Ufisadi mkubwa kwenye mchakato wa kuwalipa fidia wananchi wanaozunguka mgodi wa North Mara

Mpinzire

JF-Expert Member
Jan 18, 2013
7,224
12,945
The Chanzo



Dar es Salaam. Mgodi wa North Mara, moja kati ya migodi miwili inayomilikiwa na kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick Gold nchini Tanzania, umekadiriwa kupoteza kati ya Dola za Kimarekani milioni 11.6 na Dola za Kimarekani milioni 31.65, kwa mwaka, kutokana na vitendo vya kihalifu vinavyoendeshwa na mtandao wa kihalifu mgodini hapo.

Kwa thamani ya fedha za Kitanzania, mgodi huo ulikuwa ukipoteza kati ya takriban Shilingi bilioni 27.5 na Shilingi bilioni 77.6 kwa mwaka.

Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya siri iliyokabidhiwa kwa Barrick Gold, kampuni ya uchimbaji dhahabu na shaba ulimwenguni, hapo Septemba 17, 2017, na Europe Conflict and Security Consulting Ltd, kampuni ya ushauri kwenye masuala ya usalama yenye makao makuu yake nchini Uingereza.

The Chanzo imeweza kuipata ripoti hiyo iliyopewa jina la Analysis: Criminal Economies in and around the North Mara Gold Mine baada ya kuwasilishwa katika Mahakama ya Uingereza kwenye kesi ya raia wa Tanzania dhidi ya Barrick Gold inayohusiana na madai ya kampuni hiyo kukiuka haki za binadamu.

Ripoti hiyo inaonesha kwamba mgodini hapo kuna wizi mkubwa wa dhahabu kutoka kwenye maeneo yenye ulinzi mkali ya mgodi huo, mara nyingi ukihusisha wafanyakazi wa mgodi, wakandarasi na maafisa wa Jeshi la Polisi waliokabidhiwa kazi ya kuimarisha ulinzi mgodini hapo.

Mbali na wizi huo, ripoti hiyo pia inabainisha uwepo wa ufisadi kwenye mchakato wa ulipaji wananchi fidia, huku wathaminishaji wa ardhi wakitoa thamani isiyo sahihi kwa ardhi ambazo wamiliki wake wanapaswa kulipwa fidia na mgodi.

Ripoti hiyo pia inataja uwepo wa matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa na mgodi kwenda Serikalini kwa ajili ya kufanya shughuli za maendeleo, na uwepo wa rushwa na hongo kwa maafisa wa mgodi na wale wa Serikali.

Mtandao huo wa kihalifu unatajwa kuwa na uwezo mkubwa wa intelijensia, operesheni na kiuratibu ndani ya mgodi huo na kwenye jamii zilizouzunguka. Kwa mujibu wa tathmini ya kampuni hiyo ya ushauri, mtandao huo wa kihalifu unakisiwa kufanya kazi kwa bajeti inayozidi Dola za Kimarekani milioni 1.5 (Shilingi bilioni 3.7) kwa mwaka.

Haifahamiki endapo kama uhalifu huu bado unaendelea katika mgodi wa North Mara kwani The Chanzo ilishindwa kupata majibu ya mara moja kutoka kwa Barrick Gold kuhusiana na suala hilo. Kampuni hiyo pia haikujibu maswali yetu yaliyotaka kufahamu endapo kama imewahi kuripoti vitendo hivyo kwa wanahisa wake au Serikali ya Tanzania.

Matukio ya hivi karibuni
Hata hivyo, taarifa hizi zinakuja wakati ambao kumekuwa na matukio kadhaa ya hivi karibuni katika mgodi wa North Mara yanayoonesha kwamba uhalifu huo wa kupangwa unaweza kuwa unaendelea mgodini hapo tangu tathmini hiyo ya Europe Conflict and Security Consulting Ltd itolewe hapo Septemba 2017.

Tukio la hivi karibuni kabisa ni lile la Machi 12, 2023, ambapo mfanyakazi wa mgodi huo aliyetambulika kwa jina la Emmanuel Chacha alifariki dunia akiwa anakwepa kukamatwa na polisi baada ya kuonekana akiwa anajishughulisha na uchimbaji haramu wa madini mgodini hapo.

