Kuelekea Dunia ya Kidijitali: Sekondari ya Zanaki yaanza kutekeleza mradi wa kujenga Jamii ya Kidijitali Tanzania

nivoj.sued

JF-Expert Member
Jul 14, 2009
221
190
1693654213521.png

Mkuu wa shule ya Zanaki ( mwenye hijabu katikati) akipokea vifaa vya tehama

Shule kongwe nchini Tanzania, Sekondari ya Zanaki, iliyoko jijini Dar es Salaam, hatimaye imefanikiwa kujiunga katika utekelezaji wa mradi wa Tanzania ya Kidijitali baada ya kupata vifaa vya tehama kwa ajili ya kufundisha masomo ya kompyuta, baada ya miaka 85 tangu ilipozaliwa mwaka 1939.

Vifaa hivyo vilivyokabidhiwa shuleni hapo kwa Mkuu wa Shule hiyo, tarahe 01 Septemba 2023, vimetolewa na taasisi mbili zilizoshirikiana.

Taasisi hizo ni asasi ya Tehama kwa Wote iliyosajiliwa nchini Tanzania, na asasi ya kigeni iitwayo Trade Desk Inc, ya Marekani.

Asasi ya Tehama kwa Wote inafadhiliwa na Kampuni ya Power Computers Tanzania Limited (PCTL).

Wafadhili hawa wameipatia shule ya Zanaki vinu 30 vya kompyuta, kiibodi 30 za kompyuta, vipanya 30 vya kompyuta, monita 30 za kompyuta, betri 3 za kutunza umeme wa dharula wa kompyuta, printa moja, skana moja, projekta moja, na seva tatu.

Aidha, wafadhili hawa wamebeba gharama za kusimika vifaa hivi kwenye chumba ambacho ni maabara ya kompyuta, katika shule ya Zanaki.

Akiongea wakati wa hafla ya kupokea vifaa hivi, Mkuu wa Shule ya Zanaki, Delvine Koka, aliwashukuru wafadhili kwa hisani hiyo.

Ndugu Mgeni rasmi, vifaa hivi vitakuwa chachu kubwa katika kurahisisha ufundishaji wa somo la kompyuta na utekelezaji wa shughuli zingine zinazohitaji matumizi ya vifaa vya Tehama. Tunasema asanteni sana kwa taasisi za The Trade Desk na Tehama kwa Wote kwa msaada huu mkubwa wa vifaa,” alisema Koka.

Kwa mujibu wa Koka, shule ya Zanaki inao wanafunzi wa kike 1,130 kuanzia kidato cha kwanza hadi kidati cha sita, na shule inao mpango mkakati wa kuhakikisha wanafunzi wote wanasoma somo la kompyuta japo kwa sasa wanafunzi wanasoma somo hili ni 132 pekee.

Hivyo, kupatikana kwa kompyuta 30 kunamaanisha kwamba kila kompyuta moja itatumiwa na wanafunzi watano wanaosoma kompyuta kwa sasa.

Kulingana na Ripoti inayoitwa Basic Education Statistics in Tanzania (BEST) ya mwaka 2021, katika shule za sekondari kila kompyuta moja inatumiwa na wanafunzi 85.

Makabidhiano ya vifaa hivyo vta tehama yalishuhudiwa na Pilly Ngarambe, aliyekuwa Mgeni Rasmi, kwa niaba ya Ofisa Elimu wa Jiji la Dar es Salaam.

Ngarambe aliwapongeza wafadhili kwa juhudi zao za kuchangia kwa hiari kwenye utekelezaji wa mipango ya serikali ya awamu ya sita, chini ya Samia Suluhu Hassan.

Jambo hili ni kubwa kwa sababu linaunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza matumizi ya Tehama katika shule zote,” alisisitiza Ngarambe.

Naye Katibu wa taasisi ya Tehama kwa Wote, Aveline Malamsha, alisema kwamba uamuzi wao wa kutoa vifaa hivi ni sehemu ya utekelezaji wa sera yao ya kutekeleza majukumu ya kitaasisis kwa jamii pana, na watendelea kufanya hivyo nchi nzima kadiri hali ya kifedha itakavyoruhusu.

"Pamoja na utoaji wa vifaa hivi hapa Zanaki, tayari tumefanya hivyo katika shule zingine tatu. Tutaendelea kufanya hivyo katika shule zote za Tanzania hatua kwa hatua. Tunatekeleza mradi huu kimkakati kwa kuandaa walimu ili baadaye walimu wawaandae wanafunzi wetu. Mpaka sasa tumefundisha walimu 200 bure mkoani Dar es Salaam," alieleza Malamsha.

Naye Mtendaji Mkuu wa kampuni ya PCTL inayofadhili asasi ya Tehama kwa Wote, Shakil Dharamsi, akiongea katika hafla hiyo aliongelea umuhimu wa tehama katika zama hizi.

Alitumia uzoefu wake hapa Tanzania kusisiyiza kwamba, bado kuna upungufu mkubwa wa vifaa vya tehama kwenye shule nyingi nchini Tanzania. Hivyo, Dharamsi akaahidi kuendelea kusaidia kila uwezo utakaporuhusu. Pia alitoa wito kwa Wadau baki kushiriki katika mradi huu muhimu kwa Taifa.

"Watoto wangu wanasoma pale Shule ya Agha Khan Mzizima. Wakifika nyumbani wanao uwezo wa kuwasha na kucheza na kompyuta. Lakini, pale ofisini kwamba wanakuja vijana wengi kutafuta kazi hawajua hata kuwasha kompyuta. Katika zama hizi hii ni changamoto inayopaswa kutunyima usingizi," alieleza kwa msisitizo Dharamsi.

Mradi wa kupunguza pengo la kidijitali kati ya makundi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kupunguza pengo hilo kati ya wanawake na wanaume, ni moja ya miradi iliyotajwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, unaotekelezwa tangu 2021 hadi 2025, chini ya serikali wa ya awamu ya sita, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, wa Tanzania.

Lengo la mradi huu ni kusaidia katika ujenzi wa Tanzania mpya yenye kusifika kwa kuwa na serikali ya kidijitali, uchumi wa kidijitali na jamii ya kidijitali.

Mkakati wa kujenga serikali ya kidijitali unataka kuhakikisha kuwa serikali inawahudumia wadau wake katika sekta zote kwa kutumia majukwaa ya kidijitali pekee.

Mkakati wa uchumi wa kidijitali ni kuhakikisha kwamba wadau wote wa kiuchumi katika sekta binafsi wanatoa huduma zao kwa kutumia tehama.

Na Mkakati wa jamii ya kidijitali ni kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anayo maarifa na ujuzi wa kumwezesha kutafuta na kupokea huduma kwa kutumia tehama.

Jitihada hizi za serikali zinatokana na ukweli kwamba, historia ya mabadiliko ya kiteknolojia inaserereka kwa kasi ambayo inamweka binadamu wa leo katikati ya fursa na changamoto, ambapo changamoto hizo zintishia kuimega jamii kati ta makundi mawili yanayotenganishwa na pengo la weledi na ustadi wa kitekinolojia.

Jamii ya binadamu umekuwepo hapa duniani kwa wastani wa miaka milioni moja. Katika kipindi hiki, jamii imepitia katika mabadiliko makuu ya kitekinolojia manne.

Mabadiliko ya kwanza ya tekinolojia yaliiwezesha jamii ya wawindaji kuingia katika maisha ya jamii yanayoongozwa na tekinolojia ya ufugaji katika miaka ya 1500KK.

Mabadiliko ya pili ya tekinolojia yakaiwezesha jamii ya wafugaji kuingia katika maisha ya yanayoongozwa na tekinolojia kilimo katika miaka ya 800KK.

Kisha, mabadiliko ya tatu ya tekinolojia yaliiwezesha jamii ya wakulima kuingia katika maisha yanayoongozwa na tekinolojia ya viwanda katika miaka ya 1700BK.

Katika kipindi cha miaka 300 ambapo wanadamu wameishi chini ya zama za viwanda kumetokea mabadiliko madogo manne ndani ya tekinolojia hii ya viwanda.

Katika miaka ya 1760, jamii za watu zililianza kuishi katika zama za kwanza za mapinduzi ya viwanda, zilizosifika kwa mitambo ya uzalishaji iliyotumia nishati ya makaa ya mawe na mvuke wa maji.

Kwenye miaka ya 1900, jamii za watu zililianza kuishi katika zama za pili za mapinduzi ya viwanda, zilizosifika kwa mitambo ya uzalishaji iliyotumia nishati ya petroli na mashine za umeme.

Halafu, katika miaka ya 1960, jamii za watu zililianza kuishi katika zama za tatu za mapinduzi ya viwanda, zilizosifika kwa mitambo ya uzalishaji iliyotumia mifumo ya elektroniki, kompyuta na mawasiliano ya simu, kila mfumo ukiwa umesimama kivyake.

Nchini Tanzania, kompyuta ya kwanza, iliyoitwa ICT 1500, ilisimikwa katika Wizara ya Fedha mwaka 1965. Kufukia mwaka 1974 kulikuwa na kompyuta saba nchini kote, Wizara ya Fedha ikiwa inayumia kompyuta iliyoitwa ICL 1900.

Na hivi karibuni, katika miaka ya 2010, jamii za watu zililianza kuishi katika zama za nne za mapinduzi ya viwanda, zinazosifika kwa mitambo ya uzalishaji iliyotumia mifumo ya elektroniki, kompyuta na mawasiliano ya simu, ukiwa imefungamanishwa pamoja na programu za kompyuta zenye akili iliyobuniwa na binadamu, yaani "artificial intelligence."

Hasa, kwa mara ya kwanza, maneno "zama za nne za mapinduzi ya viwanda," yalitumika rasmi mwaka 2016 kwa mara ya kwanza, kupitia kitabu kitwacho "The Fourth Industrial Revolution," kilichoandikwa na Klaus Schwab, Rais wa Jukwaa la Uchumi Duniani wakari huo. Katika kitabu hiki, Schwab (2016:7) alisema kwamba,

“The Fourth Industrial Revolution is characterised by unprecedented and simultaneous advances in artificial intelligence (AI), robotics, the internet of things, autonomous vehicles, 3D printing, nan otechnology, biotechnology, materials science, energy storage, quantum computing and others [which] are redefining industries, blurring traditional boundaries, and creating new opportunities.”

Ni kwa kuzingatia mtiririko huu wa kihistoria, na changamoto zake kwa Taifa changa kama Tanzania, mwaka 2019, Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, hayati John Magufuli, alianzisha Wizara Kamili ya TEHAMA ili kuchochea kasi ya kudijitalisha Tanzania. Na sasa, Rais wa Serikali ya Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan, anasema "Kazi Iendelee."

Linabaki ni suala la kitafii ili kubaini "kazi inaendelea" kwa kasi kiasi gani na kasi mchepuko kiasi gani. Lakini, jambo moja lililo wazi ni kwamba wadau wa sekta binafsi, kama vile PCTL, The Trade Desk na Kompyuta kwa Wote, wako mbioni kusukuma gurudumu la Tanzania ya Kidijitali. Kazi Iendelee.
 
Back
Top Bottom