Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,483
- 40,004
Kwa kweli watu wengi wanaoitakia mema nchi yetu walishangazwa na madai hayo na vitendo vya ndugu zetu hao. Hii si mara ya kwanza kwa nchi yetu kufanya zoezi la marekebisho ya Katiba au hata kuandika upya Katiba tangu Uhuru na Muungano. Mara zote hizo iliundwa Tume ya kukusanya maoni ya wananchi ambayo iliundwa na Rais. Ndivyo ilivyokuwa wakati wa Rais wa Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi na Rais wa tatu Mzee Benjamin Mkapa. Mwalimu Julius Nyerere alifanya hivyo mara tatu. Mara ya kwanza mwaka 1963 wakati wa kubadilisha mfumo wa vyama vingi kwenda Chama kimoja, Rais aliunda Tume ya Mheshimiwa Rashid Kawawa, Amon Nsekela. Mara ya pili wakati wa kutengeneza Katiba ya Kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 aliunda Tume ya Mzee Sheikh Thabit Kombo.
Mwaka 1984 Mabadiliko ya Katiba ya 1977 yaliyoweka ukomo wa Urais na kuingiza katika Katiba Haki za Binadamu, yaliyotokana na mchakato uliokuwa ni wa Kichama, ambapo CCM ilikusanya maoni kupitia mtandao wa kichama kuanzia Matawi hadi kufikia Makao Makuu. Wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi wa Awamu ya Pili, kulikuwa na Tume ya Jaji Mkuu Francis Nyalali iliyotuletea mabadiliko ya nane ya Katiba yaliyoruhusu vyama vingi vya siasa. Wakati wa Rais wa Awamu ya Tatu, mzee Benjamin Mkapa kuliundwa Tume ya Jaji Kisanga iliyoleta mabadiliko ya 13 na 14 ya Katiba ya nchi.
Hivyo la ajabu lipi kwa Rais wa sasa kuunda Tume ya Katiba? Amepungukiwa nini Kikatiba na Kisheria ambacho Marais wenzake walikuwa nacho katika madaraka yao? Hakipo hata kimoja! Madaraka waliyokuwa nayo Marais waliomtangulia ndiyo aliyonayo Rais wa sasa. Hajapungukiwa chochote kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi. Kwa kweli hakuna hoja yoyote ya msingi ya kumuengua Rais katika mchakato wa kutengeneza Katiba ya nchi. Haipo hoja ya Kikatiba wala ya Kisheria. Hivi Rais asipounda Tume, nani aiunde Tume hiyo? Na huyo atakayeunda atapatikanaje?
Kwa haraka inawezekana kudhaniwa kuwa Rais Kikwete ameweza kutetea kwanini yeye ndiye aanzishe na kusimamia mchakato wa Katiba Mpya. Kwamba alitumia madaraka yale yale ambayo yalitumiwa na viongozi wengine wa nyuma- japo mara zote hizo haikuwa kuhusu Katiba Mpya bali kubadilisha katiba iliyokuwepo na kuiboresha na pale ambapo kulikuwa na kwenda kwenye Katiba ya kudumu kulifanyika katika mazingira ya chama kimoja na hivyo kuondoa hoja ya ushiriki wa vyama vingine na hata kuhoji. Rais ndiye alikuwa mkuu wa chama hicho kimoja na ndiye mkuu wa serikali na hivyo inaeleweka kwanini ilikuwa hivyo. Hili halihalalishi hali iyo kurudiwa sasa katika uelewa wetu wa demokrasia ya vyama vingi na ukuu wa wananchi (siyo chama kama ilivyokuwa zamani).
Hatujawahi kuwepo hapa tulipo sasa. Njia hizo za zamani zilizotumika ndizo zilipotufikisha hapa na tunahitaji ubunifu wa hali ya juu. Kurudia mambo yale yale kwa namna ile ile kuna jina lake lakini kwa vile tunaishi katika zama mpya tungetarajia ubunifu zaidi.
Katiba ya sasa haimpi Rais kuanzisha mchakato wa kuandika Katiba Mpya ana uwezo akitaka wa kusimamia kwa kupitia chama chake mchakato wa kufanya mabadiliko ya katiba ya sasa. Lakini kwa vile anachotaka ni katiba Mpya napendekeza kuwa Katiba ya sasa haina madaraka hayo kwa Rais au kwa mtu mwingine yeyote na kiukali kabisa tunaweza kugeuza na kudai zoezi zima haliwezi kufanya na wale walioapa kulinda Katiba ya sasa! Hakuna kipengele chochote kinachohusiana na kuandika katiba mpya katika Katiba yetu ya sasa. Sasa kama hakuna imekuwaje Rais aamini kuwa ana madaraka ya kuanzisha hata kuitisha Bunge la Katiba?
Kujibu swali lake la mwisho ni kuwa:
a. Kabla ya kuundwa kwa tume hiyo ya kukusanya maoni ilitakiwa kwanza yafanyike mabadiliko katika Katiba ya sasa ambayo yangeweza utaratibu wa kuandika Upya Katiba ya nchi. Katiba ya sasa inaruhusu kufanyiwa mabadiliko tu (ammendments) lakini hairuhusu kuwepo kwa mchakato wa kuandika Katiba Mpya.
b. Mabadiliko hayo ya Katiba ya kuweka mchakato ndio yangejadili nani na kwa vipi teuzi za tume ya kuandika Katiba unatakiwa kufanyika. Haiwezekani Rais aliyeko madarakani anajiamulia tu kuandika Katiba Upya yeye mwenyewe halafu wengine wafuate; Tukumbuke tamko la kuandika Katiba Mpya lilitolewa kwenye salamu za mwaka mpya! Halikutolewa Bungeni na wala hakukuwa na utaratibu wa kuonesha kuwa umejali wananchi. Ulikuwa ni uamuzi binafsi wa Kikwete. Tukumbuke kuwa kwenye hotuba ile hakusema "amedhamiria" la hasha alisema "ameamua".
c. Ni kutoka hapo sasa ndio sheria ya kusimamia mchakato wa kuelekea Katiba Mpya ungeweka. Ina maana ya kwamba suala la Kuandika Katiba Mpya lingewekwa ndani ya Katiba ya sasa na kuangaliwa kama tunavyoangalia yale mambo 8 ambayo yanahitaji ridhaa ya pande mbili za Muungano (theluthi mbili ya wajumbe). Lakini kwa hivi ilivyo Kikwete na Shein wataamua wao wenyewe. Sasa hiyo sheria ndio ingezingatia maoni ya watu wengine.
Utaona basi kuwa kosa la kwanza limefanyika kwa kutozingatia Katiba ya sasa kwanza - haina mchakato wa kuandika Katiba Mpya - na hivyo kufanya hoja ya Katiba Mpya haiwezi kutolewa na wale walioapa kuilinda ya sasa na kama inatolewa walitakiwa kwanza kufanyia mabadiliko hii Katiba ili wajipe uwezo wa kuzungumzia "katiba mpya".
Kwa vile suala la Katiba Mpya basi ni la nje ya watawala wetu wa sasa ni wazi kuwa toka mwanzo ushiriki wao ulitakiwa uwepo na siyo mtindo huu wa kuburuzana na kuwapa wananchi taarifa zisizo za kweli kwa ajili ya faida za kisiasa (political expediency). Badala ya kusahihisha makosa wameamua kuendelea katika kukosea. Wananchi wafanye nini?
a. Watahamasishana wasishiriki kwenye hiyo tume na kuwaachia wana CCM wakaambizane wanayotaka kuyasikia. Yaani A total boycott of the exercise. Hakuna namna ya kuwalazimisha wananchi washiriki. Na kama tulivyoona leo hata wana CCM wenyewe hawako katika hali ya kuruka ruka sana na kufurahia mchakato wenyewe.
b. Watasubiri ije siku ya kupiga kura ya maoni watahamasishana kwenda kuungusha kwenye sanduku la kura kuwaonesha watawala kuwa wananchi ndio wako supreme zaidi ya Rais na Bunge. Kwa vile wamekubali kuweka kiwango cha chini ya asilimia 50 kupitisha ni kiwango kidogo sana kukifikia! kwani upinzani unahitaji kuhamasisha asilimia 51 tu!
Sioni dalili yoyote ya watawala kukaa pamoja na kama tuliyoyashuhudia wiki hii ni mfano basi Kikwete hayuko tayari hata kukubali hoja za upande wa pili - ila upande wake ndio anataka ukubaliwe bila kuhojiwa au kupingwa. Na uamuzi wa kuweka adhabu kwa watu watakopinga mchakato huu umethibitisha pasipo shaka kuwa kwa njia ya kawaida haiwezekni kushinda isipokuwa kwa shurti, vitisho na vifungo.
Utabiri wangu: Mswada huu utarudishwa mapema tena Bungeni ili ufanyiwe marekebisho kama walivyofanya kwenye msaada ya gharama za uchaguzi ambao wengine tuliupinga na kuonesha makosa mapema wakang'ang'ania na kusaini kwa mbwembwe lakini miezi mitatu tu baadaye wakaurudisha na bado wanahitaji kuufanyia marekebisho. Mswada huu ukiwa sheria hautekelezeki, haukubaliki, na watawalazimisha watu kuupuza. Tunaposema katiba ni 'mama' hatusemi tu hivi hivi. Sasa mama habambikiziwi! Vingenevyo wapo Watanzania ambao wataiona katiba ijayo kuwa ni 'katiba ya kambo'! Hawataipenda, hawataizingatia na watajaribu kweli kweli kuibadilisha. Kama Rais wa sasa ameweza kufanya hivi bila kuulizwa na mtu guess what akija Rais mwingine?
Hadi wakubali kusikiliza upande wa pili na kufuata ile kanuni ya kwanza - KATIBA LAZIMA ITOKE KWA WANANCHI WENYEWE. Kuanzia mfumo wa kuwashirikisha wananchi, nani anasimamia na inafikiwa vipi ni lazima iwe inasimama kwenye madaraka ya wananchi kutawala.
Last edited by a moderator: