Dotto C. Rangimoto
JF-Expert Member
- Nov 22, 2012
- 1,985
- 1,284
Alalae alalae, nataka kumueleza,
Azinduke na akae, maneno sije poteza,
Kuna kisiki nikwae, uchao chajitegeza,
Atakalo akatae, adhabu yake gereza,
Alalae namweleza, ya sasa sio ya kae.
Alalae alalae, aamke akiweza,
Ndotoni asishangae, na muda kuupoteza,
Apate mwenza azae, waishi uingereza,
Kizinduka aduwae, yu kitandani ateza,
Alalae namweleza, ya sasa sio ya kae.
Alalae Alalae, amelalia jeneza,
Akubali akatae, yeye kalitengeneza,
Kwa ujinga azubae, kaburi lenda mmeza,
Vizuri ajiandae, tusi kulitokomeza,
Alalae namweleza, ya sasa sio ya kae.
Alalae Alalae, yatosha niloeleza,
Si mtoto akomae, awate kujilegeza,
Dunia sasa si kae, ile ya kubembeleza,
Ushauri wangu atwae, apate kujiongeza,
Alalae namweleza, ya sasa sio ya kae.
**************
Alalae naweza kuwa mimi, wewe au yeyote ambaye bado hataki kuamini kuwa zama za sasa si za kale, na ya kwamba twatakikana kubadili mbinu na njia za kupambana na adui yuleyule ambaye sasa kaja kivingine au atumia mbinu nyingine.
Wewe uliyelala tangu enzi za vita ya majimaji, wazinduka sasa na silaha zako za maji, huku ukidhani adui yetu ni mtanzania mwenzetu kumbe ni yuleyule Mjerumani, lakini sasa anatumia watanzania wenzetu ambao ni vibaraka kwa mataifa ya Ulaya.
Watumishi wa umma na viongozi wanaofanya dili za kifisadi kwa maslahi yao na makampuni ya Ulaya, hao ndio wanaotumiwa na wakoloni mamboleo kuendeleza makoloni yao.
Wanasiasa wanao zunguka nchi za Ulaya kwa lengo la kuichafua nchi kisa tu wameshindwa uchaguzi, wanasiasa hao nao pia wanatumiwa na hawa wakoloni. Watapigwa kiki, injini ikiwaka wapate dili za kuuza silaha na kukomba rasilimali za nchi yetu kirhisi.
Wewe uliyelala, fahamu mbele yetu kuna ma.vi mabichi na mkojo wa nguruwe, kisha vyote hivyo vyawekwa katika karatasi ya kura, twaambiwa tuchaguwe. Hatuna hiyari ya kuchagua "kilicho bora" bali twalazimishwa kuchagua "kilicho afadhali". Matokeo yake, ma.vi mabichi yaunda serikali, mkojo wa nguruwe waunda kambi ya upinzani.
Twapata maradhi ya tumbo kwa uchafu huu wa ukosefu wa uadilifu kwa vyama vikubwa na venye kutegemewa nchini. Daktari akituuliza twaumwa nini au twajisikiaje, twajibu kwa pamoja kama tuna wazimu, "ku-nya hatunyi ila kuharisha matata" Allahu Akbar sote sasa tumekuwa hamsini rasi hamsini majinuni.
Alalae anaweza kuwa mimi, wewe au yeyote yule ambaye anadhani kwamba CCM ni mkoloni, na akabaki kutumia mbinu zilezile tulizo zitumia kumtoa mkoloni. Mtu huyo amelala, anahitaji kuzinduka, CCM si mkoloni, hatujawahi kuchagua wakoloni, bali CCM tumeichagua wenyewe.
Alalae naweza kuwa mimi, wewe au yeyote yule, ambaye anadhani Kikwete aliongoza nchi kama alivyoongoza Mkapa, na Magufuli anaongoza kama alivyoongoza Kikwete, na hadi sasa akabaki kutumia mbinu ileile aliyotumia kumtoa Mkapa na Kikwete katika kumtoa Magufuli 2020. Mtu huyu ni mjinga kwa sababu mbili.
Mosi mbinu hizo zimeshindwa kuitoa CCM madarakani enzi za Mkapa na Kikwete, lakini kubwa zaidi mtindo wa uongozi wa Magufuli tafauti na wa Kikwete na wa Mkapa. Kama ni wewe, umelala zinduka!
Tafuta njia ya kupambana na ulaghai unaotumia jina la "HAPA KAZI TU" na achana na njia uliyoitumia kupambana na ulaghai wa "HARI MPYA NA KASI MPYA"
Zinduka na ufahamu kuwa 2020 usitoe kitanda chako kwenye ma.vi mabichi na kukipeleka kwenye mkojo wa nguruwe, utafanya kosa kubwa sana! Kumbuka Samweli alipokwenda kwenye nyumba ya Yese wa kabila wa Yuda, aliwaacha wote kuwapaka mafuta, ila akaenda kumpaka mafuta mtoto mdogo asiyewahi fanya au onja dhambi.
"Yese akawapitisha wanawe saba mbele ya Samweli. Samweli akamwambia Yese, Bwana hakuwachagua hawa. Kisha Samweli akamwambia Yese, Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hata atakapokuja huku. Basi akatuma mtu, naye akamleta kwao. Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbo lake lilikuwa la kupendeza. Bwana akasema, Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye."
1 Samweli 16:10-12
Zinduka na amua huku ukizingatia sababu za mwana mdogo wa Yese kupakwa mafuta na kuachwa mijitu mizima na midevu yao.
Dotto Rangimto Chamchua(Njano5)
Call/ whats app 0622845394 Morogoro.