Zitto ana kibarua kizito

Asha Abdala

JF-Expert Member
Mar 21, 2007
1,130
44
Na Tambwe Hizza

HIVI karibuni, Rais Jakaya Kikwete aliunda kamati maalum ya kushughulikia masuala ya madini, huku akimteua Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) kuwa mmoja wa wajumbe.

Kilichofuatia baada ya hapo, wote tunakijua, lakini mbaya zaidi kwa upande wa upinzani ni kwamba, inaonyesha au kuthibitisha kwamba ni wazito kuelewa mambo.

Katika kusherehesha hoja yangu hiyo, nitatoa mifano michache mingine, ikiwa inanigusa mimi mwenyewe, lakini kwa kuwa ni mambo yaliyopita sidhani kama itakuwa vibaya kuyasema angalau kwa uchache.

Wapinzani kwa mtazamo wangu hupenda kufanya mambo bila kwanza kuangalia kwa kina athari na faida zake. Kiongozi anaweza kuchukua hatua au kuwashawishi wenzake wakubaliane naye na hatimaye kupitisha katika vikao au hata nje ya kikao maamuzi ambayo baada ya hapo ukimuuliza faida yake, hata yeye hajui.

Mwaka 1995 niligombea ubunge jimbo la Temeke kupitia NCCR Mageuzi na nilikuwa mmoja kati ya wagombea waliokuwa wanapewa nafasi kubwa ya kushinda kwa sababu mbalimbali za wakati huo.

Baada ya uchaguzi wa Dar es Salaam kusimamishwa na tume ya uchaguzi na kupangwa kufanyika baada ya wiki mbili, huku matokeo yaliyokuwa yakitangazwa kutoka mikoani yakionyesha aliyekuwa mgombea urais kupitia CCM, Benjamin Wiliam Mkapa anaongoza kwa kura nyingi, aliyekuwa mgombea urais kupitia NCCR Augustino Mrema, akatangaza chama chake kujitoa na hakitashiriki katika uchaguzi huo kwa nafasi zote, ya urais na ubunge.

Kwa kuwa matokeo yalikuwa tayari yanaonyesha kwamba mgombea wa CCM alikuwa ameshapata kura nyingi ambazo Mrema asingeweza kuzifikia hata kama kura zote za Dar es Salaam angepewa yeye, hatua hiyo ilipokelewa na wengi wa wagombea wa Dar es Salaam kama hatua ya tukose wote.

Wagombea wengine wa Dar es Salaam wakampinga, wakaendelea na uchaguzi na Dk. Lamwai akashinda katika Jimbo la Ubungo kwa kishindo, jambo ambalo lilimuudhi sana Mrema ambaye baadaye alionyesha chuki za wazi wazi kwa Dk. Lamwai zilizosababisha baadaye apoteze jimbo lake.

Wapo wanaosema Mrema alimsaidia Venance Ngula kushinda kesi ya kupinga ushindi wa Dk. Lamwai kama ni kweli au la mimi sijui, lakini Mungu anajua.

Vitimbi vilivyofuatia baada ya hapo viliishia kwa Dk. Lamwai kwenda katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa salama na amani kama wengi wetu tulivyoishia kufanya.

Lakini ukiangalia mzozo huo ulioanzia kwa Dk. Lamwai kupinga maamuzi ya mwenyekiti nje ya vikao na nje ya madaraka yake kikatiba, mpaka leo ukimuuliza Mrema faida yake ni nini hawezi kukujibu.

Kama hilo halitoshi, mimi ambaye kwa ujinga na utoto tu niliamua kumuunga mkono Mrema kama mwenyekiti wangu wakati huo ndio nilipata balaa zaidi.

Mara tu uchaguzi ulipokwisha, viongozi wa wilaya wakaandaa kundi kubwa la wahuni kuja kunidai fedha za uwakala wakinilazimisha kwenda katika tume ya uchaguzi kuchukua fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya mawakala wangu.

Wengi waliokuwa wagombea walipata fedha za bure wakati ule kwani baada ya Mrema kutangaza kujitoa baadhi ya vyama vikiwemo CUF na UDP vilimuunga mkono, jambo lililosababisha tume kutangaza kwamba wagombea wanaoshiriki kwa kuwa walishateuliwa na tume hivyo basi wana haki ya kwenda kuchukua fedha hizo wao wenyewe.

Wengi walikwenda wakazichukua na hawakuweka mawakala katika uchaguzi huo kwa kuwa walikuwa wanajijua hawana nafasi yoyote katika uchaguzi huo.

