Rubawa
JF-Expert Member
- Dec 25, 2015
- 2,055
- 3,267
Awamu ya tano inavyomtesa Rais wa zamani
Na Ahmed Rajab
KUNA vimurimuri vingi na viini macho visivyosemeka katika siasa za nchi nyingi za Kiafrika. Tunayaona katika nchi hizo aghalabu huwa si hakika ya mambo yalivyo, hasa yale yafanywayo na viongozi wa mataifa hayo.
Tuuchukulie mfano wa Botswana, nchi inayosemekana kuwa na idadi kubwa zaidi ya ng’ombe kuliko wanadamu milioni mbili ushei waishio huko. Nchi hiyo inasifika kuwa ni ya kidemokrasia kushinda zote zilizo katika bara la Afrika, tukiitenga Mauritius iliyo katika Bahari ya Hindi. Lakini hakika ya mambo ni kwamba sifa hiyo haistahiki kupewa Botswana.
La mwanzo la kuzingatiwa ni kwamba tangu iwe huru (Septemba 30, 1966) hadi sasa imekuwa ikitawaliwa na chama hicho hicho kimoja cha Botswana Democratic Party (BDP).
Uchaguzi wa mwisho ulifanywa Oktoba 23 mwaka huu kuwachagua wabunge na madiwani wa serikali za mitaa. Kwa mara nyingine tena, kama ilivyokuwa katika chaguzi zote zilizotanguliwa chama cha BDP kiliibuka na ushindi, kikinyakua viti 38 kati ya viti 57 vya bunge vilivyowaniwa katika uchaguzi. BDP kilijiongezea kiti kimoja zaidi bungeni kuongezea vile ilivyoshinda katika uchaguzi mkuu wa 2014.
Matokeo hayo ya uchaguzi yanatoa funzo kwa wenye kuzifuatilizia siasa za vyama katika nchi za Kiafrika, hususan vyama vilivyo madarakani kwa muda mrefu na vyenye kutikiswa kwa dhoruba zinazotokea ndani ya vyama hivyo. Nina hakika kwamba wapinzani katika nchi kadhaa za Kiafrika, wakiwemo wa Tanzania, wanayatafakari kwa kina yaliyojiri Botswana. Na kama hawakuandaa vikao vya kuutathmini uchaguzi uliopita wa Botswana basi hasara ni yao.
Swali kuu la kuulizwa ni: ilikwendaje hata chama cha BDP cha Rais mpya Mokgweetsi Masisi kikajipatia ushindi mkubwa kiasi hicho? Tukumbuke kwamba katika uchaguzi uliopita wa 2014 idadi ya kura ambazo BDP kilipata zilipungua sana.
Hilo ni swali la msingi kwa sababu BDP kilipata pigo mwezi wa Mei pale Ian Khama, Rais wa zamani wa Botswana na aliyewahi pia kuwa rais wa chama hicho, alipokihama na kujiunga na chama kipya cha Botswana Patriotic Front (BPF) kilichomeguka kutoka BDP.
Kuna baadhi ya wachambuzi walioamini kwamba kwa kukimbiwa na kigogo kama Khama, mtoto wa Baba wa Taifa wa Botswana na muasisi wa BDP, chama hicho kilikabiliwa na hatari ya kudhurika kwa kupoteza wabunge wengi. Hilo halikutokea.
Badala yake, kama tulivyokwishagusia, BDP kilijiongezea mbunge mmoja. BPF, chama cha Khama, kilishinda viti vitatu tu vya bunge na vyote vilikuwa viti vya majimbo ya uchaguzi yaliyo kwenye ngome kuu ya Khama, katika eneo la Central District ambako ni kwao Khama pamoja na kwa watu wake Wabamangwato.
Isitoshe, hata kiongozi wa BPF, Biggie Butale, alishindwa alikogombea katika jimbo la uchaguzi la Tati West.
