Tatizo la CCM ni kubwa sana na linagusa hata maslahi ya Taifa. Tatizo la CCM linagusa hata tasnia nyingine. Tatizo la CCM linagusa hata vyama vingine vya siasa (Angalia Igunga CUF vs Chadema). Tatizo la CCM linagusa hata imani za watu (Bakwata, KKKT, RC, etc). Kwa maana hiyo, kujadili CCM unajadili mustakabali wa Taifa. Ndio maana hata wapinzani wakisimama wanajadili matatizo ya CCM maana ndio wanashika dola.
Tukirudi kwenye hoja ya kubadili Mwenyekiti wa CCM, tutake tusitake (Japo naona hapa inakwepwa) hii inatokana na mkakati wa kujibu mapigo kuhusu uvuaji gamba uliopangwa kuanza na watu watatu, Rostam Azizi, Edward Lowassa na Andrew Chenge. Bila shaka na bila kuuma uma maneno, ni waandishi wa habari na wana JF ndio ambao walikua wakitaka hatua zichukuliwe na kwa kuanzia waliwataja watatu hawa, lakini ghafla watatu hawa wamepata watetezi wa ajabu na wale ambao wameamua kufuata 'ushauri' wa waandishi na wana JF sasa wanashambuliwa. Jambo la kusikitisha sana ni kwamba ukiangalia thread za nyuma, michango ya watu imebadilika kabisa. Sikatai michango yenye muelekeo wa kisiasa kwa maana mwana Chadema ana haki ya kutetea maslahi ya chama chake na mwana CCM ana haki ya kutetea maslahi ya chama chake, kama ilivyo kwa wana CUF, NCCR, TLP, SAU na wengineo, lakini ni vyema wote wawe na msimamo kwa maana kukumbuka maneno yao ya awali na nini wanasimamia. Siamini hata kidogo mtu ambaye kwa zaidi ya miaka mitano umekua ukimuona 'mchafu', kabla hata ya kujisafisha eti kwa sababu tu anataka kung'olewa anabadilika na kuwa 'shujaa' wako. Naomba tuwe wakweli na tuelewe kwamba uvuaji magamba ni msemo tu tena uliokolezwa na vyombo vya habari na watu wengine (wakiwamo CCM) wakaubeba. Msemo huo ulitokana na hotuba ya JK ambayo alitoa mfano wa nyoka ambaye anajivua gamba lakini humu JF wengi wa wachangiaji muhimu ndio walitaka hawa watu wang'olewe CCM na serikalini na tunakumbuka Chenge alipochaguliwa katika baraza la mawaziri kwa mara ya pilli watu walisema kwamba CCM inajimaliza kwa kuwapa nafasi watu wachafu na ilizungumzwa kwamba Chenge atakuaje kwenye kamati ya maadili ya CCM wakati yeye hana maadili. Sasa anatakiwa kuondoka wanaotaka aondoke wanabezwa na kupewa majina mabaya.
Nape ana udhaifu wake kama binadamu kama ilivyo kwa JK, na wenzake ndani ya CCM. Wote ni binadamu na wana mapungufu yao na penye hoja na wao wajadiliwe lakini kibaya ni pale ambapo wanapozungumzia uchafu wa watu wengine wanajibiwa kwa kushambuliwa, hapo hatujengi. Ni sawa na kipindi ambacho Sitta alipokua anawabana watu bungeni, majibu yake ni kushambuliwa. Ni sawa na polisi anayekamata mwizi, kabla hajamfikisha unaanza kumshambulia kwamba ni mlevi na amwachie mhalifu kwa kuwa na yeye ni mlevi wa kupindukia. Haiwezekani, tumkamate na kumshughulikia mhalifu ndipo turudi kujadili ulevi wa polisi wetu.
Jambo moja la msingi ambalo JK, Nape na wenzake wajue ni kwamba kina Lowassa, Rostam na Chenge wanajipanga na wana mikakati mingi ya kisayansi sana na wana nyenzo na uwezo mkubwa katika kujipanga na kusimamia wanachokitaka, kinyume chake kina JK wanategemea nguvu ya dola na upepo wa kisiasa, mambo ambayo kwa sasa yanazidiwa nguvu na mikakati ya wenzao (kina EL) ambayo inaonekana kwamba wamejipanga vilivyo. Mikakati ya kina Lowassa kwa sasa inazidi kupenya hata kwenye serikali na hata ndani ya vyama vya upinzani na kwenye vyombo vya habari. Wamefanikiwa sana na watazidi kufanikiwa kiasi kwamba wamekua na nguvu kana kwamba ndio wao wanaoendesha serikali. JK na kundi lake wanapaswa kusoma alama za nyakati na sasa imefika mahali wao wamekua wanyonge.Itabidi kina JK wajiulize ikiwa sasa wanakua wanyonge, watakapoondika madarakani watakuaje? Wajiandae kwa mabaya zaidi. Nasikia wameanza kulainika na kuona kwamba salama yao iko mikononi mwa Lowassa akiwa Rais, huko ni kujidanganya na naamini hayo ni mafanikio ya mikakati mizito ya kina Lowassa. Hii sinema ya CCM ni sinema ya hatari sana na ambayo siku si nyingi itakua na matokeo mabaya ambayo hayajawahi kutokea katika historia ya nchi yetu. Baadhi ya mambo yamegusiwa humu katika thread nyingine, ikiwamo ila habari ya kumtahadharisha Membe ambayo nayo ni muendelezo wa mikakati ya kundi fulani kujijengea uhalali na kutisha wengine. Hatari ni kwamba kumezungumzwa mambo yanayogusa uhai wa watu. MUNGU ATUNUSURU tuendako ni hatari.