Rubawa
JF-Expert Member
- Dec 25, 2015
- 2,055
- 3,266
BARAZANI
Na Ahmed Rajab
BWANA Said Hilali, mzaliwa wa Nairobi, Kenya, ni sahibu yangu wa miaka mingi. Ana mtandao mkubwa wa kisiasa na amekaa kama mtu mwenye mikono ya pweza. Anawafikia wakubwa wa nchi za Magharibi na viongozi wengi wa Kiafrika, hususan wa mataifa yenye kuongea Kifaransa.
Kwa muda mrefu amekuwa akiwashauri marais wa Burkina Faso. Kwanza alikuwa mshauri muhtasi wa Rais aliyepinduliwa Blaise Compaoré na sasa ni mshauri wa Rais Roch Marc Christian Kaboré.
Juzi kwenye mtandao wa Facebook Hilali alikumbusha nilipokuwa naye miaka michache iliyopita katika uwanja wa Kasarani, Nairobi, pamoja na Kalonzo Musyoka, wakati huo akiwa makamu wa rais wa Kenya.
Tulipokuwa tunapiga soga Kipchoge Keino, mwanariadha mkongwe aliyekuwa bingwa wa kukimbia mita 1,500, alitukaribia. Wakati huo Keino alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Olimpiki ya Kenya. Ilikuwa mara yangu ya kwanza kumuona tangu nikutane naye London miaka ya 1970.
Katika maongezi yetu kuna maneno aliyomwambia Hilali ambayo ndiyo hasa yaliyomfanya aikumbuke siku hiyo baada ya ushindi wa kumeremeta alioupata mwanariadha wa Kenya Eliud Kipchoge katika mbio za Marathon Jumamosi iliyopita.
Kipchoge ni mwanadamu wa mwanzo kukimbia mbio hizo katika muda ulio kasoro ya saa mbili. Alikimbia masafa ya kilomita 42.2 katika muda wa saa moja, dakika 59 na sekunde 40 katika mashindano ya Ineos Challenge, yaliyofanywa Vienna, Austria. Kwa ushindi huo alijinyakulia nishani ya dhahabu.
Tulipokuwa Kasarani Keino alimwambia Hilali kwamba “Katika [mashindano ya] michezo aliye bora ndiye anayeshinda.” Kwa hayo Keino alikuwa anajipigia debe mwenyewe kwani kama sikosei ameshinda nishani nne za dhahabu katika mashindano mbalimbali ya riadha. Alishinda kwa sababu alikuwa bora kushinda wenzake aliokuwa akishindana nao.
Kauli hiyo ya Keino haihitaji ufafanuzi mkubwa. Daima ushindi huwaendea walio bora kwa lolote lile. Naliwe la michezo, masomo au la siasa.
Siku mbili hizi Waafrika wengi wamekuwa wakijivunia uafrika wao baada ya ushindi huo wa Kipchoge na baada ya waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed Ali kutunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel Oktoba 11.
Kipchoge na Abiy wamekuwa wakitukuzwa kwa sababu wamelipa sifa bara la Afrika. Ushindi wa Kipchoge ni wa dhahiri, ni safi, hauna ubishi. Wa Abiy una walakini. Sisemi kama hastahiki na bora ametunukiwa yeye na sio Donald Trump, Rais wa Marekani, au Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa Israel.
Bila ya shaka walioamua kumtunukia Tuzo ya Amani Nobel Abiy walifanya hivyo kwa kuamini kwamba Abiy ni kiongozi aliye bora miongoni mwa viongozi wenzake duniani. Abiy aliwavutia kwa juhudi zake za kufungua ukurasa mpya wa amani baina ya Ethiopia na Eritrea nchi zilizopigana vita kwa miaka miwili kuanzia 1998. Uhasama wa miaka zaidi ya 20 baina ya nchi hizo mbili ulitoweka baada ya Abiy kushika hatamu za uongozi wa Ethiopia Aprili 2018. Hilo ni fanikio kubwa.
Alijitahidi kuzipatanisha nchi zao. Hatimaye Abiy na mwenzake wa Eritrea, Rais Isaias Afwerki, walitiliana saini mkataba wa amani Septemba 16, 2018 huko Jeddah, Saudi Arabia. Hata hivyo, baadhi ya watu wanahoji kwamba hakuna kubwa lililobadilika hasa kwa upande wa Eritrea.
Tunasikia kwamba Eritrea bado watu wanakamatwa ovyo ovyo na mfumo wa demokrasia umeminywa na kubinywa mpaka umekauka.
Kuna mifano kadhaa yenye kuthibitisha hayo. Wa kwanza ni kwamba baada ya mkataba wa amani watu walikuwa wakiruhusiwa kuvuka mpaka na kuingia Ethiopia kutoka Eritrea lakini muda si muda Eritrea ikaufunga tena mpaka. Sehemu za kuvukia mpaka kama ile ya Zalambessa, ambazo ni muhimu kwa usafirishaji wa watu na bidhaa, hivi sasa zimefungwa.
Ingawa Ethiopia na Eritrea zilitiana saini mikataba mingi ya kibiashara tangu zilipopatana Septemba mwaka jana mikataba hiyo hadi sasa haijatekelezwa. Ndio maana kuna wengi wasemao kwamba amani iliyopatikana baina ya Ethiopia na Eritrea ni amani ya kwenye karats tu.
Jengo la ubalozi wa Eritrea jijini Addis Ababa limeendelea kufungwa. Ziara za mara kwa mara za kutembeleana zilizokuwa zikifanywa na Abiy na Isaias zimesita. Na sasa kuna hofu kwamba Tuzo ya Nobel aliyotunukiwa Abiy inaweza kumfanya Isaias azidi kununa kwa kumuonea wivu mwenzake na kumfanya aikorofishe amani iliyopo.
Nionavyo ni kwamba yale mahaba tuliyoyashuhudia yakimea mwaka jana baina ya serikali ya Abiy na ile ya Isaias yanapwaya. Isaias haoneshi dalili za kuregeza kamba na kuwaachia wananchi wenzake wa Eritrea wawe na uhuru kama walio nao wenzao wa Ethiopia.
Serikali ya Isaias inachukua hadhari kujikinga na “uchokozi” wa raia wa Eritrea wenye kutaka pawepo mageuzi katika mfumo wa kisiasa ili demokrasia ya kweli iweze kushamiri.
Serikali ya Isaias, kinyume na ile ya Abiy, haitaki pawepo na upinzani wa aina yo yote dhidi ya utawala wake.
Kwa upande wa Ethiopia, Abiy amefanikiwa, kwa kiwango kikubwa, kuleta amani na utengamano nchini mwake na kuitanua demokrasia. Kwa vitendo vyake Abiy anaonekana kuwa ni kiongozi mwenye kujiamini.
Pamoja na kujiamini kwa ayafanyayo, Abiy pia anaamini kwa dhati kwamba mapenzi yana nguvu zaidi ya silaha nzito kama vifaru vya kijeshi au makombora ya kisasa. Huo ndio ujumbe ambao mwaka jana alikwenda nao Asmara, mji mkuu wa Eritrea, alipofanya ziara yake ya kwanza ya kuitembelea nchi hiyo akiwa waziri mkuu.
Hata hivyo na juu ya yote hayo wapo Waethiopia wengi wasioridhika na namna Abiy anavyoiendesha nchi. Wenye kumponda wana haki ya kufanya hivyo kwa sababu hiyo ni haki yao ya kidemokrasia. Hakuna junaha.
Shutuma kubwa inayomkabili ni ya kuwapendelea watu wa kabila lake la Oromo. Wapo pia wenye kumlaumu kwamba ana tabia ya kujifanyia mambo bila ya mpango.
