SoC03 Mfumo wa elimu ya Tanzania una cha kujifunza kutoka mitaala ya kimataifa?

Stories of Change - 2023 Competition

Haas

New Member
Aug 15, 2022
1
1
Kutoka katika fukwe za Bahari ya Hindi hadi katika kilele cha mlima Kilimanjaro, Tanzania imejawa na utajiri wa asili, tamaduni mbalimbali, na watu wenye upeo mkubwa. Lakini katikati ya haya yote, kuna hazina isiyoweza kulinganishwa na chochote: elimu ya Tanzania. Elimu, kama msingi wa maendeleo na ustawi, inashika nafasi muhimu katika ujenzi wa taifa imara na lenye mafanikio. Mfumo wa elimu wa Tanzania unajumuisha nguvu na changamoto ambazo huathiri maisha na ndoto za mamilioni ya wanafunzi wanaojitahidi kujipatia elimu bora. Ni katika taswira hii tuzingatie mapungufu yaliyopo na jitihada zinazohitajika ili kuiboresha mfumo huu wa elimu ambao una athari kubwa kwa mustakabali wa taifa letu.

Katika chapisho hili tutaangalia kwa kina mapungufu yanayokabili mfumo wa elimu ya Tanzania na kujaribu kuvumbua njia za kuleta maboresho yenye ufanisi na endelevu.

Hapa Tanzania zipo shule kadhaa zinazotumia mitaaala ya kimataifa kama International Baccalaureate(IB) na Cambridge International curriculum. Wapo wazazi hapa Tanzania hasa wale wenye kipato na wenye kupenda kufanya tafiti za kutosha kabla ya kuamua shule ipi na mtaala upi ni sahihi kwa watoto wao wameamua kuwapeleka watoto wao kwenye shule zinaotumia mitaala ya kimataifa.

Kwa kifupi shule za kimataifa ni taasisi za elimu ambazo zinafuata mitaala na mifumo ya elimu inayotambuliwa na kutumiwa kimataifa. Shule hizi zinajulikana kwa kutoa elimu bora kwa wanafunzi kutoka tamaduni tofauti na mataifa mbalimbali. Mitaala inayotumiwa mara nyingi katika shule za kimataifa ni pamoja na International Baccalaureate (IB), Cambridge International Curriculum, au mitaala mingine inayozingatia viwango vya kimataifa.

Shule za kimataifa zinathamini ujifunzaji wa vitendo, stadi za maisha, kufikiri kwa kina, na ujuzi wa kimataifa. Wanafunzi hupata nafasi ya kujifunza katika mazingira yanayowakutanisha na wanafunzi kutoka tamaduni tofauti, kuongeza uelewa wao wa tamaduni mbalimbali, na kukuza uwezo wao wa kuzungumza lugha za kigeni.


Wahamiaji wengi pamoja na watanzania wenye Asili ya Asia huwapeleka watoto wao kwenye shule hizi zinazotumia mitaala ya IB au Cambridge hapa nchini.

Nina maswali mawili hapa kwako ndugu msomaji wa andiko hili; swali la kwanza ni je, umewahi kujiuliza ni kwanini makundi tajwa hapo juu huamua kuwapeleka watoto wao katika shule zinazotumia mitaala hiyo?

Natumai umewahi kuona au kusikia usaili katika wizara au taasisi mbalimbali binafsi au za serikali hapa Tanzania. Katika usaili wanaojitokeza kwa asilimia kubwa ni wale waliosoma katika shule zinazotumia mtaala wa hapa nyumbani.

Hali hii inanileta kwenye swali langu la pili; je, umewahi kujiuliza wanaosoma katika shule zinazotumia mitaala ya Cambridge pamoja na IB na kuhitimu elimu yao ya sekondari katika shule kama IST, DIA,Braeburn, Feza International, HOPAC, UWCEA(Moshi International School),St. Constantine, Almuntazir Islamic International School na nyinginezo zenye mitaala hiyo, kwanini hatuwaoni kwa wingi katika usaili wa taasisi mbalimbali hapa nchini?

Tanzania inaweza kuchunguza mitaala ya shule za IB, Cambridge na shule nyingine za kimataifa ili kuboresha mtaala wa ndani. Mitaala hii inazingatia zaidi ujifunzaji unaolenga mwanafunzi kuendeleza ujuzi wa kufikiri kwa kina, na kukuza stadi za maisha. Tanzania inaweza kubuni au kuboresha mtaala wake kuwa wenye kuzingatia ujifunzaji wa vitendo, uwezo wa kujifunza kwa kujitegemea, na ujuzi wa kufikiri kwa ubunifu.

