Kati ya Sitta na CHADEMA mnafiki ni nani?

sulphadoxine

JF-Expert Member
Nov 1, 2010
2,257
645

MNAFIKI ni mtu mwongo mwenye matendo kinyume na maneno yake; mtu anayefanya jambo tofauti na anavyoahidi; mzandiki.
Akilihutubia Bunge hivi karibuni, Mbunge wa Urambo Mashariki, pia Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, alisema wabunge wa CHADEMA ni “wanafiki kwa kukataa posho wakati baadhi yao wamekuwa wakipokea kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita. Warejeshe posho hizo ndiyo wananchi watawaelewa … na wataendelea kuwa wapinzani.”
Inaelekea hoja ya wabunge wa CHADEMA kutaka posho za wabunge ziondolewe ili zisaidie katika maendeleo ya wananchi, inawakera mno wenzao wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao ndio wengi Bungeni. Mara zote CHADEMA kinapopeleka hoja ya kuwatetea wananchi wanyonge, wabunge wa CCM hutumia wingi wao kuzomea na kupinga. Hii inadhihirisha jinsi wanavyojali masilahi yao badala ya wananchi.
Tangu mwaka 1995 CHADEMA kimekuwa mstari wa mbele kufichua ubadhirifu na ufisadi unaofanywa na watumishi wa serikali ya CCM kwa kutaja majina yao na fedha walizokwapua. Mara zote CCM kimekuwa kikikanusha huku watuhumiwa wakitishia kushitaki wasipoombwa radhi kwa kuchafuliwa majina.
Baada ya mambo kuwa bayana, CCM ileile iliyokuwa ikikataa uwepo wa mafisadi, kupitia wabunge wake, kikakubali iundwe tume ya Bunge kuchunguza mkataba wa Richmond. Matokeo yake, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa akajiuzulu baada ya kuhusishwa na mkataba unaoiumiza nchi mpaka leo. Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na Waziri wa Maliasili na Utalii, Ibrahim Msabaha nao wakajiuzulu nyadhifa zao.
Baadhi ya viongozi waliotajwa katika ufisadi wamefunguliwa mashitaka mahakamani; wachache wamehukumiwa, baadhi kesi zao zinaendelea na wengi wangali huru. Ufisadi uliofichuliwa na CHADEMA ni ukwapuzi wa fedha za Kagoda, Meremeta, Green Gold, Tangold, EPA, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na ununuzi wa Rada iliyomlazimu Andrew Chenge aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa serikali ajiuzulu.
Hali ilivyozidi kuwa mbaya kwa serikali ya CCM, rais Kikwete akatangaza chama ‘kujivua gamba’ akiwa na maana ya chama chake kujisafisha. Kujivua magamba maana yake ni kukubali ukweli kuwa ni wachafu. Halmashauri Kuu ya CCM ikatoa siku 90 kwa wanaojihisi kuhusika na kashfa wanazotuhumiwa, wajivue magamba wenyewe vinginevyo baada ya muda huo kwisha, wapewe barua za kuwapambua nyadhifa zao katika chama.
Watu hao ambao baadaye waliitwa ‘mapacha watatu’, walipewa muda wa kuanzia Aprili 20 mpaka Julai 20 wawe wamejiondoa wenyewe. Tarehe 13 Julai, siku saba kabla ya muda waliopewa kufikia kikomo, Rostam Abdulrasul Aziz, mmoja wa ‘mapacha’ hao na ambaye pia alikuwa mbunge wa Igunga, akabwaga manyanga. Huyu anatuhumiwa kuingiza mitambo ya Richmond kwa mkataba wenye shaka na ambao umeiweka nchi kizani mpaka sasa.
Kabla ya tukio hilo, Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa wa CCM, Nape Nnauye akifuatana na Katibu Mkuu wa chama hicho na wajumbe wengine wazito wamekuwa wakipita maeneo mbalimbali ya nchi kueleza jinsi kashfa ya ufisadi inavyokitafuna chama chao.
Nape amekuwa akisema kuwa lazima CCM iwabaini na kuwaondoa waovu wote ndani ya chama na serikali kwa sababu “watendaji wa serikali ni wauza duka linalomilikiwa na CCM.” Waziri Sitta naye anasema hawawezi kuinyamazia vita dhidi ya ufisadi mpaka watakapohakikisha watuhumiwa wote wanajitoa ndani ya chama hicho.
Kisichoeleweka ni kwamba CCM na serikali yake mwanzoni ilipinga kwa nguvu zote tuhuma za CHADEMA lakini sasa inakubali kula matapishi yake! Kumbe basi CCM kinapaswa kukishukuru CHADEMA kwa kuwazibua masikio na kuwatoa viongozi wake tongotongo zilizowafanya wasione mbele.
Mwanzoni nilifafanua maana ya ‘mnafiki’ kuwa ni mwongo; mtu anayefanya jambo kinyume na anavyoahidi; mzandiki. Samwel Sitta, Harrison Mwakyembe, Nape Nnauye, Victor Mwambalaswa, Daniel Porokwa, Fred Mpendazoe na baadaye Paul Makonda wanatajwa kwenye kitabu cha “Tutashinda” alichoandika Fred Mpendazoe kuwa waanzilishi wa Chama Cha Jamii (rejea uk. 92).
Mpendazoe, Sitta, Mwakyembe na Nnauye walikutana mara kwa mara kwenye vinywaji pale Mlimani City jijini Dar es Salaam wakiepuka kutiliwa shaka na maofisa wa Usalama wa Taifa.
Kwa kuwa Nape Nnauye alikuwa katika ofisi ndogo ya Makao Makuu ya CCM pale Lumumba, alisaidia kuiba siri za mipango na vikao vya CCM zikiwamo zile zilizohusu kuwafukuza waliohisiwa kuwamo kwenye mpango wa kuanzisha chama kipya cha siasa (rejea uk. 93).
Wakati Sitta na Mwakyembe walikuwa wanawasiliana na wafadhili ili kupata fedha za kugharimia uanzishwaji wa chama, Nape alifuatilia kwa siri taratibu za utawala uliowekwa, kwa niaba ya wenzake. Mwakyembe alisaidia sana kuandaa nyaraka zote za kisheria zilizokuwa zikihitajika kwa ajili ya CCJ (rejea uk. 94).
Hapa ni dhahiri kuwa Samuel Sitta, Harrison Mwakyembe na Nape Nnauye walikuwa ndumilakuwili kwa maana ya mguu mmoja ndani (CCM) na mwingine ukiwa n-nje (CCJ). Kati ya watu hawa na wabunge wa CHADEMA, ni nani wanafiki?
Unafiki wao unathibitishwa na Mpendazoe anaposema: “Watu saba tulihusika kuasisi CCJ, lakini baadhi walitusaliti mapema na tayari wamezawadiwa vyeo na serikali ya chama kile kile ambacho sasa wanalumbana ndani na n-nje ya vikao.”
Katika kitabu chake Mpendazoe anasema: “Sitta, Mwakyembe, Nape na Porokwa walinisaliti, hawakujiunga tena na CCJ kama tulivyokuwa tumekubaliana. Kila mmoja alibadili mawazo dakika za mwisho baada ya kupewa na kuahidiwa vyeo ndani ya CCM.” (rejea uk. 103).
Fred Mpendazoe alijiondoa CCM na kuacha ubunge miezi saba kabla ya kumaliza kipindi chake bungeni. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alisema: “Nimeishi kwa matumaini kwa muda mrefu, nikitegemea siku moja mambo yatabadilika ndani ya CCM. Mpaka leo sioni dalili. Ni heri niheshimu dhamira yangu kama Mwalimu Nyerere alivyotuasa kwamba CCM si mama yangu. “Nasononeka CCM imegeuka gulio la kila mtafuta cheo na utajiri haramu. CCM imegeuka kimbilio la kila mwenye dhamira ya ulanguzi. CCM imepoteza maadili ya uongozi na imekuwa ngome ya mafisadi wanaoutafuna utajiri wa nchi yetu.”
Bila shaka Sitta na kundi lake wanajua kwa undani sasa maana ya unafiki ni nini na wanafiki ni kina nani. Kama walikuwa waanzilishi kindakindaki wa Chama Cha Jamii (CCJ) huku wakivaa magwanda ya CCM na baadaye kumwacha mwenzao solemba baada ya kuahidiwa na kupewa vyeo ni wasaliti wasiofaa kuaminiwa hata na huko CCM kawenyewe!


 
Back
Top Bottom