An empty stomach is not a good political adviser

Dr am 4 real PhD

JF-Expert Member
Jun 30, 2016
6,501
11,991
Kichwa Cha habari hii nime Quote from Albert Einstein.

Nawasalim wote, amani ya bwana iwe nanyi.

Kwa Sasa dunia inakabiliwa na wimbi kubwa la ugonjwa wa korona.
Eee Mwenyezi MUNGU tuokoe sisi Waja wako.

Leo asubuhi katika Soma Soma yangu habari nilikutana na Andiko la ndugu
DANIEL MARARI, Attorney & Law analyst
Let me copy & paste makala yake na tutafakari wote kwa pamoja.

Kosa la Uchochezi
Chini ya fungu la 52 (1) la Sheria ya Huduma ya Habari nia ya uchochezi maana yake ni nia ya:

(a) ya kujenga chuki au dharau au kuhamasisha manung’uniko dhidi ya utawala halali wa serikali;
(b) kuhamasisha wakazi wa Jamhuri ya Muungano kujaribu kubadilisha, kwa njia isiyo halali, jambo lolote katika Jamhuri ya Muungano.
(c) kujenga chuki, dharau na kuamsha manung’uniko dhidi ya utoaji haki (mahakama) ndani ya Jamhuri ya Muungano.
(d) kuamsha malalamiko (discontent) na manung’uniko (dissatisfaction) miongoni mwa watu au kundi la watu wa Jamhuri ya Muungano.
(e) kukuza hisia za uhasama na uadui baina ya makundi mbalimbali ya kijamii.

Tafsiri hii ya “nia ya uchochezi” ni pana sana kiasi kwamba kila kauli ya kukosoa sera au matendo ya serikali itahesabika kuwa uchochezi. Kwa mantiki tafsiri hii inakinzana na haki ya kikatiba ya uhuru wa kujieleza kwa sababu katiba inatambua uhuru wa kutoa mawazo ya aina zote.

Hata hivyo hoja ya msingi inabaki kuwa tutatofautishaje ukosoaji unaofanywa kwa nia njema na ule unaofanywa kwa nia ya uchochezi? Tunachoweza kusema hapa kwa kuanzia ni kwamba, kwa ujumla, malalamiko, manunguniko au upinzani ni sehemu mojawapo ya utawala wa kidemokrasia. Wote hatuwezi kuwa na mawazo sawa na kipimo cha uzalendo sio jinsi tunavyoweza kushindana kuisifu serikali. Watu huonesha uzalendo wao kwa namna tofauti. Wengine hushiriki katika ukosoaji na mijadala ya kujenga huku wakibainisha mapungufu ya sera za serikali kwa ni ya kuboresha. Lugha ya kueleza maoni au ujumbe huo inaweza kuwa kali lakini sio uchochezi. Hilo pia ni sehemu ya uzalendo. Hivyo basi, kupiga marufuku malalamiko au manung’uniko ya msingi kwa mwavuli wa uchochezi sio tu ni kukosa busara bali pia ni kuingilia uhuru na haki za kidemokrasia za uhuru wa habari na kujieleza.

Lakini, kwa jinsi Sheria ya Huduma ya Habari ilivyo, hususani fungu la 52(1)(a), ni rahisi sana kila kauli au lugha kali inayokosoa serikali kuchukuliwa kama uchochezi hasa pale watu wanapohoji matumizi mabaya ya pesa za umma, utoaji haki, au matumizi mabaya ya nguvu za dola dhidi ya raia. Kwa mantiki hii watu wataendelea kushtakiwa chini ya sheria hii mbaya na swali litakalokuwa linaibuka kila mara ni kujua nia ya uchochezi (seditious intent) ni ipi. Tutaitambuaje na tutawezaje kuchora mstari kati ya kauli au maudhui ya nia njema (good faith) ya kukosoa kwa nia ya kurekebisha jambo na ya nia mbaya ya “kichochezi”?

Vigumu kuthibitisha nia peke yake

Kwa sheria ilivyo sasa (fungu la 52(1) na 53), kosa la uchochezi linahitaji kuthibitisha viti viwili: (1) tendo la kichochezi , mf. kutoa kauli au chapisho na (2) nia ya kichochezi. Ni rahisi kuthibitisha kauli au chapisho. Tatizo ni kuthibitisha nia na mpaka kati ya nia njema na nia ya kichochezi. Kutambua nia ya mtu ni ngumu sana bila kuwepo matendo yanayotekeleza na kudhihirisha nia hiyo. Ndio maana kisheria mtu hawezi kuadhibiwa kwa kuwa na nia au mawazo maovu tu, bila matendo yanayodhihirisha nia hiyo. Katika kesi ya Green vs The Queen, (1458), Chief Justice Brian wa Uingereza aliwahi kusema “the intent of man cannot be tried for the devil himself knows not the intent of man” (Tafsiri huria:- “nia ya mtu haiwezi kuadhibiwa, kwa sababu hata shetani mwenyewe hajui mtu anawaza nini”). Kuwa na nia ya kutenda maovu sio kosa, mpaka pale mtu atakapochukua hatua (vitendo) kutekeleza nia yake hiyo. Vivyo hivyo, ni vigumu sana kiuhalisia kubainisha nia ya kichochezi bila kuwa na kigezo au mwongozo mwingine wa kisheria wa kuweka mpaka kati ya kauli ambazo ni sehemu ya uhuru wa kujieleza na zile zinazodaiwa kuwa za kichochezi.

Kuthibitisha nia kwenye shtaka la uchochezi, ni lazima kwanza kuthibitisha kwanza (a) uwepo wa nia ya uchochezi, na pili (b) kwamba nia hiyo ililenga kutimiza au imetimiza mojawapo ya makosa yaliyoainishwa katika fungu la 52(1)(a)-(e), mfano kujaribu kubadilisha utawala wa nchi kinyume na sheria, kujenga chuki dhidi ya mahakama au kujenga uhasama baina ya makundi ya kijamii. Tatizo la sheria linaanzia hapa. Fungu la 52(1)(a), kwa mfano, linasema uchochezi ni pamoja na nia ya kujenga chuki, dharau au kuhamasisha manung’uniko dhidi ya utawala halali wa serikali. Kwenye fungu la 52(1)(d), kulalamika dhidi ya mfumo mbovu wa utoaji haki ni uchochezi.

Maana yake ni kwamba mtu anaweza kwa mfano kuadhibiwa kwa uchochezi pale atakapotoa kauli ya kulalamikia rushwa mahakamani, upendeleo au uendeshaji/ucheleweshwaji wa kesi; mashtaka yanaweza pia kuletwa dhidi ya mtu anayetoa manung’uniko dhidi ya utendaji wa serikali kimsingi, mambo ambayo kimsingi sio kosa kisheria. Kwenye sheria zetu za jinai, hakuna kosa liitwalo — kulalamkia au kuchukia serikali au mahakama. Huo ndio msingi wa hoja yetu kuwa tafsiri ya uchochezi iliyowekwa kwenue sheria ni pana sana na kunahitajika kigezo cha kupima kauli za kichochezi.

Kuhusu kutambua uchochezi, sheria ingeweza kurekebishwa iseme maudhui ya kichochezi ni yale yanayochochea watu kufanya fujo au kuvuruga amani (disrupt public order) au kuangusha serikali kwa mabavu na njia isiyo halali, kwa kuzingatia hali halisi ya wakati huo. Vilevile, sheria ingeweza kuweka kigezo kingine kuwa kauli za kichochezi ziwe zile ambazo, hata kama hazijasababisha kosa kutendeka, zina nguvu ya kuchochea vurugu au machafuko moja kwa moja ndani ya muda mfupi. Maana yake uchochezi uwe ni ule wenye madhara/athari ya moja kwa moja kwa msikilizaji, kwa maana ya uwezekano wa kuamsha au kuwajaza watu chuki, hasira, uhasama au uadui wenye athari — utakaopelekea wao kutenda makosa kufuatia kauli hiyo, na sio chuki, malalamiko au manung’uniko ya kawaida tu. Kama, kwa mfano, mwanasiasa ataamka atoe kauli ya kuhamasisha watu au kundi moja la jamii kushambulia kundi lingine, basi, (1) shambulizi likitokea, au (2) kama kweli kuna uwezekano wa shambulio hilo kutokea, kunakuwa na uhusiano wa moja kwa moja kati ya kauli iliyotolewa na kosa lililotendeka au linaloweza kutendeka, na tunaweza kudai uchochezi umefanyika.

Muktadha (contex) wa kauli za kichochezi
Uwezo wa kauli kuchochea uhasama au uadui unategemea pia nafasi ya mtoa kauli katika jamii na muktadha/mazingira ya jamii husika kwa wakati huo, na urahisi wa watu wenyewe kushawishika. Kuthibitisha kuwa kuna watu wamehamasika na kuingiwa na chuki na uadui ni kazi ngumu kwa sababu chuki na uhasama ni hisia ambazo hudhihirika tu kama watu wakiziweka kwenye matendo na ndio maana italazimu kuangalia muktadha (context) na madhara/athari (effect) ya kauli yenyewe. Kauli peke yake kwa juu juu tu (at face value), haiwezi kuwa ya kichochezi bila kuthibitisha uwezekano (likelihood) wa kauli hiyo kuchochea uhasama au makosa ya jinai kama tulivyobainisha hapo juu. Uwezekano huu uwe dhahiri (real) kwa kuzingatia hali halisi ya jamii husika. Nchi yenye amani na utulivu kwa mfano, haiwezi kudumbukia kwenye machafuko au vurugu kwa kauli tu za hapa na pale zinazokosoa sera, misimamo au matendo ya serikali.

Hoja dhidi ya Uchochezi
Utetezi thabiti dhidi ya kosa la uchochezi ni madai ya haki ya uhuru wa kujieleza na uhuru wa kushiriki katika shughuli za utawala wa serikali. Katika nchi inayoamini katika utawala wa kidemokrasia, wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali inapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi (Ibara ya (8)(1)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano). Huu ndio msingi wa watu kupewa haki ya kushiriki katika shughuli za utawala (Ibara ya 21 ya Katiba) na uhuru wa kutoa maoni (kujieleza) kuhusu sera au mwenendo wa serikali na taasisi zake (Ibara ya 18).

Kwa kuzingatia uhuru wa kujieleza na kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, si halali kuadhibu watu kwa kauli zinazokosoa vikali uendeshaji wa shughuli za umma kwa kigezo tu kwamba zinachochea chuki na manung’uniko. Pale watu au makundi mbalimbali ya kijamii wanapotumia kutumia uhuru wa kujieleza kuwasilisha hoja, madai au malalamiko yao kwa njia mbalimbali, ni haki yao ya kidemokrasia. Kushtaki watu kwa kauli za kuhoji masuala ya umma, ni kinyume na Katiba, sheria na busara ya kawaida. Msingi wa demokrasia ni wengi waamue na wachache wenye maoni tofauti wasikilizwe sio kuadhibiwa kwa mawazo yao hayo chini ya sheria kandamizi za kichochezi.

Mipaka ya Uhuru wa Kujieleza
Kimsingi, haki karibu zote za kikatiba zina mipaka fulani. Kwa mujibu wa Ibara ya 30 ya Katiba, matumizi ya haki na uhuru binafsi wa mtu hayapaswi kuathiri haki za watu wengine. Haki ya uhuru wa kujieleza inaweza kuwekewa mipaka fulani ili, kwa mfano, kulinda sifa, haki na uhuru wa watu wengine au maisha binafsi ya watu wanaohusika katika mashauri mahakamani, kuzuia kutoa habari za siri, au kuwezesha jambo jingine lolote kufanyika ambalo linastawisha au kuhifadhi maslahi ya taifa kwa jumla.

