Sumu nne zinazoua ubora wa siasa ya nchi yetu!

Feb 15, 2013
14
3
SUMU NNE ZINAZOUA UBORA WA SIASA YA NCHI YETU!

Tanzania ni nchi iliyosifika na kujizolea umaarufu kwa miaka mingi sana kwa utulivu na kuwa na mfano wa kuigwa katika utaratibu wa kubadilishana uongozi kwa amani.Tumeshuhudia nchi nyingi zikiingia katika machafuko na vita hasa kipindi cha uchaguzi unapokaribia au baada ya matokeo kutangazwa,pia zipo nchi nyingi bado ambazo viongozi wake wamekaa kwa muda mrefu sana madarakani na kuchukuliwa kama vile madikteta na wananchi kuonyesha kuwachoka na kutaka kuleta mabadiliko ya lazima.

Hapa kwetu Tanzania utaratibu wa kubadilishana madaraka ni matunda ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye aliamua kwa makusudi bila kulazimishwa kuachia madaraka na kulipa neno “kung’atuka” umarufu sana wakati akiondoka madarakani.Wakati mwalimu anaondoka madarakani alitaja sababu tatu za kuondoka kwake lakini mojawapo alisema,kama katika miaka takribani 24 aliyokaa madarakani alishindwa kufanya kile alichokuwa anatakiwa kufanya hivyo basi hata akipewa muda zaidi hataweza kuleta mabadiliko yoyote.

Pamoja na utamaduni huu kuwa mzuri na kufuatwa kwa muda wote tangu alipoondoka bado mwenendo wa siasa za nchi yetu umezidi kubadilika na kukabiliana na changamoto mpya kila siku.Kwa upande mwingine ni kitendo cha viongozi na wananchi “kurelax” ama kubweteka na sifa za mara kwa mara kuwa Tanzania ni kisiwa cha amani.Na hapa wengi wameshindwa kutofautisha katia ya AMANI NA UTULIVU na IMANI na UVUMILIVU,nadhani sisi tuko kundi la pili kwa sasa tulishahama lile la kwanza.Mara nyingi tumefikia kiwango cha kufikiri kuwa yale yanayowapata nchi nyingine,sisi hayawezi kutupata kabisa.Tunapoangalia tatizo la ukabila Kenya tunajisemea mioyoni mwetu kuwa mambo haya hayana nafasi hapa kwetu,ila mwenendo wa sasa uanonyesha tofauti.

Mwalimu nyerere alisema ili nchi iendelee inahitaji mambo 4:

(i)WATU-Hatuna upungufu katika hili sensa ya mwisho iliyofanyika ilisema tuko milioni 45.

(ii)ARDHI-Sisi ni matajiri wa ardhi afrika mashariki na bado hatujaweza kuitumia,mfano kwenye kilimo tunatumia 4% ya ardhi yote inayofaa kwa kilimo.

(iii)UONGOZI BORA-Hapa bado sana, tunajikongoja kwa mbali mno tukitafunwa na rushwa,kukosa uwajibikaji na matumizi mabaya ya madaraka na kufuja mali za umma.

(iv)SIASA SAFI-Ya kwetu bado ni chafu mno na inahitaji kusafishwa hasa,na hili ndilo ninalotaka kuzungumzia hapa.


  • Nguvu ya pesa na rushwa

Jambo la kwanza la hatari linalokabili mwenendo wa siasa yetu ni matumizi makubwa ya pesa katika kusaka uongozi na kushawishi wapiga kura.Hili linashindana kati ya vyama na vyama,ndani ya chaguzi za vyama na kati ya vyama na wananchi.Mfumo wa uendeshaji wa siasa za nchi yetu kwa sasa umetoa mwanya mkubwa kwa pesa kuwa ndiyo nguzo ya ubora wa uongozi.

Kwenye maeneo mengi kipindi cha uchaguzi kimebatizwa kuwa ni kipindi cha mavuno,viongozi wa ngazi ya chini ya vyama na wananchi wa kawaida hufurahia kipindi hiki.Sifa ya kwanza ya mgombea makini kwa leo si sera zake bali ni pesa zake kwanza.Jamii yetu ni maskini sana hivyo pesa ni lazima kiwe kivutio cha nguvu kubwa kwao,mfumo umeachia hili likaota mizizi na kuwa la kawaida.Huko nyuma lilitungiwa hadi sheria na kubadilishwa jina kutoka rushwa kuwa takrima,jina tofauti lakini nia ni ileile;kuwapumbaza watu macho na kuwafanya wamchague mtu Fulani kwa fedha zake.Ni lazima niweke wazi kuwa inawezekana kabisa mtu kuwa na fedha nyingi na kuwa na uwezo mkubwa wa uongozi,inawezekana.Ila katika hali yoyote ile pesa haitakiwi kutumika kama kishawishi katika kushinda uchaguzi kwa lugha nyepesi kununua kura.

Katika chaguzi zilizopita hapa nchini zipo sehemu waliokuwa wanatafuta vyeo walikuwa wanagawa pesa katika vikao vyao kwa wajumbe wanaohusika katika kupitisha majina katika ngazi mbalimbali na wengine hata kugawa vitu kwa wananchi maskini hasa katika chama tawala CCM; wengine waligawa unga, mchele na hata nguo katika maeneo mbalimbali.Kwa mwananchi wa hali ya chini ambaye kula yake ni shida, mambo haya madogo yanaweza kumshawishi na kubadili uamuzi wa mwelekeo wa kura yake.

Mambo mawili ya msingi yanatakiwa kufanyika katika jambo hili; moja ni kuendelea kutoa elimu ya uraia kwa wancnhi wetu wote.Maeneo kadhaa hasa ya mijini siku hizi wameelimika kwa kiwango cha kuridhisha na si ajabu ukaona mtu hana hata pesa akashinda uchaguzi na Yule aliyekuwa akitumia pesa zake kuhonga wapiga kura anashindwa vibaya.Elimu iende vijijini zaidi kwani hasa huko ndiko kuna wapiga kura wengi na wanaodanganyika kwa urahisi kutokana na hali ya umaskini inayowakabili.

Pia katika kukabiliana na hilo ni lazima taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa (PCCB) iongezewe watenda kazi na ifanye kazi yake usiku na mchana.Kuchukia rushwa ni utamaduni unaojengwa na watu kuhofia madhara na aibu ya kukamatwa au kuhusishwa na rushwa.Ni lazima ionekane waziwazi kuwa swala hili linashughulikiwa tena kwa vitendo na uwazi ili kumfanya kila mtu aogope kujihusisha na rushwa na asione ufahari kabisa.Hatari ya kuchagua viongozi kwa misingi ya rushwa ni kupata viongozi wasio na uwezo lakini pia kupata viongozi wenye nia ya kutumia nafasi zao kibiashara na si kutumikia waliowachagua.Lakini hatari nyingine kubwa ni kuwanyima fursa wale ambao wana uwezo na nia ya dhati kuongoza jamii zao kwa sababu tu ya kukosa pesa ya kushawishi kuchaguliwa.

Ni muhimu mfumo wetu wa kuchagua viongozi wa siasa ukajikita katika uwezo wa mtu kimawazo na kifikra kuliko uwezo wa kifedha zaidi,nadhani uwezo wa kiongozi kuona mbali na kuijua njia anayotaka kupeleka watu atakaowaongoza ni muhimu zaidi kuliko uwezo wake wa kifedha.

Kwa kuruhusu matumizi makubwa ya fedha katika kusaka nafasi,watu wengi wanaotafuta uongozi wamejikuta wakitumia rasilimali nyingi ya fedha na muda katika kuipata nafasi hiyo,matokeo yake wakishaingia katika nafasi zao kutumia muda mwingi kujiweka sawa kwa kurejesha gharama walizotumia katika kampeni na kuwa na muda mchache kuwatumikia wananchi.Kiongozi anapotumia muda mchache kuwatumikia wananchi wake ni kusema kuwa anazorotesha maendeleo ya eneo lake analoliongoza na Taifa kwa jumla.Matumizi ya pesa katika kushawishi kupata nafasi za kisiasa ni hatari kwa siasa ya nchi yetu.



  • Historia ya jina lako katika siasa

Mwaka 2008 nilipata fursa ya kuhudhuria kikao kimoja kilichohusisha viongozi wa ngazi ya juu ya serikali yetu.Katika kusalimiana tukiwa nje ya kikao hiko nikajikuta niko na watu wenye nafasi kubwa sana serikalini, katika hali niliyoitarajia nikakuta wote wanafahamina isipokuwa mimi sifahamiki na wote.Ndipo mmoja kwa ujasiri akaniuliza,”wewe ni nani”, nikamjibu kwa kujiamini naitwa Joel Nanauka.Baada ya hapo swali lililofuata lilikuwa”Nanauka alishawahi kuwa nani/kushika nafasi gani”?.

Siasa ya Leo ndiyo inakwenda hivyo hapa Tanzania, baba yako alikuwa nani? lakini swali ambalo tunakosa ujasiri wa kujiuliza hata hao wenye majina kwa sasa wapo ambao baba zao walikuwa wakulima tu wakaida.Ingawa inawezekana kabisa(si lazima iwe hivyo) baba akiwa kiongozi na mtoto akawa kiongozi mzuri,pia inawezekana kabisa baba asiwe kiongozi kabisa na mtoto akawa kiongozi mzuri.

Siasa ya sasa inaonekana kama inachukua “shape” ya koo,ndugu na jamaa Fulani,hata kama wapo wapya wengi tu wanaoingia lakini ukweli unabaki palepale kuwa swala la baba yako alikuwa nani linaendelea kujipenyeza na kupata mizizi,wengi wameendelea kutumainia historia zao au wale wanaowafahamu kuwabeba katika harakati zao.Hivi karibuni nilikutana na msemo mpya katika siasa “BMW” wakimaanisha baba,mama,mtoto.Ni msemo unaotka kueleza kuwa siasa sasa inachukua mkondo wa kindugu zaidi.

Hakuna ubaya kuwa na ndugu wote mkawa katika uongozi wa kisiasa lakini yapo mambo ya msingi ya kuzingatia;

(i)Huyo ndugu anayepewa nafasi ana uwezo unaoendana na hiyo nafasi au anapewa kwa sababu ni ndugu?

(ii)Uteuzi au uchaguzi wa ndugu huyo katika nafasi ulifanywa kwa haki kwa kuzingatia (process) michakato halali iliyowekwa au alipewa upendeleo wa kutopitishwa katika utaratibu maalumu kwa sababu ni ndugu

(iii)Je,nafasi anayopewa haitakuwa na mgongano wa kimaslahi kama mtu na ndugu yake pale itakapohitajika mmmoja amwajibishe mwingine au mmoja ni sehemu ya kumtathmini/kumkagua mwingine?

Mambo haya yakizingatiwa yataepusha watu kupata nafasi kwa kutumia historia ya MAJINA YAO badala ya SIFA ZAO.Hata kwenye kampeni siku hizi tumesikia minon’gono utasikia,mgombea huyu ametumwa na bwana mkubwa.Na kwa sababu bwana mkubwa yuko kimya na viongozi wa eneo hilo hawataki kumwaibisha bwana mkubwa utaona jinsi atakavyobebwa na kuhakikisha anashinda hata kama uwezo ni mdogo.

Hii staili ya baba yako alikuwa nani,ni hatari kwa taifa lijalo kwani itajenga tabaka mbili ya WATAWALA na WATAWALIWA.Na watu wakishaanza kujenga hisia za kuwa kuna tabaka ambalo ndilo huamua hatima yetu bila ridhaa yetu huanza kufikiria kuhusu UASI na KISASI.


  • Udini na ukabila

Udini na ukabila unashika chati kila kunapokucha, siku hizi ni kawaida kusikia watoto wa shule ya msingi wakihesabu mawaziri waislamu ni wangapi na mawaziri wakristo ni wangapi.Kila Rais anapofanya uteuzi wake ni kawaida watu kuangalia uwiano uliopo wa kidini kati ya wale aliowateua katika nafasi hizo.

Tumefika hapo kwa sababu kila dini inahofu kuwa kuna eneo ambalo dini isiyo yake inapendelewa katika nafasi za kiuongozi si kwa sababu ya uwezo wa mtu huyo bali kwa sababu ya dini ya mtu huyo.Ukitembelea mitandao ya kijamii siku hizi watu hawana sitiri tena,limeshakuwa tatizo dhahiri lisilojificha kushutumu dini flani au chama Fulani na kukiambatanisha na siasa za kidini.

Uchaguzi unapofika,makanisani na misikitini kampeni zinapigwa,suala si sifa za mgombea tena suala kubwa ni dini yetu.Bahati mbaya hutokea pale ambapo mgombea mwenye uwezo mkubwa wa uongozi dini anayotokea ina wafuasi wachache katika eneo hilo basi atapoteza nafasi hiyo kwa sababu wale wa dini nyingine watampigia kura wa dini yao hata bila kuangalia uwezo.

Mtu anapotumia kigezo cha dini Kama ndio kigezo kikuu katika kuchagua kiongozi anadhoofisha uwezo wake wa kufanya maamuzi ya busara ili kupata kiongozi bora kwa manufaa ya jamii aliyotoka na Taifa kwa ujumla.

