Kudo
JF-Expert Member
- Nov 2, 2017
- 1,809
- 6,081
RIWAYA; KAMANDA WA ZAMU.
NA; BAHATI K MWAMBA.
WHATSAPP; 0658564341.
1.
Alikuwa akitetemeka mwili na roho, jasho lilimmwagika hadi kwenye ncha za vidole vyake vya miguu na mikono, miwani aliyokuwa ameivaa ni kama haikuwa ikimsaidia kwa lolote kwa sababu hakuwa akiona mbali zaidi ya kuliona zulia lenye rangi nyekundu alilokuwa ametandika juu ya sakafu sebuleni kwake. Uvutaji wake wa hewa ulikuwa umebadilika kwa kiasi kikubwa na alikuwa akiivuta harakaharaka na kwa sauti kubwa kiasi kwamba mtu yeyote angelikuwa nje ya mlango wa nyumba yake angelisikia, kwa sababu ya kuvuta kiasi kikubwa cha hewa kuliko uwezo wa mapafu yake, kifua kilijaa na alianza kukohoa mfululizo hadi misuli ya kichwa ikamtutumka na jicho kuwa jekundu mithili ya pilipili hoho iliyovunwa. Kukohoa huko kilimfanya ainue shingo yake kwa mara ya kwanza tangu alipotembelewa na mgeni wa ajabu, mgeni ambae wakati huo alikuwa mbali na hapo alipokuwa. Macho yake yaliangukia pale alipokuwa amekaa mgeni ambae alimfanya akose amani kwa zaidi ya nusu saa nzima, aliuona mfuko uliokunjwa vema ukiwa umetulia palepale alipokuwa amekaa mgeni wake aliyeingia ndani kwake kwa namna ya ajabu ambayo hakuwahi kuitarajia kama itatokea kwenye maisha yake. Aliinuka huku miguu yake ikiwa haina nguvu kabisa na alikuwa akitetemeka, akaufikia mlango wake na kuufunga kwa funguo kisha akazitupa kwenye sofa na kurejea kukitazama kitasa cha mlango wake, alitikisa kichwa kwa kusikitika ni kama hakuwa anaamini kitu kilichokuwa kimetokea muda mfupi uliopita. Akainua macho yake na kutazama ukutani, akaiona saa ambayo mishale yake ilisoma majira ya saa saba na nusu usiku, muda wa wanga kama wasemavyo waswahili na kweli ulikuwa ni muda wa wanga na yeye ni mmoja wa watu waliowangiwa na kiumbe halisi ambae hakuhitaji mazingaombwe kuonekana. Utata kwake namna kiumbe yule alivyoweza kuingia ndani kwake ikiwa alifunga milango yote, kuanzia mageti mawili ya nje na milango miwili, wa kuingilia sebuleni na ule wa kuingia kwenye chumba alichokuwa akilala. Alikaa kwenye sofa huku akizishusha pumzi zake kwa nguvu na ahueni ya kuona ni angalau amebaki peke yake ndani ya nyumba yake aliyoanza kuiogopa. Akili yake ilianza kuchanganua mambo kwa usahihi kidogo baada ya hofu kuanza kutoweka, akakumbuka kuitafuta simu yake na mikono yake ilianza kujipapasa na alijikuta akiangusha tabasamu la chuki baada ya kugundua alikuwa amevaa boksa na hakuwa na nguo nyingine yoyote mwilini mwake, akainuka kivivu na kuelekea chumbani kwake, akaikuta simu ipo kitandani kando ya mto aliokuwa ameegesha kichwa chake wakati alipoenda kulala. Akaichukua na kuanza kuzitafuta namba za simu za watu kadhaa aliiona wanastahili kujua kilichomkuta na ikiwezekana washauriane jambo la kufanya. Majina mengi aliyapita ijapokuwa yote yalikuwa na umuhimu mkubwa kwake, lakini jina moja likapata hadhi ya kuwa nambari moja kupigiwa na lilikuwa ni jina la aliyewahi kuwa bosi wake kwenye benki ambayo alikuwa akiifanyia kazi hadi wakati huo wakati bosi wake huyo akiwa anafanya kazi tawi jingine la benki hiyohiyo aliyokuwa akiifanyia kazi.
