, vifaa wananinunulia sasa...


Mwandishi:
Je, mama yenu hakuacha vitu vyovyote ambavyo vingeweza kuwasaidia wewe na mdogo wako Neema katika maisha yenu


George:
(Anafuta machozi), Mama aliacha kitabu cha benki chenye pesa nyingi pamoja na viti, vitanda, sufuria, kabati na vyombo vingi lakini Bibi yetu na wajomba walivificha vitu hivyo na kutuambia kuwa vimeibiwa kikiwemo kitabu cha benki ambacho kimebakia picha ya marehemu mama na namba ya Posta.


Mwandishi:
Huyo mdogo wako Neema yuko wapi?


George:
Anaishi ujombani huko huko na nasikia bibi kafariki sasa sijui yeye ana hali gani (anafuta machozi).


Mwandishi:
nasema kuwa baada ya kuona maisha pale Moshi - Himo yamekushinda uliamua kuja Dar es Salaam?


George:
Ndiyo


Mwandishi:
Nauli ya kuja huku Dar-Es-Salaam uliipata wapi?


George:
(Anacheka kidogo) kwa kusema ukweli ilibidi niende kwa jirani yetu pale Himo na kufungua begi lake na kumwiba sh. 10,000 ambayo nilikuja nayo hadi Dar.


Mwandishi:
Ulikuwa mwaka gani?

George: Mwaka 1997.

Mwandishi:
Unasema uliiba pesa! Hujui kama wizi ni dhambi au basi ni kwanini huyo jirani yako hukumwomba pesa na badala yake ukaamua kumwibia?


Geogre:
Ni kweli dada mwandishi najua wizi ni dhambi lakini nilijua nikiomba hawatanipa. Hata hivyo, naomba Mungu anisamehe.

Lakini hata hivyo, lingine ni kwamba kuomba nilishindwa kwa vile nilidhani kuwa nikiomba pesa kwa huyo jirani nitakuwa nimetibua dili hivyo niliona bora nimwibie.

Mwandishi:
Hukuogopa kushikwa ama kuuawa kwa wizi?


George:
(Kimya kidogo)hata mimi sasa nakiri nilifanya kosa hata mbele za Mungu na siku nyingine sirudii.


Mwandishi:
Hapa Dar es Salaam ulifikia wapi?


George:
Baada ya kufika kwenye kituo cha Kisutu nilikutana na rafiki yangu Joel ambaye tunatoka kijiji kimoja naye ni mtoto wa mitaani, nilipomsimulia sababu ya kuja huku aliniambia nisiangaike kuna kituo cha Dogodogo ambapo naye alikuwa akiishi hivyo alinileta hadi hapa ambapo hadi leo naendelea kuishi, wala sikuangaika baada ya kufika Dar.


Mwandishi:
umesema kuwa unasoma darasa la tatu je nani alishughulika kukutafutia shule?


Goerge:
Ni hawa watu wa Dogodogo Senta.


Mwandishi:
Je kwenye mtihani wa kupanda darasa umekuwa wa ngapi?


George:
(Kimya).


Mwandishi:
Je unapendelea masomo gani na kazi gani?


Geogre:
Napendelea masomo ya Hisabati, Kiingereza, Jografia na historia na kazi napendelea yoyote ile itakayoweza kunipa pesa ya kujitunza mwenyewe na mdogo wangu Neema (akaanza kulia tena).


Mwandishi:
Je unatoa ujumbe gani kwa wajomba zako na huyo baba yako Paschael wa Moshi mjini?


George:
Kwa upande wa wajomba zangu nasema hivi mbona tangu mama yetu afariki hawatupatii vitu vya mama; hata kile kitabu cha benki na vingine?

Hata kama Paschael naye amenikataa, kwa jinsi ninavyoona tunafana, mimi najua ndiye baba ingawa sina neno naye maana siwezi kumlazimisha.
MWISHO.

 
Haya mahojihano ya mwaka gani? Ila asante kwa kutujuza migogoro ya familia inavyotesa watoto.
 
Habari bora,,bado naomba JUKWAA LA:MAISHA MIKASA NA USHAURI
 
Unajua kuna baadhi ya wanawake wakikasirika wanawaambia waume zao 'huyu mtoto si mwanao' wakati wanajua ni mtoto wa baba huyo huyo ila wanataka kuwakera wezao ili kutoa hasira zao... Inabidi kujifunza ktk hili!
Wanawake tuache kuropoka wakati wa hasira, na wanaume mjaribu kutafuta ukweli wa jambo na sio nanyi mnachukulia jambo kubwa namna hiyo kimchezomchezo tu!!
 
Siku zote ugomvi wa baba na mama waathirika wakuu niwatoto. Wazazi tusiwe tunaangalia upande wetu tuu. Linapotokea tatizo tujaribu kuwawekea mazingira mazuri watoto kwafaida ya baadae. Mungu atawasaidia hao watoto.
 
Back
Top Bottom