Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,478
- 39,997
Mkuu pengine nazungumza lugha usoifahamu..Vatican ni Taasisi ambayo imeunda nchi ndani ya Italy..Labda nikuulize wewe kwa nini Vatican hakuna watoto wanaozaliwa? Kwa nini raia wa Vatican ni wazawa toka nchi tofauti duniani ambao uraia wao unatokana vyeo vyao ktk dini ya Katoliki..Au labda nambie wewe hao raia wake wanazaliana vipi? na pengine nijulishe kama wapo raia wasiohusiana kabisa na Kanisa! maanake nijuavyo mimi Vatican ni Taasisi iliyopewa au chukua eneo na kulifanya nchi ya utawala wa kanisa hilo.
Mkuu wangu tusibishane ili mradi kubishana kwa sababu swala la kuita nchi ni mfumo tu tuloweka sisi na umekubalika..Hata Macca wakiamua kuifanya nchi wanaweza ingawa najua fika itakuwa kaazi kubwa na wala sii utaratibu unaokubalika kiislaam. hivyo haiwezekanai kidini lakini kidunia inawezekana na ikakubalika.
Nitarudia kusema kama hakuna Taasisi ya Katoliki nchi hiyo haipo..hakuna vyama wala wananchi wanaozaana kujenga jamii hiyo. Hata wewe kesho unaweza kuwa raia wa Vatican pengine Pengo ana ganda la Vatican na kama hanaipo siku atakuwa..hakuzaliwa wala hana asili yoyote ya uzawa wala kuishi....who knows!
Vatican ni Taasisi iliyochukua eneo muhimu la kidini toka mji wa Rome na kuifanya nchi ili Pope aweze kuongoza dunia ya Kikatoliki..Hapa ndipo wanapoweza ku control makanisa yote duniani
na wafuasi wake ambao hata wewe pamoja na kuwa Mtanzania unashirikishwa ktk policies and authority of the papacy popote ulipo..
ifupi, Vatican wanaishi viongozi wa dini na raia wake ni waumini wote wa kanisa katoliki sehemu yoyote duniani....Go figure!
Kwanza nikushukuru kwa taarifa hizi nyingi na madai haya mengi juu ya Vatican na Ukatoliki ambayo umeyapendekeza kama ni ukweli kabisa. Ninaamini kuwa unayaamini uliyoyoyasema kuwa ni kweli na hivyo wengine wanaosoma wayapokee pia kama ni ukweli. Ni kusudio langu kuonesha kuwa yote uliyoyasema hayakubaliani na ukweli wa kihistoria na kihalisia kuhusu Vatican, Ukatoliki na Wakatoliki.
Umesema mambo kadhaa ambayo labda niyatenganishe kutoka insha fupi hapo juu. Umedai kwamba:
- Vatican ni Taasisi ambayo imeunda nchi ndani ya Italia baada ya kuchukua au kupewa ardhi ili Papa atawale dunia ya ukatoliki (hivyo Vatican siyo nchi)
- Vatican siyo nchi kwa sababu uraia wa wananchi wake hautokani na uzawa
- Mtu yeyote anaweza kuwa raia wa Vatican (kutumia maneno "hata wewe waweza"
- Vatican wanaishi viongozi wa dini
- Raia wake ni waumini wote wa Kanisa Katoliki sehemu yoyote duniani.
Hofu yangu ni kuwa baadhi ya watu ambao wamesoma maelezo yake yawezekana wameyachukulia kama ni ukweli bila kuhoji msingi wake au ukweli wake. Na kutoka katika kuyaamini kwa sababu yamekaa kama "facts" basi na wao wanaweza kujikuta wanayarudia kwa watu wengine na taarifa sahihi ikaendelea kupitisha kutoka mtu mmoja kwenda mwingine.
1. VATICAN NI TAASISI
Hili ni jibu rahisi ambalo mtu yeyote anaweza kuangalia kwa urahisi kwenye intaneti au maktaba. Jina kamili ni Nchi ya Vatican City (Vatican City State). Jina la "Vatican" ni la zamani na limetangulia Upapa kwani linatokana na jina la Kilatini "Mons Vaticanus" yaani "Mlima wa Vatican". Historia inasema ni katika mlima (kwa kweli ni kilima) ndipo Mt. Petro aliuawa kwa kusulubiwa kichwa chini miguu juu na ni juu ya kabuli lake ndipo kanisa la Mt. Petro lilijengwa ambalo baadaye limeendelea kukuzwa hadi kufikia hilo tunalolijua kama St. Peter's Basilica.
