Zitto: Watanzania wamegeuzwa wakodishaji wa ardhi

Zitto: Watanzania wamegeuzwa wakodishaji wa ardhi

Dotto C. Rangimoto

JF-Expert Member
Joined
Nov 22, 2012
Posts
1,985
Reaction score
1,286
Watanzania wamegeuzwa wakodishaji wa ardhi
MHE. KABWE ZUBERI ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Moja ya changamoto kubwa sana ya uchumi wa Tanzania ni kutokuwa na uchumi unaokua kwa asilimia 7 kwa wastani wa takribani mwongo mmoja uliopita lakini kutokupunguza umaskini. Hiyo ndiyo changamoto yetu kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu inayotolewa ni kwamba sekta ya kilimo haikui vya kutosha ili kuweza kuhakikisha kwamba Watanzania wengi ambao wanahusika na sekta hii wanafaidika na ukuaji wa uchumi. Kwa muda mrefu sekta yetu ya kilimo imekuwa ikikua kwa takribani asilimia 4 tu toka mwaka 2000. Kwa hiyo, ni kama a flat lined growth, haikui kwa kiwango kile ambacho inaweza ikachochea uchumi mpana zaidi kuweza kukua na kupunguza umaskini wa Watanzania kwa kasi ambayo inatakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wenzetu wa Uganda na Ethiopia mwongo mmoja uliopita wamepunguza umaskini kwa takribani asilimia 25, sisi tumepunguza umaskini kutoka asilimia 34 mpaka asilimia 28. Kwa hiyo, ni takribani asilimia 6 tu hivi. Bado hatujawa na umaskini unaopungua kuendana na kasi ya ukuaji wa uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa suluhisho ni kilimo na katika suluhisho hili, Serikali inatekeleza miradi kadhaa. Kwenye Mpango miradi hiyo iko ukurasa wa 34 na 59 na mingi ni ndani ya SAGCOT. Ni dhahiri kwamba, tunahitaji kilimo kikue. Nilikuwa nasoma taarifa moja ambayo Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango aliandika karika brief ya REPOA Na. 37 ya mwaka 2013 ambayo ningependa kumnukuu, anasema:-

”The growth rate in agriculture will need to increase from 4.4% average over the period of 2000 to 2010 to reach an average of 6% per annum through 2025”. Huyu ni Dokta Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mwaka jana wakulima wamelima, tumefanya intervention, tumepeleka mbegu, pembejeo, tumewapa subsidy, wamevuna chakula kingi kwelikweli. Tumeambiwa kwamba katika mchele mahitaji yetu ya ndani ni kama tani 900,000 lakini wakulima wamevuna tani 1,300,000. Katika mahindi, mahitaji yetu ya ndani ni tani milioni 12 kwa mwaka, wakulima wamelima tani milioni 16 za mahindi lakini mahindi haya mpaka sasa yako ndani, mvua zinanyesha, hakuna maghala, maana yake ni kwamba Serikali haikufanya sequencing katika Mpango. Unapowahamasisha watu walime ni lazima ujenge utaratibu ambao kutakuwa na hifadhi ya hicho chakula cha ziada ambacho kimelimwa. Hakuna sequencing, kwamba hakijafanyika kitu cha kuhakikisha chakula hiki hakiharibiki. Maana yake ni kwamba mwakani wakulima watakuwa wamepoteza ile ari waliyokuwa nayo ya kulima kwa sababu hata wakilima bado utaratibu wa soko unakuwa haujatengenezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri, sasa hivi tunaenda na mfumo wa soko kwamba, tunatarajia Private Sector ndiyo itafanya jukumu hili la kununua lakini haiwezekani! Katika ripoti hiyo hiyo ya taarifa ambayo Dokta Mpango ameiandika, ametoa Messages Nane muhimu kwa ajili ya ukuaji wa uchumi. Message Na. 5 anasema; “a strong developmental state” kwamba, dola ni lazima iingie pale ambapo Private Sector haiwezi kuingia. Sasa dola ilipaswa kujiandaa kwamba kuna mavuno ya ziada. Ukiwaachia wafanyabiashara wa kawaida wataenda kununua mahindi kwa bei ya chini zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunaambiwa kwamba wastani wa mkulima aweze kuuza kilo moja gharama yake ni shilingi 350. Wafanyabiashara wanaenda kununua mahindi kwa shilingi 250 mpaka 200. Maana yake ni kwamba, mkulima huyu badala ya kumuondoa kwenye umaskini, tunamzidisha katika dimbwi la umaskini. Sasa haya ndiyo mambo ambayo tulitakiwa tuyaone yanapatiwa majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona humu Serikali inasema kwamba inataka kujenga maghala lakini unajenga ghala Songea la tani 5000, mahindi yaliyozidi Songea ni zaidi ya tani milioni moja au tani 500,000 au 50,000. Tukumbuke kwamba hili suala la maghala wala siyo jipya. Nyote hapa mliokulia vijijini mnakumbuka kila Kijiji cha Ujamaa wakati ule kilikuwa kina ghala la kijiji lakini kwa sababu ya utekelezaji mbovu wa Sera ya Ubinafsishaji, kila kitu kiliuzwa, tunaenda kuanza upya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Mkuu juzi ametoa taarifa alikuwa Poland, alikuwa ameenda kutafuta msaada wa kujengewa mgahala. Haya mambo kama tungekuwa tumeya-plan toka mwanzo, tungerudisha utaratibu ule wa kuwa na mgahala vijijini kwa ajili ya kutunza chakula na kuweza ku-link maghala na masoko ya ndani na masoko ya nje. Kwa hiyo, haya ni mambo ambayo yanapaswa kuwa addressed katika Mpango wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika hili la SAGCOT, tunasema tuwezesha wakulima wakubwa walime halafu watawasaidia wakulima wadogo through out growers scheme. Hakuna shida ya out growers scheme, tatizo linalokuja ni kwamba, sasa hivi Watanzania wamegeuzwa wakodishaji wa mashamba ya hawa wakulima wakubwa. Hatuwezi kujenga uchumi namna hiyo, kwa sababu hawa wananchi hauwamilikishi ardhi. Wenzetu wanachokifanya kwenye mipango kama hii ni kwamba, kama una hekta 60,000 unataka zilimwe kisasa, theluthi mbili ya zile hekta 60,000 unawapa wakulima wako unawamilikisha, theluthi moja ndiyo unampa mkulima mkubwa. Kwa hiyo, yule mkulima mkubwa anapolima anakuwa pamoja na wale wakulima wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa kinachoendelea katika sehemu kubwa ya SAGCOT hasa kule Kilombero mashamba makubwa wamepewa wawekezaji wakubwa, halafu wale wakulima ambao ni out growers wanawenda kukodisha. Kwa hiyo, tunawageuza wananchi wetu kuwa manamba na wakodishaji wa ardhi. Huo uchumi utakaokua utakuwa ni kwenye numbers na si kwa wananchi kwa sababu hawatakuwa wamemiliki huo uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba jambo hili lirekebishwe. Maeneo yote ambayo kulikuwa kuna mashamba makubwa ya Serikali, wanapopewa wawekezaji wakubwa wanarudi kuwakodishia wananchi, kwa nini tusiwape wananchi tukawa-link na wale wawekezaji wakubwa, wakalima kwa pamoja na uchumi ukawafaidisha watu wote kwa pamoja? Hiyo ndiyo hoja ambayo inabidi tui-address katika Mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kulizungumzia ni akiba. Nchi yetu hivi sasa savings to GDP Ratio ni 16%. Unapotaka uchumi wako ukue (akina Dokta Mpango wanajua hili) kwamba, unahitaji total factor productivity kwa level ya uchumi wetu ya between 2% and 2.5%. Ili upate hiyo total factor productivity ni lazma uweke akiba. Uwekaji akiba Tanzania ni 16%. China uwekaji wake wa akiba ni 50% ya GDP. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa solution ni nini? Hifadhi ya jamii kwa mkulima. Tuweke mazingira ambayo mkulima atajiwekea akiba kwenye hifadhi ya jamii. Ile akiba tutaitumia kwenye uwekezaji wa miundombinu ya kilimo kwa sababu hifadhi ya jamii liability yake ni long term na uwekezaji kwenye kilimo return yake ni long term, kwa hiyo, vinaendana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba, ni lazima kwenye Mpango tufanye amendment tuhakikishe kwamba yale maeneo ambayo tunafanya intervention kama SAGCOT, kuna wakulima wadogo milioni mbili watafaaidika, tuwa-link na hifadhi ya jamii. Tukifanya hivyo tutaongeza savings nchini na tutapata fedha za kujenga miradi yote ya umwagiliaji kwa sababu social security ni long term liability na investment kwenye kilimo ni long term liability. Haya ndiyo mambo ambayo tunapaswa tuyaone kwenye Mpango na yataiepusha nchi kuondoka huko baadaye kuwa na kundi kubwa la wazee ambao hawana hifadhi ya jamii kwa sababu watakuwa wamejiwekea akiba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo napendekeza, hoja yangu ya mwisho, naomba unipe dakika moja tu, kila mkulima anayechangia shilingi 20,000 kwenye hifadhi ya jamii, Serikali imuwekee shilingi 10,000. Tukifanya hivyo tutapa wakulima wengi sana ambao wataingia kwenye hifadhi ya jamii na wakifanya hivyo tutapata savings kubwa sana na tuta-solve matatizo mengi sana. Haya matatizo tuliyonayo ya Benki ya Kilimo kukosa mtaji hayatakuwepo kwa sababu watakwenda kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii watakopa kwa ajili ya hiyo Benki ya Kilimo, tutajenga miundombinu vijijini na tutahakikisha kwamba, uchumi wetu unawafaidisha Watanzania wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ndiyo mapendekezo yangu ambayo naomba muyaweke katika Mpango. Ninaamini yatafanyiwa kazi ili kuweza kuhakikisha kwamba nchi yetu inakwenda mbele.
Waheshimiwa Wabunge, naomba nirudie kusema kwamba, turudi kwenye Mpango, tuujadili Mpango, tuukosoe Mpango, tutoe mapendekezo kwenye Mpango, tuachane na porojo za kisiasa. Mheshimiwa Mbatia ametuongoza, Mama yangu Diana Chilolo ameturudisha kulekule kwa jana, kwa jana hakufai, leo ndiyo kuzuri, twende mbele tuwasaidie wananchi wetu kwa kuwa na Mpango bora na mzuri.
 
Back
Top Bottom