Wakati mwingine kwa kutambua udhaifu wa jamii yetu wako wanasiasa ambao hutumia karata ya dini na ukabila katika kuomba kura katika maeneo Fulani Fulani.Nchi yetu ni kubwa na watu huweka makazi hata katika mikoa ambayo sio asilia yao, lakini kama mtu ameishi hapo kwa miaka mingi ameifahamu jamii hiyo na kuwa sehemu ya jamii hiyo kutozughumza kwa ufanisi lugha ya watu hao haipaswi kuwa kigezo cha kumnyima uongozi.

Ni muhimu taratibu za kampeni zikaeleza wazi na kupinga na kueleza adhabu kali atakayeikabili yeyote ambaye atatumia lugha yake ya asili ya eneo hilo kupigia kampeni kwa nia ya kuonyesha kuwa mpinzani wake hafai kwa sababu hiyo,kwa kuzingatia kuwa lugha rasmi ya nchi ni Kiswahili na nio inatumika katika vyombo vya uwakilshi.Matumizi ya lugha za asili yaruhusiwe sehemu zenye jamii za kiasili ambazo bado hawajachanganyika na jamii zingine kama vile wahadzabe.Tena katika sheria ni vyema kueleza utaratibu wa kutumia wakalimani(watafsiri wa lugha) katika jamii kama hizi.Matumizi ya karata ya dini misikitini na makanisani kwa wagombea iwe ni sababu tosha ya kumfanya mgombea huyo kupoteza sifa ya uongozi mara moja.

Kwa upande wa viongozi wenye dhamana kwa sasa,suala la udini na ukabila linatakiwa liendelee kukemewa mara kwa mara tena kwa vitendo vya waziwazi.Mtu yeyote anayeonyesha kutumia ukabila au dini yake kwenye siasa aonywe hadharani mbele ya watanzania wote.Nakumbuka mwalimu Nyerere aliwahi kusema,bado suala la ukabila liko ndani ya damu ya watanzania.Akieleza kisa cha waziri wake mmoja akiwa kwenye ndege na ilipotaka kupata matatizo kwa mara ya kwanza akasema kwa kiingereza ”My God”,mara ya pili akasema kwa Kiswahili”mungu wangu” mara ya tatu akasema neno la kisukuma”maweee”,hii ni kuonyesha hata kwa viongozi wa ngazi ya juu kabisa bado ukabila/udini unaweza kuwa bado uko ndani yao.

Tulishuhudia miaka ya hivi karibuni vijana wa chama cha mapinduzi na kile kilichoitwa azimio la bagamoyo wakisema Rais ajaye hawezi kutoka kaskazini,kwa nini?atatoka wapi?wao ndio wanajua.Lakini ni kiongozi gani aliwakemea?ni kama vile ilonekana sawa kabisa,haya ndiyo mambo yanayofanya ajenda ya ukabila na udini katika siasa kushika hatamu.

Ni kweli huwezi kuzuia watu kufikiria kupendelea dini/kabila yao,lakini inawezekana kabisa kuzuia vitendo vya watu hao kupendelea dini au kabila yao.Kazi ya kiongozi ni kuonyesha anachukizwa na jambo hilo,haifurahii na hayuko tayari kulivumilia hata kidogo.Kila linapotokea mara moja lazima likemewe kwa nguvu zote bila kujali aliyelifanya ni nani na ana cheo gani.

Waswahili husema ukicheka na nyani utavuna mabua,tukicheka na udini na ukabila tutavuna Tanzania yenye vipande.Mambo haya yasipokemewa kwa nguvu sana,si ajabu majukwaa ya siasa mwaka 2015 yakageuzwa ni MIKUTANO YA INJILIA kwa MAASKOFU kuja kushawishi wakristo kuchagua mkristo mwenzao na kuwa MIHADHAR ya MASHEHE kuja kushawishi waislamu kumchagua muislam mwenzao.


  • Chuki na visasi na kuharibiana sifa (Character assassination).

Siasa ya Tanzania imeingiwa na chuki na visasi,si mara moja au mara mbili watu kutangaza kuhofia uhai wao kwa madai ya wapinzani wao wa kisiasa wanataka kumuangamiza.Na haya matokeo ya sumu,tindikali na kuvamiwa kwa watu mbalimbali yameongeza woga kwa watu wanaojihusisha na siasa.

