Chama cha Kikomunisti cha China chaendelea kuwa na mvuto kwa nchi za dunia ya tatu kutokana na msimamo mkali wa kuzingatia maadili

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,034
VCG111473740537.jpg


Katika siku za hivi karibuni Rais Xi Jinping wa China aliongoza mikutano ya kamati mbalimbali za Chama cha Kikomunisti cha China. Kikiwa ni chama tawala cha China, na mchango wake katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii, vikao vya kamati hizo ambavyo ni muhimu katika utendaji wa chama, vimekuwa vikifuatiliwa na wadau mbalimbali wa siasa na utawala.



Huenda Chama cha Kikomunisti cha China ni chama chenye tofauti nyingine na vyama vingine duniani, lakini pia ni moja ya vyama vyenye mvuto mkubwa sana kwa wanazuoni na watu wa kawaida wa Afrika, kutokana na uwezo mkubwa kiliouonesha katika kujenga nchi, kutumikia umma na kupambana na maovu, hasa ufisadi.



Kwenye moja ya hotuba muhimu alizotoa Rais Xi Jinping kwenye mkutano wa kamati ya nidhamu ya Chama cha Kikomunisti cha China, Rais Xi alitaja mambo mawili yanayostahili kufuatiliwa. Moja ni mageuzi ndani ya chama, kwa lengo la kukifanya chama hicho kiende na wakati na kukidhi mahitaji ya sasa ya uongozi. La pili, ni nidhamu na maadili ndani ya chama, hasa kupambana na ufisadi.



Changamoto kubwa ambayo imekuwa inatajwa na wasomi wa nchi za Afrika kuhusu vyama tawala vya nchi za Afrika ni kwamba vingi bado viko kwenye mkao wa ukombozi wa kisiasa na kulinda uhuru wa nchi, vikilinganishwa na Chama cha Kikomunisti cha China, hilo ni moja ya maeneo ambayo wasomi wengi wananaona kuwa vyama hivyo bila kujali tofauti ya kiitikadi, vinatakiwa kujifunza kutoka kwa CPC.



La pili ambao limekuwa na mvuto mkubwa kwa watu wa kawaida wa nchi za Afrika, ni udhati na ujasiri ulioonyeshwa na CPC katika kusimamia nidhamu ndani yake. Kamati kuu ya 20 ya kusimamia nidhamu ya chama cha Kikomunisti cha China imeendelea kupambana vikali na utovu wa nidhamu na kuwaadhibu vikali wale wanaotovuka. Shirika la habari la China Xinhua limetoa takwimu za kazi zilizofanywa na kamati hiyo kati ya Januari hadi Septemba mwaka 2023, zikionesha kuwa kesi zaidi ya laki 4.7 zilifikishwa mbele ya vyombo vya sheria, kati ya hizo elfu 65 ziliwahusu maofisa wa ngazi ya miji, 46,000 ziliwahusu wale waliokuwa madarakani au waliomaliza muda wao ndani ya Chama wa ngazi ya chini.



Itakumbukwa kuwa miaka kumi iliyopita Rais Xi Jinping alianzisha kampeni kali ya kupambana na ufisadi, na kusema hakuna “chui” wala “nzi” atakayenusurika kwenye mapambano dhidi ya ufisadi, akiwa na maana kuwa, sio maofisa wakubwa au maofisa wadogo watakaonusurika kwenye vita dhidi ya ufisadi. Inawezekana kuwa baadhi ya watu wakafikiri kuwa kampeni hii imesahaulika, lakini ukweli ni kuwa imepata mafanikio makubwa na ufisadi umepungua sana. Hata hivyo kama ilivyo katika sehemu mbalimbali duniani, mafisadi wanabuni mbinu mpya kila siku, uzuri ni kuwa mapambano dhidi ya ufisadi ni endelevu.



Kama vyama tawala vya nchi za Afrika vinaweza kujitahidi kufanya mageuzi ya haraka na kukidhi ya mahitaji ya uongozi ya sasa, yaani kuziletea nguvu nchi na kuboresha maisha ya wananchi wanaowaongoza, na kama vinaweza kujifunza kujiendesha kwa nidhamu kali, haitakuwa jambo la ajabu kuona nchi za Afrika zinakuwa na mwelekeo wa maendeleo kama ilivyo China.
 
Back
Top Bottom