SoC03 Serikali iboreshe usafiri wa anga Ili kupanua wigo wa usafiri na usafirishaji nchini

Stories of Change - 2023 Competition

Tukuza hospitality

JF-Expert Member
Jul 30, 2022
243
615
Constantine J. Samali Mauki

Utangulizi
Nikiwa mtoto, nilijua watu wanaosafiri kwa ndege ni watalii (kwa maana ya wazungu), matajiri, na viongozi wakubwa wa Serikali. Nilipokuwa mkubwa na mpaka sasa, naona mtizamo wangu bado ni uleule niliokuwa nao nikiwa mtoto, kwamba usafiri wa ndege ni wa watalii, matajiri na viongozi wakubwa wa serikali.

Hii ina maana gani? Makundi haya niliyotaja ni ya watu wachache sana, ukilinganisha na mamilioni ya Watanzania wanaosafiri kila siku kwa kutumia vyombo vingine vya usafiri, kama baiskeli, pikipiki, magari (makubwa kwa madogo), magari moshi, mitumbwi, mashua, boti, meli na kadhalika. Kwa kifupi, Watanzania wengi (Ikiwa ni pamoja na mimi) huchukulia usafiri wa ndege kama anasa!

Kati ya Watanzania karibu milioni 62 (kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022), wanaosafiri kila mwaka ni zaidi ya milioni 40; na kwa mujibu wa jarida la Ifahamu Tanzania (Oktoba 2, 2020), kwa mwaka 2020 idadi ya abiria wa usafiri wa ndege nchini Tanzania, ilikuwa milioni tatu, kati yao asilimia 48 walikuwa watalii kutoka nje ya nchi na asilimia 52 walikuwa ni Watanzania (sawa na watu 1,560,000). Hii ina maana, kati ya Watanzania milioni 40 ambao tunaamini wanasafiri kila mwaka, ni asilimia 4 tu wanaotumia usafiri wa anga.

Kumbe mtizamo wangu ya kuwa wanaosafiri kwa ndege ni watalii wa nje, matajiri na viongozi wakubwa wa serikali ni sahihi! Maana kwa mujibu wa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (2022), idadi ya vijiji na mitaa Tanzania ni 16,582 (vijiji 12,319 na mitaa 4,263). Kwa hesabu ya Watanzania wanaosafiri kwa ndege kila mwaka, kila kijiji/mtaa ni wastani wa watu 94 tu wanaopata huduma hii; hivyo, kama kila kijiji/mtaa una wasafiri 2500, kati yao ni 94 tu wanaomudu usafiri wa ndege (sawa na asilimia 3.76, kwa makadirio ya karibu ni sawa na asilimia 4).

Kielelezo Na. 1: Moja ya Ndege za Shirika la Ndege Tanzania
Ndege ya ATC.. Ifahamu tanzania.com.png

Chanzo: Blog ya Ifahamu Tanzania

Kwanini Idadi ya Watanzania Wanaosafiri kwa Ndege Bado ni Ndogo?
Ukweli ni kwamba, kuna uwekezaji mdogo sana katika sekta ya usafiri wa anga, kuanzia miundombinu, hasa viwanja vya ndege kuwa vichache na vingi vikiwa katika viwango vidogo na/au uchakavu; na makampuni ya ndege nchini Tanzania ni machache. Hoja hii inathibitishwa na jarida la Ifahamu Tanzania (Oktoba 2, 2020), ambapo linasema, licha ya historia ya muda mrefu ya sekta ya usafiri katika kuleta maendeleo ya nchi, uwepo wa makampuni machache ya ndege za kimataifa, na za kitaifa, unadumaza maendeleo ya usafiri wa anga. Wakati ambao njia nyingi za safari zina umbali mwingi, na huhitaji kusafiri kwa masaa mengi kwa njia ya barabara, lakini bado uhitaji wa usafiri wa anga umeendelea kuwa chini, na haukuwi kwa haraka ukilinganisha na nchi nyingine. Uhitaji mdogo, gharama kubwa za uendeshaji, na ushindani mdogo umepelekea bei za tiketi za ndege kuwa kubwa ukilinganisha na sehemu nyingine duniani, na hali hii imeathiri ukuaji wa sekta hii ya usafiri wa anga.