Mapapa kwa muda mrefu walikuwa na utawala wa Kanisa na utawala wa kisiasa (secular) na wakiwa na kazi hizo mbili waliweza kutawala maeneo mbalimbali ambayo yalijulikana kama "Majimbo ya Papa – Papal States". Mfumo huu wa upili (duality) wa Papa kuwa mtawala wa Kanisa na maeneo ulidumu kwa karibu miaka elfu hadi mwanzoni mwa karne ya 19 ambapo Ufalme wa Italia ulipoundwa. Tukumbuke kuwa Italia wakati huo ilikuwa ni mgawanyo wa falme na himaya ndogo ndogo kama za Sicily, Tuscany, Sardinia, Savoy, Nice n.k kila mmoja ikiwa na mkuu wake na Papa naye alikuwa na eneo lake.
Vita kati ya falme hizo na watawala wa Austria na Ufaransa na wenyewe kwa wenyewe ndizo zilizosababisha hatimaye Waitaliano kutaka kuungana chini ya kiongozi au uongozi mmoja. Hadi inafikia 1870 maeneo na mali ya Papa yalikuwa katika hatari ya kuchukuliwa na watawala wapya wakiongozwa na ufalme wa Piedmont (makao yake makuu Turin). Kuanzia wakati huo hadi 1929 kulikuwa na kile kinachoitwa na wanahistoria kuwa ni "Swali kuhusu Roma" yaani katika Italia hiyo mpya Papa (ambaye alikuwa anatawala pia maeneo yake akiwa na mabalozi na nchi nyingine zikiwa na ubalozi naye atakuwa nani wakati taifa sasa ni Ufalme wa Italia?
Na yeye Papa alikataa kuondoka hata Vatikani hadi suala hilo litatuliwe kwani kwa upande wake hakuwa tayari kumtambua mfalme mpya wa Italia. Kulikuwa na makubaliano ambayo yalimruhusu Papa kuendelea kufanya kazi zake kupokea mabalozi n.k kama wakuu wengine wa nchi.
Mfalme mpya wa Italia hakumnyanyasa sana Papa lakini alitaifisha mali kadhaa za Papa ikiwemo maskani yake ya Quirinal ambayo leo hii ndio maskani rasmi ya Rais wa Italia. Papa Pius IX ndiyo alikuwa mtawala wa mwisho wa tawala mbalimbali za kipapa (yale maeneo niliyoyataja hapo juu) baada ya Jiji la Roma nalo kuchukuliwa na kumfanya ajitangaze kuwa amekuwa "mfungwa ndani ya Kuta za Vatican".
Mgongano kati ya Ufalme wa Italia na Papa ulimalizika kwa makubaliano maarufu yajulikanayo kama Makubaliano ya Lateran (Unaweza kutafuta yanaitwa Lateran Treaty) ambayo yalimaliza swali la Uroma kwa kuitambua Vatican kama nchi hakimiya (sovereign state) na kuhakikisha mali zake nyingine hazichukuliwi n.k Kutokana na hilo Vatican siyo sehemu ya Italia ni nchi kamili iliyoundwa kwa mkataba halali uliouingiwa kati ya Benito Musolini kwa niaba ya Mfalme Victor Emmanuel III na Waziri wa Mambo ya Nje wa Papa Cardinali Gaspari kwa niaba ya Papa Pius IX.
Ni vizuri nitenganishe vitu ambavyo kwa mtu asiye Mkatoliki (na hata Wakatoliki wengine) hawavielewi. Kuna kitu tunakiita "Holy See" na kuna "Vatican City State". Mambo mengi tunayoyaona yanafanywa na Papa au Kanisa Katoliki n.k yanafanywa na Holy See na siyo nchi ya Vatican.
