Riziki Shahari: Hakuna Elimu Bila Walimu, Serikali Imalize Ukosefu wa Walimu

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
610
1,540
HOTUBA YA MSEMAJI WA SEKTA YA ELIMU ACT WAZALENDO NDG. RIZIKI S. MNGWALI KUHUSU HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA KWA MWAKA WA FEDHA 2022-2023
Utangulizi:

Ndugu Waandishi wa Habari,
Jana tarehe 10 Mei 2022 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipokea na kuanza kujadili hotuba ya bajeti wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2022/23 ambapo itajadiliwa kwa siku mbili (2) (jana na leo mjadala unaendelea na Bunge litaidhinisha bajeti hiyo).

Tunafahamu kuwa Bajeti ni nguzo muhimu sana katika kugharamia utoaji wa huduma ya elimu hapa nchini. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ni mshauri mkuu wa Serikali kuhusu mfumo wa elimu, hivyo hutoa miongozo kwa taasisi za elimu na mashirika yanayochangia katika malengo ya Serikali kuhusu elimu. Majukumu yake makuu ni kupanga mikakati, sera, na mipango ya mageuzi na maendeleo ya elimu; na kuandaa rasimu ya kanuni na taratibu, na kusimamia utekelezaji wake.

Kutokana na umuhimu wake, bajeti ya Sekta ya Elimu imekua ikifuatiliwa na wananchi pamoja na wadau mbalimbali na wadau wamekua wakitoa maoni yao kuhusu vipaumbele vya bajeti. Hivyobasi, kutokana na umuhimu huu, ACT Wazalendo kupitia Msemaji wa Sekta ya Elimu tumefanya uchambuzi wa makadirio ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka wa fedha 2022/23. Katika hotuba hii, uchambuzi wetu utahusisha maeneo nane (8) kuhusu bajeti ya Elimu ya mwaka huu.

Ndugu Waandishi wa Habari
Bajeti ya Elimu kwa kawaida inashughulikiwa na wizara mbili, Wizara iliyo chini Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Tayari Chama Chetu kimeshatoa mtazamo wake na maeneo ya kipaumbele kupitia Msemaji wa sekta ya TAMISEMI na Maendeleo vijijini baadhi ya mambo yanayoangukia kwenye sekta ya Elimu. Leo tutazungumzia Sekta ya Elimu kwa muktadha wa majukumu na vipaumbele kutokana wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

1. Usimamizi duni wa utoaji wa Elimu ya Awali, Msingi na Sekondari Nchini.

Mwaka 2016, serikali ilianza kutekeleza mpango wa elimu ya msingi bila malipo. Huu ni mkakati mzuri wa serikali kuhakikisha kwamba watoto wote wa kitanzania wanapata elimu ya msingi bila vikwazo vya ada. Katika utekelezaji wa sera hii Serikali imelegalega kwenye kusimamia utoaji wa huduma, miundombinu na gharama. Takwimu zinaonyesha upungufu mkubwa sana wa walimu kuanzia ngazi ya awali, shule za msingi na sekondari. Vyumba vya madarasa vya madarasa na vitabu. Pia, kwa muda mrefu serikali imeshindwa kufanya ukaguzi kwa ufanisi kwenye shule za msingi na sekondari ili kukagua na kudhibiti ubora wa elimu inayotolewa.

Pamoja na changamoto hizo, wizara ya Elimu imekuwa na utekelezaji duni sana wa utoaji wa fidia ya kugharamia elimu bila malipo, jambo linaloathiri zaidi mfumo wa Elimu msingi. Waraka wa Ruzuku kwa Shule za Msingi za Serikali (elimu bila malipo) 2015 unataka Serikali kutoa fidia ya shilingi 10,000 na shilingi 25,000 kwa mwaka kwa kila mwanafunzi katika shule za msingi na sekondari mtawalia; ambapo wizara itatumia asilimia 40 kununua vitabu na kusambaza shuleni.

Kwa mujibu CAG inaonyesha kuwa ili kukidhi mahitaji ya vitabu kwa wanafunzi katika shule za msingi za Serikali vilihitajika vitabu 6,323,566 kwa mamlaka 22 za Serikali za Mitaa. Hata hivyo, ni vitabu vya kiada 1,467,829 (sawa asilimia 23) vilisambazwa katika mwaka huo ikionesha upungufu wa vitabu 4,855,737 vyenye thamani ya shilingi bilioni 19.42. Utoaji pungufu wa vitabu kwa shule za msingi na sekondari kuna athari matokeo na kitaalum ya mwanafunzi.

ACT Wazalendo tunaitaka serikali kuhakikisha inasimamia elimu kwa uboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia, kutoa ajira za moja kwa moja za walimu ili kupunguza uhaba wa walimu, kutoa gharama za nyenzo na vifaa kama vile vitabu na mengineyo. Pili, serikali iongeze fedha ya ruzuku kwa wanafunzi kutokana na uhalisia wa gharama za bidhaa kwa sasa.

2. Wanafunzi kukatisha masomo kabla ya kumaliza Elimu msingi (Darasa la Saba)

Taarifa ya utekelezaji ya wizara na takwimu mbalimbali zimekuwa zikionyesha kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi kwa ngazi ya darasa la kwanza, kwa miaka kadhaa. Pamoja na ongezeko kubwa la udahili bado Serikali imeshindwa kufuatilia anguko kubwa la Watoto wanaoshindwa kumaliza elimu ya msingi darasa la saba (7).

Ripoti ya Mdhibiti na Mkuguzi Mkuu wa Hesaba za Serikali (CAG) imebainisha kuwa kwa miaka mitatu yaani kuanzia 2018 hadi 2021 kwa sampuli za shule kutoka mamlaka za serikali za mitaa 27 zikionyesha wanafunzi wanaoshindwa kumaliza shule ya msingi kwa kukatisha masomo yao ni asilimia 2.06 ya wanafunzi walioandikishwa. Idadi hii ni kubwa, inakinzana na malengo yaliyowekwa na serikali kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano kiliweka kiwango halisi cha uwiano wa uandikishaji wa elimu ya msingi kuwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2022.

Kwa mujibu Takwimu za Utafiti za Elimu (BEST 2020), zinaonyesha kiwango cha wanafunzi kukatisha masomo kwa sababu mbalimbali ni wanafunzi 166,991 sawa na asilimia 1.6 ya wanafunzi waliondikishwa ambao walikuwa 10,174,237. Huku utoro ukichukua asilimia 97.5 ya sababu zote ikifuatiwa na vifo pamoja na ujauzito kwa watoto wa kike.

Katika hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/23 haijawekea mkazo wa namna ya kukabiliana na hali hiyo ili kuhakikisha kuwa kila mtoto anapata haki ya elimu kama malengo tulivyojiwekea.

ACT Wazalendo inaitaka serikali kuhakikisha kuwa kila mtoto wa kike aliyepata mimba akiwa shule anamaliza elimu yake kama ilivyokusudiwa kwa kusimamia utekelezaji wa ahadi ya kuruhusu kumrejesha mtoto wa shule shuleni. Pili, kukomesha ukali dhidi ya watoto ili kuhakikisha watoto wanakuwa huru kushiriki na kupata elimu.

Mwisho, kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kujenga shule kuongeza idadi ya shule maeneo ya karibu ili kupunguza umbali.

3. Uthibiti wa ubora katika Elimu ya ufundi na Mafunzo ya ufundi stadi haupewi kipaumbele nchini.
Wizara ya Elimu kupitia Baraza la Taifa la Elimu linasimamia elimu ya ufundi nchini. Katika uchambuzi wetu wa hotuba ya wizara tumeona kuwa kuna udhibiti mdogo sana wa ubora kwa kuwa kiasi cha fedha kinachotengwa kwa ajili ukaguzi hakikiwezeshi wizara kutekeleza majukumu yake. Kwa miaka zaidi ya sita kuanzia 2016 hadi sasa kiwango cha bajeti kwa ajili ukaguzi huwa ni hafifu mno.

Kwa mujibu wa taarifa ya CAG 2020/21, serikali imefanya ukaguzi wa ubora katika vituo 73 kati ya 779 jambo ambalo ni kinyume na sheria na kanuni za Usimamizi wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi. Vituo visivyokaguliwa vinaweza visikidhi viwango vinavyohitajika nabado visibainike kwakuwa havijafikiwa, hivyo vitatoa elimu isiyo na ubora. Aidha, ubora wa vyuo vya ufundi unaathiriwa kutokana na upungufu mkubwa wa wakufunzi na walimu ukilinganisha na idadi ya wanafunzi.

Vilevile, uwezo mdogo wa vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kudahili wanafunzi. Idadi ya wanafunzi wanaohitimu shule za msingi na sekondari na kukosa fursa ya kuendelea na masomo ni kubwa ni wastani wa wanafunzi milioni moja huku uwezo (wanafunzi wanaodahiliwa ni 266,000.

Ili kuweza kukabilia na changamoto hizi ACT Wazalendo tuliona ni muhimu kuweka mkazo, Ilani ya Uchaguzi 2020 tulibainisha kuwa tutahakisha;

i. Kuwa katika Kila Mamlaka ya Serikali za Mitaa (Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji) kunakuwa na angalau Chuo kimoja cha Mafunzo ya Ufundi (VETA),

ii. Elimu ya Mafunzo ya Ufundi (VETA) inatolewa bila malipo ya ada.

iii. Inaweka mfumo utakaomuwezesha mhitimu wa chuo cha VETA kuweza kujiendeza zaidi kielimu na kujiunga na mifumo mingine ya elimu.

iv. Kunakuwa na vyuo vya Ufundi Mchundo (Technical Schools) vyenye uwezo wa kudahili wanafunzi wasiopungua 10,000, angalau katika nusu ya Mikoa ya Tanzania Bara.

4. Hakuna Elimu bila Walimu, Serikali imalize tatizo la walimu katika taasisi za Elimu.

Katika hotuba ya Waziri wa Elimu imeelezea jitihada na mikakati ya wizara ya kuhakikisha inaongeza udhahili wa walimu katika vyuo vya walimu nchini. Kwa mujibu wa taarifa ya wizara serikali imeweza kudahili jumla ya wanafunzi wa Astashahada ya elimu ya msingi kuwa 10,975 (wanawake 5,824 na wanaume 5,151), stashahada ya ualimu sekondari miaka miwili 2,663 (wanawake 1,037 na wanaume 1,626) na sashahada maalum ya ualimu sekondari sayansi miaka mitatu 5,540 (wanawake 1,973 na wanaume 3,567) na hivyo kufanya vyuo vya ualimu vya Serikali kuwa na jumla ya wanafunzi 19,178. Idadi hii ni kwa ngazi ya astashahada na stashahada pekee, bado wanafunzi wanaodahiliwa kwa ngazi ya shahada.

Pamoja na taarifa hizi, kiwango cha serikali kuajiri walimu ni kidogo sana. Uwiano wa wanafunzi wanaogharamiwa na serikali kusomea ualimu na mahitaji halisi haushabihiani na kasi ya ajira zinazotolewa na serikali. Hii inaifanya jitihada za serikali za kudahili walimu kukosa maana. Ni dhahiri kuwa idadi ya wahitimu wa masomo ya ualimu ingeweza kupunguza mahitaji yaliyopo sasa katika taasisi za elimu. Pia, uhaba wa walimu unavikumba pia vyuo na vyuo vikuu, lakini nako hakuna jitihada za kuondoka katika mkwamo huo.

ACT tunaendelea kutoa rai kwa serikali kurejesha mfumo wa ajira za walimu za moja kwa moja ili kukabiliana na changamoto ya upungufu mkubwa na walimu na kuboresha elimu yetu.

Kwa kufahamu changamoto za uhaba wa walimu hususani vyuo vikuu ACT Wazalendo katika Ilani ya Uchaguzi 2020 tulisema kuwa “Serikali ya ACT itaajiri wahadhiri wasiopungua 5,000 kwa miaka mitano ili kupunguza uwiano mkubwa uliopo kati ya wahadhiri na wanafunzi.” Hivyobasi, serikali ichukue mawazo haya ili kuborsha Elimu yetu.

5. Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu inaendeleza ubaguzi katika mfumo wetu wa Elimu.

Mfumo wa ugharamiaji wa elimu yetu hususani katika ngazi ya elimu ya Ufundi, Elimu ya juu na vyuo vya utabibu bado inaweka vikwazo kwa watoto wetu kupata elimu kwa kadri ya vipawa, vipaji na uwezo wao. Tunatambua jitihada za serikali za kuongeza bajeti kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaosoma elimu ya juu, lakini bado wastani wa asilimia 17 hadi 42 ya wanafunzi wenye uhitaji wa kupata mikopo kwa ajili ya kuendelea na maasomo ya elimu ya juu wanashindwa kupata mikopo hiyo na wengine wanalazimika kusitisha masomo.