“Hujui ni muda wa kutafuta watoto we kijana! Au hujui mi ni mke wa mtu na huu ni wasaa sahihi wa mume kunimiliki?” Sauti ya mwanamke wa makamo ilifoka kimasihara huku mwisho ikimalizia kwa cheko la usichukulie siriuzi mpenzi..
“Kabina!” Jamaa aliita kwa sauti ambayo haikuonekana kulainishwa na utani wa mwanamke aliyetoka katikati ya usingizi mzito. Upande wa pili ulikaa kimya kwa sekunde zipatazo thelathini hivi kabla ya kusikika tena..
“Miaka zaidi ya sita sijawahi kusikia ukiniita kwa jina langu... Kuna tatizo?” Kabina aliuliza akiwa mnyonge wa sauti, hakuwa ametarajia kuitwa hivyo na mwanaume ambae alikuwa ni tulizo la nafsi yake, mwanaume aliyejua kuusindikiza utu uzima wake akiwa mjane wa watoto wawili waliozodiwa na mwanaume wake kwa umri wa miaka sita pekee, kiufupi alikuwa anapapatuliwa na kijana mwenye rika la wanawe wa kuzaa, lakini angeliona vipi ajabu ikiwa moyo hauna soni? Moyo waweza penda pasipofikiriwa seuze kwa kijana barobaro mwenye sifa zote za kuwa mume wa mtu? Mshangaeni lakini mwenzenu hujihisi fahari akiwekwa kwenye kona ya uwanja usio na aibu, uwanja wa fujo za kidunia, kwake ilikuwa ni fahari kupelekwa puta, iwe mashariki ama magharibi ilimradi nafsi yake itasuuzika na mwili utaondolewa uchovu wote na kuachwa salama na barobaro wake.
“Tatizo lipo!” Jamaa alisema kwa sauti ileile isiyotetereshwa na lawama za mpenzi wake, mpenzi ambae alimfaa kwa kila hali; alimtoa mtaani alipokuwa akihangaikia ajira na kumwajiri kwenye benki kubwa aliyokuwa akiisimamia kama meneja, akamtoa kuishi kwenye mitaa yenye waswahili wengi na kumpangishia kwenye mitaa ya watu wastaarabu, ambao waswahili waliwaita washua. Alimtoa kwenye usafiri wa daladala na bodaboda na kumnunulia gari zuri la kutembelea lenye hadhi ya ujana wake. Joseph Mkweche aliamua kuyalipa yote aliyoyendewa na mwanamama huyo kwa suluba ya sita kwa sita, alihakikisha haishiwi mbinu za kumchakaza mwanamama huyo ambae alinogewa haswaa na ufundi wake na kila akifikishwa mlimani iwe kwa kutafunwa au kulambwa kama koni, alihakikisha anatoa zawadi nzuri zaidi ili asije kuzikosa raha hizo na zikahamia kwa mwanamke mwingine.
“Tatizo gani?” Kabina aliuliza kwa sauti yake halisi, sauti ambayo ni wafanyakazi wake pekee huwa wanaelewa ina maana gani wakiisikia, sauti isiyo na chembe ya mzaha.
“Fisi mwekundu!” Joseph alisema huku akimeza mate, lakini hakupewa nafasi ya kuzungumza neno la ziada.
“Usizunguke sana.. sema tatizo!” Kabina Mkwepu alifoka kwa sauti kubwa, Joseph aliisikia vema na alitambua mwenzake alikuwa kwenye mchecheto mkubwa wa kutaka kujua tatizo.
“Nimekwambia ni Fisi mwekundu. Tatizo ni Fisi mwekundu.” Joseph alisisitiza.
“Una maanisha nini unaposema Fisi mwekundu?” Kabina aliuliza akiwa haelewi sawasawa kilichomaanishwa.
“Usitake kunambia jambo la muhimu namna ile ulishalisahau kirahisi hivyo, kuwa makini kidogo kwenye kumbukumbu zako.” Joseph alimwakia.
“Fisi...mmmh Fisi, Fisi.. oh my God! Unamaanisha Mbitiyaza?” Kabina aliuliza kwa wahka huku sauti ya godoro ikisikika kumaanisha alikuwa anashuka kitandani.
“Kumbe hujazeeka, ni huyohuyo Mbitiyaza kwa kisukuma na ulinitafsilia mwenyewe kuwa ni Fisi mwekundu kwa kiswahili.”