Holy See (Kiti cha Papa a.k.a Upapa) ni utawala wa kidini wa Baba Mtakatifu ndani ya Kanisa Katoliki ambao huundwa na Papa mwenyewe na Kuria ya Roma wakati Vatican City State inaongozwa na Gavana wa Vatican chini ya Papa. Vyote viwili vinahusiana lakini si kitu kimoja. Utawala wa Papa basi siyo jamhuri (yenye kuhitaji vyama vya siasa kupiga kura n.k) bali ni Ufalme kamili – absolute monarchy. Maana yake ni kuwa Papa ana mamlaka yote ya kutunga sheria, haki, na utawala. Kutokana na hili utaona kuwa mabalozi wote hupelekwa Holy See na siyo Vatican na hata kile tunachoita Ubalozi wa Vatican kimsingi ni ubalozi wa Upapa – mfalme.
Kanisa Katoliki la Tanzania au la mahali linauongozi wake katika mambo ya askofu wake. Hivyo balozi wa Holy See hayuko juu ya Pengo kwani yeye yuko kwa kumwakilisha mfalme (Papa) kwa serikali ya Tanzania na Tanzania inapeleka balozi wake huko. Kutokana na ukweli kuwa Holy See ndiyo yenye mlolongo wa huduma ya kibalozi ya zamani zaidi duniani kuliko nchi nyingine yeyote (kuanzia 325AD) nchi kadhaa zina mabalozi wake huko. Miongoni mwa nchi za Kiislamu ambazo zinatambua hili na zina uhusiano wa kibalozi na Holy See ni pamoja na:
Morocco
Misri
Iran
Iraq
Uturuki
Palestine
Azeirjabain
Tanzania kama nchi hizo nayo ina ubalozi kwa Papa na hili si tatizo kuwa na ubalozi na taifa la kidini. Tanzania ina balozi Saudi Arabia ambao ni ufalme, tuna ubalozi Jordani ambao ni Ufalme na tuna mahusiano ya kibalozi na Falme za Kiarabu. Hizi zote ni falme ambazo zina msingi wa kidini kama vile ulivyo Upapa na dini ya Kikatoliki. Hakuna mtu ambaye amewahi kuhoji kwanini Tanzania ina husiana na nchi hizi au kwanini Jordani ina ubalozi Tanzania wakati ni ufalme wa utawala wa Kiislamu? Kumbe la msingi ni kuwa kwa vile hizi zote ni nchi halali na tunazitambua hivyo hakuna tatizo la kuwa na balozi nazo. Hili ni kweli tangu wakati wa Nyerere hadi leo hii.
Kwa hiyo, Vatican siyo "taasisi" bali ni nchi kamili, iliyoundwa kufuatia mkataba wa Laterani ambaye mkuu wake ni Papa. Haijawahi kuchukua eneo la nchi nyingine au mtu mwingine ili liwe chini ya Papa bali Papa ndiye alinyang'anywa maeneo aliyokuwa akiyatawala kwa karibu miaka elfu kufuatia vita vya Waitalia vilivyoiunganisha Italia. Kwa mkataba wa Laterani na nyongeza yake aliachiwa hiyo Vatican City pamoja na maeneo mengine ambayo yako nje ya kuta za Vatican (kama maktaba, makanisa yaliyopo sehemu mbalimbali za Italia na magazi mengine ya kipapa).
Kwa mtu yeyote anayejisikia kubisha anatakiwa aeleze ni Vatican City imetoka wapi na ilikuwa taasisi kwa utaratibu gani?
2: HAKUNA URAIA WA KUZALIWA HIVYO SI NCHI
Kwanza, niseme si kweli; Uraia wa Vatican unaweza kupatikana kwa watoto na wenza wa maofisa wanaofanya kazi Vatican. Kwa watoto hadi watakapofikisha miaka 25. Uraia ni suala la kisheria na kila nchi ina utaratibu wake. Mkataba wa Laterani nilioutaja hapo juu ndio unasimamia uraia wa Vatican vile vile. Raia wa Vatican ambaye anapoteza uraia wa Vatican au wa nchi yake (kwa wale wenye uraia wa nchi mbili) basi kwa mujibu wa Laterani anapata uraia wa Italia automatically.