Takwimu za miaka sita (6) zinaonyesha idadi ya waombaji waliokosa mikopo ni kama ufuatao; kwa mwaka wa masomo 2016/2017 ni asilimia 42 ya waombaji hawakupata, mwaka wa fedha 2017/2018 ni asilimia 26 hawakupata, 2018/19 ni asilimia 28 hawakupata, 2019/20 asilimia 26 hawakupata, 2020/21 asilimia 17 hawakupata na kwa mwaka 2021/22 asilimia 29 hawakupata.

Yapo malalamiko, taarifa na ushahidi juu ya changamoto zinazowapata wanafunzi na wazazi katika kuhakikisha watoto wao wanapata elimu ya juu. Uwezo na ufasi katika utambuzi, vigezo na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wenye uhitaji umekuwa na mjadala na hata wakati mwingine umewahi kusababisha migomo na maandamano.

Licha ya hayo yote Serikali ya CCM, haijatoa jawabu la kuondokana na dhahama hizi. Sisi ACT Wazalendo tuna amini kuwa ili kupanua wigo wa wanafunzi kuendelea na masomo katika ngazi ya elimu ya juu ni kwa serikali kubeba gharama hususani ada, malipo ya mafunzo kwa vitendo, fedha za vitabu na viandikwa. Kwa kufanya hivi tutaondosha minyukano na kutoa fursa sawa ya kupata elimu bila kujali kipato cha mtu.

Tutaondosha matabaka ya watoto wa wenye nacho na wasio nacho kwenye kuwania elimu.
Kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020 ACT Wazalendo tulibanisha kuwa “Itafuta mikopo yote ya miaka ya nyuma iliyotolewa kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu.Italipa Ada ya Masomo (Tuition Fee), Fedha za Vitabu (Stationeries), na gharama za Mafunzo kwa Vitendo (Field Studies/Internship) kwa kila mwanafunzi anayedahiliwa kwenye Chuo Kikuu. Itatunga Sheria kuhakikisha kuwa Mikopo ya Elimu ya juu itakuwa ni kwa ajili ya gharama za kujikimu tu (Meals & Accomodations).”

Kwa upande wa wanafunzi wanao dahiliwa ngazi ya vyuo vya kati na vyuo vya ufundi wao ndio hawajatazamwi kabisa. Kwa kuwa chombo hiki (Bodi ya mikopo) kisheria hakihusiki na mfumo wa ugharamiaji kwenye ngazi ya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, haipewi lawama Lakini nako kuna changamoto kubwa sana.

Hotuba ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/23 haijajibu changamoto za muda wote kuhusu mfumo wa ugharamiaji wa Elimu ya juu.

6. Mapitio ya utekelezaji wa bajeti fedha za miradi ya maendeleo ya Elimu

Katika mwaka wa fedha 2021/22 wizara ilipitisha bajeti ya Shilingi 994,711,772,676.29 kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo. Kati ya fedha hizo bilioni 570 zilikuwa kwa ajili ya kugharamia mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu. Serikali inafanya makusudi kuchanga fedha za mikopo ya elimu ya juu katika fedha za maendeleo kwa kuwa fedha hizo huonekana kuwa ni nyingi lakini fedha zinazokwenda kutekeleza miradi halisi ya maendeleo ni kidogo sana. Kwa kutazama fedha hizo kwa mwaka jana fedha za mikopo zinachukua asilimia 57 za fedha zote za miradi.

Katika mwaka wa fedha 2022/23 Wizara imeomba kuidhinishiwa fedha shilingi 959,547,439,000.00 kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo, ni fedha pungufu kwa kulinganisha na bajeti ya mwaka jana. Pia, kiasi kinachoenda kuhudumia gharama za mikopo kitaendelea kupanda kutokana kuongezeka kwa idadi ya wahitimu kidato cha sita mwaka huu.

ACT Wazalendo tunapendekeza kutenganishwa kwa fedha za miradi halisi ya Maendeleo katika bajeti na fedha kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu kwa kuzianzishia fungu maalum ili fedha za miradi halisi ya maendeleo ziweze kuonekana na kufuatiliwa utekelezaji wake;

7. Haki ya Elimu Kwa mtoto wa Kike

Serikali ilitangaza rasmi kuwa mwanafunzi wa kike akipata ujauzito apata fursa ya kurejea shule pindi atakapojifungua. Lakini kupitia Hotuba ya bajeti ya Waziri wa Elimu inaonyesha kuna dalili za kuwarejesha kwa dirisha jingine llakini sio katika mfumo rasmi. Tunaisisitiza serikali kusimamia haki ya watoto wa kike kwa kuwarejesha kwenye mfumo rasmi wa elimu badala ya utaratibu wa kuwarejesha nje ya mfumo rasmi.

8. Elimu ya Mfunzo kwa vitendo kwa Elimu ya juu
Mfumo wa sasa wa kutoa mfunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu (Elimu ya Juu) ni miezi 2 au wiki 56 na ugharamiaji wake bado unabebwa katika mabega ya mwanafunzi mwenyewe au mzazi. Katika kuimarisha ubora na ufanisi wa kujifunza kwa wanafunzi wa elimu ya juu, ni muhimu sana wanafunzi wapate muda mrefu zaidi kuanzia miezi sita (6) hadi mwaka ili kuwajengea uzoefu na umahiri kwenye fani anayosomea.

Katika, mabadiliko ya mitaala na sera ya elimu ni serikali inapaswa kutazama upya utaratibu wa sasa kwa kuwa haumwandai vya kutosha mwanafunzi kumudu fani yake kutokana na kukosa muda wa kujifunza kwa vitendo.
Katika Ilani ya Uchaguzi ya ACT Wazalendo tuzungumzia kutoa vivutio kwa makampuni au taasisi binafsi zitakazo toa nafasi ya wanafunzi kujifunza kwa vitendo.

Pia, Serikali kuhakikisha inalipia kwa fani zote kwa kipindi kisichopungua miezi sita ili wanafunzi wote wapitie mafunzo kwa vitendo kikamilifu, vilevile kuweka utaratibu wa kutumia matokeo ya mafunzo kwa vitendo katika utoaji ajira ili kuhimiza wanafunzi kuona umuhimu wa mafunzo kwa vitendo.

Hitimisho.

Kwa kuhitimisha, Usimamizi wa sekta ya Elimu kugawanywa katika wizara takribani zaidi ya tatu yaani, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya TAMISEMI na wizara ya Maendeleo ya jamii, jinsia na watoto (kwa baadhi ya masuala) kuna fanya mpango wa bajeti kwenye sekta ya Elimu kuyumbishwa kwa vipaumbele vyake.

Ni muhimu kwa serikali kuhakikisha sekta ya Elimu inasimamiwa na wizara moja. Pia, changamoto nyingi za kibajeti na kisera zinatokana na kukosekana kwa mwafaka wa kitaifa juu ya aina ya Elimu tunayoitaka, hivyo ni muhimu mchakato wa Mapitio ya Sera iwahusishe wadau wote.

Tunafahamu hatua za serikali kufanya mapitio ya sera ya elimu ya mwaka 2014 na mitaala ya elimu, ni muhimu kuwe na mjadala wa kitaifa juu ya masuala kadhaa yakiwemu lugha ya kufundishia na kujifunzia, mfumo wa upimaji, tathimini na utambulizi (awards), uwezo wa uongozi, usimamizi na utawala wa elimu, ubora wa mitaala pamoja na ithibati na udhibiti wa ubora wa shule na vyuo katika ujumla wake.


Ahsante sana!

Ndg. Riziki Shahari Mngwali
Msemaji wa Sekta ya Elimu- ACT Wazalendo
11 Mei 2022

IMG-20220511-WA0008(1).jpg
 
Huko vijijini shule hazina walimu, unakuta shule ya wanafunzi 2,000 ina walimu wanne. Sasa hapo hata mwalimu anaweza kukumbuka majina ya watoto wote.

Hata wale wanaohitaji msaada wa ziada si rahisi kugundulika. Tunarudi kule kwenye literacy level ya taifa kuwa chini ya 50%. Watoto wengi wanamaliza shule ya msingi hawajui kusoma na kuandika.
 
Back
Top Bottom