Abdulrahman Babu hakuupinga Muungano lakini…

Hamid Rubawa

Member
May 23, 2018
72
202
Na Ahmed Rajab

SIKU ilipotangazwa kwamba Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zitaungana, Abdulrahman Mohamed Babu aliyekuwa waziri wa mambo ya nje na biashara za nje wa Zanzibar, hakuwako visiwani. Alikuwa Jakarta, Indonesia, alikokwenda kutafuta masoko ya karafuu za Zanzibar, zao lililokuwa likiipatia Zanzibar pato lake kubwa la fedha za kigeni. Indonesia ilikuwa mshitiri mkuu wa karafuu, ambazo ikizitumia kutengenezea sigara, dawa ya meno na viungo vya mapishi.

Kwa vile wakati huo Babu alikuwa Jakarta, hakuhudhuria pia kikao cha Baraza la Mapinduzi ambapo Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, alipolizungumza hadharani kwa mara ya kwanza suala la kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar.

Babu, alipotua Nairobi akielekea Zanzibar, aliulizwa na waandishi wa habari maoni yake kuhusu muungano. Bila ya kusita alijibu kwamba aliuunga mkono. Na aliashiria kana kwamba alikuwa akijua kwamba utaundwa. Ukweli wa mambo ni kwamba alikuwa hajui. Aliushtukia ghafla bin vuu.

Kwa hakika, takriban dunia nzima siku hiyo ilishangazwa na tangazo hilo. Isipokuwa Marekani na Uingereza. Nchi hizo zikijua na mapema kitachojiri kwani zilihusika tangu mwanzo katika mkakati wa uundwaji wa Muungano wenyewe.

Jawabu ya Babu, alipokuwa Nairobi, ilikuwa jawabu ya kutarajiwa kutoka mdomoni mwa mwanasiasa mwerevu na aliyekuwa macho kisiasa saa ishirini na nne na aliyejua jinsi ya kujiepusha na majungu yaliyokuwa yakipikwa dhidi yake wakati wa mapinduzi ya Zanzibar yalipokuwa ya moto moto. Kwa hakika, kabla ya kufunga safari kutoka Jakarta kurudi nyumbani, Babu alipokea telegramu kutoka kwa mmoja wa washirika wake iliyomshauri asirudi Zanzibar. Ilikuwa ni njama ya kumtenganisha na Mapinduzi. Babu aliipuuza telegramu hiyo.

Alipoikanyaga ardhi ya Unguja na baada ya kuzungumza na wenzake wa itikadi moja waliokuwa serikalini, wakiwa pamoja na Abdallah Kassim Hanga, Babu alifahamu kwamba lengo la nchi hizo mbili kuungana lilikuwa kuunda serikali ya shirikisho. Kwa mintarafu hayo, Hanga aliyekuwa akienziwa na Warussi aliokuwa akiwaamini, alimualika wakili mmoja kutoka Urusi kwenda Zanzibar kuishauri serikali ya huko juu ya mfumo wa Katiba ya Shirikisho. Na alifanya hivyo pengine kwa sababu Muungano wa Sovieti wa siku hizo ulioiunganisha Urusi na Jamhuri nyingine za Kisoshalisti za Kisovieti ulikuwa wa muundo wa shirikisho.

Babu, kwa upande wake, pamoja na Salim Rashid aliyekuwa katibu wa Baraza la Mapinduzi, walimualika wakili wa sheria za kimataifa kutoka Uganda, Dani Wadada Nabudere, aliyekuwa na muelekeo kama wao wa kiitikadi wa Umarx, ende kuishauri serikali ya Zanzibar. Lakini Nabudere alipofika Zanzibar alikuta mambo yamekwenda kwa kasi na kuwepo kwake kusingesaidia kitu. Alifunga safari akarudi kwao.

Kuundwa kwa Muungano kulikuwa mtihani mkubwa kwa Babu. Sababu ni kwamba Muungano uliasisiwa katika mazingira ya Vita Baridi, kati ya mataifa ya Magharibi yaliyokuwa yakifuata mfumo wa kibepari na mataifa ya Mashariki, yaliyokuwa yakifuata mfumo wa kisoshalisti na baadhi yao yakiwa ya kikomunisti.

Mataifa ya Magharibi, yakiongozwa na Marekani, yaliiona Zanzibar kuwa imo mbioni kugeuka na kuwa “Cuba ya Afrika Mashariki.” Dhana hiyo iliyatia hofu madola hayo. Hayakutaka mfumo ulio mbadala ufanikiwe, hasa katika nchi changa za Kiafrika.

Kwa hivyo, tangu litolewe lile liitwalo “Tangazo la Machi 8” lililosomwa na Komredi Ali Mahfoudh kwenye mkutano wa hadhara, uliofanywa kwenye Uwanja wa Mnazi Mmoja, Unguja na kuhutubiwa na Karume na Babu, nchi za Magharibi ziliingiwa kiwewe. Tangazo hilo, ambalo kwa kweli ndilo lililoiweka misingi ya kinadharia ya Mapinduzi, lilizitisha nchi za Magharibi.

Miongoni mwa mambo yaliyotangazwa humo yalikuwa pamoja na utaifishwaji wa ardhi, kupigwa marufuku jumuiya za kikabila, na kutolewa huduma bure za kijamii kwa wananchi. Takriban hatua zote zilizotangazwa Machi 8 zilikuwa zimetoka kwenye Ilani ya Chama cha zamani cha Umma Party.

Kiitikadi zilielemea upande wa nchi za Mashariki, hususan za Urusi na China. Nchi hizo nazo zilikwishaonesha kwamba zilikuwa tayari kuisaidia Zanzibar kwa hali na mali ili ipate ufanisi wa haraka. Kwa vile Zanzibar ni visiwa vidogo ilikuwa wazi kwamba nchi za Mashariki zilikuwa na uwezo wa kuibadili taswira ya Zanzibar na kuifanya yenye kustawi katika muda mfupi.

Nchi za Magharibi hazikutaka hayo yatokee, ya Zanzibar kugeuzwa mfano wa maendeleo na ustawi wa kisoshalisti. Nchi hizo zilihamanika zikaanza kutafuta njia za kuyakaba Mapinduzi ya Zanzibar. Na si nchi hizo za Magharibi tu lakini hata Tanganyika nayo iliingiwa na wahka. Zanzibar ya kisoshalisti iliyostawi ilikuwa kitisho kwa Tanganyika ya kibepari iliyokuwa ikiendeshwa na Rais Julius Nyerere.

Wananchi wa Tanganyika walikuwa wakifuatilia kwa makini hatua zilizokuwa zikitangazwa na serikali mpya ya Zanzibar. Walivutiwa na hatua hizo licha ya kuwa hali halisi za mambo visiwani walikuwa hawazijui.

Tusisahau pia kwamba mnamo Januari 19 na 20 majeshi ya Tanganyika yaliasi. Waasi walivishika vituo nyeti vilivyokuwa Dar es Salaam na Tabora. Nyerere alilazimika kwenda kujificha. Akaingiwa na aibu ya kuomba msaada wa kijeshi kutoka Uingereza, nchi ambayo miaka mitatu kabla iliipa uhuru Tanganyika. Lau Waingereza wangelikataa kwenda kumwokoa Nyerere, inamkinika sana kwamba huo ungelikuwa mwisho wake wa kisiasa.

Kwa ufupi, Mapinduzi ya Zanzibar yalikuwa kitisho kikubwa kwa viongozi wa madola ya Magharibi na pia kwa Nyerere. Kwa viongozi wa Magharibi yalikuwa mfano mbaya kwa Waafrika watakaotaka kuleta mageuzi kama hayo katika nchi zao. Na kwa Watanganyika yalikuwa mfano mzuri wa kuigwa kwa waliokuwa wakitaka kuleta mabadiliko ya kunyanyua hali za walala hoi.

Ndipo viongozi wa Magharibi na Nyerere wakaona lazima pasukwe mkakati wa kuyazima Mapinduzi ya Zanzibar. Kwa ustadi na ujanja mkubwa pakatolewa hilo wazo la kuundwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Si bure kwamba mshauri mkuu wa Nyerere wakati wa mchakato mzima wa kuasisiwa Muungano alikuwa Roland Brown, mwanasheria mkuu wa serikali ya Tanganyika aliyekuwa raia wa Uingereza. Yeye ndiye aliyependekeza kwamba Muungano huo uigize muundo wa muungano kati ya Ireland ya Kaskazini na sehemu zilizobaki za Uingereza (Great Britain).

Kufikia Machi, 1964 malengo ya madola makuu ya Magharibi na ya Nyerere kuhusu mapinduzi ya Zanzibar yalisadifu kuwa mamoja: kuyaua mapinduzi hayo.

Babu aliyafahamu hayo na aliamini kwamba Muungano utazivuruga azma na dhamira za mapinduzi za kuunda jamii yenye usawa itayojengeka juu ya misingi ya usoshalisti wa kisayansi. Ingawa waasisi halisi wa mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 hawakuwa na itikadi hiyo (kwao wao mapinduzi yalikuwa na maana ya kuupindua usultani), wanamapinduzi wa kinadharia kina Babu, Ali Sultan Issa, Khamis Abdalla Ameir, Ahmed Badawi Qullatein, Hanga, Hassan Nassor Moyo, Abdulaziz Twala na Saleh Saadallah, wakiamini kwamba wangeweza kuyatumia mapinduzi kuyabirua maisha ya walio wengi Zanzibar.

Mtihani mkubwa uliomkabili Babu ni kwamba yeye alikuwa muumini mkuu wa Umajumui wa Afrika (Pan-Africanism). Kwa hivyo, ni muhali kwake kuukanya Muungano kabisa kabisa kama ilivyo kwa wengi wetu wenye kutaka nchi za Afrika ziungane.

Msimamo wa Babu kuhusu Umajumui wa Afrika umeelezwa kwa ufasaha mkubwa katika uchambuzi wa msomi wa Kimisri Zeyad el Nabolsi. Msomi huyu aliye katika Chuo Kikuu cha Cornell, Marekani, amechapisha makala mengi ya kifalsafa yakihusika na nadharia za Umarx na Ulenin. Kwenye kitabu kilichochapishwa mwaka jana na State University of New York kiitwacho “The Future of Lenin: Power, Politics and Revolution in the Twenty-First Century” el Nabolsi ana makala yenye ilani ya “Lenin and East African Marxism: Abdulrahman Mohamed Babu and Dani Wadada Nabudere”.

Katika makala hayo yaliyoshiba fikra na uchambuzi wa kinadharia, el Nabolsi ameuchambua kwa kina msimamo wa Babu juu ya Umajumui wa Afrika na amesema kwamba Babu ametoa mchango mkubwa katika kuziendeleza nadharia za Umarx na Ulenin kuhusu dhana za uzalendo. El Nabolsi pia amegusia jinsi Babu pamoja na Nabudere walivyoiponda dhana ya Nyerere ya “Usoshalisti wa Kiafrika” (Ujamaa, ingawa El Nabolsi hajalitumia neno hilo.)

Sasa tukirudi katika mada yetu na historia ya Babu na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tunaweza kusema kwamba mchakato wa fikra zake ulifuata mikondo ifuatayo: kwanza aliupinga kimawazo (hakutamka hadharani isipokuwa miongoni mwa makomredi wake wa karibu), lakini mbio mbio baada ya kutafakari zaidi aliuona kwa ulikuwa na maslahi kwa itikadi ya Umarx na Ulenin kwa vile Tanganyika ni nchi kubwa yenye wakaazi wengi itakuwa rahisi kuzipenyeza fikra za kiitikadi za Usoshalisti wa Kisayansi kuwafikia Watanganyika na pengine hata kuvuka mipaka ya Tanganyika.

Msimamo huo, kwa kweli, ulikuwa sahihi. Yaliyojiri baadaye yalithibitisha kwamba aliagulia sawasawa. Haikuchukua muda baada ya Muungano kusimama kusikia misamiati ya kisiasa na kijamii ya wananchi wa Tanganyika yakibadilika na yakiigiza yale ya Zanzibar. Dhana kama, kwa mfano, za ubepari, ubwanyenye, tabaka za kijamii, usoshalisti, unyonyaji, zikaingia katika misamiati ya kawaida ya wananchi wa Tanganyika.

Tija nyingine kubwa iliyopatikana ni ile ya kumjulisha Nyerere kwa Wakomunisti wa Kichina na kwa Wachina hao kuwa tayari kuisaidia Tanzania katika nyanja tafauti za maendeleo ikiwa pamoja na ujenzi wa Reli ya Tazara baina ya Tanzania na Zambia.

Juu ya yote hayo, na juu ya hata msimamo wake wa Umajumui wa Afrika, Muungano wa Tanzania ukimla roho Babu. Sidhani kama kuna Mzanzibari mwenye chembe ya uzalendo asiyeionea uchungu nchi yake kwa jinsi inavyokuwa inazidi kuonewa na mshirika wake katika Muungano kila miaka ikisonga mbele.

Babu akilijadili sana suala hili faraghani na hadharani. Gazeti la Dira la Zanzibar, ambalo sasa ni marehemu, lilikuwa na makala katika toleo lake la Juni 13-19, 2003, yenye ilani “Muungano huu ni wa bandia”. Hiyo nukuu ni ya maneno ya Babu kwenye mahojiano aliyofanyiwa kabla wakati wa uhai wake.

Katika makala hayo, Babu amenukuliwa akitamka mengi hata kusema kwamba yeye binafsi hakuwa akijali kama serikali ingemrejesha Sultani (Seyyid Jamshid bin Abdallah) kama raia wa kawaida. Kuhusu Muungano, Babu alisema kwamba akipinga lile wazo la kuwa na Muungano wa serikali tatu. Akitaka Muungano wa aina nyingine: “wa mikataba sio wa Katiba.” Alishauri kwamba pawepo na Muungano wa Mikataba kama ule wa Ulaya (EU) wenye kufuata mkataba wa Maastricht.

Babu alikumbusha kwamba daima Zanzibar imekuwa ikiathiri yanayojiri Bara, kwa maana ya Tanganyika. Alisema kwamba siku zote Zanzibar ilikuwa kituo cha maendeleo na kwamba Ukiristo, Usoshalisti na Umarx vyote vilikuja Afrika kupitia Zanzibar.

Ahmed Rajab ni mwandishi wa kimataifa na mchambuzi. Ana shahada ya Falsafa kutoka Birkbeck, Chuo Kikuu cha London, Postgraduate Diploma (Urbanisation in Developing Countries) kutoka University College, London na shahada ya MA (African Political Economy na Modern African Literature) kutoka Chuo Kikuu cha Sussex.

Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; X:mad:ahmedrajab

2022 Gazeti La Dunia

Screenshot_20230726-210823_Chrome.jpg
 
View attachment 2700017
Asante.
 
Back
Top Bottom