“Imekuwaje tena?” Kabina aliuliza huku mapigo yake ya moyo yakianza kuongeza kasi ya usukumaji damu, kwake hilo jina lilimaanisha matatizo na popote likitajwa yeye hukosa amani kabisa.
“Alikuwa hapa kwangu dakika kumi zilizopita.” Joseph alisema.
“Kwako? Aliwezaje kufika hapo? Una uhakika na unachokisema?” Kabina aliuliza akiwa haamini anachoambiwa.
“Unanibishia au huniamini? Unahisi naweza kuweka utani kwa kulitaja jina kama hilo? Usinikosee tafadhali...” Joseph alitupa tuhuma ili maelezo yake yaaminike.
“Labda nikwambie kitu ambacho sikuwahi kukushirikisha, Shija Mbitiyaza Lupandagila Masalu alishakufa na alizikwa kwenye makaburi ya magereza akiwa na pingu mikononi, labda ulikuwa unamuota na ukaamua kuniharibia usingizi wangu.” Kabina alijaribu kumwelewesha.
“Sijawahi kuota nabebwa na mikono yenye joto kutoka kitandani kwangu hadi sebuleni, sijawahi kuota ndoto na nikaamka nikakuta nilichokiota kipo hadi sasa nakitazama. Ukweli mchungu, kama mlidhani Fisi mwekundu kafa mtakuwa mnakosea, jipangeni na anataka pesa zake.” Joseph Mkweche alisema kwa msisitizo.
“Huyo Shija uliyemuota kakwambia nini?” Kabina aliuliza.
“Amenambia kesho anakuja kuchukua milioni kumi na tano benki, anataka azikute hizo pesa kwenye dirisha langu. Amenihakikishia atakuwa benki saa tano na nusu ahsubuhi.” Joseph alisema alichoagizwa na mtu aliyeitwa Shija Mbitiyaza Lupandagila Masalu, mtu ambae walisadiki alishafariki miaka michache nyuma tena akiwa kwenye mikono ya askari magereza.
“Unaona sasa, nimekwambia umemuota Fisi mwekundu, mtu anawezaje kutaka kuingia benki kwa wizi atoe taarifa saa chache kabla ya muda wa uhalifu? Amka bwana, usingizi wa muda huu usitupite kirahisi na kama umenikumbuka ni vema unambie nije usiku huu kukumasaji kidogo mume wangu...” Kabina aliongea kwa kulegeza sauti.
“Kanambia muda huohuo pia atakuwa ofisini kwako kudai pesa yake, amenambia atawadai wote wenye pesa zake.” Joseph Mkweche akaongeza lakini ni kama hakuwa akieleweka kwa Kanika ambae aliishia kucheka kimahaba na kujaribu kumpooza kwa maneno matamu, hakuwa akiamini kama kweli mtu waliyethibitishiwa kifo chake anaweza kuwa hai ikiwa kifo chake kilitokea akiwa chini ya mikono ya taasisi imara ya ulinzi na usalama.
“Sijachanganyikiwa Kabina, nipo timamu na afya yangu na nikwambie ukweli..” Joseph alinyamaza kidogo kisha akaendelea..
“Jamaa haonekani kutania, anaweza kufanya kama alivyosema ila kama unahisi nipo ndotoni, naomba nikutakie usiku mwema na pole kwa usumbufu.” Alikata simu na kuitupa pembeni yake, usingizi haukuwa na faida yoyote kwake na badala, macho kodo bila hata lepe la usingizi na hakuwa tayari kulala, picha ya mwanaume mwenye mikono imara ikimnyanyua kitandani iliutisha ubongo wake, sauti nzito yenye mamlaka kutoka kwa mwanaume huyo aliyeingia ndani kwake kwa kufungua kitasa cha mlango kwa namna aliyojua yeye, ikawa ni tishio lingine la usingizi wake lakini tishio kubwa zaidi ni pale jamaa huyo mwenye nguvu za ajabu alipomkumbusha jambo ambalo alilishiriki miaka kadhaa iliyopita, jambo hilo lilisababisha mtikisiko mkubwa kwenye familia za baadhi ya watu ambao kwa asilimia kubwa hawakuwa na uhusika lakini msalaba ukawaangukia, wao waliohusika waliendelea na maisha yao kwa amani kabisa hadi siku hiyo aliyotembelewa na huyo mgeni ndipo alipoanza kuhisi amani yao ipo mashakani, angelipata vipi usingizi?
