Asante Magufuli kwa kuelewa hoja, sasa fanya kweli

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,739
40,864
Na. M. M. Mwanakijiji

Kwa ufupi kilichotokea jana - kwa wale ambao labda wanahitaji tafsiri zaidi - ni kuwa Rais amesema tuhuma zinazomkabili Mkuu wa Mkoa wa Dar Bw. Paul Makonda hazijamfanya afikilie mara mbili uteuzi wake. Hili nilazime lieleweke vizuri. Ni kweli kuwa Rais ndiye aliyemteua na ni yeye pekee anayeweza kutengua uteuzi wake. Bila ya shaka njia nyingine pekee ya kawaida kuondolewa katika nafasi yake ni kama Makonda atashtakiwa kwa makosa ya uhalifu ambayo yanamfanya apoteze sifa ya kuwa kiongozi wa umma chini ya sheria ya Maadili ya viongozi. Hivyo, Magufuli amesikiliza yote ambayo watu wengi wameyasema, kuanzia ya vyeti (ambalo kwangu nilisema ni dogo sana) na hili la kutumia madaraka vibaya n.k na ameona kuwa bado Makonda anamfaa.

Rais ambaye ndiye mamlaka ya uteuzi imesema ina imani na Makonda na kuwa aendelee kufanya kazi. Hoja ya Makonda kuondolewa imefungwa hapo. Period.

Lakini pia Rais amesema kitu kingine kizuri ambacho wengine tumekipazia sauti; kwamba taifa limejikuta kwa karibu miezi miwili tunazungumza mambo ambayo ni kweli kabisa hayaongezi unga kwenye sufuria, wala kuongeza chaki kwenye shule. Tumekaa kana kwamba tumegeuka na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Wambeya wa Tanzania (JMWTZ). Na kwenye mitandao ndio kabisa tunafuatilia ni udaku, ubuyu, umbeya gani umeingia leo na kwa namna fulani imekuwa ni burudani ya aina yake kwenye inbox za watu mbalimbali. Nani anatuhumiwa nini, nani kalala wapi na nani?

Sasa Rais ameona hili na kauli yake jana imenipa matumaini; kwamba, amewataka wananchi wa Dar-es-Salaam (na bila ya shaka wa Tanzania nzima) kuwa "tujiendeleze katika masuala ya maendeleo, na ustawi wa Watanzania. Tumejielekeza mno kwenye masuala ya udaku, yanayotupotezea muda, ambayo hayatupunguzii hata njaa tuliyonayo, hayatoi matatizo ya msongano katika jiji la Dar-es-Salaam, hayatuongezei hata shibe... haya ndiyo yanachukua muda wetu mwingine." na akaongeza kuwa inatupasa "tuzungumze uchumi na Watanzania na maendeleo yao. Tujiendeleze katika mambo ya maendeleo"

Mimi nakubaliana na Rais na labda niseme labda Rais anakubaliana na mimi pia. Lakini haitoshi kwa yeye kututaka sisi wengine wote tuzungumze mambo ya maendeleo. Haitoshi kwa yeye kutaka watu wa Dar-es-Salaam wazungumze mambo ya uchumi wakati yeye na serikali yake ndio wanawaondoa watu kwenye mazungumzo ya maendeleo na uchumi!

Kama nilivyosema katika makala yangu moja huko nyuma; kwa sisi tuliomuunga mkono na kukataa mabadiliko yale feki kinachotuudhi sana na kukera kwa wakati mmoja ni kuwa tunaanza kuona yale yale ambayo tuliyoyakataa! Matamanio yetu ni kuwa serikali ya awamu ya tano kweli ingejikita kwenye "kazi tu"! Bahati mbaya sasa imekuwa ni "Hapa Mikwara Tu", "Hapa Vitisho Tu", "Hapa Kukomoana Tu" na "Hapa Udaku tu!"

