Elections 2010 Mchakato wa kuapishwa mawakala jimbo la singida mashariki - UCHAKACHUAJI WA KUTISHA

George Maige Nhigula Jr.

JF-Expert Member
Mar 14, 2008
470
149
Friday, October 29, 2010

Mchakato wa kuapishwa kwa mawakala Jimbo la Singida Mashariki-Uchakachuaji ukatishao tamaa



Jana nilikuwa kwenye mchakato wa kuapishwa kwa mawakala watakaosimamia na kuangalia kura za wagombea ili zisiende kusikokusudiwa na kusiko kwa matakwa ya wapiga kura.

Shughuli hii ilifanyikia katika shule ya Msingi Makiungu. Mbali na zoezi hili, pia kulikuwa na semina kwa ajili ya wasimamizi wa uchaguzi.

Zoezi hili la kuapishwa kwa mawakala halikwenda vizuri hata kidogo. Mchakato huu ulikuwa na dosari mbalimbali na ambazo kwa kiasi kikubwa zitakuwa na adhari sana kwa vyama vya upinzani na hasa chama cha demokrasia na maendeleo(CHADEMA)

Majina mengi ya watu waliojitolea kuwa mawakala wa vyama walijikuta wakikosa nafasi hizo na badala yake kuchukuliwa na watu wengine bila hata kuwa na sababu za kueleweka.

Kwa mujibu wa wananchi wanasema kuwa majina ya watu waliotakiwa kuapishwa ni yale yaliyotolewa na ofisi ya tume ya uchaguzi ngazi ya wilaya ambayo yaliwasilishwa na wagombea wa vyama husika.

Kasoro nyingine iliyojitokeza ni ile ya mtu mmoja kuwa wakala wa vyama viwili kwa wakati mmoja wakati wapo wale waliojitolea kwa dhati katika kusimamia na kulinda kura za vyama husika kizalendo na kwa moyo wote, lakini wakaikosa nafasi.

Miongoni mwa mawakala wa Chadema, wapo mawakala wawili ambao watu hawakuweza kuwafahamu kabisa na ilibidi wafuatiliwe kwa ukaribu ili kuweza kutambua uhalali wao wa kuweza kuwa mawakala wa Chadema pamoja na kuwa walikuwa wameshaapishwa.

Niliwashuhudia mawakala wa Chadema muda mfupi kabla ya kuapishwa. Ni ukweli usiopingika kuwa, wengi wao walikuwa ni wazee na akinamama ambao wengi walionekana wasio na uelewa wa mambo ya uchaguzi na ambao wataweza kurubuniwa kirahisi mno. Tetesi zinasema kuwa chama tawala katika jimbo hili kimetenga takribani Tsh 800,000 kwa kila kituo cha uchaguzi kwa ajili ya kuhonga endapo mambo yatakuwa sivyo kwa upande wao. Kama hili ni la kweli, basi kwa hali ya mawakala wa Chadema kwa jinsi nilivyowaona na namna walivyopatikana, basi kuna hatari kubwa sana ya Chadema kuangukia pua. Na kwa hili, Chadema itabidi ijilaumu kwani wawakilishi wa chadema waliokuwa wanasimamia zoezi hili angalao nao walitakiwa wapewe list ya majina ya mawakala waliokubalika na chama na ambayo pia ndiyo iliyotumwa kwenye ofisi ya Tume ya uchaguzi ngazi ya wilaya kama kweli utaratibu huu ulikuwepo.

Binafsi nilikuwa miongoni mwa watu niliojitolea kusimamia kura za Chadema lakini kwa bahati mbaya ama nzuri, jina langu halikuonekana. Hakukuwa na sababu za kueleweka kwa nini ikawa hivyo. Kilichonishangaza zaidi ni kuwa, mawakala wa chadema walikuwa wengi, na mara baada ya majina kutajwa, ya wale watakaoapishwa, basi kundi lile likawa kama limegawanywa mara mbili. Yani ikawa kama vile idadi ya mawakala ilichukuliwa mara mbili zaidi ya wale waliokuwa wanahitajika. Hapa nina wasiwasi sana wa kuwepo kwa"mapandikizi" ambayo yataweza kufanikisha kirahisi wizi wa kura.
Kwa utafiti mdogo nilioufanya, mawakala walioachwa, walionekana kujua nini wangetakiwa kufanya na waliokuwa na ujasiri, walikuwa ni watu waliokuwa tayari kusimamia haki na kukitetea chama chao. Inasemekana watu hawa waliwekwa kando kwa makusudi kamili na hili linadhaniwa kuwa lilifanywa baada ya majina yaliyokubaliwa chamani kuwasilishwa kwenye ofisi ya tume ya uchaguzi ngazi ya wilaya.

Jambo jingine ambalo nililishuhudia ni hili la mawakala kuhamishwa kwenda kusimamia vituo ambavyo hawakujiandikisha. Hili nililiona kwa mawakala wa Chadema, sijui kwa mawakala wa vyama vingine kama hali hii ilijitokeza. Hii inamaanisha kuwa, mawakala waliopangwa kwenye vituo tofauti na walivyojiandikisha, wataikosa fursa ya kupiga kura. Kwa maana hii, kama kuna mchezo mchafu, na kama mawakala hawa ni wakereketwa wa kweli wa Chadema, basi kwa mtindo huu, kura nyingi za Chadema zitapotea.

Kuna swali la kujiuliza hapa, Chadema ilikuwaje wasiwapatie madiwani wao ambao pia wanagombea (ambao ndio walionekana kuwa watendaji wakuu kwenye zoezi hili) nakala za majina ambayo chama kiliyaafiki? Pengine kwa hili, hawana budi kujilaumu.

Nimalizie kwa kusema kuwa, kwa hali niliyoiona katika mchakato huu wa kuapishwa mawakala, kama hali ndio hii kwenye vingi ya vijiji vyetu, basi upinzani hususani Chadema wanaweza kupoteza kura nyingi ambazo zilikuwa halali yao. Na urahisi huu wa kuweka mapandikizi hususani vijijini ni miongoni mwa sababu zifanyazo mara nyingi vijijini vyama vya upinzani kuangukia pua na hatimaye watu wanasema kuwa CCM inapendwa na watu wa vijijini eti kwa sababu ni chama cha Mwalimu Nyerere.


SOURCE "Mwangaza": Mchakato wa kuapishwa kwa mawakala Jimbo la Singida Mashariki-Uchakachuaji ukatishao tamaa
 
Back
Top Bottom