Exuper Kachenje na Claud Mshana
SERIKALI imesema kuwa, wamiliki wa mgodi wa North Mara walitoa maelezo ya uongo dhidi ya malalamiko ya wananchi kuwa mgodi huo unatiririsha maji ya sumu yaliyosababisha vifo vya watu, wanyama na kuathiri mazingira.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Balozi Khamis Kagasheki alisema hayo juzi baada ya kutembelea mgodi huo kwa maagizo ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda ili kujionea hali halisi na kujua ukweli wa mambo.
Wananchi wa maeneo yanayozunguka mgodi huo wamekuwa wakieleza kuwa kumekuwepo na sumu inayovuja na kuingia kwenye Mto Tigite na kusababisha vifo vya viumbe walio kwenye mto huo, wanyama wao waliokunywa maji hayo na kukauka kwa mimea iliyo kandokando ya mto huo unaotegemewa na vijiji vitatu.
Picha za magazeti na televisheni zimekuwa zikionyesha watu walioathirika vibaya kwenye ngozi na ambao walieleza kuwa walipata athari hizo baada ya kutumia maji ya mto huo, huku ikielezwa kuwa ng'ombe zaidi ya 200 wamekufa baada ya kunywa maji hayo.
Hata hivyo, Barrick ilikanusha madai hayo na kusema kuwa, uchunguzi uliofanywa na mgodi huo kwa kushirikiana na watendaji wa serikali pamoja na mganga wa wilaya hiyo ulionyesha hakuna ukweli wowote katika malalamiko ya wananchi wa eneo hilo.
Hata hivyo, Balozi Kagasheki aliiambia TBC1 kuwa katika ziara yake kwenye mgodi huo unaomilikiwa na Barrick Gold ya Canada amebaini kuwepo na athari kubwa kwa viumbe na mazingira.
Alisema awali alitembezwa na uongozi wa Barrick kwenye maeneo kadhaa na ikaonekana kuwa hakuna tatizo, lakini alitokea mwananchi mmoja aliyemwelezea kuwa ni msamaria mwema ambaye alimshika mkono na kumwambia kuwa maeneo aliyoonyeshwa sio ambayo yanalalamikiwa na kumpeleka kwenye tatizo halisi.
Alisema alimfuata msamaria huyo na kuonyeshwa hali halisi ambayo waziri huyo aliielezea kuwa "ni mbaya na ya kusikitisha" na akasema anashangazwa na kitendo cha uongozi wa mgodi huo kudanganya.
"Nasikitika sana uongozi wa mgodi kunidanganya. Niliyoyaona nitayapeleka kwa waziri mkuu... kwa kweli si nzuri, itabidi nifikishe ripoti kwa waziri mkuu," alisema naibu waziri huyo akionekana kukasirika.
Kagasheki, aliyekuwa akihojiwa na kituo cha televisheni cha TBC1, alisema inasikitisha zaidi kwa kuwa wakati mwingine inakuwa vigumu kuielewa serikali kwa matukio kama hayo na mimi kuwa naibu waziri wa wizara hiyo inayohusika na usalama wa watu na mali zao, atatekeleza wajibu wake katika kuhakikisha usalama wa wakazi wa eneo linalozunguka mgodi huo.
Katika wiki za hivi karibuni vyombo vya habari viliripoti kutokea kwa vifo vya watu zaidi ya 21 na ng'ombe 200 huku wengine wakiathirika kutokana na kunywa maji ya Mto Tigithe unaopita katika Kata ya Kibasuka wilayani Tarime Mkoa wa Mara.
Diwani wa kata hiyo, ambaye aliibua malalamiko hayo, anashikiliwa na polisi na amefunguliwa mashtaka akidaiwa kutoa taarifa za uongo kuhusu vifo hivyo.
Wiki iliyopita Jumuiya ya Kikristo Tanzania pamoja wanaharakati wengine wa mazingira na haki za binadamu, walitoa tamko kutaka wahusika hao wachukuliwe hatua, ikiwa ni pamoja na kumtaka waziri mwenye dhamana ya mazingira, Batilda Buriani ajiuzulu kutokana na kashfa hiyo.
Walisema kuwa, upo ushahidi wa kutosha kuwa watu walikufa kutokana na kunywa maji ya sumu na kwamba wapo tayari kuchukuliwa hatua ikiwemo kufikishwa mahakamani iwapo jambo hilo halina ukweli ambapo pia walitaka kuundwa kwa tume huru kuchunguza kashfa hiyo.
Nao Wabunge waliochangia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Batilda Buriani walitaka serikali kulichukulia suala la Mgodi wa North Mara kwa uzito unaostahili na kuunda tume kuchunguza madhara yanayodaiwa kutokea kwa wananchi waliotumia maji yenye kemikali katika Mto Tigite.
Mbunge wa Tarime (Chadema), Charles Mwera alisema serikali inapaswa kuwawajibisha wote waliopima maji hayo na kusema kuwa, hayana kemikali hatari na kuongeza kuwa waziri atakapokuja kujibu hoja aeleze amefanya ziara ngapi katika maeneo hayo.
Mto huo wa Tigite unategemewa na zaidi ya familia 2,534 walio katika vijiji vya Kewanja, Nyangoto na Matongo ambazo zinaathirika moja kwa moja. Pia vijiji vya Wegita, Nyakurungu na Nyarwana wanaathirika na mto huo ambao unaungana na Mto Timbe unaopita kijiji cha Mtongo na baadaye kuelekea Ziwa Victoria.
Tangu mapema mwezi Mei, wakazi wa vijiji hivyo wamekuwa wakilalamika kuwa kumekuwepo na uvujaji wa takataka zenye sumu kutoka mgodi huo na kwamba mifugo yao ilifariki kutokana na kunywa maji ya mto huo. Pia walidai mimea iliyo pembezoni mwa mto huo inakauka na kwamba waliona samaki wengi wakiwa wamekufa.
Barrick, ambayo inadai kuwa mgodi huo hautoi kabisa maji machafu yenye sumu, imeeleza kuwa kuvuja kwa takataka hizo zenye sumu kulitokana na vitendo vya wakazi wa vijiji hivyo kuharibu mabomba kwa lengo la kuhujumu.
Mgodi huo umekuwa na matatizo na wananchi wa maeneo yanayouzunguka tangu ulipoanzishwa, baadhi yakitokana na wananchi kutoridhika na fidia waliyopewa kwa kuhamishwa eneo hilo, uchafuzi wa mazingira na mapigano ya mara kwa mara yanayotokana na wananchi kuvamia mgodini kila wakati miamba inapolipuliwa.
Source: Mwananchi
Hivi Kikwete anasoma au anapata habari kama hizi? na kama hapati au whatever kisingizio atakachotoa kuhusiana na hili, je anaendelea kujiita kuwa ni Raisi wa Tanzania na kamanda mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama wa watanzania wote (ikiwemo hawa wa North Mara) ?