Ansbert Ngurumo alipozungumzia maandamano enzi za JK

jingalao

JF-Expert Member
Oct 12, 2011
35,053
28,245
CHADEMA itacheza muziki huu wa JK Jazz Band?

Ansbert Ngurumo

KAULI za Rais Jakaya Kikwete, Waziri wake, Steven Wassira na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, John Chiligati, Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, wapambe wake Augustine Mrema (TLP), John Cheyo (UDP) na Anne Kilango (CCM) dhidi ya maandamano na mikutano ya CHADEMA imedhihirisha uchovu wa kisiasa unaowakabili.

Wote pamoja wamejigeuza kikundi cha sanaa za kisiasa kinachoimba tenzi za watawala dhidi ya wananchi. Uzoefu wao umegeuka ukale usioendana na usasa wa siasa za Tanzania.

Katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi uliopita, Rais Kikwete alilalama kinyonge kwamba maandamano ya CHADEMA yanatishia amani na yanalenga kuiondoa serikali yake madarakani; akaomba wananchi wawapuuze wanasiasa hao wa upinzani.

Wananchi wakampuuza. Wameendelea kuomba CHADEMA iandae maandamano na mikutano mingine katika maeneo yao. Kati ya maandamano na mikutano yote iliyofanyika Kanda ya Ziwa, nimeshuhudia miwili.

Wananchi wanaandamana kwa hiari yao. Hawalazimishwi. Hawanuni. Hawatishani. Hawapigani. Hawakanyagani. Wanaimba nyimbo "za harakati."

Wanasikiliza hotuba za viongozi kwa utulivu wa hali ya juu. Inapobidi wanashangilia au wanapiga makofi.

Kwa vitendo hivi, wanachama na wafuasi wa CHADEMA wamedhihirisha mambo mawili. La kwanza ni amani. Wanaandamana kwa amani, na wanahudhuria mikutano yao kwa amani.

Kwa maana hiyo, mikutano ya CHADEMA haihatarishi amani. Kama kuna amani iko hatarini kwa sababu ya mikutano hiyo, ni amani ya watawala. Amani ya wananchi inalindwa na wananchi wenyewe.

La pili ni majibu yao kwa Rais Kikwete. Hawakuhitaji kumjibu kwa maneno bali kwa vitendo.

Na hili linatufikirisha na kutueleza kwamba amani ya wananchi inakuwa hatarini pale ambapo vyombo vya dola vinaingilia maandamano na mikutano ya wananchi.

Imetokea Arusha. Maandamano yalianza kwa amani. Polisi walipoingilia, kwa msukumo wa kisiasa, ndipo vurugu zikatokea. Hata siku ya mazishi ya mashujaa waliouawa, ambayo kimsingi ndiyo ingekuwa na shari, ilikuwa ya amani na utulivu kwa sababu moja tu &[HASHTAG]#8211[/HASHTAG]; polisi hawakujihusisha na maandamano hayo.

Katika maandamano ya Mwanza, Musoma, Shinyanga na Bukoba, polisi hawakuvuruga maandamano na mikutano ya CHADEMA. Yalifanyika kwa amani.

Kwa mantiki hii, wananchi wamekejeli vitisho vya Rais Kikwete. Na watu wote wenye akili timamu, wanajua kuwa hofu ya JK inatokana na ukweli kwamba &[HASHTAG]#8216[/HASHTAG];amekataliwa na wananchi.'

Rais wa nchi aliyechaguliwa kihalali na anayeamini kwamba anaungwa mkono na wananchi, hawezi kuwa na sababu ya kuonyesha hofu kama hii iliyodhihirishwa na Kikwete.

Anachokiogopa, na kinachosababisha woga wake anakijua mwenyewe. Kiongozi jasiri halalami. Anapaswa kutoa hotuba yenye kuonyesha mamlaka inayolingana na nafasi yake. Hii ya JK ilikuwa hotuba dhaifu.

Kwa bahati mbaya, Wassira, Tendwa, Chiligati, Kilango, Mrema na Cheyo wamejiingiza katika kuimba hofu ya Rais Kikwete. Wakajidhalilisha.

Wassira anasema: "CHADEMA wanaandamana kueneza chuki&[HASHTAG]#8230[/HASHTAG];wameshindwa kwa njia ya kidemokrasia, wanataka kutumia nguvu &[HASHTAG]#8230[/HASHTAG];tunachotaka ni amani. Ni wazi CHADEMA wanaonyesha wao ni washari, wanawatia wananchi hofu. Kama wana hoja wasubiri kikao cha Bunge."

Kilango anasema: "Maandamano yale yanahamasisha vurugu nchini." Mrema anasema: "CHADEMA wanapaswa watumie njia za kikatiba za kuiondoa CCM madarakani." Chiligati anasema: "Ni vema CHADEMA ikajipanga kwa Uchaguzi Mkuu wa 2015."

Kwa kifupi, JK ameunda jazz band dhaifu yenye kuundwa na wanaojiita wakongwe, ambao wamebainika kuwa wachovu wa siasa za kileo.

Mkusanyiko wa kauli hizi za wapambe wa Rais Kikwete unaonyesha upungufu mkubwa wa upeo na ujuzi. Wanakariri na kuimba kauli ya rais kama watoto.