Wahitimu kutoka katika shule hizi huwa na uwezo unaohitajika na vyuo mbalimbali duniani hivyo kupata nafasi za kujiendeleza kiurahisi kwa kupata ufadhili wa masomo au vinginevyo. Safari yao ya taaluma huendelea na hatimae kuwa na ujuzi unaohitajika na wenye kuwawezesha kufanya kazi katika taasisi mbalimbali duniani au kufungua taasisi/kampuni zao wenyewe. Elimu wanayoipata huwafungua fikra na kuwafanya kuwa watu ambao wapo tayari kukabiliana na changamoto za ulimwengu na watu wake na sio changamoto zilizopo ndani ya mipaka ya taifa moja dogo la Africa ya Mashariki peke yake. Natumai sasa umepata majibu ya maswali mawili niliyoyauliza hapo awali ya kwamba kwanini wazazi na wahamiaji wengi huwapeleka watoto wao katika shule hizi na kwanini hatusongamani na wahitimu wa shule hizi katika usaili wa taasisi mbalimbali hapa nchini.


Nini kifanyike hapa kwetu?

Kwanza, kukiri uwepo wa tatizo katika mfumo wetu wa elimu na kuweka nia thabiti na njia madhubuti za utatuzi wa tatizo.

Mafunzo na Maendeleo ya Walimu: Ni muhimu kuwekeza katika mafunzo na maendeleo ya walimu kitaaluma na kiuchumi ili kuwajengea ujuzi na maarifa yanayohitajika kuendeleza mbinu za kufundishia na kujifunza zinazolingana na mifumo ya kimataifa. Shule za kimataifa zinafanya mafunzo na mikutano ya mara kwa mara ili kuboresha ujuzi wa walimu wao. Tanzania inaweza kuiga mfano huu na kuweka mikakati madhubuti ya kutoa mafunzo ya mara kwa mara na motisha stahiki kwa walimu ili kuwawezesha kutekeleza mabadiliko katika mbinu za ufundishaji.

Rasilimali na Miundombinu: Tunahitaji kuwekeza katika miundombinu ya elimu na kuongeza upatikanaji wa rasilimali zinazohitajika kwa ufanisi wa elimu. Tujitahidi kuwa na mazingira bora ya kujifunzia, vifaa vya kisasa, na maktaba zenye aina mbalimbali za vitabu. Kwa kujenga na kuimarisha miundombinu ya elimu, tutaweza kutoa mazingira bora zaidi kwa wanafunzi na walimu kufanya kazi.

Kuhamasisha Ubunifu na Uvumbuzi: Tunaweza kuweka mazingira ya kukuza ubunifu na uvumbuzi katika mfumo wa elimu. Hii inaweza kujumuisha kuanzisha vituo vya kisayansi, mashindano ya ubunifu, na mafunzo ya stadi za maisha zinazohimiza uvumbuzi na ujasiriamali.

Ni wazi kuwa mambo tajwa hapo juu pamoja na mengine yenye tija kwa ukuaji na ustawi wa elimu yetu yanahitaji uwekezaji wa kifedha, sera Madhubuti, pamoja na watu werevu na wenye weledi wa kutosha katika nyanja ya elimu. Serikali imeamua kufanya elimu bila malipo na inachukua jukumu la kubeba mzigo wote huu kwa asilimia kubwa.

Serikali na wadau wa elimu pamoja na wananchi kwa ujumla wao wanapaswa kutambua kuwa jambo hili sio dogo na wenzetu katika mataifa mengine walitumia nguvu kubwa kufika walipo leo. Elimu bora ni gharama na ndio maana malipo katika shule hizi za kimataifa ni makubwa mno kutokana na vile wanavyovifanya ikiwemo tafiti, safari/ziara za kimasomo, mishahara minono kwa walimu, miundombinu wezeshi pamoja na mambo mengine.

Mwisho, elimu inapaswa kuwa suala la kitaifa na lisifungwe na masuala ya kisiasa. Uamuzi na utekelezaji wa sera za elimu lazima uwe na lengo la kuboresha elimu na kutoa fursa sawa kwa wanafunzi wote. Tunaweza kujifunza kutoka nchi nyingine ambazo zimefanikiwa kuweka mfumo thabiti wa elimu, kama vile Finland ambayo imejitahidi kuondoa siasa katika elimu na kuzingatia ubora wa mchakato wa kufundisha na kujifunza.



BRAEBURN TUITION FEE.png
DIA FACILITIES.png
IST TUITION FEE.png
 
Back
Top Bottom