Kadhalika kuna hofu kwamba kamatakamata ya wanaharakati imeanza tena Addis Ababa na kwamba wakosoaji wa Abiy wananyimwa ruhusa ya kufanya mikutano ya hadhara dhidi yake. Mfano wa karibuni ni wa jioni ya Jumamosi iliyopita ambapo vijana watatu walitiwa mbaroni na polisi barabarani karibu na Merkato, ile marikiti ya Addis, iliyo kubwa kushinda marikiti zote za aina yake barani Afrika.
Eskinder Nega, mwandishi na mwanaharakati mwenye kutetea haki za binadamu, alipanga kufanya mkutano mkubwa wa hadhara Jumamosi iliyopita dhidi ya Abiy. Maudhui ya mkutano yalikuwa kwamba mpango wa mageuzi wa Abiy haukufanikiwa.
Watawala wa Addis hawakupenda. Wakaandaa maandamano ya kumpongeza Abiy kwa kutunukiwa Tuzo ya Nobel yafanyike kwenye uwanja ule ule wa Mesqel jijini Addis Ababa ambako ndiko kulikokuwa kufanywe mkutano wa kina Eskinder. Polisi wakatangaza kwamba hakuna mkutano uliokuwa ufanywe kwenye uwanja wa Mesqel.
Isitoshe, inasemekana kwamba washirika wakuu wa Eskinder wamekamatwa. Kati yao ni mwanaharakati Nathnael Yalemzewd.
Ni wazi kwamba Abiy amejitahidi kuleta mageuzi mengi ya kuondosha kero na adha zinazowakumba wapinzani nchini mwake. Ni wazi pia kwamba anakabiliwa na changamoto nyingi na kubwa hasa kwa nchi kama yake yenye makabila yenye lugha na tamaduni tofauti na yenye mazoea ya kupigana na kutoana roho.
Kaulimbiu yake ambayo ndiyo falsafa yake ni “Medemer” ambayo wenyewe wanaitafsiri kuwa ni “maridhiano”. Kwa ufupi, Abiy amejitolea kuwa mkunga wa kuizalisha Ethiopia mpya ya kidemokrasia kutoka tumbo la udikteta.
Anachofanya Abiy na kinachomtafautisha na viongozi wa kimabavu walio katika ukanda wa Afrika ya Mashariki ni kujenga hema kubwa litalowasitiri Waethiopia wote milioni 100. Ndani ya hema hilo anawalisha yaliyo muhimu katika kuijenga demokrasia na kuhakikisha kama nchi yao inastawi kiuchumi na kijamii.
Katika muda mfupi tangu ashike usukani wa kuiendesha Ethiopia Abiy amefanya mageuzi mengi na makubwa ya kuisukuma mbele Ethiopia. Washirika wake wakuu wenye kumsaidia ni Lemma Mergersa, waziri wa ulinzi, na Gedu Andargachew, waziri wa mambo ya nje.
Lemma ni wa kabila la Oromo na aliwahi kuwa rais wa jimbo la Oromia. Gedu ni wa kabila la Amhara na aliwahi kuwa rais wa jimbo la Amhara kutoka 2013 hadi mwaka huu.
Si hayo tu bali kuna mengi mengine aliyoyatenda yenye kumfanya afikiriwe kuwa kiongozi bora Afrika.
Nadhani la muhimu na adhimu kushinda yote ni mchango wake katika ufumbuzi wa mgogoro wa Sudan baada ya kupinduliwa Rais Omar Hassan al Bashir Aprili mwaka huu. Abiy alisaidia sana kuipoza hali ya mambo iliyokuwa moto baina ya waandamanaji na majeshi ya Sudan.
Hatimaye, kwa ushirikiano pia wa Muungano wa Afrika (AU), palipatikana masikilizano ya jinsi wapinzani na wanajeshi watavyoiendesha Sudan na kuifikisha katika mfumo kamili wa kidemokrasi.
Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab