Halafu wapo waungwana wanaunga mkono wabunge kufanya vurugu, kutoka nje ya bunge. Akili za wabunge kwa hadhi wanayoipata ya kuingia bungeni kwa kupigiwa kura na mamilioni ya wananchi, hazikupaswa kufanana na zile za masela wa mitaani, ambao hugombana bila ya kuwa na sababu zenye kuingia akilini. Siungi mkono kwa namna yoyote ile uamuzi wa kuingiza bungeni wale FFU, lakini pia siungi mkono tabia za wabunge kujiona wapo huru sana, kujiona wana kila haki ya kufanya watakalo. Zinaweza kuwa ni enzi za kufanya kila kitu kwa uwazi bila ya watu kunyimwa demokrasia ya kufanya maamuzi na kushiriki mijadala, lakini heshima ni kitu cha bure.
Hao watoto wanaojifunza ujinga kutoka kwa baadhi ya hulka potofu za wanasiasa wetu, wanakua huku wakiamini katika akili zisizokuwa za kistaarabu. Wanakua wakiamini katika ukosefu wa adabu, wanakua wakiamini katika majibizano na watu waliowazidi umri na mamlaka. Inajengwa jamii ya watu wenye mentality za kuasi kila jambo, lakini hali hii inajificha katika taswira ya uhuru wa wanajamii. Mtoto anachapwa viboko shuleni ili ajue maana ya utii, lakini baadhi ya hulka za wabunge wetu zinafanana na wale watoto ambao hawakuguswa na fimbo hata kidogo. Inakuwa vigumu kumsema vibaya kijana ambaye anamsumbua mzazi wake kwa sababu ya utukutu, halafu ndani ya siku hiyo hiyo moja unashuhudia uhuni na ukosefu wa maadili ndani ya bunge la Jamhuri ya Muungano.
JamiiForums uses cookies to help personalise content, tailor your experience and to keep you logged in if you register.
By continuing to use this site, you are consenting to our use of cookies.