Pdidy
JF-Expert Member
- Nov 22, 2007
- 50,956
- 22,150
Mhandisi awa mganga wa wilaya
Jackson Odoyo
Jackson Odoyo
HALMASHAURI ya Manispaa ya Shinyanga, imemteua mtu asiyekuwa na taaluma ya udaktari kuwa Kaimu Mganga Mkuu wa Manispaa hiyo (DMO), baada ya aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo, Dk Nasoro Rwabudongo kufariki dunia.
Habari zilizopatikana jana kutoka Shinyanga zinaeleza kuwa, Kaimu DMO huyo, Kasimu Thadeo ni mtaalam wa Uhandisi wa Afya ya Mazingira (Sanitation Engineering).
"Thadeo hana taaluma ya afya na wala si daktari kama anavyoitwa ingawa alipewa nafasi hiyo katika mazingira ya kufahamiana na baadhi ya watendaji wa manispaa na kwa kuwa hana taaluma ya afya, amekuwa akiendesha mambo kinyume na taratibu za afya," kilisema chanzo kimoja.
Thadeo alipoulizwa kuhusu suala hilo alikiri kwamba hana taaluma ya udaktari, lakini alikanusha kwamba amepewa nafasi ya kukaimu nafasi hiyo kwa makosa. Ni kweli mimi si daktari.
Nilikaimishwa ofisi hii baada ya daktari aliyekuwepo kwenda masomoni na kabla ya kurudi akafariki dunia akiwa huko na baada ya hapo nikaendelea kuwa DMO kwa sababu nina taaluma ya usafishaji 'cleanliness' na hii ilitokana na utaratibu wa ofisi hii kuwa na vitengo viwili ambavyo ni kitengo cha kinga na tiba ambalo ndilo eneo la daktari na eneo jingine ni la usafishaji ambalo ndilo eneo langu, hivyo mimi nikawa kama msimamizi wa masuala ya usafi na si masuala ya kinga na tiba," alisema Thadeo na kuongeza:
"Sijashika nafasi hii kimakosa na wala kazi zangu haziendani na matibabu, hivyo nitaendelea kushika nafasi hii mpaka serikali itakapoleta mtu atakayeshika nafasi hii.
Mimi nimeishika nafasi hii kama mtawala. Kazi ninazofanya ni za utawala tu lakini kazi zinazolenga masuala ya taaluma ya udaktari ninawatumia madaktari wa manispaa na wala mimi sichomi sindano wala siendi hospitalini.
Thadeo alisema pamoja na kwamba yeye sio daktari anafanya kazi kwa karibu na madaktari wa manispaa akimtaja, Dk Edith Kuezi kuwa amekuwa akifanya kazi naye kwa karibu.
Akizungumzia suala hilo, Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Mstahiki Hassan Mwendapole alisema kwamba, Thadeo alishika nafasi hiyo kwa sababu ndiye pekee mwenye elimu ya chuo kikuu katika idara ya afya ya Manispaa hiyo.
Alisema akiwa mwajiri wa Thadeo, anafahamu kwamba hana taaluma ya udaktari, bali ya afya ya mazingira na kwa nafasi hiyo aliyonayo katika manispaa hiyo ni ya utawala na si matibabu.
"Ni kweli huyo bwana hana taaluma ya afya na wala si daktari, bali ana taaluma ya afya ya mazingira na ni mtu pekee mwenye elimu ya chuo kikuu katika idara ya afya, hivyo tuliamua tumpe nafasi hiyo kwa sababu nafasi kama hiyo haiwezi kushikwa na mtu asiyekuwa na elimu ya chuo kikuu," alisema Mwendapole.
Alipoulizwa kwa nini wasichukue daktari kutoka katika Hospitali ya Mkoa ili aweze kushika nafasi hiyo, alisema: "Ni kweli tungeweza kufanya hivyo na kwa kuwa umenipa ushauri mzuri nitalifanyia kazi ingawa tulishaomba daktari mwenye elimu ya chuo kikuu aje kushika nafasi hiyo."
Kuhusu malalamiko ya wataalam wa afya kuwa Thedeo anakiuka kanuni na taratibu za taaluma ya afya tangu aliposhika nafasi hiyo alisema: "Mimi sina taarifa hiyo ila nitalifanyia kazi haraka iwezekanavyo."