Rais hafanyi tena ziara za kushtukiza, viongozi wengi wanaonekana wamerudi kwenye default position - ya kutegeana, kuangaliana na kusubiriana. Siyo hivyo tu, hata huko juu sijui kama wanataka watu wajadili mambo mengine au la; tangu mwishoni mwa mwaka jana tumezungumza masuala ya Godbless Lema, mara ya mambo ya Zitto, mara madudu gani sijui Bungeni, mara hili mara lile; sasa hao Watanzania watakaa saa ngapi na kujadiliana masuala ya muhimu ya kitaifa au mahali wanapoishi?

Kuna habari kwa mfano huko Dodoma - Makao Makuu ya nchi kuna mahali kina mama wanaambiwa waendee na maji yao kwenye kituo cha afya ambacho kinatarajiwa kuwa hospitali teule kwa sababu kituo hakina maji na sisi tumekaa tunashindana juu ya cheti cheti cheti! Taifa zima! Tumekaa Lissu asigombee asigombee, tunatumia raslimali kumkamata toka Dodoma na kumleta Dar na baadaye kumuachia! Halafu watu wazungumze kuhusu maendeleo yapi? Kwenye eneo hilo hilo Dodoma watu wamejenga mochwari sijui genius gani na sasa haiwezi kutumika kwa sababu imejengwa hovyo na sisi tumekaa kushindana kwenye nani anajua zaidi undani wa chumba cha mwingine!*

Hivyo, na kubaliana na Rais kwamba imetosha kujitoa kwenye mijadala ya maendeleo. Watu maskini wa taifa kama la kwetu "kupoteza" muda ni uhalifu kwa vizazi vijavyo. Watoto wetu wanakaa na kutuangalia tunavyojibishana kwenye luninga na wanatuona tunavyokenua macho tunapopeana mipasho wenyewe tukiamini tunatunishiana misuli! Tunawalaani hawa watoto na uzao wao! Hakuna kiongozi anayezungumzia Maktaba katika kila wilaya au kila kijiji - si mpaka watoto waende maktaba umewahi kuona lini waziri au mbunge ameenda maktaba!? Tunawatendea dhambi isiyosameheka watoto ambao wanahangaika kupata chanzo, tunatenda dhambi isiyosameheka baada ya kuwapa matumaini watoto masuala ya madawati lakini bado tumewalaani kwenye madarasa yasiyo salama na shule ambazo ziko chini ya viwango vya matumizi ya binadamu!

Wakati mwingine tunaafikiria kweli Tanzania ni Dar na hivyo porojo za watu wa Dar zinatakiwa zimeze mijadala ya watu wa Kigoma, Rukwa, Katavi, Singida, Taboda n.k! Kuna watu wanadhani tumelaaniwa, ukweli ni kuwa tunajilaani sisi wenyewe kila kukicha na kupitisha laana hiyo kwa watoto wetu na Mungu aturuhumie tusije kupitisha kwa watoto wa watoto wetu!

Ni kwa sababu hiyo miye nina maombi tu kuwa Raisa ameonesha kuelewa haja ya mjadala wa kitaifa kurudi kwenye masuala ya kitaifa. Basi atengeneze njia.

1. Siyo kila anayembishia awe na ugomvi naye -iwe Bungeni au nje ya Bunge. Aache Bunge lifanye mambo yake.
2. Kesi zile za kisiasa hasa ambazo zinaonekana kukandamiza haki za wanasiasa mbalimbali zifutwe ili watu waendelee na shughuli zao na raslimali zetu zitumike kwenye mambo mengine.
3. Kamata kamata nayo ikome; inapotokea mtu anakamatwa basi iwe kwa kitu ambacho kweli kina uhalifu au tishio la uhalifu ndani yake.
4. Kesi zinazohusiana na uhuru wa maoni na mawazo zifutwe nazo kwani kama alivyosema Rais mwenyewe watu wana uhuru mkubwa wa kusema. Waachwe watu waseme, wale watakaosema vitu vya kihalifu kweli wakamatwe kama ilivyo sehemu nyingine duniani. Tusikamate watu kwa sababu wamesema jambo la kukera au kuudhi hata kama ni la kweli. Tunawapa watu sababu ya kusema mambo mengi na kuyaacha ya maendeleo.
5. Serikali iendelee na shughuli za kusimamia nidhamu, kufanya kazi na utendaji kazi. Tuachane na mambo petty na Rais mwenyewe aoneshe hili. Afanye kama ni kujisahihisha na kuiweka timu yake pamoja. Hakuna sababu ya yeye kuonekana anashindana na watendaji wake kwani inawafanya watu waseme mambo mengine ambayo labda hata hayana ukweli lakini kwa vile wamepewa sababu watasema!

Ni ombi langu kuwa Rais arudi kwenye ahadi zake za uchaguzi, na kuwa alikuwa amesema yeye ni Rais wa wanyonge na wanyonge ni wote; na kuwa alisema hatowaangusha. Ni ombi langu na kilio changu kuwa asituangushe! Kama aliahidi kutukuvumilia ubovu, uzembe, ufisadi n.k basi asionekane kuvumilia fulani fulani. Aliahidi kuwatumikia Watanzania sikumbuki kama aliahidi kuwalingishia Watanzania urais wake!

Na niseme neno moja tu kwa Makonda. Una bahati kuwa Rais ameonesha imani yake kwako. Ni wakati wa wewe mwenyewe kujiangalia, kujisahihisha na kutengeneza ulipobomoka. Usije kukaa na kutegemea imani ya Rais tu ukaamini unaweza kufanya lolote. Kikwete alikuwa na mtu wa karibu kama Kitwana Kondo; na tunajua ukaribu wake na Ditopile lakini tulisema humu sisi wakati ule na sheria ilifuata mkondo. Magufuli amekuacha si kwa sababu unafanya vizuri; amekuacha ili kufunga vinywa vya sauti zilizokuwa zinampigia kelele; amekuacha ili kuwaambia watu "yeye ndiyo alfa na omega wa utawala nchini" kitu ambacho ni kweli. Usichukulie hili kama kukubalika kwake. Sasa hivi unajukumu la kujenga imani ya wananchi unaowaongoza na hasa ambao wamekwazwa na kauli zake ambazo hazijapimwa wakati mwingine ne vitendo vyako ambavyo vinaonekana kutumia madaraka vibaya. Rais kakuambia uchape kazi, tafadhali nenda kachape kazi, tatua matatizo ya watu wa Dar, onesha heshima kwa mkubwa na mdogo (sijui kwanini kijana mdogo hukuweza kujishikia muamvuli wakati umeenda kufungua barabara bandari juzi ile!?). Ni lazima uanze kuonesha unakomaa katika hekima vinginevyo, ukiondolewa au ukiondoka hakuna atakayekusikitikia au kukulia!

Haya turudi kwenye mijadala ya maendeleo:

NB*: WAJAWAZITO NA WAGONJWA WATAKIWA WAENDE NA MAJI HOSPITALI!
 
Dah we jamaa kitambo sana umepoteza unachokisimamia. Sasa unahangaika kutafuta huka na kule!
 
Anatuambia tuache udaku wakati ni yeye juzi aliyesema anapenda SHILAWADU? Inashangaza sana.

BTW leo kwa mara ya kwanza nimesoma bandiko lako lote,naam...unaanza kurudi kwenye ubora wako.
Bila shaka ule mgao wa 'mihogo' umeanza kupungua au umeisha kabisa hahahaaa.
 
Mwanakijiji..Makala nzuri

Lakini Kauli ya Rais haitoshi kuesema eti mjadala umefungwa

Inapobidi rais inabidi awajibike kwa kauli zake...Amechaguliwa na wananchi na aliye Alfa na Omega ni wananchi na sio Rais

Power yake kama ilivyotafsiriwa na katiba inatokana na kura alizopewa na wananchi

Pale ambapo mtu tuliyemchagua kama kiongozi wetu anakengeuka...Jamii lazima tupaze sauti na kumrudisha kwenye mstari.

Makosa yaliyofanywa na makonda ni mengi sana na yanayostahili kufukuzwa mara moja kwenye utumishi wa Ummma

Haki inapaswa kutendeka kama ilivyotendeka kwa yule Mkurugenzi aliyewatisha askari kwa bunduki Morogoro

Haki inapaswa kutendeka kama kwa kitwanga aliyeingia kazini amelewa

Haki inapaswa kutendeka kama ambavyo wale wenye elimu isiyoeleweka walivyofukuzwa kazi

Tunapoongelea Utawala bora na utawala unaofuata Katiba na Sheria hakuna ambaye ni exception....Kila mtu anaguswa nao.

Kipindi hiki ambapo haki ya kuongea imezibwa...uhuru wa kujieeleza umezibwa...Social media ndio imebaki kimbilio la wananchi.....kwa hio kwa kiongozi makini hawezi ku ignore tuhuma zilizo za kweli eti kisa zinatoka kwenye social media.

Huyo sio yeye kama alivyojinadi kuwa anachukua hatua kwa uzembe wowote.

Tunachoshuhudia ni kuwa anaonea watu tu...kumbe hata hasimamii maadili wala hapambani na Rushwa
 
Na bado watu wataendelea na Makonda tu wakata wanajua ata wainame wainuke Makonda atumbuliwi......
 
Taratibu mjomba , Unatueleza Watanzania kuwa kutumia matokeo ya mtu mwingine kujiendeleza kielimu ni Jambo dogo?, Wewe nadhani unaelewa vizuri unachokisema lakini umeamua kujitoa ufahamu katika hilo!. NIKUKUMBUSHE TU KUWA HILO NI KOSA LA JINAI NA KIFUNGO CHAKE NI MIAKA SABA JELA!

Nakubaliana na wewe kuhusu Mijadala, Watanzania tuna haki ya kujadili chochote ilimradi hatuvunji sheria, hakuna mwenye haki au power ya kudictate Watanzania wajadili nini katika hayo wenye haki nayo!. Kama wewe unataka kujadili uchumi fine, jadili uchumi, kama mtu mwingine anataka kujadili mpira fine, wacha ajadili mpira!, Kama mtu anataka kujadili Shilawadu mwache ajadili Shilawadu

Nashangaa katika kuzungumza yote, unajaribu kupiga polish Makosa mabaya kabisa yaliyofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar, This is ridiculous, Nilitegemea Kuwa Ungesimamia Principle ya sheria ni msumeno, Kwamba imani ya Rais kwa Makonda si kinga yake ya Kushtakiwa kwa Makosa aliyoyafanya, Nilitegemea Uungane na wananchi kutaka Makonda ashitakiwe kama wananchi wengine wengi wanavyoshtakiwa kwa makosa kama yale yale aliyoyafanya Makonda,na kama akihukumiwa basi kwa kuwa Rais anaridhika na anamuamini ampe msamaha wa Raisi kisha amteue tena kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, hili limo ndani ya mamlaka ya Raisi.

Lakini huu Ushauri unaoutoa kwa Makonda, Ni kama Ushauri kwa Mtoto Mtundu mwnye Tabia ya Kuwazibua Vibao wageni, halafu anakimbilia kwa baba yake huku analia, Baba anambembeleza kwa kumwambia "Usilie mwanangu eeeh, lakini usirudie tena eeeeh, haya chukua hii elfu kumin ukanunue chipsi na kuku".Nikukumbushe wewe Mwanakijiji MAKONDA HATUHUMIWI KWA MAKOSA YA KAWAIDA YA KIKAZI, MAKONDA ANATUHUMIWA KUFANYA JINAI!

Na unapotwambia kuwa Raisi katika nchi hii ni Alfa na Omega hiyo siyo kweli, Siyo kweli kwa sababu Raisi hana Nguvu za Kuufanya Uongo uwe Kweli au kuufanya Ukweli uwe Uwongo!, Raisi hana Mamlaka kuifanya haki iwe batili au batili iwe haki, Kiufupi Kama kweli tunafuata Utawala wa Sheria nchini basi Haitakiwi raisi kuzuia Sheria isifuate Mkondo wake kama kuna jinai imetendeka!.

Ni lazima Tuseme Ukweli, Msema Ukweli ni mpenzi wa Mungu.
 
Mkuu umeongea vizuri,,umeng'ata na kupuliza, ila nina machache tu ya kukuambia..Ushauri uliompa anayejiita makonda umepotea njia mkuu wangu.
 
Back
Top Bottom