Kwa hiyo na mimi nikalazimishwa kwenda kuzichukua, nikakataa kwa kuwa uchaguzi tuliususia na mawakala hatukuweka, lakini wenzangu wakadai mbona wamechukua lazima nikachukue.

Sakata halikuishia hapo, siku moja nikiwa katika foleni ya magari pale Chuo cha Ufundi nikielekea mjini nikasikia kundi kubwa la watu likiandamana na kuimba.

Lilipoona gari langu likaja kunivamia na kunipeleka hadi tume ya uchaguzi kwa nguvu na gari langu nikiwa nimeliacha pale.

Kwa hasira nilizokuwa nazo kwa kitendo kile cha uonevu walichonifanyia, nilipofika tume ya uchaguzi waliponiingiza ndani na kwa nguvu eti nikachukue fedha nikaomba msaada kwa kamanda aliyekuwa anasimamia usalama wa pale ambaye aliwasiliana na polisi kituo cha kati ambao bila hiyana walifika na kuwasambaratisha, jambo lililosababisha baadhi yao kupata majeraha kwa ujinga tu.

Wanamuunga mkono mwenyekiti tujitoe nimejitoa, wanataka hela nilishindwa kuwaelewa na hadi leo sijawaelewa, maana walitaka nikaibie tugawane, lakini hadi leo akiulizwa Mrema na wote waliokuwa wakimuunga mkono faida iliyopatikana kwa uamuzi ule hakuna na vita alivyopigwa Dk. Lamwai baada ya pale hakuna faida yoyote iliyopatikana.

Jitihada zangu za kumuomba Mrema anisaidie ili nisiendelee kusumbuliwa ziligonga mwamba, lakini nilipomshitaki Kihiyo mahakamani na hatimaye kiti kuwa wazi alikuwa wa kwanza kujitokeza kugombea na kusahau misukosuko yote niliyoipata nikakasirika nikaamua kuachana na chama hicho, nikaondoka na kujiunga na CUF.

Tafsiri yao kwa jambo hilo ilikuwa kwamba, eti mimi nimetumwa na CCM nigombee kwa CUF ili kupunguza kura za Mrema asishinde.

Kila nililosema kuhusu Mrema kwamba hafai nikadaiwa kuwa kibaraka wa CCM kama wengine wote waliopingana naye ndani ya chama chake wakati huo na baadaye TLP walivyodaiwa bila kuwasahau wabunge ambao walikuwa viongozi ambao alitaka waachie uongozi au ubunge, lakini wasifanye kazi mbili.

Lakini yeye alipopata ubunge mwaka 1996 akaacha kulisema hilo, mwaka 1996 mwishoni mgogoro wa NCCR ulipopamba moto niliandika makala ukurasa mzima katika gazeti la Majira kumuomba aachane na mpango wa kuwatimua viongozi wenzake kwa kuwa wakishikilia katiba kuna hatari ya kuwa na uongozi seti mbili.

Wapambe wake walipoisoma wakanishambulia sana kwamba najipendekeza na kujaribu kujiosha kwa kuwa nilitoka huko na mengine kadha wa kadha ambayo siwezi kuyaandika gazetini.

Lakini matokeo yake kila mtu anajua aliuacha ubunge huku akiupenda na kukikimbia chama hicho akiwa na wale waliokuwa wakiitwa 'Tutamfuata Lyatonga Popote (TLP)', ukiwa ni ushindi mkubwa kwa wale aliotaka kuwang'oa, mwaka 1995.

Wapinzani walipata takribani asilimia 40 ya kura zote za urais, waliokuwa wakipenda mageuzi wakati huo (wengi wamerudi CCM) walishauri wapinzani waungane tayari kwa kuikabili CCM mwaka 2000.

Lakini hawakukubali na Mrema akiwa kiranja, na matokeo yake, mwaka 2000 kura za mgombea wa CCM zikaongezeka kwa takribani asilimia 10, Mrema akapokonywa nafasi ya pili na Profesa Ibrahim Lipumba ambaye aliungwa mkono na Chadema.

Viti vya wapinzani vikapungua bungeni kutoka 58 mpaka kanuni ikabadilishwa ili upinzani uweze kuunda serikali kivuli bungeni kwa viti chini ya 30 kama kanuni ya awali ilivyohitaji.

Mwaka 2005 yakawa hayo hayo hawakuungana matokeo yake Rais Kikwete akachukua karibu kura zote za urais na wapinzani kuambulia viti 7 tu kati ya viti 182 vya upande wa Tanzania bara.

Hili lilitokea hata baada ya vyama vya upinzani kukutana Dodoma katika Ukumbi wa CCT Februari 2001 ambako walikubaliana uchaguzi wa mwaka 2004 wa serikali za mitaa vijiji na vitongoji utumike kama kigezo cha kuungana na kuachiana majimbo.

