Luhaga Mpina (mb), akichangia kuhusu taarifa za kamati za kudumu za bunge za PAC, LAAC na PIC

Jun 25, 2022
3
7
1. UTANGULIZI
Taarifa za Kamati ya PAC na LAAC zinawasilishwa bungeni baada ya kufanya uchambuzi wa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 na Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya Mwaka 2008 inayofafanua masharti muhimu kwa ajili ya kuwezesha ukaguzi, uandaaji wa Ripoti za CAG, uwasilishaji wake, kujadiliwa na Kamati na hatimaye Bunge.

Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imekuwa ikiwasilishwa kila mwaka ikiwa na hoja nyingi zenye kuashiria wizi, uzembe, ubadhirifu, ufujaji na ufisadi mkubwa wa fedha na rasilimali za umma. Hoja nyingi zimekuwa zikijirudia kila mwaka huku utekelezaji wa hoja za mkaguzi ukiwa mdogo na usiokuwa na mrejesho madhubuti kwa umma. Lakini pia uchukuaji wa hatua kwa wahusika ni hafifu.

2. Uwasilishaji wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Kamati za ukaguzi za PAC na LAAC bungeni.

Awali nianze kwa kukupongeza sana Mheshimiwa Spika, Dk. Tulia Ackson pamoja na Kamati ya Uongozi ya Bunge kwa kutenga muda wa kutosha kujadili taarifa za kamati za ukaguzi za PAC na LAAC bungeni. Nawapongeza na kuwashukuru kwa kusikia kilio cha muda mrefu cha waheshimiwa wabunge kuomba kamati hizi zitengewe muda wa kutosha ili kuwapa fursa waheshimiwa wabunge kupitia kwa kina Ripoti ya CAG katika hatua muhimu ya kuisimamia Serikali.

Awali taarifa za kamati hizi muhimu hazikupewa uzito unaostahili bungeni ambapo taarifa zilikuwa zinawasilishwa kwa muda wa siku moja na kuamualiwa, wachangiaji wachache na kila mchangiaji anapewa dakika 5 za kuzungumza bungeni. Hali hii ililinyima fursa Bunge kutekeleza wajibu wake wa kikatiba kikamilifu na kutumika kama rubber - stamp ya kuhalalisha wizi, uzembe, ufujaji, ubadhirifu na ufisadi wa fedha za umma unaofanywa na baadhi ya watumishi wa Serikali.

Leo hii tunashuhudia muda wa kujadili hoja za kamati hizi bungeni ukiongezwa kutoka siku 1 ya awali hadi siku 5 lakini pia muda wa wachangiaji kuongezwa kutoka dakika 5 hadi dakika 15 na idadi ya wachangiaji kuongezeka. Suala hili limetufurahisha sana wawakilishi wa wananchi na huu ni uthibitisho tosha kuwa Mheshimiwa Spika Dk Tulia Ackson Mwansasu wewe ni mzalendo wa kweli.

Pamoja na marekebisho haya tunayoendelea kuyafanya katika uwasilishaji wa taarifa za kamati za ukaguzi na Ripoti ya CAG bungeni bado kuna changamoto kama ifuatavyo:-

(i) Taarifa za Kamati za ukaguzi PAC na LAAC hazionyeshi mrejesho wa utekelezaji wa hoja za CAG na hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahusika waliotajwa katika Ripoti ya CAG ya mwaka wa fedha uliopita.

(ii) Taarifa za Kamati za PAC na LAAC kushindwa kuchambua hoja zote zilizotajwa katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na badala yake zimekuwa zikichagua hoja chache na kuziwasilisha bungeni, hali hiyo inasababisha Bunge kukosa fursa ya kuelewa utekelezaji wa hoja zingine zilizoachwa na kamati.

(iii) Taarifa za ukaguzi za PPRA, TAKUKURU na Mbio za Mwenge wa Uhuru haziwasilishwi na kujadiliwa bungeni wala Kamati za ukaguzi za PAC na LAAC hazifanyi uchambuzi wa taarifa hizo muhimu.

