Abrakadabra za siasa zisituchanganye | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Abrakadabra za siasa zisituchanganye

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by Dopas, Sep 17, 2010.

 1. D

  Dopas JF-Expert Member

  #1
  Sep 17, 2010
  Joined: Aug 14, 2010
  Messages: 1,151
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 135
  NAAPA huu ndio muda wa kulishwa ahadi hadi tunajiona pepo ikitusogelea.

  Nasema kama kila kinachosemwa kitatekelezwa mbona Bongo itageuka pepo mwanangu?

  Kama kila ziwa kubwa hapa nchini litakuwa na meli kubwa mpya ni kipi tena tutakuwa tumebakisha kwa wale wanaoishi kando kando ya maziwa?

  Naiona nchi ya maziwa na asali ikitujia mwishoni mwa Oktoba. Mimi simo.

  Si tumesikia hata kule kwa wakina Nshomile watapewa uwanja wa kimataifa wa ndege?

  Nasikia watu wa Bukoba sasa sio meli mpya tu lakini na uwanja wa kisasa wamehaidiwa utajengwa. Sasa sisi tunasubiri tu kula matoke yanayotoka Bukoba kwa ndege kuletwa huku na huko!

  Lakini uwanja huo ukijengwa hivi tuna ndege za kutua huko? Nauliza mniambie maana nasikia lile shirika lenu la ndege lipo chumba cha wagonjwa mahututi wenyewe wanaita ICU.

  Simo lakini ukweli ndo huo! Najitoa mtoto wa mama miye. Kigoma nao nasikia wamehakikishiwa mji utageuka kuwa kama Dubai.

  Hivi mbona hamuwaulizi hasa hao walioko madarakani kwa nini hawakufanya hayo yote kipindi kilichopita? Mimi simo lakini anapokuja mtu leo na kukuhakikishia maisha bora wakati hata yale ya kawaida hujawahi kuyaopata inabidi ukune kichwa mara mbili.

  Hawa watawala si walikuwepo siku zote? Hizo pesa za kununulia ndege na meli ndio wamezipata hivi karibuni? Si wameshindwa kuendesha shirika la ndege hadi wakaenda kuwatafuta wakina Khambaita waje kutuendeshea hilo shirika?

  Kabla hajahaidi makubwa hebu tuwaulizeni hawa wasafiri wanaotumia reli ya kati shida wanazozipata. Nikimbie mbio kabla sijaitwa mchochezi miye.

  Nasikia badala ya kujadili mambo ya msingi yanayolisibu taifa letu mmebaki kushupalia nani analala chumba kipi akiwa na nani. Simo huko. Nasema tunapaswa kujadili mambo mazito yanayotukwamisha sio kujadili nani malaika na yupi ni shetani.

  Nimemsikia mgombea mmoja akisema Watanzania wengi wako kwenye swaumu karibia mwaka mzima hata kama wao sio waislamu.

  Tunafunga miezi isiyo ya toba tena bila kupata thawabu! Bado hamjui wapo watu kibao ambao kupata mlo wa siku ni bahati nasibu?

  Usione wengine wakila na kusaza, wapo wengi hawana hata tonge moja kwa kutwa nzima. Si niliwaambia katika kaya yetu wapo watu wanafanya karamu katikati ya msiba? Nikimbie mbio katika haya yote. Simo mtoto wa mama miye.

  Nasikia kwa mara nyingine tena siasa zetu zinahusishwa na uchawi. Mola wangu! Huyu Sheikh Yahaya Hussein ana nini na siasa zetu? Si mmemsikia kwenye vyombo vya habari akisema eti ile fedheha iliyomkumba mkuu wa kaya pale Jangwani akaishiwa nguvu eti ni mambo ya “kuchezeana.”

  Tumefika huko Yarabi. Afya ya mkuu wa nchi bado inaangaliwa kwenye mitulinga na manyanga?

  Mbona kama nakumbuka vizuri kuna wakati Pinda yule Mizengo alishawahi kuwazuia waganga wa kienyeji kufanya uganga wao? Yawezekana walishafunguliwa lakini ndio tunafika hadi kwa bwana rais? Simo tena simo.

  Sasa ikulu wasipokanusha taarifa kwamba rais wetu analindwa na sheik yahaya na wasipokanusha kwamba kuanguka kwa rais kulitokana na kuchezewa, watakuwa wanatuweka njia panda.

  Nasema simo ila haya ya kuingiza ushirikina kwenye mambo ya kitaifa yanazua maswali. Nasema simo kwenye haya yote.

  Na hao washabiki wanaosababisha vurugu kwenye kampeni nao wametumwa na nani? Nasikia Mzee wa Kiraracha alilazimika kulala uvunguni mwa gari yake kunusuru nafsi yake isije ikapokonywa kwenye mwili na wahuni anaowahusisha na chama cha siasa.

  Ni kweli kura zinaleta kula lakini tusifikie hapo pa kutoana ngeu jaamani. Tena wanaotoana ngeu wala sio wagombea, ni washabiki wao ambao wala huwezi kujua kama wana chochote cha kufaidi. Watu wengine utadhani wamepungukiwa akili. Badala ya kunadi sera mnapanga fujo? Hii ndio amani na utulivu mnayojivunia eh? Nasema tena simo ila kama siasa ndio hizi wacha tu niendelee na kilimo change ingawa sijaona tija hadi sasa. Najitoa mzima mzima miye. Simo kabisa!

  Na huu uandishi uliokosa weledi nani kaupa nafasi kwenye jamii yetu? Kama mmeamua kuwa nyenzo za kuwabeba wanasiasa muwapendao mimi sioni tatizo ikiwa tu mtajitambulihs arasmi mrengo wenu.

  Mbona hakuna anayewalalamikia gazeti la Uhuru? Sote si tunajua linamilikiwa na chama nambari wahedi? Hivyo hata tukisoma majigambo au mabaya ya wapinzani tunajua namna ya kupata usawa wa habari maana mmiliki tunaijua itikadi yake.

  Tatizo lipo kwenye vyombo vinavyojidai ni huru huku vikiandika kwa kuegemea.

  Nasema hizi njaa za reja reja zitatuumiza. Badala ya kusema kweli tena kweli tupu wanafikia mahali wanasema uongo kwa lengo la kushibisha tumbo kwa siku mbili-tatu!

  Tumefika huko nawaapia. Nasikia wapo waliofikia hadi kusambaza gazeti la kuchafua wengine bure.

  Yakitokea hayo hakuna anayeitwa idara ya habari maelezo kuonywa lakini mwana mwema Kubenea akiandika anayoandika anaonywa. Tumefika huko enyi wana.

  Na haya tuliyosikia eti kuna nyenzo za ikulu zinatumika kwenye kampeni mbona inatisha walimwengu? Si mmemsikia John Tendwa akisema CCM kimetumia picha za ikulu kumnadi mgombea wao.

  Kama unaona picha ya mgombea amezungukwa na vikosi vyetu vya ulinzi na usalama bado utasema tuko kwenye uwanja sawa wa ushindani?

  Iweje picha za mgombea akitekeleza majukumu yake ya kikazi serikalini zichukuliwe kwa kampeni?

  Anapotimiza majuku yake huko serikalini si tunamlipa mshahara? Sasa iweje watu wanachukulia kwamba ni hisani anafanya? Si aliomba kazi tukampa na tunamlipa? Sasa cha ajabu ni kipi kama anatimiza sehemu ya wajibu?

  Kwani hamjui kwamba hatutakiwi kumsifu mtu kwa kutimiza wajibu badala yake tunapaswa kupiga kelele pale ambapo hapajafanyiwa kazi?

  Nani aliwadanganya kuetekeleza ahadi ni hisani? Najitoa kabisa enyi wana. Msinitaje kwenye hili, nasema simo tena simo!

  By Simo-Mzee wa kujitoa, Tanzania Daima 18/9/2010
   
Loading...