Ajali za barabarani ni matokeo ya kufeli kwa mfumo wa usalama barabarani

Ajali za barabarani ni matokeo ya kufeli kwa mfumo wa usalama barabarani

figganigga

Platinum Member
Joined
Oct 17, 2010
Posts
26,662
Reaction score
59,100
Kwa mujibu wa Mfumo Salama wa Usalama Barabarani (Safe system approach), kunapotokea ajali barabarani, maana yake kuna sehemu kwenye mfumo wa usalama barabarani ni dhaifu na hivyo pamefeli. Kufeli huko husababisha madhara mbalimbali ikiwemo ajali yenyewe, vifo, majeruhi, na uharibifu wa mali.

Mfumo wa usalama barabarani unahusisha vitu vitano:
1. Usimamizi madhubuti wa usalama barabarani
2. Barabara salama
3. Magari salama
4. Watu salama
5. Huduma baada ya ajali

Kikifeli chochote kwenye huu mfumo matokeo yake ni ajali. Naam, watu watakufa au kujeruhiwa. Kwenye mfumo huu kunahusisha watu wengi wakiwemo polisi, mamlaka za barabara, mamlaka za udhibiti, watu wenyewe, nk.

Hivyo, kwa asilimia kubwa ajali sio jambo la ghafla sana. Huwa kuna viashiria kwamba kuna siku hapa itatokea ajali, au kuna siku tabia hii itasababisha ajali. Viashiria viko vingi, lakini baadhi ni:

1. Shimo linaloanza barabarani bila kuzibwa kwa muda mrefu
2. Kona zisizo na alama wala viashiria
3. Barabara zisizo na mistari ya kumwongoza dereva
4. Kutokuwepo au kutokufanya kazi kwa taa za barabarani
5. Gari kutokuwa na taa au kutembea na taa moja tu ya mbele (chongo) au kutokuwa na taa za breki
6. Gari kutokuwa na utepe angavu
7. Kutoweka kiashiria baada ya gari kuharibika
8. Gari lililoharibika kukaa muda mrefu barabarani au kandoni mwa barabara bila kuondolewa wakati mamlaka zipo tu
9. Gari kuruhusiwa kuendelea na safari huku likiwa na ubovu, uwe wa tairi au chochote kile
10. Askari wa usalama barabarani kuacha kujikita kukagua makosa hatarishi na badala yake kujikita katika vitu visivyo hatarishi au kubaki barabarani kama watazamaji tu
11. Kuacha gari liendelee na safari huku likiwa na abiria waliozidi (excess)
12. Kutokagua magari kabla ya safari kama ulivyo utaratibu
13. Kupasisha madereva wasio na sifa
14. Kupasisha shule za udereva zisizokidhi vigezo
15. Kuacha madereva waendelee kutanua bila hatua zozote kuchukuliwa
16. Kutochukua hatua madhubuti kwa madereva wanaozidi mwendo ulioruhusiwa
17. Kutochukua hatua kwa madereva wanaovateki bila kuzingatia mistari
18. Kutengeneza uswahiba usio wa kawaida unaofanya msimamizi wa sheria akose nguvu za kusimamia sheria
19. Kupuuza taarifa au malalamiko ya wananchi kuhusu hali fulani hatarishi barabarani
20. Nk (unaweza ongezea)
Yote haya ni viashiria vya udhaifu kwenye mfumo unaoweza kuufanya mfumo ufeli wakati wowote. Na ukifeli tu matokeo yake ni ajali.

Kufeli kwa mfumo huwa kunaanza kuonesha dalili (symptoms). Dalili hizo ni pamoja na almanusura (near misses), tabia fulani za kujirudia rudia au kujiamini sana. Tukichukulia ajali iliyotokea mlima wa pugu Machi 2025, viashiria vya kufeli kwa mfumo vilishaanza kujitokeza na hasa kutokana na kukosekana kwa uratibu mzuri kati ya mkandarasi na Polisi wanaotakiwa kusimamia usalama barabarani eneo hilo. Wananchi walishaona dalili na kuanza kulalamikia. Kitendo cha mkandarasi kutoa njia nyembamba na chache pale kukachochea tabia ya madereva kukosa uvumilivu, na hivyo kuanza kutanua.

Matokeo ya kutanua ni kufunga njia pande zote au moja, na hivyo watu kulazimika kusubiri muda mrefu. Njia inapokuwa na nafasi upande mmoja dereva aliyetanua atalazimika kutoka kwa spidi kubwa ili awahi mbele bila kukutana na gari inayokuja (oncoming traffic) matokeo yake ni ajali kama tulivyoona na kugharimu maisha ya watu, na sio watu tu mtu mkubwa na muhimu sana katika mfumo wa usimamizi wa mfumo wa usalama barabarani?

Ndio maana baada ya ajali, swali kuu linapaswa kuwa Kwa nini ajali hii imetokea? na sio nani amesababisha ajali hiii? Kutafuta majibu ya swali hili la pili, mara nyingi kunaleta majibu(answers) na sio majawabu (solutions). Barabarani tunatakiwa tutafute majawabu na sio majibu. Tunatakiwa kutafuta majawabu kwa kupitia upya mfumo mzima wa usalama barabarani eneo husika na ajali na kisha kuja na afua (interventions) na mpango kazi(action plan) ya kutengeneza afua hizo.

Je, hatukuwahi kuiona kero ya ujenzi inavyoweza kuchochea ajali pale? Je tulichukua hatua gani? Je hatukuwahi kujua kuwa daladala zinatanua hivyo pale? Na je, tulichukua hatua gani za kimkakati, badala ya kumtegemea askari mmoja au wawili?
 
Back
Top Bottom