Wakati Joseph Mkweche akishindwa kupata hata lepe la usingizi ili kuyatafuta mapambazuko, Kabina Mkwepu nae hakuwa na amani moyoni mwake. Kitendo cha Joseph kumkatia simu na kisha kuacha kupokea alipompigia ni kama kiliamsha hisia zake zilizolala, hisia za ukweli wa alichaombiwa na ili kulithibitisha hilo ilimlazimu kufanya jambo ambalo alishalisahau kwa zaidi ya miezi kumi na sita, hakulisahau bahati mbaya, alilisahau makusudi kabisa na ilikuwa ni kwa lengo zuri la kiusalama baina yake na wenzake wachache ambao walishakubaliana kuwasiliana endapo kutakuwa na shida ya muhimu sana. Aliitafuta namba aliyokuwa ameihifadhi kwa jina la G.Afande. Akaipata na kuipiga, ikaita kwa mara ya kwanza na haikupokelewa, akasonya huku akirejea kuipiga tena ila ikabaki kuwa vilevile, haikupokelewa. Akatukana kimya kimya na kuiweka kando simu yake huku akianza kuwaza kitu cha kufanya kwa usiku huo ili kupata uhakika wa habari aliyoisikia, akakata shauri kwa kutaka kufanya jambo lingine lakini kabla hajaanza utekelezaji, simu yake ikaita na mpigaji alikuwa ni G.Afande.
“Nilikuwa katikati ya ufundi maana sikuwepo nyumbani kwa karibuni miezi mitatu.” Jamaa alisema huku akicheka.
“Ooh, pole sana kwa bugudha..” Kabina alisema huku nae akicheka.
“Kuna nini? Si kawaida simu yako!” Alisema.
“Huyo uliyekuwa unamfinya upo nae karibu?” Aliulizwa.
“Hapana! Simu yako ni ngumu kuisikiliza mbele ya mtu yeyote.” Jamaa alijibu.
“Sawa.. Unataarifa zozote kuhusu Fisi mwekundu?” Kabina aliuliza. Ukapita ukimya mfupi wa mshangao kwa yule bwana aliyeseviwa kwa jina la G.Afande.
“Una maanisha Shija Mbitiyaza Lupandagila Masalu?” G. Aliuliza.
“Kwani yupo mwingine unaemfahamu?”
“Huyo jamaa si tulishazika kila kitu kuhusu yeye? Unaniulizaje taarifa zake tena, au umemuota?”
“Hebu mpigie yule binti atupe uhakika, nahisi kuna kitu hakipo sawa.”
“Yule binti ni mtaalamu anaetumiwa na idara zetu zote za siri kunyamazisha watu, hawezi kufanya kosa lenye kutuchora. Pia shuhuda wetu alihakikisha jamaa anazikwa kwenye futi sita akiwa na pingu mikononi, haiwezi kuwa maajabu kwa lolote.”
“Mpigie akupashe lolote.. Mpigie sasa hivi.” Kabina alisema na kukata simu, akabaki akiwa anaitazama huku akianza kuingiwa na mawazo yaliyomfanya alikumbuke shuka lake, akalivuta na kulizungusha mwilini mwake ili limsaidie kupambana na ubaridi ulioivamia ngozi yake ghafla na asijue ni kwa sababu gani. Aliyakumbuka macho makali ya Shija Mbitiyaza, macho ambayo alipata kuyaona siku moja tu tena siku ambayo ilikuwa ni siku ya mwisho kabla ya tukio alilohusika nalo kutokea, aliyaona macho yenye ukatili wa kutisha na kuogofya na hata alipopewa sifa nzuri za mtu huyo bado hakuwa na imani na kile alichoambiwa, kwa hisia zake za kike alijikuta akimwogopa mtu huyo ambae alikuwa ameshapewa historia yake kwa kifupi sana, historia ambayo ilianzia huko Misungwi alikozaliwa na kukulia kisha ikahamia kwenye kambi ya jeshi la kujenga taifa huko Rwamkoma, wilayani Butiama mkoa wa Mara. Baada ya hapo ikahamia Orujolo, Arusha kwenye kambi ya jeshi la wananchi na haikuishia hapo tu, ikaenda hadi mkoani Morogoro kwenye kambi ya wanajeshi wenye sifa za ziada kuliko wenzao, sifa ya ukakamavu na usugu kiasi wakapachikwa jina la komando. Baada ya hapo wasifu wake uliendelea kutanuka pale alipokuwa miongoni mwa wanajeshi walioenda kujiunga na kundi la walinda amani nchini Sudan, baadae alienda kulinda amani nchini Mali na huko ndiko uanajeshi wake ulipokoma, alivyoenda sivyo alivyorudi. Alienda kwa kivuli cha mlinda amani lakini alirudi kama mzamiaji na aliufanya siri uwepo wake nchini kwake, miaka michache mbele maisha yalimfanya ajitokeze lakini kwa namna nyingine ambayo ni ngumu mtu kuilewa, jina lake aliongezea majina mengine mawili ili apate kazi kwenye moja ya kampuni za ulinzi zenye kuwalipa vizuri wafanyakazi wake, akafanikiwa kuipata na maisha yake yakaanza kusogea kwa namna ambayo hakuwa ameitarajia, maisha magumu ya mshahara usiokidhi mahitaji yake ya mwezi mzima, lakini hakuwa na namna zaidi ya kukubaliana na hali halisi ya maisha hayo mapya, maisha ya taabu na yaliyochangiwa na kujifichaficha kila muda ili kutotambulika na watu aliyoamini ni wabaya wake, watu walioiwinda roho yake usiku na mchana. Kitumbua chake kilichokuwa kinampa shibe kidogokidogo kikatumbukia nyongo, wasifu wake ukakoma akiwa kwenye moja ya magereza magumu kuyaishi na hapo ile hostoria yake asiyopenda kuisimulia kwa watu ikawa imetamatishwa kwa namna ambayo hata yeye hakuwa ameelewa, wakamzika na maisha yake.
“Lakini picha za mwili wake zilipigwa na tukaziona... Inawezekanaje arejee na uhai wake?” Kabina alizidi kujiuliza pasipo na kupata majibu.
“Itakuwa Jose alikuwa kwenye ndoto na hataki kuamini kama ilikuwa bahati ndoto mbaya kwake.” Aliwaza huku akikata shauri arejee kitandani ili asiendelee kuitafuta sonona ya kujilazimisha. Akajilaza chali na kujivuta shuka hadi kifuani, akafumba macho taratibu na kupiga mwayo wa kuita usingizi. Dakika moja haikukatika tangu ajilaze kitandani kabla ya simu yake kuita kwa fujo, akaipuuza ili kupima shida ya mpigaji kwa kuamini kama asingelipigiwa tena ina maana mpigaji hakuwa na shida ya maana sana, akaacha iite hadi ikate. Sekunde chache baadae ilianza kuita tena, akainuka taratibu na kuishika mkononi mwake, akalitazama jina la mpigaji, akajikuta akinywea kwa kuwa hakurajia kusikia habari njema.
“Tuna msiba mzito...” Sauti iliunguruma kwa wasiwasi.
“Msiba! Nani tena?” Kabina aliuliza kwa wahka.
“Yule binti ameaga Dunia, majirani wameiona maiti yake usiku huu baada ya kuona hatoki ndani tangu mchana na milango ipo wazi...”
“Amekufa kwa kuuawa au?”
“Ripoti ya awali inaonekana alikufa kwa kukosa pumzi, shingo yake ina alama za vidole na bado polisi wanafanyia kazi alama hizo.”
“Majirani wanasemaje?”
“Walimuona jamaa mmoja mrefu mwenye mwili wa chuma akiingia na hawakumuona akitoka hadi walipoigundua maiti ya mwenzao.”
“Alivaa nguo gani huyo mtu?”
“Kofia nyeusi, shati la damu ya mzee na suruali ya michezo..”
“Nakurudia sekunde chache...” Kabina alisema na kukata simu, haraka haraka alimpigia Joseph Mkweche aliyekuwa amelihifadhi jina lake kwenye simu kwa jina, Tulizo.
“Ulisema Fisi alikuwa amevaa nguo gani?” Aliuliza kwa sauti yenye kitetemeshi..
“Kofia, shati la damu ya mzee na suruali ya michezo na buti za jeshi...” Joseph alijibu.
“Basi unabahati kuwa hai, kamuua askari magereza wa kike jioni ya leo.. He’s alive..” Kabina alisema na kukata simu yake, akarejea kumpigia G.Afande..
“Fisi Mwekundu anaishi... Anaweza kuwa mzimu au mtu halisi ila yupo hai...” Alisema huku akitupa shuka kando na kushuka kitandani akiwa amejisitiri kwa nguo ya ndani pekee.
“Haiwezekani bwana...!”, Jamaa alikataa.
“Kwa hiyo unahisi nani kamuua dokta?” Aliulizwa.
“Wapo wengi wanaoweza kufanya hivyo, anaweza kuwa hata mpenzi wake.” Jamaa alijibu kinyonge.
“Mpenzi wake anaweza kuvaa nguo zenye ufanano na mgeni aliyemtembelea kijana wangu usiku huu?”
“Una maanisha mtu mwenye mavazi kama yaliyokwenye ripoti ya upelelezi amemtembelea mtu wako? Kasemaje mtu huyo? Huyo kijana anamjua Fisi Mwekundu?”
“Joseph hawezi kunidanganya mimi wala hawezi kukudanganya. Shija Mbitiyaza amemtembea usiku huu na amemwambia kesho anaenda kuzifuata pesa zake benki kuanzia saa tano ahsubuhi.”
“Una imani ya kwamba marehemu anaweza kufufuka?”
“Una maana gani?”
“Namaanisha tayari Fisi alishakufa na tukazika, pengine kuna mtu mwingine mwenye jambo na kijana wako na si Mbitiyaza Lupandagila.”
“Niliwaza kama wewe lakini uliponipasha kifo cha yule binti na ukanipa ripoti ya mshukiwa wa kwanza, nachelea kusema kwamba, mizimu ya kisukuma imeamka.”
“Kwa hiyo tufanye nini?”
“Sikiliza George..” Kabina alisema kisha akanyamaza kidogo kabla ya kuendelea..
“Wewe ni Kamanda wa polisi naomba usiku huu usilale uhakikishe unapata uhakika wa kifo cha mwanamke huyo, wasiliana na askari wenzake ujue wao wanasema nini... Lakini ahsubuhi pia itatulazimu kuongeza ulinzi kwenye benki yetu, kuanzia ninapofanyia kazi hadi kule anakufanyia kazi Joseph, tufanye mambo kwa umakini ili kujua nani anataka kutuchezea akili...” Kabina alitua.
“Hapa sherehe ameingia mmasai, silali tena.” Kamishina wa polisi, George Kilomba alisema na kukata simu huku jasho likiwa limamtoka, alijiuliza swali, inawezekanaje marehemu aonekane hai? Na kama siyo marehemu ni nani mwenye wajihi wa kufanana nae? Kwa nini tabibu wa magereza ameuawa? Kila swali halikuwa na jibu lake na hakuona wa kumjibu zaidi ya kuuacha muda uwe mwamuzi wa mwisho. Usingizi haukuwa miliki yake tena na badala yake akaamua kukimbilia bafuni kujimwagia maji kabla hajachukua kitabu na kuanza kusoma ili kuisubiri ahsubuhi iliyokuwa mbali nae.
Mapambazuko yalikuwa ni neema kwa kila mtu aliyeamka salama bila mawaa kichwani mwake, lakini yalikuwa ni chungu kwa yeyote aliyelala na kiporo cha mazongemazonge na miongoni mwao ni Kamanda wa kanda maalumu Dar es laam, George Kilomba na wenzake. Yeye aliamka akiwa na lengo moja tu la kuhakikisha anaweka usalama nje ya benki ya biashara na ndani ya benki huku vijana wake wakiwa na picha ya mtu waliyehisi anaweza kuingia ndani ya benki kwa wema au kwa ubaya, ndani ya benki waliingizwa watu wawili wenye silaha na walijifanya kama wateja wa kawaida waliowahi kupata huduma lakini hawakuhangaika na kupata huduma zaidi ya kujizungusha pasi na kueleweka, nje ya benki kulikuwa na kundi kubwa la askari polisi wenye silaha waliokwenye sare na wasio na sare. Licha ya kuwa na taarifa za uwezekano wa matawi mawili yaliyokuwa katikati ya jiji kutembelewa na mtu mmoja lakini nguvu kubwa ikawekwa kwenye tawi lililokuwa mitaa ya Kariakoo, kwa nini? Kwa sababu tawi jingine kubwa lilikuwa kando ya kituo kituo kikuu cha polisi Dar es laam, umbali wa mita nne tu na mita moja kutoka kituo cha daladala. Kwa akili za kawaida ingelikuwa ngumu kwa mtu mwenye nia yoyote kufanya hujuma yake hapo ikiwa kuna askari lukuki umbali mfupi kuliko kawaida. Tawi la Kariakoo ndiko alikofanyia kazi mwanamama Kabina Mkwepu na tawi lilikokando ya kituo kikuu kilikuwa ni kituo cha kazi cha bwana Joseph Mkweche. Hadi inafika saa tano na nusu hakukuwa na kitu chochote chenye kuashiria uwepo wa mtu aliyeitwa Shija Mbitiyaza Lupandagila Masalu, hali ilikuwa shwari sehemu zote za kazi na watu waliendelea kuingia na kutoka wakiwa na amani, kwa Joseph hali ilikuwa tofauti kila aliyefika dirishani kwake alikuwa anahakikisha ameiona vema sura yake, moyoni mwake hakuwa na amani kabisa kila alipomkumbuka mgeni wa ajabu aliyefika nyumbani kwake usiku wa maanani, pengine angelikuwa na amani kama asingeliambiwa mtu huyo alikuwa ni marehemu kwa miaka zaidi ya miwili nyuma, pia mtu huyohuyo aliyesadikika kufa kabla ya kumtembelea usiku alikuwa ametoka kufanya mauaji mahali fulani, mauaji ya mmoja wa watu waliokuwa wakidaiwa na huyo jamaa aliyeaminika alishafariki. Hali yake ilizidi kuwa mbaya zaidi alipohisi ni yeye atakaefuata kuuawa. Saa tano ilipotimia aliamua kuondoka kwenye dirisha lake na akaelekea kantini kwa ajili ya kupata kiamsha kinywa. Haikuwa kama alivyotaka iwe, chai kwake ikawa ni dawa chungu mdomoni kiasi kwamba alishindwa kunywa angalau funda mbili za chai wala kutafuna skonzi zilizokuwa kwenye sahani kando ya kikombe cha chai. Kila mara saa yake ilikutana na jicho lake na mishale aliona ni kama haisogei. Dakika alizopaswa kutumia kuamsha kinywa zilimalizika akiwa bado anaangaliana na kikombe kilichojaa chai, kwa kuwa hakutaka watu wengine wajue hali aliyokuwa nayo akaamua kuelekea maliwatoni angalau kupunguza muungurumo wa tumbo lake. Chooni napo hakufanya lolote licha ya tumbo la kukata kumsumbua, wakati anainuka ili kuzipandisha nguo zake ndipo alipogundua alikuwa anatetemeka na mwili wake ulikuwa umeloa jasho licha ya kiyoyozi kupuliza kila mahali ndani ya benki. Ilikuwa bado ni saa tano licha ya kujizungusha mara zote hizo angalau ule muda wa madai upite, wazo moja likampitia kichwani na akaamua kulifanyia kazi, aliona ni vema atoke nje ya jengo kwa kuzuga anaenda kutafuta dawa za kutuliza maumivu ya tumbo. Huko nje aliona ni bora kuitumia nafasi hiyo kumpigi mtu wake wa karibu, Kabina Mkwepu.
“Nambie baba wa kifua changu..” Kabina aliitikia punde baada ya kupokea simu, sauti yake ikawa faraja kwenye moyo wa Joseph Mkweche ambae alijikuta akifumba macho na kuzishusha pumzi zake kwa tuo.
“Siko sawa tangu usiku wa jana...” Alisema kinyonge huku akivuta pua zake kukabiliana na hali ya mafua iliyoanza kumwandama.
“Usijali sana kwa kuwa jambo hili linafanyiwa kazi kwa umakini mkubwa ili kuzijua mbivu na mbichi, ulinzi upo kila mahali kuhakikisha kama kweli huyo mtu yupo na atajitokeza basi aishie mikononi mwa polisi.” Kabina alimtia moyo.
“Mkishamkamata mtu aliyeandikiwa ripoti ya kifo kwa ushahidi usio na chembe ya shaka mtafanya nae nini?” Joseph aliuliza.
“Itafahamika tukishamtia mikononi na atasaidia serikali kuwaibua waliotengeneza kifo chake.” Kabina alimjibu.
“Lakini kwa nini tusimpe mgao hata kidogo? Naiona hatari huko mbele..” Joseph alionesha shaka yake.
“Upo tayari kutoa kiasi gani kwenye mgao wako? Sikia nikwambie, yeyote aliyekuwa kwenye lile gari hatakiwi kupata hata sumni wala hatakiwi kuwepo Duniani... Mgao ni kwa watu makini tu...” Kabina alisema kwa sauti ndogo ambayo hata ungelikuwa karibu yake angalau mita moja ingelikuwia ugumu kumsikia...
“Nilitoka nje kidogo, naomba niwahi kazini..” Joseph alisema na kukata simu yake huku akiinua mkono wake wenye saa na kuyatazama majira yake ambayo yalikuwa ni kuelekea saa sita na dakika mbili mchana, ikiwa imepita saa moja zaidi tangu alipotoka ofisini. Akarejea dirishani kwake ikiwa ni saa sita na dakika kumi, akaita wateja waliokuwa kwenye foleni na kuendelea kuwasikiliza huku akiwa hajaupoteza umakini wake kwa kila mteja wa kiume aliyelikaribia dirisha alilokuwa akifanyia kazi. Hadi inafika saa saba na dakika ishirini, dakika kumi kabla ya wahudumu wa benki kujumuika kwenye chakula cha mchana, hakukuwa na mgeni yeyote wa kutisha aliyezitembelea benki zote na hapo likafanyika kosa pande zote mbili; askari polisi waliokuwa wameweka ulinzi nje na ndani ya tawi la benki Kariakoo walikata shauri la kuondoka kuendelea na majukumu mengine huku kamanda wao ambae alikuwa anajua kinachoendelea akimpigia simu Kabina na kumwambia uamuzi wake wa kuondoa askari lindoni wakaendelee na majukumu mengine.
“Kijana wako alikuwa anaota..” Alisema baada ya simu yake kupokelewa.
“Inawezekana kweli alikuwa anaota, marehemu hawezi fufuka bwana.” Kabina nae alikubaliana na Kamanda George Kilomba na askari wakaondolewa. Upande mwingine Joseph nae umakini ulipungua na alikuwa anawaza mlo wa mchana ambao kwake ungelimpa muda wa kuikimbia ofisi yake angalau kwa muda wa dakika ishirini hadi ishirini na tano. Ziliposalia dakika mbili kabla ya saa saba na nusu mchana kuna mambo mawili yalikuwa yanatokea sehemu mbili tofauti na sehemu zote zilihusiana, tawi la benki ya biashara Kariakoo kulikuwa na mteja akiondoka ndani ya benki akiwa ameusahau mfuko mdogo ambao ulikuwa na mzigo uliofungwa vizuri kwenye karatasi. Wakati huohuo kwenye dirisha namba nne ambalo lilihudumiwa na Joseph Mkweche, mwanamke mmoja aliyejifunga vizuri kichwa chake na mavazi marefu yakifunika sehemu kubwa ya mwili wake, alikuwa analifikia dirisha huku akiwa na karatasi mkononi na haikuwa mhuri wa benki aliyokuwepo bali ilikuwa ni karatasi nyeupe yenye maandishi machache juu yake.
“Naomba huduma tafadhali..” Mwanamke alisema kwa sauti iliyoisaliti jinsia aliyoamua kujivika, aliongea kwa sauti nzito ya kiume kiasi cha kumshitua Joseph Mkweche ambae alikuwa ameinamia kompyuta yake akitaka kufunga mahesabu ya kuanzia ahsubuhi hadi mchana. Kilichomshitua si sauti ya kiume ya mtu ambae hakuwa ameuona ujio wake, bali ni kuisikia sauti ya mtu aliyemnyima amani tangu usiku hadi wakati huo, akainua macho yake kujihakikishia kama kweli aliyekuwa mbele yake alikuwa ni Fisi mwekundu. Hakuwa amekosea, mbele yake alisimama mwanaume aliye kwenye mavazi ya kike na mkononi mwake alikuwa na karatasi yenye maandishi makubwa yaliyokolezwa.
‘UKILETA UJANJA NALIPUA BOMU.’ Joseph Mkweche aliyasoma hayo maneno na akajikuta akitetemeka kwa hofu.