Ni Kama vile falsafa ya siasa ya Tanzania imebadilika sasa, kwa leo watu huona hawezi akawa kiongozi hadi Fulani akiwa hayupo.Viongozi wanaopata madaraka wakati mwingine hujikuta wakitumia muda mwingi kuwashughulika wabaya wao kisiasa na kutumia muda mchache katika kuleta maendeleo.

Makundi ynayohasimiana yako kila mahali,ndani ya vyama vya siasa huyu anamchukia huyu,na huyu hampendi huyu.Mbaya zaidi vijana ambao ndio walitegemewa wakae chini wafikiri kama tumaini jipya la siasa ya nchi yetu nao wameingizwa humo ndani.Kila ukipitia mitandao ya jamii siku hizi,ni vijana ndio hutumika katika malumbano haya.

Vijana wa leo hawapendi kuchangia katika mambo ya MSINGI (ISSUES OF NATION INTEREST) kuchwa kutwa wanajadili WATU.Mada yeyote inayojadili mtu;kumkosoa,kumtusi au kumshabikia itapata wateja wengi wa kuichangia lakini chochote kitakachohitaji watu kufikiri na kutoa mawazo mbadala wachangiaji watakuwa wachache.Fikra zetu(mindset) inaendelea kulemazwa taratibu na kujikuta inafurahishwa na HADITHI na KUCHAMBUA watu badala ya UTAFITI na UCHAMBUZI ili kupata suluhisho.Kitu ambacho wengi wameshinddwa kuelewa ni kuwa hiyo ni strategy (mkakati) ya kuua uwezo wa kufikiri wa viongozi wa kesho,tusikubali wafanikiwe kwa kizazi chetu.Mtu husemwa kwa muda Fulani kisha watu hukinai taarifa hizo,lakini pia taarifa nyingi za kuua sifa za watu kwa sababu hufanyika kwa nia (motive) mbaya huendelea kukomaza uadui wa makundi ya kisiasa na visasi juu yao.Masuala ya msingi ndio yanatakiwa yapewe kipaumbele katika mijadala yetu ya kila siku kwa mustakabali mwema wa Taifa letu.

Tumefikia mahali sasa watu hutunga mambo kadhaa yasiyo kweli na kutafuta vithibitisho vya uongo na kuchafua majina ya wapinzania wao wa kisiasa ndani ya vyama au vyama kwa vyama ili wao washinde nafasi za uongozi.Ikifika wakati wa kampeni tofauti na wenzetu wenye kamati za mikakati ya kampeni namna ya kushawishi watu kupiga kura,huku kwetu sasa tuna zile kamati za MAJUNGU,tunasema mambo yasiyo na mantiki na yenye nia ya kubomoa sifa za watu na mbaya zaidi ni pale unapokuta mengi ni ya kutunga.

Siasa ya nchi yetu inahama taratibu kutoka katika ushindani wa HOJA na inakuwa ni ushindani wa VIOJA.Kwa sasa si tena nani ana sera nzuri za maendeleo bali ni nani ana mambo mengi machafu ya kumchafua mwenzake.Kutumia muda mwingi kutueleza ubaya wa mwenzako na kutokutuambia uzuri wako si dalili nzuri ya uwezo wa kiuongozi, kwa sababu kuna siku utakuwa wewe ndio uko kwenye nafasi hiyo unayoitaka, utatueleza nini?

Sifa ya kwanza ya kiongozi ni kuwa na Vision(Maono),lazima wananchi waelewe unataka kuwafanyia nini wananchi wako.Na hii ndiyo inatakiwa iwe sababu ya kwanza kuwavutia kukuchagua wewe,kisha mabaya ya mwenzako yanayoendana na kushindwa kwake kiuongozi (failure of leadership) iwe ni jambo la kuhalalishia mbadala wako,nadhani ndivyo nchi zilizoendelea wanavyoshindana.Wanashindana kwa SERA zaidi na sio kwa KELELE na MATUSI.

Naamini hatujapotoka sana kwa hapa tulipo,tuna nafasi ya kuunyosha mstari wetu na kurudi katika siasa za kistarabu kwa mustakabali wa Taifa letu.Tujenge Taifa bora la leo na la vizazi vijavyo pia.Vijana wawe msatri wa mbele katika kuwa makini katika maamuzi (rational) na kutokubali kuwa nguvu ya kueneza na kusimamia yanayobomoa taifa letu.


TAIFA KWANZA.

MUNGU IBARIKI TANZANIA.

Joel Nanauka

jnanauka@gmail.com
 
Back
Top Bottom