Kwa Li Qiaoyang, kijana shabiki wa kutalii kutoka mkoa wa Shandong, mashariki mwa China, ndoto ya likizo si kutembelea majumba ya makumbusho katika nchi za Ulaya ama fukwe za Asia Kusini Mashariki. Badala yake, anaota ndoto ya kwenda kutembelea uwanda mpana wa mbuga za Afrika.
Li, aliyezaliwa miaka ya 1990, anasema ametembelea Misri na Morocco, nchi zilizo Kaskazini mwa Afrika, na mwaka huu anataka kwenda Tanzania kupiga picha za wanyama. Li, ambaye tayari ametembelea mapiramidi na Hekalu la Luxor nchini Misri mwaka 2016, na kutalii kwa gari kupitia Casablanca na Jangwa la Sahara nchini Morocco mwaka 2020, anaonekana kuvutiwa sana na bara la Afrika. Anasema mandhari za kipekee za asili za Afrika na utamaduni ni vitu vinavyomvutia sana, na Wachina wengi vijana wana shauku na kuvutiwa navyo.
Li ni kati ya wimbi la vijana wa Kichina wanaopenda kutalii wanaoelekeza macho yao barani Afrika, bara lenye uwanda mpana wa mbuga, majangwa, idadi kubwa ya wanyamapori, na hazina kubwa ya urithi wa asili na utamaduni. Mwelekeo huu unachochewa zaidi na sera nzuri za wageni kuingia katika nchi husika, kama vile kufutwa kwa mahitaji ya visa na kupata visa unapoingia katika nchi mbalimbali za Afrika.
Tofauti na kizazi cha wazee ambao mara nyingi wanapendelea mipango iliyoandaliwa katika makundi ya watalii, aina hii mpya ya watalii wenye umri wa miaka 30, wanapendelea uhuru wa kutembelea wanapotaka na kujipangia ratiba. Afrika, ambayo mara nyingi inaonekana kama ni mbali na ya kushangaza, ina mvuto mkubwa kwa wale wanaopenda kutembelea sehemu ambazo hazijawahi kufikiwa kabla.
Mabadiliko haya katika filosofia ya utalii yanaonekana wazi kabisa katika mitandao ya kijamii. Katika APP ya mtindo wa maisha ya Rednote, utafutaji wa ‘safari za Afrika’ unapata jumbe ambazo zimevutia kwa urahisi zaidi ya majibu 200. Raia wanajadili kwa uwazi gharama na njia, mara nyingi wakitaka kupata uzoefu wa juu wa binafsi barani Afrika.
Soko la utalii limeshika kasi joto la shauku hii. Xie Ran, meneja katika kampuni ya utalii iliyoko mji wa pwani wa Qingdao mkoani Shandong, anashuhudia ongezeko la wasafiri wanaoelekea Afrika katika miaka michache iliyopita. Wateja wa kampuni hiyo wanaoenda kutalii Afrika wameongezeka kutoka karibu 100 mwaka 2023 hadi 190 mwaka 2024, na kufikia karibu 240 mwaka 2025.
Kampuni ya utalii ya kimataifa ya GZL iliyoko Guangzhou, mkoa wa Guangdong, kusini mwa China, imesema maulizo ya jumla ya vivutio vya utalii barani Afrika yaliongezeka kwa asilimia 50 hadi 60 katika miezi ya karibuni, huku maagizo ya sehemu zinazohusisha Afrika Kusini na Visiwa vya Vanilla yakiongezeka kwa karibu asilimia 40.
Profesa Wu Liyun, wa Akademia ya Utalii na Utamaduni katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Beijing, China, anasema uzuri wa asili na utamaduni wa Afrika una mvuto wa kipekee ambao unawavutia watalii wa China, na kuongeza kuwa, kushuhudia msimu wa Uhamaji Mkubwa, umekuwa ni mvuto kwa watalii wengi.
Profesa Wu anasema, utalii wa nje wa China umeendelea kwa kasi, na kwa watalii wa mara kwa mara ambao tayari wametembelea nchi jirani, kwenda katika maeneo ya mbali kama Afrika ni uamuzi wa asili kwa kuwa wanapata uzoefu mkubwa zaidi wa utalii.