Liyumba atoka selo na kuzua utata
na Asha Bani
Tanzania Daima 18/2/09
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana ilimwachia kwa dhamana
iliyozua utata, aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba.
Utata huo ulitokana na kauli ya Wakili wa Jamhuri, Justas Mlokozi, kuonyesha kushangazwa na uamuzi wa Hakimu, Khadija Msongo, wa kumwachia mtuhumiwa licha ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana aliyopewa.
Moja ya masharti ambayo wakili huyo alidai hayakutimizwa na Liyumba ni pamoja na kuwasilisha mahakamani hati zenye thamani ya
sh bilioni 55, wadhamini wawili wa serikali wakiwa na barua kutoka kwa waajiri wao na kukabidhi hati ya kusafiria mahakamani hapo.
Lakini Liyumba aliwasilisha hati yenye thamani ya sh milioni 884, hati ya kusafiria ambayo muda wake wa matumizi umekwisha, huku wadhamini wawili wakiwa hawana barua zilizosainiwa na mwajiri wao kama masharti yalivyotolewa na mahakama.
Yeye ndiye hakimu aliyetoa uamuzi huo lakini na sisi upande wa jamhuri tunaenda kukaa kikao na kufanya majadiliano, ikiwezekana tutasonga mbele ili kujua uhalali wa dhamana hiyo, haiwezekani kwani hata robo ya masharti ya dhamana aliyowekewa hayajatimia, alidai Mlokozi.
Aidha, upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Hudson Ndusyepo, uliwasilisha maombi ya dhamana hiyo juzi ambapo jana Hakimu Khadija alipitia hati za dhamana hizo na kutoa mchanganuo wa hati mbalimbali bila kusema mahali zilipo wala thamani ya mali hizo kama inavyotakiwa.
Akisoma mchanganuo wa hati hizo, Hakimu Khadija alisema, Liyumba amewasilisha hati ya nyumba anayomiliki yeye mwenyewe yenye namba AO 320091, yenye thamani ya sh milioni 884 na plot namba 011493, 234198 za wamiliki tofauti, lakini hakutaja majina ya wamiliki wala mahali zilipo, tofauti na hati za dhamana zinavyotakiwa kutajwa majina, wamiliki na mahali zilipo.
Aidha, Hakimu Msongo alitaja shamba alilosema linamilikiwa na
Jamila Nzota ambaye alikuwa Hakimu wa Mahakama ya Temeke, ambaye pia anashitakiwa kwa kosa la kula rushwa katika mahakama hiyo huku hukumu yake ikitarajiwa kutolewa mwezi ujao.
Kama masharti ya dhamana yanavyodai mshitakiwa alitakiwa kuwasilisha hati ya kusafiria, lakini aliwasilisha hati yenye namba AO32-009-12- ya mwaka 2007 ambayo mawakili wa upande wa Jamhuri walipinga kupokelewa kwa hati hiyo.
Ingawa upande wa Jamhuri ulipinga kupokewa kwa hati hiyo, Hakimu Msongo alipuuza na kutaka kuendelea na masuala mengine huku hati iliyokuwa imekwisha muda wake tangu mwaka 2007 ikipokewa mahakamani hapo.
Wakili wa upande wa Jamhuri, Mlokozi, alidai hata hati za mali ambazo zimewasilishwa zimechanganywa, ikiwa ni pamoja na mali zinazohamishika na zisizohamishika, hivyo kutojua mchanganuo wa mali hizo na kuitaka mahakama kupitia thamani ya mali hizo, ikiwa ni pamoja na kuthaminisha mali na fedha ambazo mtuhumiwa alitakiwa kuweka dhamana.
Kutokana na mabishano hayo, hakimu alitupilia mbali madai yote ya upande wa Jamhuri na kumwachia Liyumba kwa dhamana huku akiagiza upande wa utetezi
kujipanga na kukamilisha masharti ya dhamana huku mtuhumiwa akiwa nje.
Aidha, kwa upande wa mtuhumiwa Deogratius Kweka, ambaye alikuwa Meneja Mradi wa benki hiyo, aliombewa kuwa nje akiwa chini ya uangalizi wa upande wa upelelezi kwa ajili ya kufanya uchunguzi ama upekuzi zaidi katika ofisi yake.
Aidha, upande wa Jamhuri uliiomba mahakama Kweka awe chini ya uangalizi wa upande wa upelelezi ili kuweza kufanya upekuzi katika ofisi yake kwa ajili ya kuisaidia mahakama kutenda haki.
Hakimu Msongo alikubalinana na ombi hilo na kutaka mshitakiwa huyo kuwa katika uangalizi mkubwa na upekuzi ufanyike wakati wa kazi na si vinginevyo.
Nje ya mahakama, kelele za vifijo na vigelegele vilirindima kutoka kwa ndugu wa Liyumba, huku ndugu wengine wakitoa vilio vya furaha, kwa kumkumbatia mtuhumiwa huyo na mwenyewe alisikika akisema kuwa twendeni nyumbani, twendeni nyumbani.
Msafara wa magari zaidi ya 10 yakiongozana na gari alilokuwa amepanda Liyumba, aina ya Luxus, lenye namba T 786 AEA, yaliondoka eneo la mahakama majira ya saa nane mchana, huku yakiacha gumzo kutoka kwa baadhi ya watu waliokuwa eneo hilo la mahakama.
Watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashitaka matatu; likiwamo la matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kuidhinisha ujenzi wa minara pacha ya BoT, maarufu kama Twin Towers, ambao umeisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221. Kesi hiyo itatajwa tena Februari 24.
My Take: Kwa mujibu wa hii habari Hakimu kachemsha!! Najiuliza kajiamini nini??!!