Hadi mwaka mwishoni mwa 2005 kulikuwa na watu 557 wenye uraia wa Vatican. Miongoni mwao ni:
Papa
58 -Makadinali (ambao wanaoishi au kufanya kazi karibu na Roma). Ni muhimu kutambua kuwa siyo makardinali wote wenye uraia wa Vatican. Kanisa Katoliki lina makardinali 199 walio hai (hadi naandika hii) ambao kati yao ni 109 ndio wanauwezo wa kupiga kura kumchagua papa (wapiga kura wanatakiwa wawe ni wale chini ya miaka 80).
293 Waklegi (mapadre, mashemasi) wanaofanya kazi katika balozi mbalimbali za Holy See pote duniani. Baadhi yao ndio kama yule Askofu Mkuu Novatus Rugambwa ambaye ameteuliwa mapema mwaka huu kuwa Balozi wa Papa huko Sao Tome na Principe.
62 Watendaji wengine wa kanisa wanaofanya kazi Vatican
101 Maafisa wa vikosi vya usalama vya Vatican wakiwemo wale Swiss Guard wanaomlinda Papa
43 Walei wengine wanaofanya kazi hapo au familia na watoto wao.
Na Vatican inatoa passport za utumishi na za kibalozi. Passport kama hizi hutolewa na taasisi kama Umoja wa Mataifa au na taasisi nyingine zinazotambulika kimataifa. Taasisi kama Umoja wa Afrika na yenyewe inatoa passport zake za utumishi na wakuu wa nchi zote 53 za Umoja huo wamepewa passport hizo pamoja na watendaji wake wengine na watu wengine mashuhuri. Kutolewa passport si lazima kuwa suala la uraia ni suala la kumtambulisha msafiri kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine na zinatumika kwa makubaliano ya kutambuliwa kwa taasisi inayotoa. Naamini hata OIC inatoa passport za namna hii kwa watendaji wake.
3: MTU YEYOTE ANAWEZA KUWA RAIA WA VATICAN
Ni kweli mtu yeyote anaweza kuwa "raia wa Vatican" endapo tu mtu huyo ametimiza masharti ya uraia huo kwa mujibu wa Katiba ya Vatican na makubaliano ya Vaticani. Siyo rahisi kuupata uraia wa Vatican. Kwani hautokani na damu tu au kuwa naturalized bali unatokana na huduma (service) au ofisi ya mtu na kutoka hapo ndipo kwa watoto au wenzi wanaweza kuupata uraia huo.
4: VATICAN WANAISHI VIONGOZI WA DINI
Hili ni kweli kiasi. Lakini siyo viongozi wa dini tu. Wanaishi wafanyakazi wa Taifa la Vatican na raia wake vile vile wakiwemo watoto wa wafanyakazi na watendaji wengine ambao si viongozi wa dini.
5:WAUMINI WAKATOLIKI POTE DUNIANI NI RAIA WA VATIKANI
Hii si kweli kabisa. Wakatoliki wote siyo raia wa Vatican. Kama nilivyosema hapo juu uraia wa Vatikani hauji kwa ubatizo au kwa kuitwa Mkatoliki unakuja kwa mujibu wa mkataba wa Laterani wa 1929. Hii ina maana kwamba Vaticani licha ya kuwa ni taifa dogo zaidi vile vile ni taifa lenye raia wachache zaidi (hawazidi 1000). Na Vatican City haina mamlaka ya aina yoyote juu ya Mkatoliki kuhusu uraia wake. Papa ana mamlaka katika masuala ya imani na dini kama kiongozi wa dini lakini siyo kama mfalme wa wakatoliki wote duniani.
Ni muhimu kutambua kuwa kama mfalme Papa ni sovereign (hakimiya) hivyo haitaji Vatican City ili kuwa sovereign. Lakini uwepo wa Vatican City unasaidia tu katika kutekeleza majukumu yake ya kisiasa na kiutawala.
Nitawaacha wengine waendelee kuchangia suala la kujiunga na OIC kwani nilishatoa maoni yangu miaka mitatu iliyopita na kujirudia itakuwa ni kurudia rudia kitu kile kile. Mjadala mzuri sana.