(iv) Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hapewi nafasi ya kuingia bungeni kutoa ufafanuzi wa kina pale inapobidi wakati hoja za Kamati za Ukaguzi za PAC na LAAC zinajadiliwa bungeni.

Kwa kuwa, hizi changamoto zinarudisha nyuma jitihada za Bunge katika kuisimamia Serikali na kupelekea hoja za ukaguzi kujirudia mara kwa mara huku wizi, uzembe, ufujaji, ubadhirifu na ufisadi kuzoeleka kama jambo la kawaida, Na kwa kuwa, Mheshimiwa Spika umeshaonyesha nia ya dhati ya kuleta mageuzi ya kweli katika Bunge lako, Hivyo basi, Bunge liazimie kwamba

(i) Kanuni za Bunge zifanyiwe marekebisho ili kumruhusu CAG kuingia bungeni pindi Taarifa za Kamati za Ukaguzi za PAC na LAAC zinapowasilishwa na kujadiliwa bungeni.

(ii) Kufanya marekebisho ya Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya Mwaka 2008 na Kanuni za Kudumu za Bunge ili kuwezesha Taarifa za Ukaguzi za PPRA, TAKUKURU na Mbio za Mwenge wa Uhuru kuwasilishwa na kujadiliwa bungeni.

(iii) Taarifa za PAC na LAAC ziwasilishwe bungeni zikiwa na kiambatisho cha jedwali la majibu ya Serikali, maoni ya mkaguzi na utekelezaji wa hoja zote zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika mwaka husika wa fedha. Pia taarifa hizo ziambatishwe na jedwali la utekelezaji wa hoja za ukaguzi na hatua zilizochukuliwa kwa wahusika kwa mwaka wa fedha uliopita.

3. Malipo yaliyofanywa na TANESCO kwa Kampuni ya Symbion Power LCC.

Kiasi cha Dola za Marekani Milioni 153.43 sawa na kiasi cha Tsh Bilioni 350 Taarifa ya Kamati inaeleza kuwa mkataba baina ya TANESCO na Symbion Power LCC wa kukodisha mitambo ya kuzalisha umeme iliyopo eneo la Ubungo Dar es Salaam uliingiwa mnamo Tarehe 7 Julai 2001 na kumalizika Tarehe 19 Septemba 2013 ambapo Mkataba huo uliongezwa miaka 2 hadi Tarehe 18 Septemba 2015.

Taarifa ya Kamati inaonyesha kuwa TANESCO na Kampuni ya Symbion walianza majadiliano ya kuwa na mkataba wa muda mrefu wa mauziano ya umeme, ‘Power Purchase Agreement’ (PPA) ambapo makubaliano ya awali yalisainiwa Tarehe 15 Septemba 2015. Kampuni ya Symbion kuiuzia TANESCO megawati 112 kwa gharama za Dola za Marekani 0.01775 kwa KWh (50% x 0.285 plus 0.0035) lakini ilipofikia Tarehe 24 Mei 2016 Kampuni ya Symbion ilitakiwa kuondoa mitambo yake kwenye Gridi ya Taifa baada ya kutokuelewana kwa pande zote mbili.

Baada ya uamuzi huo kujitokeza mashauri 2 ya madai dhidi ya TANESCO yalifunguliwa na Kampuni ya Symbion katika Chemba ya Kimataifa ya Biashara (ICC) na Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) kwa kuidai TANESCO Dola za Marekani 1,566,254,652.41. Ilipofikia mnamo Tarehe 21 Mei 2021 pande hizo mbili TANESCO na Kampuni ya Symbion Power LCC zilifikia makubaliano (Deed of Setlement) ambapo makubaliano yalikuwa malipo ya dola za Marekani Milioni 153.43 sawa na kiasi cha Tsh Bilioni 350 bila kujumuisha kodi na gharama zinginezo.

Taarifa ya Kamati ya PAC haikufanya uchambuzi wa kina kuliwezesha Bunge kuelewa msingi wa malipo yaliyofanywa na Serikali kwa Kampuni ya Symbion yapo mambo mengi yaliyopaswa kuzingatiwa na kutolewa ufafanuzi kama ifuatavyo:-

(i) Je msingi wa makubaliano wa TANESCO kuilipa Symbion kiasi cha Tsh Bilioni 350 ulikuwa ni nini, kwanini taarifa haijaeleza kifungu cha mkataba kilichokiukwa na kupelekea nchi kulipishwa mabilioni ya fedha ambapo PPA ilikuwa na miezi 10 tu tangu iingiwe Tarehe 15 Septemba 2015.

(ii) Taarifa ya Kamati ya PAC haijaeleza kama kulifanyika tathmini ya kina kujua malimbikizo ya kodi na madai mbalimbali ya Serikali kwa Kampuni ya Symbion Power LCC tangu kuingia mkataba mnamo Tarehe 7 Julai 2001 (miaka 21 iliyopita) kabla ya kufikia uamuzi wa kuwalipa fidia ya Tsh Bilioni 350.

(iii) Taarifa ya Kamati ya PAC haijaeleza msingi wa kuongezwa muda wa mkataba baina ya TANESCO na Kampuni ya Symbion Power LLC Tarehe 15 Septemba 2015 wakati mkataba huo ulikuwa umebakiza siku tatu tu kufika mwisho wake tarehe 18 Septemba 2015

Mkataba huo uliokuwa ukilitia hasara taifa na kuifanya TANESCO ishindwe kujiendesha na kutoa huduma bora kwa wananchi umehuishwa na kuongezwa muda mrefu wakati miradi mikubwa ya kitaifa ya kuzalisha umeme wa Megawati 583 ilikuwa katika hatua za mwisho kukamilika. Mradi wa kufua umeme wa Kinyerezi I (Megawati 150) ulikamilika mwaka 2016, Kinyerezi II (Megawati 248) ulikamilika mwaka 2018 na Kinyerezi I extension (Megawati 185) ambao uko hatua za mwisho kukamilika na huku utekelezaji wa miradi mingine ya kimkakati ya uzalishaji umeme maeneo mbalimbali nchini ilikuwa ikiendelea.

Kukamilika kwa Miradi hii kulikuwa kunalifanya taifa letu kuwa na umeme wa ziada katika Gridi ya Taifa na kuliwezesha taifa kuziuzia umeme nchi jirani, sababu za kuhuisha mkataba baina ya TANESCO na Kampuni ya Symbion Power LLC, Tarehe 15 Septemba 2015 wenye uzalishaji wa Megawati 112 zilikuwa zimelenga kufanikisha kitu gani wakati Taifa lilikuwa linaenda kuongeza Megawati 583 katika Gridi ya Taifa kwa kipindi kifupi.

(iv) Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilishaagiza mkataba huu kusikitishwa kutokana na gharama kubwa za kuiuzia umeme TANESCO hali iliyokuwa inapelekea Serikali kulipa madeni ya TANESCO mara kwa mara, ni nani alitoa kibali cha TANESCO kuingia mkataba upya wakati nchi ilikuwa kwenye uchaguzi?.

(v) Mara tu baada ya makubaliano baina ya TANESCO na Kampuni ya Symbion Power LLC, Serikali ililipa fedha hizo Mei 2021 kiasi cha Tsh Bilioni 350. Je kiasi hicho cha fedha kiliruhusiwa na nani wakati Bunge lilikuwa limeshapitisha Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2020/2021 na kwanini ilipe Serikali na sio TANESCO. Je kulikuwa na udharura gani wa kufanya malipo hayo kwa haraka?

(vi) Taarifa ya Kamati inaeleza dosari za usimamizi wa mkataba na kutofanyika kwa upembuzi yakinifu kabla ya kuvunja mkataba kati ya TANESCO na Symbion Power LLC lakini haiwataji wahusika ni akina nani na haielezi ni hatua gani zimechukuliwa kwa wahusika waliolisababishia taifa hasara kubwa.