Pamoja na hii mipaka, bado Katiba inaelekeza kuwa hatua au masharti yoyote ya kudhibiti haki za kikatiba lazima yatimize vigezo hivi: (1) yawekwe kwa mujibu wa sheria (na sio kauli, agizo au tamko la mtu), (2) yawe kweli ya lazima na muhimu kwa ajili ya kutimiza lengo halali la kisheria (necessary to pursue a legitimate aim) na (3) yawe na kipimo cha uwiano (proportional) na lengo lenyewe. Masharti haya yamethibitishwa pia na Mahakama Kuu ya Tanzania katika kesi ya Hayati Christopher Mtikila vs AG (2005).

Kama tulivyobainisha hapo juu ni kweli kwamba uhuru wa kujieleza unaweza kuwekewa mipaka nyakati fulani (restrictions), kwa sababu mbalimbali. Hata hivyo matakwa au maslahi hayo ya umma hayapaswi kupewa uzito sawa na haki yenyewe ya uhuru wa kujieleza. Tukisema kila kauli inayokera au kuudhi viongozi ni uchochezi na kinyume na maslahi ya umma, basi kuna hatari ya haki ya uhuru wa kujieleza kwenye Katiba kuwa kiinimacho tu. Lazima tuwe na kipimo cha uwiano kati ya uhuru wa kujieleza na uchochezi ili tujue ni wakati gani mtu atahesabika kuwa amevuka mpaka na kuvunja sheria. Kama kanuni au sharti la sheria (legal principle), haki ya uhuru wa kujieleza ina thamani na nafasi kubwa zaidi kuliko matakwa mengine ya muda (expediency). Thamani yake ni kubwa kiasi kwamba uhuru huu haupaswi kuwekewa masharti au kuminywa isipokuwa tu kama athari zitakazosababishwa kwa kuruhusu uhuru wa kujieleza ni kubwa na hatari kwa ustawi wa taifa. Kama hoja ni hatari ya kujenga chuki, uadui au uhasama, au fujo, basi iwe ni hatari inayoweza kutokea kweli (imminent) kwa kutathmini mazingira yaliyopo na isiwe dhana au jambo la kufikirika tu. Uhasama au chuki inayodaiwa kujengwa iwe dhahiri.

Kuwe na ushahidi kuwa kweli kuwa kuna watu wameshawishika kutenda kosa. Kama hakuna uhusiano wowote kati ya maoni au kauli iliyotolewa na madhara yanayohofiwa kutokea ni vigumu kudai kwamba uchochezi umetendeka. Kwamba kauli au hoja inakera, kuudhi au kukejeli tu, bila dalili au ushahidi unaoonesha kuwa watu wamejazwa chuki, na bila matendo mengine yoyote, haitoshi kuwa ya kichochezi kwa sababu kuu tatu. Kwanza, hazilengi kuchochea watu kutenda makosa ya jinai; pili, hakuna ushahidi wa watu waliochukizwa au kuhasimishwa; na tatu, kauli hizo ni sehemu ya uhuru wa kutoa maoni, habari na dhana zozote kwa mujibu ya Katiba.

Kwa kuhitimisha, uhuru wa kujieleza unajumuisha habari, maoni na dhana zinazokera, kuudhi na kukosoa, ili mradi zisivunje sheria. Sheria ya Huduma za Habari inaminya kwa kiasi uhuru huu na hivyo inahitaji kurekebishwa ili uchochezi uwe ni ule tu wa kuhamasisha fujo na vurugu au kujaribu kupindua serikali.

Wasalam,

#MUNGU IBARIKI AFRICA
#MUNGU IBARIKI TANZANIA
 
Back
Top Bottom