Kwa kupata wabunge watatu, BPF kiliishika nafasi ya tatu kikipitwa na Umbrella for Democratic Change (UDC), muungano wa vyama vya Botswana National Front, Botswana Movement for Democracy na Botswana People’s Party). Muungano huo uliojinyakulia viti 15 vya bunge ulivipoteza viti vitatu miongoni mwa viti ilivyoshinda katika uchaguzi wa 2014.
Masisi ni rais wa tano wa Botswana. Wa kwanza alikuwa Sir Seretse Khama, babake Ian Khama, aliyetawala tangu 1966 hadi alipofariki 1980. Sir Seretse alifuatiwa na Quett Masire (1980-1998), Festus Mogae (1998-2008) na Ian Khama (2008-2018).
Awamu ya tano ya urais wa Botswana ilianza kuingia ukorofi mwezi mmoja tu baada ya Masisi kuapishwa kuwa Rais mpya, Aprili mwaka jana. Ukorofi wenyewe ulikuwa mzozano baina yake na Khama. Kilichochongea mzozano huo ni hatua ya mwanzo aliyoichukua Masisi baada ya kuapishwa kuwa Rais. Alimfukuza kazi mkuu wa idara ya usalama (DSI), Isaac Kgosi.
Khama na Kgosi wametoka mbali. Kwa muda mrefu walipokuwa wote wawili jeshini, Kgosi alikuwa msaidizi wake Khama. Akimhudumia kwa mambo mengi. Akimfulia na kumpigia pasi nguo zake, akimtandikia kitanda, akimsafishia viatui vyake na mambo kama hayo.
Kwa kumwachisha kazi asiwe mkuu idara ya usalama, Masisi alikuwa akicheza na moto. Machoni mwa Khama, Masisi alifanya dhambi kubwa. Kgosi akilindwa na Khama mwenyewe. Alikuwa miongoni mwa wale waliodhaniwa kwamba hawawezi kuguswa na yeyote kwa lolote walifanyalo. Kwa miaka mingi alikuwa akitamba chini ya mbawa za Khama.
Kisha Kgosi akitisha. Akiwatia watu hofu na idara yake ikiogopwa, hasa kwa vile watumishi wake wakitembea na silaha na walikuwa tayari kuzitumia.
Tukiviacha vitisho vyake kuna jengine lililomponza Kgosi. Amekuwa akigubikwa na shutuma nzito za ufisadi. Shutuma hizo zimekuwa zikimuandama tangu Khama alipokuwa Rais.
Hivi karibuni palitokea maajabu kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Gaborone pale Kgosi aliyekuwa anarudi kutoka safari ya nchi za Arabuni na India, akiandamana na mkewe na watoto wao, alipokamatwa kwa izara na kutiwa pingu.
Serikali ilisema ilimtia nguvuni kwa kosa la jinai la kukwepa kulipa kodi. Kuna uvumi kwamba Kgosi anaandamwa pia kwa shutuma za ufisadi wa hali ya juu. Na si yeye tu bali pia washirika wengine wa Khama. Kambi ya Khama imeingiwa na hofu kwamba Masisi anaanza polepole, lengo lake likiwa kumnasa Khama kwa shutuma za ufisadi.
Tetesi zilizoenea katika ngazi za juu za BDP ni kwamba usuhuba baina ya Khama na Masisi ulianza kuharibika baada ya Masisi kumuendea kinyume Khama. Inavyosemekana ni kwamba Khama alipomteua Masisi awe makamu wake na mrithi wa urais, walikubaliana kwamba Masisi atapokuwa Rais atamteue nduguye Khama, Tshekedi Khama, awe makamu wake.
Baada ya kuapishwa, Rais Masisi alimgeukia Khama kwa kuyapuuza mapatano yao kuhusu uteuzi wa makamu wa Rais. Badala ya kumteua Tshekedi Khama, Masisi alimteua Slumber Tsogwane, waziri wa zamani wa serikali za mitaa na maendeleo ya vijijini, awe makamu wake. Tsogwane ni mkimya, hana mbwembwe na hajitwezi.
Masisi pia amezibirua sera kadhaa za Khama. Kwa mfano, wakati Khama alipokuwa Rais watu kadhaa walio raia wa kigeni walinyimwa ruhusa ya kuingia Botswana. Kadhalika, kuna raia wakigeni waliokuwa wakifanya kazi nchini humo waliofukuzwa na kurudishwa makwao. Haijulikani kwa nini hasa wageni hao walifukuzwa nchini. Tangu Masisi ashike madaraka hatua kama hizo za kufukuzafukuza wageni hazichukuliwi tena.
Wakati Masisi alipokuwa anaonesha dalili za kujizatiti madarakani kwa kuchukua hatua alizohisi yeye kuwa ni sawa, huku nyuma pande la kina Khama ndani ya BDP lilikuwa linaandaa mkakati wa kumpindua ndani ya chama. Wafuasi wa Khama walimpanga mwanahabari wa zamani aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya nje, Dk. Pelonomi Venson-Moitoi, achuane na Masisi katika uchaguzi wa urais wa chama. Hawakufua dafu.
Desemba 17, 2018 bibi huyo alitangaza kwamba atagombea urais wa BDP. Siku ya pili yake Masisi alimfukuza uwaziri. Aprili mwaka huu Venson-Moitoi alimwandikia barua katibu mkuu wa BDP akisema kwamba anajitoa kutoka kwenye uchaguzi huo kwa sababu “ulichakachuliwa” tangu mwanzo. Halafu pakazushwa utata juu ya uraia wake. Ilimradi ni yayo kwa yayo, ya huku na ya huko.
Kweli chama cha BDP kilitikisika kwa mgongano baina ya Khama na Masisi lakini hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa chama hicho kufikwa na mtikisiko kama huo. Mivutano mikali yalikwishawahi kutokea ndani ya chama hicho. Vigogo kadhaa walikiacha mkono na baadaye walirudi na kupokelewa. Ni mithili na tunayoyashuhudia ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), chama kikongwe kinaichotawala Tanzania licha ya kwamba kinajikokota.
Khama na wafuasi wake wamekuwa wakihoji kwamba alikuwa Rais aliyeustawisha utawala mwema. Wanakumbusha kwamba alisimama kidete kuupinga utawala wa kimabavu wa Robert Mugabe nchini Zimbabwe nchi mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Hata hivyo, kuna wenye kumlaumu Khama mwenyewe kwamba yeye pia akitawala kimabavu na akiruhusu ufisadi, ingawa kulikuwa na kuzidiana kati yake na Mugabe. Mahasimu wake dani ya BDP wanahoji kwamba namna Khama alivyokuwa akitawala ndio sababu ya chama hicho kukimbiwa na wanachama wake na kukosa wingi mkuu wa kura katika uchaguzi wa 2014.
Baada ya kuuacha urais wa BDP, Khama alishindwa kumdhibiti Masisi ndani ya chama. Alijikuta ametengwa na kila alipokuwa akijaribu kujizatiti alijikuta akipigwa chenga na Masisi. Mtandao wa Khama ndani ya BDP haukuwa imara kama alivyodhania. Na Masisi akimbana kila upande.
Nje ya BDP Khama alishindwa kuufanya upinzani mpana wa Botswana uwe pamoja naye. Bila ya vyama vya upinzani kuungana na kuwa kitu kimoja ni muhali kwa chama kama cha BDP kung’olewa madarakani. Kuna hila nyingi zinazotumiwa na vyama vya aina hiyo kuselelea madarakani. Vinaweza vikashindwa kwa urahisi lakini pale tu upinzani unapokuwa imara kama tulivyoshuhudia Kenya, Lesotho, Malawi na Zambia.
Mwezi uliopita, Masisi alitoa wito akimbembeleza Khama “arudi nyumbani”, yaani arejee ndani ya BDP, chama alichokiunda baba yake na kilichoutetea uhuru wa Botswana. Khama alijibu kwa kusema kwamba hicho chama chake cha zamani “kimekufa”.
Chanzo: Raia Mwema
Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab