Yasinsta Cornel: Ubadhirifu na Ucheleweshaji wa Miradi ya maji; Tatizo kwa upatikanaji wa maji nchini,

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
617
1,541
Waziri Kivuli wa Maji wa ACT Wazalendo Ndg. Yasinta Cornel Awiti amesema kuendelea kwa vitendo vya uzembe na ubadhirifu katika miradi ya maji ni chanzo cha tatizo la upatikanaji duni wa huduma ya maji nchini. Hivyo, ametaka uwajibishwaji wa watu wote wanaohusika na vitendo vya uzembe na ubadhirifu ili kuhakikisha matumizi ya fedha za umma yanaenda kutatua changamoto sugu za maji.

Kauli hiyo ameitoa alipokutana na waandishi wa habari leo Ijumaa Mei 10, 2024 katika uchambuzi wa bajeti ya wizara ya maji kwa mwaka wa fedha 2024/25, katika Ukumbi wa Hichilema Makao Makuu ya ACT Wazalendo.

Aidha, Waziri Kivuli Yasinta ameonyesha kusikitishwa na mwenendo wa kushuka kwa bajeti kiasi cha shilingi bilioni 128.5 sawa na 17% kutoka shilingi bilioni 756.2 mwaka 2023/24 hadi shilingi bilioni 627.7 mwaka huu. Amesema wakati ikishuhudiwa kusua sua kwa miradi mingi ya maji kutokana na ufinyu wa bajeti lakini Serikali inaenda kupunguza bajeti. Hivyo, ameitaka Serikali kuongeza bajeti kufikia wastani wa trilioni 2 kwa mwaka ndani ya miaka 5 ili kukabiliana na changamoto za ukosefu wa maji.

Kwa upande mwingine, amezungumzia suala la malalamiko ya wananchi ya ucheleweshwaji wa kuunganishwa na huduma za maji. Amesema kwa mujibu wa CAG wananchi wanacheleweshewa kuunganisha kati ya siku 5 mpaka siku 408. Na pia, amesema anaunga mkono matumizi ya dira za malipo ya kabla ili kuondoa ubambikiaji wa ankara za maji.

Vile vile, ameeleza tatizo la usambazaji na upatikanaji duni wa huduma za maji hasa vijijini kutowekewa mkazo na Serikali. Amekosoa taarifa ya Waziri wa maji juu ya hali ya upatikanaji wa huduma za maji safi ambayo ametaja ni asilimia 79.6. Waziri Kivuli amesema asilimia hizo zinatajwa kwa maana miradi iliyofika sio upatikanaji wa huduma ya maji. Taarifa ya Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS 2023) inaonyesha miradi ya maji iliyowekezwa vijijini takribani asilimia 38 haifanyi kazi kwa ufanisi au imekoma kabisa kutoa huduma na zaidi ya vijiji 497 nchini Tanzania havijafikiwa na mradi wowote wa maji.

Pia, amezungumzia kuhusu ucheleweshwaji wa kukamilika kwa miradi ya maji. Amesema changamoto ya kuchelewa kukamilika kwa miradi ya maji ni kubwa jambo linalosababisha tatizo la upatikanaji wa maji. Amesema ipo orodha kubwa ya miradi iliyoanzishwa ingine tangu 2014 hadi leo haijakamilika na inapelekewa fedha kila mwaka.
Amehitimisha kuwa uchambuzi huo unaonesha kuwa mwenendo wa bajeti ya Maji haulengi kumaliza tatizo la maji nchini. Miradi mingi bado haijakamilika na iliyokamilika haitoi maji, lakini bado kasi ya wananchi kuvuta maji ni ndogo sana kutokana na gharama kubwa za kuunganishwa na huduma hiyo.

Imetolewa na;
Ndg. Abdallah Khamis
Mkuu wa Habari na Mawasiliano-ScaRo
ACT Wazalendo
Mei 10, 2024.
 
Back
Top Bottom