Inawezakanaje watu hawa wanaojiita wakongwe wa siasa hawafuatilii mikutano ya wapinzani wao, hata kujua hali halisi na hisia halisi za wananchi?

Wanashindwaje kuona kwamba vyombo vya dola ndivyo vinachafua amani kwa kutumia mabavu badala ya akili? Wanashindwaje kutambua kwamba kule ambako vyombo hivyo vimejiweka mbali mikutano hiyo imefanyika na kumalizika kwa amani?

Lakini wanasahau kuwa ukongwe wao unatambulika ndani ya CCM. JK, Kilango na Chiligati hawajawahi kufanya siasa za upinzani. Wanawezaje kuwa mabingwa wa kufundisha wapinzani namna bora ya kuipinga serikali na CCM?

Wassira aliwahi kuwa mpinzani, lakini hakuvuma kwa sababu alikuwa na malengo mafupi. Hatujasahau kwamba safari yake kisiasa katika upinzani ilikatishwa pale alipobainika mahakamani kwamba alitoa rushwa akiwa mgombea ubunge (Bunda) wa NCCR-Mageuzi, dhidi ya Joseph Warioba wa CCM, katika uchaguzi wa 1995.

Hata aliporejea CCM, waliompokea walidai kwamba ilikuwa kwa sababu ya "kuganga njaa." Hawezi kuaminika katika masuala ya kitaifa.

Ni ishara ya wazi ya uroho wa madaraka. Aliyakosa kwenye upinzani, akayapata CCM. Hana sifa ya kukejeli waliodumu katika mapambano yaliyomshinda yeye. Hawezi kuwa mwalimu wa CHADEMA juu ya jinsi bora ya kuipinga CCM.

Mrema na Cheyo ni majeruhi wa kisiasa wa CCM. Wameua vyama vyao. Wamebaki na uenyekiti na ubunge kama &[HASHTAG]#8216[/HASHTAG];mali binafsi na urithi pekee' walionao kutoka kwenye vyama vyao.

Hata ubunge wao ni matokeo ya ushirikiano mzuri kutoka CCM. Hata uenyekiti wao katika kamati za Bunge wanazoongoza ni zawadi kutoka CCM.

Nani angetarajia wanasiasa hawa hawa watoe hoja yoyote ya kuibana CCM? Nani anatarajia waunge mkono hoja za CHADEMA ambayo imewapokonya ulingo wa siasa za upinzani?

Siasa za uchumia tumbo haziwezi kudumisha upinzani. Wala wachumia matumbo hawawezi kuwa walimu bora wa upinzani.

Kama alivyosema Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, hoja zinazosababisha maandamano na mikutano ya CHADEMA zimetokana na udhaifu wa serikali. CHADEMA inasimamia hoja za wananchi. Wananchi wanaunga mkono harakati za CHADEMA kwa kuwa zinawahusu.

Hofu ya JK na vitisho ya Wassira havitasaidia kupunguza au kudhibiti nguvu za CHADEMA. Na kama Chiligati angejua maana ya kazi ya siasa, alipaswa kutambua kuwa maandalizi ya uchaguzi wa 2015 yalianza mwaka jana.

Wanachofanya CHADEMA sasa ndiyo kazi ya siasa wanayopaswa kufanya. CHADEMA ni chama kinachokua. CCM ni chama kinachozeeka na kufa.

Hata uwezo mdogo wa kufikiri wa viongozi wa CCM na wapambe wao, ni ushahidi mwingine kwamba nguvu mpya ya kisiasa inayogusa maisha ya wananchi ni CHADEMA.

Na unyonge huu unaodhihirishwa na kina Wassira ndio umeiua CCM na ndiyo sehemu ya sababu ya kukua na kupendwa kwa CHADEMA.

Kinachoshangaza ni kwamba watawala wanaiogopa CHADEMA wakati inafanya kazi ya siasa, ingekuwaje kama ingehamishia nguvu zake katika mkakati tofauti, hasa katika enzi hizi, ambapo inaungwa mkono na umma?

Wanataka CHADEMA ifanye siasa kwa kutumia staili na kauli za ki-CCM? Wanataka ifanye kazi ya CCM, na istahili kuitwa chama cha upinzani? Baada ya kufanikiwa kuvivuruga na kuviua vyama vingine vya upinzani, watawala hawa wanadhani hii ndiyo njia rahisi ya kuimaliza CHADEMA?

Ole wao CHADEMA kama watawaruhusu kina Wassira kuwafundisha siasa. Ole wao kama watasikiliza na kucheza muziki huu wa JK Jazz Band!
 
Sasa Chadema mmeanza kukimbilia nje ili kuendeleza juhudi zenu za siku nyingi za kutaka popularity ya kisiasa kwa kuitukana Serikali na kusingizia Serikali.
 
Ngurumo anasema......


Anachokiogopa, na kinachosababisha woga wake anakijua mwenyewe. Kiongozi jasiri halalami. Anapaswa kutoa hotuba yenye kuonyesha mamlaka inayolingana na nafasi yake. Hii ya JK ilikuwa hotuba dhaifu.
 
Ngurumo anasema......


Anachokiogopa, na kinachosababisha woga wake anakijua mwenyewe. Kiongozi jasiri halalami. Anapaswa kutoa hotuba yenye kuonyesha mamlaka inayolingana na nafasi yake. Hii ya JK ilikuwa hotuba dhaifu.
 
Back
Top Bottom