Nchi nyingine usafiri wa anga ni rahisi, na wa kawaida kwa wananchi wengi. Kwa mfano, nchi ya Jirani ya Kongo DRC, ambayo ina changamoto nyingi, hasa za kiusalama, lakini wananchi wa jiji la Lubumbashi wanakwenda jiji la Kinshasa kwa ndege kufanya biashara na kurudi siku hiyohiyo, na wa Kinshasa vivyohivyo. Umbali kati ya majiji haya ni kilomita 1,567 (kwa ndege) na kilomita 2320 (kwa barabara). Kumbe usafiri wa anga ni muhimu, sii tu kwa uchumi wa nchi, bali pia kwa kipato cha mtu mmoja mmoja.
Kielezo Na. 2: Moja ya Ndege za "Precisionar"
Precisonair TZ.png

Chanzo: Google: Precisionair

Sekta ya Usafiri wa Anga Inahitaji Wawekezaji Zaidi
Kwa miaka mingi nimeshuhudia mashirika mawili ya ndege yakitoa huduma ya usafiri wa ndege nchini kwa ushindani, haya ni Air Tanzania na Precision Air. Air Tanzania, ni shirika la umma wakati "Precisionair" ni kampuni binafsi. Yapo mashirika mengine yanayotoa huduma hii, lakini kwa kiasi na maeneo kidogo sana. Miaka ya karibuni, Kampuni ya ndege ya "Fast Jet" iliingia nchini na kutoa huduma kwa bei nafuu sana, ukilinganisha na makampuni mengine, kuna kipindi nauli ilikuwa karibu au sawa na ya basi. Kwa kipindi ambacho shirika hili linafanya kazi hapa, watu wengi ambao hawakuwahi kufikiria kupanda ndege, walipanda "Fast Jet"; na hii ilileta ushindani mkubwa kati yake na mashirika mengine ya usafiri wa anga.
Kwa bahati mbaya, mpaka wakati huu naandika Makala haya, "Fast Jet" haifanyi tena kazi Tanzania, kwa zaidi ya miaka miwili sasa. Mimi binafsi sijui sababu zilizolifanya shirika hili kuacha kufanya kazi Tanzania.

Mapendekezo
Serikali iwezeshe uwekezaji wa sekta binafsi katika usafiri wa anga; hii ni pamoja na viwanja vya ndege, na ndege zenyewe, kupitia mfumo wa Ushirikiano wa Sekta binafsi na Umma (“Private Public Sector – PPP”). Hii itaongeza wawekezaji katika sekta hii, jambo litakaloongeza idadi ya makampuni ya ndege yatakayoshindana kutoa huduma, na hivyo kufanya nauli kupungua.

Serikali ibinafsishe Shirika lake la "Air Tanzania" kwa kuwauzia hisa nyingi wananchi, ili liendeshwe kibiashara na kwa ueledi zaidi, na hivyo kuepukana na hasara zinazoripotiwa kila mara.
.
Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine, iboreshe njia nyingine za usafiri, hasa treni za kisasa, angalau kila mkoa wa Tanzania ufikiwe na treni. Hii pia ni njia ya kurahisisha usafiri kwa ujumla, ambapo itafanya uhitaji wa usafiri wa anga kupungua, na hivyo kuchangia nauli za ndege kupungua.

Hitimisho
Serikali iweke mazingira mazuri na wezeshi yatakayovutia wananchi, mmoja mmoja au kwa kuungana kuwekeza katika sekta ya usafiri wa anga.

Marejeo
Ifahamu Tanzania (Oktoba 2, 2020), Usafiri wa – Ndege za Abiria na Mizigo.
Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (2022), Vijiji na Mitaa Tanzania.
 
Back
Top Bottom