Wakati polisi na Baarick walidai kwamba Chacha alifariki baada ya kudondoka, familia ya kijana huyo ilitilia mashaka taarifa hizo, ikidai kuna uwezekano mkubwa kwamba mpendwa wao huyo alifariki baada ya kupigwa risasi, ikihitaji uchunguzi zaidi kufanyika juu ya tukio hilo.

Uwepo wa mtandao huu wa kihalifu mgodini hapo pia uliwahi kuthibitishwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Happy, ambaye kwenye mahojiano yake na gazeti la Mwananchi mnamo Julai 31, 2022, alihusisha uhalifu huo na baadhi ya vigogo wa chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM).

“Kuna watu wanajificha kwenye nguo za kijani kwa kujifanya wana-CCM kufanya uhalifu, baadhi wanaingia kwenye uongozi wa vijiji kufanikisha malengo yao,” alisema Happy. “Hii haikubaliki. Naviagiza vyombo vya dola kuwasaka wote, hasa wale mapapa wanaofadhili mtandao huu wa wizi.”

“Huu mtandao lazima umalizwe,” aliongeza Happy kwenye mahojiano yake hayo na Mwananchi. “Vyombo vya dola fanyeni oparesheni bila kumuonea mtu wala kumuacha mwizi, wakamateni wote, kamateni mapapa wanaoongoza mtandao huu bila kujali nafasi za uongozi kwa sababu mhalifu ni mhalifu tu.”

Happy hakuweza kuendelea kutimiza azma yake ya kuusambaratisha mtandao huo kwani wiki moja baadaye uteuzi wake ulitenguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye panga-pangua yake kwenye safu ya wakuu wa miko na wilaya.

Kwenye habari yao hiyo, Mwananchi pia ilimripoti Meneja wa Mgodi wa North Mara, Apolinary Lyambiko, ambaye pia alikiri uwepo wa mtandao huo, akisema kwamba kwa mwaka 2021 pekee, jumla ya matukio 76 ya wizi wa mawe yenye dhahabu yaliripotiwa mgodini hapo.

Uthibitisho wa uwepo wa mtandao huo wa kihalifu mtandaoni hapo pia ulibainishwa kwenye nyaraka zilizowekwa hadharani wakati wa kesi hiyo inayoendelea katika Mahakama ya nchini Uingereza dhidi ya Barrick Gold.

‘Wavamizi’
Taarifa za mtandao huu wa kihalifu pia zinakuja wakati ambao Barrick Gold imekuwa ikivutana na jamii zilizokaribu na mgodi wake wa North Mara, ikilalamika kuhusiana na shughuli za wachimbaji wadogo mgodini hapo na watu kutoka jamii hizo kuvamia eneo la mgodi na kufanya vitendo vya kihalifu.

Namna ya kukabiliana na “wavamizi” hawa kumekuwa kukiiweka Barrick Gold matatani, huku mashirika ya haki za binadamu, hususan shirika la RAID la nchini Uingereza, likiishutumu Barrick kukiuka haki za msingi za binadamu wakati wa kutekeleza juhudi za kuzuia “uvamizi” huo.

Lakini kwa mujibu wa tathmini iliyofanywa na Europe Conflict and Security Consulting Ltd na kuwekwa wazi kwenye kesi inayoendelea huko Uingereza, hasara inayotokana na “uvamizi” huu ni ndogo sana ikilinganishwa na hasara inayotokana na uhalifu unaofanywa na mtandao wa kihalifu mgodini hapo.

Kwa mfano, tathmini hiyo inaonesha kwamba uhalifu unaotokana na mtandao wa kihalifu unakadiriwa kufikia Dola za Kimarekani milioni 2.5 (Shilingi bilioni 6.2), kwa mwaka, wakati ule unaotokana na “wavamizi” unasimama kwenye Dola za Kimarekani 200,000 (Shilingi milioni 501), kwa mwaka.

Kwenye tathmini yao hiyo, Europe Conflict and Security Consulting Ltd wamebainisha athari mbalimbali zitokanazo na uhalifu huo wa kimtandao, ikiwemo kuongezeka kwa biashara ya ukahaba na maradhi ya ngono mgodini hapo na maeneo yanayouzunguka mgodi huo.
 
Back
Top Bottom