Kwa kuwa, hakuna maelezo ya kutosha kwenye jambo hili lililoingizia hasara kubwa nchi yetu ya kiasi cha Tsh Bilioni 350 huku kukiwepo na mahitaji makubwa ya fedha kugharamia huduma muhimu na maendeleo ya nchi tena kipindi kibaya ambacho nchi ilikuwa kwenye mtikisiko mkubwa wa uchumi kutokana na janga la Korona (Uviko-19), Na kwa kuwa, ufafanuzi wa kina haujaonekana kwenye Taarifa ya Kamati ya PAC wala Ripoti ya CAG,

Hivyo basi, Bunge liazimie kwamba iundwe Kamati teule ya Bunge kuchunguza suala hili ili kupata uhalali na haki za watanzania katika mkataba huo.

4. Malimbikizo ya Kodi za Makinikia Trilioni 360
Taarifa ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2019/2020 ilibaini kuwepo kwa kodi zilizoshikiliwa kiasi cha Tsh Trilioni 360 katika Mahakama za rufani za kodi ambazo Mahakama ya Rufaa (CAT), Bodi ya Rufani za Kodi (TRAB) na Baraza la Rufani za Kodi (TRAT). Malimbikizo haya yalijumuisha madeni ya malimbikizo ya kodi kutoka kwenye makampuni ya madini (Makinikia).

Serikali kupitia Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dk. Mwigulu Lameck Nchemba ililiambia Bunge wakati akijibu swali langu hapa bungeni Tarehe 23 Septemba 2022 kuwa maamuzi yaliyofikiwa kati ya Kampuni ya Barrick na Serikali tarehe 24 Januari 2020 Serikali iliamua kusamehe malimbikizo ya kodi ya Trilioni 360 baada ya kukubaliana na Kampuni ya Barrick kulipa Dola za Marekani Milioni 300 ambayo ni sawa na Tsh Bilioni 700. Waziri Mwigulu alilieleza Bunge kuwa makubaliano hayo yalifanyika chini ya uongozi wa Hayati Dk. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa awamu ya Tano katika sherehe iliyofanyika Ikulu Tarehe 24 Januari 2020.

Maelezo ya Waziri Dk. Mwigulu Nchemba yanakinzana na Taarifa za Ukaguzi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za Mwaka 2019/2020 na Mwaka 2020/2021.

Kwa mujibu wa maelezo ya Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba kuwa kodi hizi zilifutwa Tarehe 24 Januari 2020 yanaleta mashaka makubwa kwani taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2019/2020 inaonyesha kuwepo kwa mashauri ya kesi za malimbikizo ya kodi za madini (Makinikia) na kama yangekuwa yamefutwa yasingeonekana kwenye taarifa ya Mkaguzi katika mwaka huo wa fedha.

Huku Waziri wa Fedha akieleza kuwa kodi hizo zimefutwa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2020/21 inaonyesha kuwa kesi za Makinikia zipatazo 45 zenye thamani ya Fedha Trilioni 5.595 ziliamuliwa katika Mamlaka za Rufani za Kodi yaani TRAB na TRAT ambapo iliagizwa Serikali kufanya majadiliano (negotiations) na walipakodi (makampuni ya madini) yanayodaiwa ili kuweka utaratibu wa namna ya kulipa kodi hiyo stahiki ya Serikali.

Mamlaka za Rufani za Kodi ziliagiza mazungumzo yafanyike baina ya Serikali na Makampuni ya Madini ya North Mara Gold Mine, Pangea Minerals Limited, Bulyanhulu Gold Mine na ABG Exploration.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aliilalamikia Serikali kwa kuchukua muda mrefu kufanya mazungumzo (negotiations) na walipa kodi makampuni ya madini. Kama madai hayo yalifutwa tangu Tarehe 24 Januari 2020 kwanini CAG alalamikie kuwepo ucheleweshaji wa majadiliano baina ya Serikali na makampuni ya madini kuhusu mashauri hayo Mwaka wa Fedha 2020/2021 (huku kuna majadiliano huku tunaambiwa kodi hizo zimesamehewa na kufutwa wananchi tuchukue lipi?)

Mahakama za Rufani za Kodi pia ziliamua kurejesha mashauri TRA yenye thamani ya shilingi Trilioni 343.5 kwa ajili ya kusikilizwa na hatua zingine katika Mwaka wa Fedha 2020/2021.

Awali Tume za uchunguzi zilizoundwa na Serikali zilionyesha namna makampuni ya madini yalivyokuwa yakikwepa kulipa kodi zaidi ya miaka 17 kwa kuweka usiri mkubwa katika utunzaji wa kumbukumbu, uwasilishaji wa taarifa mbili tofauti ya mapato ya kodi inayowasilishwa serikalini na inayotumwa kwenye kampuni mama nje ya nchi.

Pia mbinu zingine walizotumia kukwepa kodi ni katika manunuzi ya mitambo, vifaa na mahitaji, uhamishaji wa bei za bidhaa na huduma (Transfer Pricing), Uhamishaji wa Mitaji (Capital Flight) ambako kulipelekea nchi yetu kupoteza mapato mengi ya kodi katika Sekta ya Madini, upotevu wa ajira na kuliingiza Taifa kwenye hasara kubwa.

Mahakama za rufani za kodi zimehitimisha mashauri 45 yenye thamani ya Tsh Trilioni 5.595 na kuagiza kufanyika majadiliano kati ya Serikali na walipakodi. Ni Mamlaka gani iliyofuta au kusamehe mapato ya kodi ya Serikali na je mamlaka hiyo inayo nguvu hiyo kisheria?

Bunge halijawahi kuletewa taarifa na Serikali ya kusamehe au kufuta madai ya malimbikizo ya kodi kwenye kesi za makinikia zenye thamani ya Trilioni 5.595 wala Trilioni 360. Jicho la Bunge katika kuisimamia Serikali ni CAG na CAG ameshatoa taarifa yake.

Nimefuatilia taarifa za mazungumzo baina ya Rais wa awamu ya tano, Hayati Dk. John Pombe Magufuli, Tume ya uchunguzi na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ya Juni 17, 2017

Pia nimefuatilia mazungumzo baina ya Rais Dk. Magufuli, Tume ya Rais ya Majadiliano na Afisa Mwendeshaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick Gold, Dk. Willem Jacobs Februari 20, 2019. Aidha nimefuatilia mazungumzo baina ya Rais Magufuli akishuhudia utiaji saini makubaliano ya kuanzisha Kampuni ya Twiga Mineral Corporation ya Januari 24, 2020 Taarifa zote hizi hakuna mahala Mheshimiwa Rais Hayati Dk. John Pombe Joseph Magufuli wala Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan inayo onyesha kuwa waliagiza kufutwa kwa madai ya malimbikizo ya kodi za makinikia kama alivyoliambia Bunge Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba Septemba 23, 2022.

Kama Taifa tunayo mahitaji makubwa ya fedha kugharamia uendeshaji wa Serikali na miradi ya maendeleo na ndio maana kodi na Tozo zinakusanywa kwa walipa kodi wote wakiwemo wananchi wanyonge pamoja na kutafuta mikopo na misaada mbalimbali ndani na nje ya nchi. Uamuzi wa kusamehe kodi ya Matrilioni ya Fedha kwa wahalifu waliokwepa kodi kwa zaidi ya miaka 17 na tena kwa nchi masikini kama Taifa letu inaleta mashaka makubwa sana.

Kwa kuwa hakuna ushahidi wala uthibitisho wowote ambao umewahi kuwasilishwa bungeni na Serikali kuhusu kufutwa kwa madai ya malimbikizo ya kodi za kampuni za madini (Makinikia) Na kwa kuwa taarifa ya Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali inakinzana na maelezo ya Serikali yaliyotolewa bungeni juu ya madai ya malimbikizo ya kodi za makampuni ya madini.

Hivyo basi Bunge liazimie kwamba

(i) Serikali iwasilishe taarifa kamili na ukweli juu ya suala la madai ya malimbikizo ya kodi za madini (Makinikia) ambazo zilikuwa zimeshikiliwa katika Bodi ya Rufani za Kodi (TRAB) na Baraza la Rufani za Kodi (TRAT) ili Bunge liweze kuchukua nafasi yake kabla Mkutano wa 9 Kikao cha 4 cha Bunge kumalizika.

(ii) Iundwe Tume ya Bunge kwenda kubaini ukweli uliofichika katika Sakata la kusamehewa kwa Malimbikizo ya Kodi katika Makampuni ya madini ya North Mara Gold Mine, Pangea Minerals Limited, Bulyanhulu Gold Mine na ABG Exploration.

5 Malimbikizo ya Kodi yasiyo na kesi Mahakamani kiasi cha Tsh Trilioni 7.54

Kwa mujibu wa Ripoti ya CAG ukusanyaji wa mapato ya Serikali umeshuka kwa 0.2% katika mwaka wa 2020/2021 sababu za kushuka kwa mapato haya hazijawekwa bayana.

Taarifa ya CAG inaonyesha kuwa TRA imeshindwa kukusanya malimbilikizo ya kodi yasiyo na kesi mahakamani yanayofikia kiasi cha Tsh Trilioni 7.54 mwaka 2020/21 ambapo malimbikizo hayo yameongezeka kwa asilimia 95 huku uwezo wa TRA kukusanya malimbikizo hayo ikiwa ni asilimia 10.4 tu. Taarifa za TRA za kila mwezi za ukusanyaji wa mapato imekuwa ikijivunia kuvuka malengo ya makusanyo ya kodi bila kutumia mabavu.

Taarifa ya Kamati ya PAC katika ukurasa wa 13 kipengele (b) inasema Malimbikizo haya yanatokana na kutokushughulikiwa ipasavyo kwa madeni ya kodi mathalani mwaka 2020/2021 ambako kulikuwa na ongezeko kubwa la 95% la madeni ya kodi ambalo ni Tsh Trilioni 3.87 na kuyafanya malimbikizo hayo kufikia Tsh Trilioni 7.54.

Taarifa hiyo ya Kamati pia inaeleza kuwa katika ukurasa wa 14 kipengele cha (f) na (g) TRA kumekuwepo na kuchelewa kutolewa mapingamizi ya kodi (Tax objection) yenye thamani ya Tsh Bilioni 102.59, pia kumekuwepo na ucheleweshaji wa usajili mapingamizi ya kodi yenye thamani ya Tsh Bilioni 65. 4

Kitendo cha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kushindwa kukusanya mapato ya Tsh Trilioni 3.87 katika mwaka wa fedha 2020/2021 huku madai haya yakiwa hayana kesi wala pingamizi yoyote mahamakani inaleta mashaka makubwa juu ya utendaji wa Mamlaka hiyo. Inaleta maswali mengi juu ya uwezo, ufuatiliaji na usimamizi wa ukusanyaji wa kodi.

Sababu zinazotolewa hazikubaliki eti TRA ina upungufu wa watumishi wa kukusanya kodi, Mamlaka ya kutoa vibali vya ajira inawezaje kuruhusu upungufu wa watumishi katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ambayo inakusanya mapato kwa ajili ya kulipa mishahara, kugharamia uendeshaji wa Serikali, kulipa Deni la Taifa, kugharamia miradi ya maendeleo iliyoahidiwa kwenye Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, miongozo na maagizo mbalimbali ya viongozi wa kitaifa.

Udhaifu huo umeifanya TRA kukusanya mapato chini ya malengo kwa 13.60% na ukusanyaji wa mapato ya Serikali kushuka kwa 0.2% ikilinganishwa na mapato ya mwaka uliopita wa 2019/2020.

Pia Tanzania ilikuwa nyuma ilipolinganishwa na nchi nyingine za Kenya na Rwanda katika uwiano wa ukusanyaji wa kodi kwa pato la taifa ambapo Tanzania ni 11.40%, Kenya 13.70% na Rwanda 15.90% ya Pato la Taifa katika Mwaka wa Fedha 2020/2021. Kwa kuwa sababu za TRA kushindwa kukusanya mapato ipasavyo hazieleweki hali inayopelekea kuendelea kupoteza mapato ya Serikali kwa kupungua wigo wa kodi na kuwepo kwa mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali,

Na Kwa kuwa upotevu wa mapato unaendelea kila mwaka na unarudisha nyuma jitihada za Serikali kutoa huduma kwa wananchi,

Hivyo basi, Bunge liazimie kwamba Serikali kabla ya kuanza Bunge la Bajeti Mwaka wa Fedha 2023/2024,

(i) Kufanyike tathmini ya mfumo wa ukusanyaji wa kodi nchini (Comprehensive Tax System Review)

(ii) Kufanyike tathmini ya uwezo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kuchukua hatua stahiki.

(iii) Kufanyike tathmini ya kina kubaini mianya yote ya upotevu wa mapato ya Serikali na kuchukua hatua stahiki.

6. Malimbikizo ya kodi yenye kesi Mahakamani kiasi cha Tsh Trilioni 5.19
Mapingamizi ya kesi za kodi katika mwaka wa fedha 2020/2021 yalifikia kiasi cha Tsh Trilioni 5.19 mapato haya yanashikiliwa kwenye mamlaka za rufani za kodi kwa muda mrefu katika Mahakama za Rufaa (CAT), Baraza la Rufani za Kodi (TRAT) na Bodi ya Rufani za Kodi (TRAB) zikisubiri kutolewa maamuzi ili mapato ya Serikali yakusanywe.

Sababu za kuchelewa kutolewa maamuzi ya rufaa za kesi hizi za kodi eti inaelezwa ni pamoja na upungufu wa wataalamu, bajeti ndogo, kukosekana kwa akidi ya wajumbe wa kusikiliza kesi za kodi katika mamlaka za rufani na kuchukua muda mrefu wa mazungumzo nje ya Mahakama.

Kwa kuwa, ucheleweshaji wa mapingamizi haya yanapunguza wigo wa kodi na kuikosesha Serikali mapato,

Na kwa kuwa, sababu zinazotajwa kuchelewesha uamuzi wa mashauri haya hazieleweki na ni uthibitisho kuwa Serikali haina dhamira ya dhati ya kumaliza mashauri hayo na kukusanya kodi stahiki za Serikali.

Hivyo Basi, Bunge liazimie kuwa Serikali ilete maelezo ya kina ya sababu zinazosababisha kuchelewa kuamuliwa kwa mashauri ya mapingamizi ya kikodi katika Bodi ya Rufani za Kodi (TRAB) na Baraza la Rufani za Kodi (TRAT) kabla ya Mkutano 9 kikao cha 4 cha Bunge kumalizika.

7. Utoaji wa mikopo ya 10% ya akina mama, vijana na wenye ulemavu

Katika Taarifa ya LAAC imeeleza kuwepo na changamoto nyingi za utoaji, ufuatiliaji na usimamizi wa mikopo ya 10% inayotolewa na Halmashauri ambapo pia kuna ushahidi kutoka maeneo tunayowakilisha kama ifuatavyo:-

(i) Halmashauri 155 kushindwa kukusanya Tsh Bilioni 47.01 zilizotolewa kwa vikundi kutokana na kukosa udhibiti mzuri wa usimamizi wa mikopo hiyo.

(ii) Kutoa mikopo kwa upendeleo kwa makundi ya watu hususan kwa watu wa mjini na mikopo kutolewa bila elimu ya kutosha kwa wakopaji.

(iii) Kutozingatia uwiano ulioainishwa kisheria wa utoaji wa mikopo ya akina Mama, vijana na wenye ulemavu wa 4:4:2

(iv) Kutoa mikopo bila kujiridhisha na uhalisia wa mipango ya biashara au uhai wa vikundi vinavyokopa

Kwa kuwa, Wastani wa kiasi kikubwa cha fedha cha Tsh Bilioni 75.7 zinazotengwa kila mwaka kwa ajili ya mikopo ya akina mama, vijana na wenye ulemavu (10% ya mapato ya ndani) ni vigumu kusimamiwa na halmashauri zetu na kwamba halmashauri nyingi hazina uwezo wa kitalaamu na kifedha kusimamia utoaji wa mikopo hiyo, Divisheni za Maendeleo ya Jamii zinazohusika na uanzishwaji wa vikundi na utoaji mikopo hazina wataalamu wabobevu katika mambo ya fedha na utoaji wa mikopo

Na kwa kuwa, Kamati za Fedha za Halmashauri zinazohusika na uidhinishaji wa mikopo hiyo zina majukumu mengi na hazina uwezo wa kitaalamu kupitia na kuidhinisha mikopo hiyo hali inayopelekea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi na urejeshaji dhaifu wa mikopo hiyo,

Hivyo Basi, Bunge liazimie kwamba Serikali au Halmashauri ziingie kwenye makubaliano (MOU) na Taasisi za Fedha ambazo zimesambaa kila wilaya mfano Benki ya CRDB na NMB ili kuziachia benki hizo suala la utoaji wa mikopo. Divisheni za Maendeleo ya Jamii zilizopo katika halmashauri zibaki na jukumu la kufanya maandalizi ya awali ya vikundi vilivyoomba kukopeshwa bila kuathiri malengo na dhamira ya Serikali ya mpango wa uanzishaji wa mikopo ya 10% ya akina mama, vijana na wenye ulemavu.

Nawasilisha,

..................................................

Luhaga Joelson Mpina (Mb)

Mbunge wa Jimbo la Kisesa (CCM)
Mpina.jpg
 
1. UTANGULIZI
Awali nianze kwa kukupongeza sana Mheshimiwa Spika, Dk.Tulia Ackson pamoja na Kamati ya Uongozi ya Bunge kwa kutenga muda wa kutosha kujadili taarifa za kamati za ukaguzi za

PAC na LAAC bungeni. Nawapongeza wawakilishi wa wananchi na huu ni uthibitisho tosha kuwa
Mheshimiwa Spika Dk Tulia Ackson Mwansasu wewe ni mzalendo wa kweli.

Nawasilisha,

..................................................

Luhaga Joelson Mpina (Mb)

Mbunge wa Jimbo la Kisesa (CCM)
Mkuu Baraka Wanzala Baraka, kwanza asante kwa bandiko hili, pili nashangaa bandiko full of nondo kama hili kuchangiwa na mchangiaji mmoja tuu na mimi ni wa pili!.
Na tatu kama hutajali unaweza kutushirikisha umeipata wapi hii doc ya Mhe. Mpina ikiwa kwenye format ya ms word doc?. Hii hoja ya ulikoipata hii nondo, ukijisikia unconfortable kutaja source, usijali!, nitakuelewa!, ila jameni JF sio mchezo!.
P
 
Mkuu Baraka Wanzala Baraka, kwanza asante kwa bandiko hili, pili nashangaa bandiko full of nondo kama hili kuchangiwa na mchangiaji mmoja tuu na mimi ni wa pili!.
Na tatu kama hutajali unaweza kutushirikisha umeipata wapi hii doc ya Mhe. Mpina ikiwa kwenye format ya ms word doc?. Hii hoja ya ulikoipata hii nondo, ukijisikia unconfortable kutaja source, usijali!, nitakuelewa!, ila jameni JF sio mchezo!.
P
Duuh. Kweli Pascal Mayalla kwa dunia hii ya teknolojia tulipofikia leo unauliza ameipata wapi doc wakati unajua imewasilishwa bungeni na ipo kwenye mitandao mbambali.

Mimi nilitegemea ungejadili hayo maudhui yaliyomo ya taarifa kuliko kumjadili mleta taarifa... Kuna mambo makubwa sana humo kama taifa tunapaswa kujiuliza maswali mengi
 
Hili bandiko limejaa nondo! Ingekuwa JF ya enzi zile mitandao ingechafuka. Kuna sarakasi zimefanyika zinatisha!
 
Duuh. Kweli Pascal Mayalla kwa dunia hii ya teknolojia tulipofikia leo unauliza ameipata wapi doc wakati unajua imewasilishwa bungeni na ipo kwenye mitandao mbambali.

Mimi nilitegemea ungejadili hayo maudhui yaliyomo ya taarifa kuliko kumjadili mleta taarifa... Kuna mambo makubwa sana humo kama taifa tunapaswa kujiuliza maswali mengi
Jf ya zamani, ukileta nondo humu kama wewe you are not the author, you have to attribute the source!. Na kwa kukusaidia zaidi, lile swali langu limesaidia kitu humu!. Kama ulisoma the sthread ilipowekwa mwanzo was the presesentation version, with doible space, sasa ndio imewekwa the public version with single space!.
Hili sio jambo dogo!.
P
 
Back
Top Bottom