Walikubaliana na mimi nilikuwepo kwamba chama chochote kitakachofanya vizuri katika uchaguzi huo eneo fulani basi wakati wa uchaguzi mkuu kiachiwe jimbo hilo kigombee na kile kitakachopata kura nyingi kitaifa dhidi ya vyama vingine kiungwe mkono kisimamishe mgombea urais jambo ambalo halikufanyika.

Nayasema yote haya si kwa nia ya kumkomoa yeyote kwa kuwa yameshapita, ila ni kutaka kuonyesha kwamba wapinzani ni wagumu kushaurika na hawaelewi nini cha kufanya na kwa hiyo Zitto anapaswa kuelewa yuko katika kundi gani na anapaswa kuwa shupavu endapo anahitaji kuitumikia nchi yake akiwa huko.

Mara tu uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 ulipokwisha, matokeo ya uchaguzi yalipotoka, nilikuwa hoi hospitali na baada ya kutoka ICU ya pale Regency Hospital.

Niliporuhusiwa nilitakiwa nipumzike nyumbani, lakini nilishindwa kujizuia siku Baraza Kuu la Taifa la CUF lilipoitishwa, nikajikongoja nikatoe mawazo yangu ambayo nilidhani yatasaidia kukiokoa chama changu bila kujua kwamba ndiyo nilikuwa naenda kujijengea msingi wa kuachana na chama hicho.

Nilikishauri chama hicho wakati wa kuunda serikali kivuli kisihusishe vyama vingine kwa vile kimefikisha idadi inayotosha kukidhi kanuni ya Bunge ya wabunge 21, nikatoa sababu ambazo kimsingi niliamini zitakilinda kisifunikwe na vyama vingine vyenye wabunge Tanzania bara na hususani Chadema ambayo ilishaonyesha kutaka kuchukua nafasi yake ya kuwa chama kikuu cha upinzani kutoka kwake baada ya kushika nafasi ya pili kwa kura za urais katika mikoa 5 ukiwemo wa Mara ambako haikutegemewa kwamba wangeweza kufikia mafanikio hayo na kupata mbunge mmoja.

Pendekezo hilo lilipokelewa na Baraza Kuu baada ya majadiliano marefu sana, sababu zangu za kimsingi zilikuwa ya kwanza kwa kuwa CUF hakina mbunge hata mmoja wa jimbo la Tanzania bara kushirikiana na vyama vyenye wabunge bara katika serikali kivuli kutawafunika, ya pili katika Bunge la 1995 na lililopita vyama viliunda serikali kivuli ya pamoja, lakini hakuna faida yoyote ambayo wapinzani walipata zaidi ya kura kupungua katika uchaguzi uliofuata wa 2005.

Baadhi ya wabunge walipoenda bungeni na kutochaguliwa katika nafasi zilizotengwa kwa ajili ya upinzani, waliporudi tu wakamuandikia mwenyekiti wa taifa na kumtaka ahakikishe uamuzi huo unaondolewa katika baraza linalofuata ambalo sikuhudhuria kutokana na vitimbi vilivyokuwa vimeanza dhidi yangu.

Ndiyo maana nasema kuwa mpinzani nchi hii ni balaa, unatakiwa uwe sugu kupindukia, kwa hiyo namshauri ndugu yangu Zitto awe mvumilivu na atekeleze majukumu yake. Hoja ya kushiriki halafu kuikana ripoti mwishoni itamuaibisha, asiikubali, atoe mchango wake na pale atakapoona mizengwe, amuarifu aliyemteua na si vinginevyo, haya ndiyo mawazo yangu na tuendelee kushirikiana katika uchambuzi wa siasa za nchi yetu.

Kutoka: http://www.freemedia.co.tz/daima/2007/12/5/makala3.php
 
huyu ni tambwe hiza yule aliyetujulisha kuwa alikuwa akipika uongo wote wa CUF!!!
Leo anaweza akawa malaika na kushauri mambo mema kweli??
hapana mimi sikubaliani na huyu mwenda wazimu anayetukana mamba wakati hajavuka mto!! amejijua lini kuwa alikuwa sahihi wakati ni mtunzi wa uongo wote wa CUF? nani asiyejua kuwa amebebwa na ndugu yake makamba ili wamwngushe kigoda kule Tanga? leo hana mpya ni mtu mzushi kwa tabia ndio maana hata akiomba kuwa kiongozi wa mtaa hawezi kuchaguliwa. namwomba sana anyamze ili tusahau pumba zake vinginevyo atakufa natural death kisiasa.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom