Stori: Richard Bukos na Issa Mnally, IJUMAA
D AR ES SALAAM: Siku za mwisho?! Askofu wa Kanisa la Jesus Deliverance Center (JDC) linalotumia kauli mbiu ya Mlima wa Matengenezo ya Maombezi lililopo Tabata- Matumbi Dar, Derik Mathias amefikishwa kwenye dawati la Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’ ya Global Publishers akidaiwa kutaka penzi la mtoto wa mzee wa kanisa lake (jina linahifadhiwa kwa sasa).
SIMU YAPIGWA OFM
Ilikuwa Februari 8, mwaka huu ambapo mtu mmoja aliyejitambulisha kuwa ni muumini wa kanisa hilo, alipiga simu chumba cha habari ya Magazeti Pendwa ya Global na kuomba kuongea na Kamanda wa OFM.
“Kamanda wa OFM, kuna askofu mmoja anaitwa Derik Mathias wa Kanisa la Jesus Deliverance Center, Tabata Matumbi ambaye amekuwa akimsumbua binti mmoja wa mzee wa kanisa lake mwenye miaka 15 akimtaka penzi licha ya binti huyo kumkatalia akimwambia yeye ‘bado mdogo’.”
HABARI ZAFIKA KWA VIONGOZI
“Kufuatia tabia hiyo, baadhi ya viongozi wa kanisa walimuweka kikao cha siri askofu wao ili kumuonya lakini yeye alisema habari hizo si za kweli.
“Unajua kwa watu wa chini yake kumuweka kikao cha kuhusu mapenzi si sawa lakini walilazimika kwani tabia hiyo ilikithiri kiasi cha kuanza kuona kama kanisa linazama huku sisi tunaona,” alisema mtoa habari huyo.
ALICHUKUA NAMBA ZA SIMU KAMA ASKOFU
Mpashaji huyo aliendelea kusema: “Binti mwenyewe anasema alipoombwa namba ya simu aliitoa akijua ni baba askofu na kwa vile baba yake ni mzee wa kanisa na yeye pia ni muumini wa kanisa hilo, hakuona kama kuna kitu kibaya.”
OFM YAZUKA TABATA, YAONESHWA MESEJI, YACHOKA!
Baada ya taarifa hizo, makamanda wa OFM walisukuma pikipiki yao hadi Tabata na kuonana uso kwa uso na mtoa habari huyo.
MESEJI ZA ASKOFU MWAAA
Mnyetishaji wetu aliamua kuwaonesha OFM meseji za simu kutoka kwa askofu huyo kwenda kwenye simu ya mtoto wa mzee wa kanisa lake.
“Hebu oneni hizi meseji kwanza. Maana sisi tulimuuliza binti, unaposema askofu anakutongoza una maana gani? Isijekuwa anakutumia meseji akisema njoo unywe soda, ukadhani ndiyo kutongozwa,” alisema mpashaji huyo huku akiitoa simu kwa OFM.
MAJIBIZANO
Meseji za askofu huyo zilionesha kuwa, ameondokea kumpenda sana binti huyo hivyo kumtaka wakutane faragha.Binti huyo ambaye mtoa taarifa wetu alisisitiza kuwa ‘bado mdogo’, alimjibu askofu:
“Mimi siwezi kufanya mchezo huo kwa kuwa najua sitaweza. Mimi bado mdogo.”
ASKOFU ACHOMBEZEA
Licha ya majibu hayo, askofu huyo akiwa hajui yuko ‘mikononi mwa shetani’, alimjibu binti huyo kuwa,anaomba amkubalie japo kwa siku moja tu na asingeweza kumfanyia kitu kibaya kwani atakuwa makini.
ASKOFU AENDA MBELE ZAIDI
Katika hali iliyoonekana kuwa, askofu huyo alielemewa na majaribu, alimuita sehemu binti huyo akimtaka wakutane lakini binti akamwambia yuko peke yake nyumbani hivyo angeshindwa.
ASKOFU AITAKA BODABODA
Baada ya jibu hilo, askofu alimuuliza binti huyo kama anaweza kuchukua bodaboda ili amfuate nyumbani hapo lakini binti huyo alikataa akimwambia itakuwa noma.
OFM YATOA ONYO KALI
Baada ya kujiridhisha na ushahidi huo mkubwa wa meseji ikiwa ni sambamba na kuihakiki namba hiyo kuwa kweli ni ya Askofu Derik, OFM inampa siku 7 kuanzia leo (Ijumaa) kuacha mara moja kumsumbua binti huyo vinginevyo, OFM itaingia kazini na kumshughulikia mara moja!