Ansbert Ngurumo: Maswali Magumu. | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Ansbert Ngurumo: Maswali Magumu.

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Speaker, Mar 11, 2012.

 1. Speaker

  Speaker JF-Expert Member

  #1
  Mar 11, 2012
  Joined: Aug 12, 2010
  Messages: 6,357
  Likes Received: 21
  Trophy Points: 135
  MADAKTARI wamegoma. Manesi hawawezi kufanya kazi ipasavyo. Kwa hiyo, nao wamegoma. Wagonjwa wanazidi kufa. Nani kawaua? Ni madaktari au serikali?

  Serikali inasema madaktari hawpaswi kugoma. Eti wakigoma wataua wagonjwa wasio na hatia. Eti watakaokufa ni wananchi wanyonge, kwa sababu rais na vigogo wenzake watapelekwa India au kokote ng’ambo.

  Kauli hii inaonyesha nia ya serikali kushughulikia madai ya madaktari? Ni kauli ya serikali inayojali? Inaonyesha umakini wa watawala? Na kama ndivyo, hivyo, na wagonjwa wanaendelea kufa; nani kawaua? Serikali au madaktari?

  Watetezi wa serikali wanasisitiza kwa nguvu; kwamba madaktari hawapaswi kugoma, kwa sababu taaluma yao ni nyeti mno. Hata serikali inasema hivyo.

  Lakini unyeti wa taaluma ya daktari unatambuliwa kwa kuwazuia kugoma wanapodai haki? Kama serikali inatambua unyeti huo, mbona haiwasikilizi?

  Mbona haiwapi stahili zao, miaka nenda, miaka rudi? Na wakati malumbano haya yakiendelea, wagonjwa wanazidi kufa. Nani kawaua? Serikali au madaktari?

  Wapo wanaodai kwamba madaktari wanafanya utoto kumtaka rais awafukuze kazi Waziri wa Afya na naibu wake. Eti wanamomonyoa mamlaka ya rais kwa “kumtaka” awafukuze. Eti wangefuata taratibu, kanuni na sheria katika kudai haki zao.

  Eti kwa madaktari kugoma, ni kielelezo kwamba wanajali masilahi yao binafsi kuliko ya wagonjwa na wananchi kwa ujumla.

  Lakini mbona hatumuulizi rais analinda masilahi ya nani kwa kukataa kuwafukuza kazi wateule wake wasioaminika kwa walio chini yao? Na waziri na naibu wake wanajali masilahi ya nini kwa kukataa kujiuzulu wakati walio chini yao wametangaza kutokuwa na imani nao?

  Kama rais na mawaziri wake wanawahurumia wagonjwa; kama hawalindi masilahi yao tu – vyeo walivyonavyo – wanafurahia nini kuona wagonjwa wanakufa, na wao wanaendelea kung’ang’ania nyadhifa zao?

  Kipi bora, waziri mmoja na naibu wake kujiuzulu au maelfu ya wagonjwa kupoteza maisha kwa sababu ya kiburi cha watawala? Kipi muhimu, mamlaka ya watawala yanayoguswa na madaktari au uhai wa wagonjwa unaopotea kwa sababu rais, waziri na naibu waziri wanapenda sana vyeo vyao?

  Na kama kugoma ni kubaya, mbona rais amegoma kuwafukuza wateule wake? Mbona amegoma kutekeleza madai halali ya madaktari? Mbona waziri na naibu wake wamegoma kujiuzulu? Mbona wamegoma kunusuru maisha ya madaktari na wagonjwa?

  Naona wapo wanaodhani kwamba ni busara kwa madaktari kurejea wodini na kuhudumia wagonjwa katika hali duni na dhalili waliyo nayo, inayosababisha wagome.

  Lakini nani asiyejua kwamba wanagoma ili wapewe nyenzo mwafaka za kuokolea maisha ya wagonjwa? Kwa nini hatuelewi kwamba madaktari wanagoma kwa niaba ya wagonjwa?

  Kimsingi, wagonjwa ndio walipaswa kuigomea serikali inayowatoza kodi, halafu inawajengea hospitali zisizo na dawa, zenye madaktari wanaonyimwa haki za msingi na vitendea kazi muhimu.

  Wagonjwa ndio walipaswa kuigomea serikali inayojenga hospitali ambazo haziruhusiwi kutibu watawala na vigogo wengine serikalini. Wagonjwa ndio wanapaswa kugomea hospitali ambazo serikali imezifanya kuwa janga la kitaifa.

  Lakini kwa kuwa afya za wagonjwa ni dhaifu, madaktari wanagoma kwa niaba yao, ili kunusuru maisha yao. Na wanajua – wagonjwa na madaktari wao – kwamba hata bila mgomo wa madaktari, wengi wa wagonjwa hao watakufa tu, kwa sababu hawapati tiba.

  Serikali na watetezi wake hawaoni kwamba hata wakiingia wodini leo, madaktari hawa wenye msongo wa moyo, wataendelea kuua wagonjwa wengi kwa “ruksa” ya serikali?

  Na kama mtu mmoja alivyosema katika mjadala mmoja wa umma, kama gari ni bovu, halina usukani imara, halina breki, tairi zimetoboka ni busara kumlazimisha dereva aendeshe gari hilo na kusafirisha abiria kwenda popote?

  Dereva anayelazimishwa kuendesha gari hilo akigoma kuliwasha, si atakuwa anatetea na kulinda uhai wa abiria? Utetezi na ulinzi huu wa dereva kwa abiria wake, una tofauti gani na ulinzi wa madaktari wa wagonjwa hawa?

  Hata kama serikali imekimbilia mahakamani kuweka pingamizi la mgomo; na hata kama Mahakama Kuu, Kitengo cha Kazi imeamuru madaktari warudi kazini, hukumu hiyo itapata wapi uhalali wa kisheria kuzuia mgomo ambao ulikuwa umeanza kabla haijatolewa?

  Hakika, hii nayo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika. Tulidai uhuru kupambana na kuwashinda maadui watatu: ujinga, maradhi na umaskini.

  Hili la mgomo wa wagonjwa kupitia kwa madaktari, ni ushahidi kwamba adui maradhi amewazidi kete watawala. Anaendelea kuua wananchi wa kawaida; vigogo wanapelekwa India na Ulaya!

  Na hili linaendelea kuhalalisha mgomo huu wa wagonjwa kupitia kwa madaktari. Na mwelekeo wa mambo unaonyesha kuwa lolote litakaloamuliwa na serikali kuhusu mgomo huu, litakuwa na athari kwa makundi mengine ya jamii.

  Baada ya wagonjwa, sasa itakuwa zamu ya wanafunzi. Maana walimu walishagoma siku nyingi. Wanaingia darasani, lakini matokeo ya mitihani yanatuonyesha matunda ya kazi yao.

  Ndiyo! Kama suala ni madaktari kuonekana wodini ili kutekeleza amri, wanaweza kurudi wakati wowote.

  Lakini wengine tunaogopa sana mgomo wa madaktari walio kazini, wasioweza kutibu wagonjwa, bali wanasubiri kusaini vyeti vya vifo vya wagonjwa wanaokufa kwa sababu serikali haitaki kutumia kodi zao kuokoa maisha yao.

  Na hata yote haya yakitokea; hata kama serikali inataka wananchi walaumu madaktari kwamba ndio wauaji wa wagonjwa; serikali imejipangaje kudhibiti matokeo ya hasira za wananchi zitokanazo na vifo hivi vya makusudi?

  Ndiyo, madaktari wanaweza kuonewa kwa sababu taaluma yao ni nyeti, imo miongoni mwa taaluma zinazozuiwa kugoma.

  Lakini ni vema tukumbuke kuwa wananchi hawajawahi kupiga kura kuchagua madaktari wa kuwatibu.

  Kwa hiyo, katika sarakasi hizi, serikali isije ikajidanganya, ikadhani wananchi hawajui nani anaua wagonjwa wetu.

  Ni yule aliyepigiwa kura atimize kile alichoahidi – kile kinachowafanya madaktari wagome sasa. Je, watawala wamejiandaa kukabiliana na hasira za wananchi?
   
 2. Speaker

  Speaker JF-Expert Member

  #2
  Mar 11, 2012
  Joined: Aug 12, 2010
  Messages: 6,357
  Likes Received: 21
  Trophy Points: 135
  Sijui kama anaye takiwa kujibu maswali ya Ngurumo huwa ana jaribu hata kuyasoma tu,
  achilia mbali kuyajibu.

  Sijui kama mgomo wa walimu ni mzuri au vipi,natamani mahakama itoe ufafanuzi juu
  ya mgomo huu wa kimya lakini unao ua elimu yetu.
   
Loading...